Monday, June 16, 2008

YATAMBUE MAGONJWA YA MSONGO WA MAWAZO

KARIBUNI wapenzi wasomaji wetu katika siku nyingine ya leo. Tumekuwa tukiangalia maana ya msongo na vyanzo vyake. Leo tutaendelea kuangalia vyanzo zaidi kuhusu msongo unaowapata watoto na dalili zake.
Vyanzo vingine ni magonjwa, wafanyakazi wengi katika eneo la kazi, mawasiliano hafifu kati ya timu, kutotoa taarifa juu ya utendaji, thamani na mchango, mabadiliko ya kiteknolojia, ukosefu wa uwazi wa majukumu na wajibu, kutoridhishwa na mafanikio ya kifedha, kuchoshwa na kazi zisizo na mvuto, tukio lisilofurahisha, mazingira ya kazi yasiyovutia na ukosefu wa ujuzi.
Inakubidi kuangalia hali yako ya msongo uliyonayo ili uweze kuikabili, na uwasaidie wengine kupunguza hali hiyo.
Kwa upande wa watoto, kama walinzi na waangalizi, watu wazima wamekuwa na tabia ya kuwaangalia watoto kwa ukaribu ili wawe na furaha na bila kuwa na mawazo. Vile vile tunaona kuwa watoto hawana majukumu makubwa ambayo yatawafanya wawe na msongo kama ilivyo kwa wazazi wao. Kwa hiyo hawana kitu cha kuwafanya wawe na wasiwasi.
Hata hivyo watoto wanakuwa na hofu na kuwa na mawazo kwa kiwango fulani. Mawazo yanakuwapo kutokana na mahitaji tuliyonayo pamoja na majukumu ambayo inabidi kuyafikia.
Hebu tuangalie vyanzo mbalimbali vya mawazo kwa watoto. Mara nyingi shinikizo linakuja kutokana na misongo ya nje kama familia, marafiki au shule, lakini inaweza kuwapata kutoka ndani. Shinikizo linalokuwepo kwetu linaweza kuwa na faida kwa sababu mara kwa mara linakuwa na tofauti kati ya kile tunachofikiri tunapaswa kukifanya na kile kitu halisi tunachokifanya katika maisha yetu.
Msongo wa mawazo unaweza kumwathiri mtu yeyote hata mtoto anayehisi kulemewa. Mtoto wa miaka miwili, kwa mfano, anaweza kuwa na wasiwasi kwa sababu mtu yeyote anahitaji kujisikia vizuri - mzazi asipokuwa karibu naye na kumridhisha. Kwa watoto ambao hawajaanza shule hali ya kutengwa na wazazi ni sababu kubwa ya wasiwasi.
Pale watoto wanapokuwa na mawazo mengi kuhusu masomo yao au matatizo mengine ya kijamii huwasababishia kuwa na msongo wa mawazo. Kwa kuongezea, wazazi wakati mwingine pasipo kujua wanaongeza mawazo katika maisha ya watoto wao. Kwa mfano, matarajio makubwa ya wazazi mara nyingi ni matazamio makubwa kwa watoto wao, na yanapokuja kinyume husababisha msongo wa mawazo kwa watoto wao. Wazazi wengi huwashinikiza, kwa njia mbalimbali, watoto wao kufanya vizuri au kuwaandikisha watoto wao katika vitu vingi vinavyoweza kusababisha mawazo yasiyokuwa ya lazima bila ya wao (wazazi) kushirikiana nao. Hii wakati mwingine kuwakatisha tamaa watoto hao na hivyo kuwa na msongo wa mawazo.
Wataalam wengi wanahisi kuwa asilimia kubwa ya watoto wanajishughulisha zaidi, hivyo wanakosa muda wa kucheza kutokana na vipaji vyao au kupumzika baada ya masomo. Watoto hulalamikia juu ya shughuli nyingi wanazojishughulisha nazo au wakati mwingine wanakataa kufanya shughuli walizopangiwa na wazazi wao wanaokuwa wana mambo mengi na kujikuta katika hali ya msongo.
Ni jambo jema mzazi kuzungumza na mtoto wake kuhusu (motto) anavyojisikia baada ya shughuli za kimasomo. Kama mtoto atalalamika, zungumza naye juu ya kumpunguzia baadhi ya shughuli. Zungumza na mtoto wako njia utakazoweza kumsaidia mtoto wako kupangilia muda wake na majukumu yake, hali itakayomfanya asiwe na wasiwasi.
Kama mtoto wako atakuwa anasikia ukiongelea matatizo ya kazini kwako, wasiwasi juu ya ndugu yako aliye mgonjwa, au matatizo ya kiuchumi unayokabiliana nayo, inamfanya naye awe na wasiwasi. Wazazi wanatakiwa kuwa makini wanapojadili mambo kama hayo wakati watoto wao wako karibu nao kwa sababu huyachukua maongezi hayo kutoka kwa wazazi wao na kuanza kuwa katika hali ya wasiwasi.
Tukio la Septemba 11, 2001 na mabadiliko katika dunia yetu tangu siku hiyo yamechangia kuongeza wasiwasi kwa watoto wengi na kwa wale wote walioathirika na tukio hilo. Watoto wanaoangalia marudio ya michezo ya matukio mbalimbali ya kutisha katika runinga au kusikia habari za kuanguka kwa ndege, vita, na ugaidi unaleta wasiwasi kuhusu usalama wao na kwa watu wanaowapenda.
Zungumza na mtoto wako kuhusu kile anachokiona au kusikia na kufuatilia kile anachokiangalia katika runinga, hivyo utaweza kumsaidia mtoto wako kuelewa kinachoendelea na kumwondoa hofu.
Pia, angalia sababu za kutatanisha kama ugonjwa, kifo kwa umpendaye au talaka, inaweza kusababisha msongo wa mawazo kwa mtoto wako. Wakati sababu hizi zinachanganyika na kusababisha shinikizo katika sura ya watoto, mawazo yanakua. Ingawa kunakuwapo na maridhiano kwa wazazi katika kupeana talaka, inakuwa ni jambo zito kwa watoto kwa sababu ulinzi wao muhimu unabadilika. Kutengana au kuachana kwa wazazi kamwe hakutawaweka watoto katika hali ya kuchagua upande wautakao au kuwaeleza ubaya wa mzazi mmojawapo, ambaye amesababisha kuwepo kwa hali hiyo.
Magonjwa ya msongo wa mawazo Si rahisi mara zote kugundua mtoto wako amepatwa na msongo. Ila utagundua kwa muda mfupi tabia yake imebadilika, mwonekano wake unabadilika, vitendo vyake au kutokwa na jasho jingi anapokuwa amelala. Hizi ni dalili za kuwa na mawazo. Baadhi ya watoto wanakumbana na mabadiliko ya kimaumbile ikiwa ni pamoja na kuumwa na tumbo na kichwa. Wengine wanataabika katika kumaliza kazi za shule wanazokuwa nazo. Wengine wanakuwa wapweke au wanakaa wenyewe kwa muda mrefu.
Watoto wamekuwa wakionyesha dalili za kuwa na mawazo kwa kuwa na tabia mpya kama kunyonya kidole, kuzungushazungusha nywele, au kugusagusa pua. Watoto wakubwa kidogo wanaanza kudanganya, kuona ufahari au kutokutii. Mtoto mwenye msongo huwa analala kwa kushtukashtuka, anakuwa mgumu kuachana na mtu anayeonyesha hisia zake katika matatizo madogo madogo na kubadilika kimasomo.
Kupunguza mawazo ya mtoto wako
Unaweza kumsaidiaje mtoto wako kuondokana na msongo? Kwa kuwa na muda mzuri wa kupumzika na kumpa lishe bora, itamsaidia kumwongezea mtoto wako uwezo. Kuwa na muda wa kuzungumza na mtoto wako kila siku. Kama atahitaji kuongea na wewe au kuwa na wewe katika chumba kimoja, kuwa na muda wa kumsikiliza. Hata pale mtoto wako atakapokuwa mkubwa muda huo wa faragha naye ni wa muhimu.
Ni vigumu kwa baadhi ya watu wanaporudi nyumbani baada ya kazi, kukaa chini na kucheza n watoto wao au kuongea nao kuhusu siku hiyo, zaidi sana kama wamepatwa na jambo lililowasababishia mawazo katika siku hiyo. Lakini unapoonyesha hali ya kujali katika maisha ya mtoto wako, unaonyesha jinsi alivyo wa muhimu kwako.
lcyngowi@yahoo.com0713 331455/0733 331455

0 Maoni:

Twitter Facebook