Sunday, June 15, 2008

EPUKA MIJADALA INAYOLETA MIFARAKANO

MAHALI popote penye mkusanyiko wa watu iwe ni majumbani, kazini, shuleni, vyuoni na sehemu nyingine mbalimbali ambazo zinakuwa na mkusanyiko wa watu, kunaweza kutokea migongano isiyokuwa ya lazima.
Hivyo basi kutokana na hali hiyo ni vizuri kila mmoja akajua na kujifunza mbinu mbalimbali za kuishi na kila mtu.
Kwani anaweza akafanya jambo ambalo anaona kwake ni zuri na wakati huo huo likawa chukizo kwa watu wengine na hii hutokana zaidi na maeneo ya mtu aliyokulia, mazingira ya familia iliyomzunguka, shule aliyosoma na malezi kutoka kwa wazazi au walezi wake.
Hivyo basi ili kukabiliana na hali hiyo ni vizuri kujua mbinu na kanuni za kuishi na watu vizuri.
Kumbuka mtu anapendwa na watu kutokana na kufuata tabia na kanuni za watu wanaomzunguka, pia mtu huchukiwa kutokana na kwenda kinyume cha kanuni za kuishi na watu vizuri wanaomzunguka.
Katika jamii inayotuzunguka ni vizuri mtu akawa na tabia ya kupenda watu kwa moyo wote, hii ina maana kuwa unapoonyesha upendo kwa mtu, uwe hivyo hadi ndani ya moyo wako na si kumuonyesha mtu tabasamu la machoni wakati ndani ya moyo umejaa unafiki.
Vile vile mheshimu kila mtu na kumuona ni wa maana na anahitajika. Penda kuwa na heshima kwa kila mtu, awe mkubwa au mdogo. Mthamini kwa kumuonyesha kuwa ni wa maana kuanzia maneno yake, matendo yake na mawazo yake yote, hata kama wakati mwingine atatoka nje ya mstari.
Kanuni nyingine ni kuwa na tabasamu la kuchangamka na kuonyesha uso wenye furaha kwa watu. Katika kanuni hii epuka tabasamu la uongo, lisilokuwa na chembe ya upendo, kwani linaleta athari katika sehemu za kazi, shuleni na kwenye mikusanyiko mbalimbali. Epuka tabia ya kulaumu, kuchamba watu au kusengenya.
Kila mtu ajizoeze kutoa shukrani kwa jambo linapotendeka. Wakati mwingine mzazi wako, bosi wako sehemu za kazi au mwalimu wako anakupa pongezi kwa jambo fulani ambalo umelifanya.
Inapotokea hivyo, usisite kuonyesha shukrani zako ili uweze kumfurahisha aliyekupongeza hata kama jambo hilo ni dogo ni vyema ukashukuru.
Tabia za ubishi na mabishano hazifai katika jamii. Kumbuka kwenye mkusanyiko wa watu mahali pote huwa kuna watu ambao wanajiona kuwa wao wanajua kila kitu hivyo jaribu kujua tabia ya kila mtu ili uweze kuishi nao na kuepuka mabishano yasiyo ya lazima.
Kumbuka huwezi kumbadilisha mtu kwa njia ya mabishano, kinachotakiwa ni kueleweshana kwa ustaarabu kwani mnapobishana wote mnakuwa wajinga.
Tabia ya upole inajenga mahusiano bora katika maeneo yenye mkusanyiko wa watu. Pamoja na upole jitahidi kuwa mtu rahisi wa kufikiwa katika ushauri na mahitaji mbalimbali ya kiofisi na kimasomo.
Mara nyingi kila mtu hupenda kupendwa hivyo basi inapotokea mwalimu, mfanyakazi mwenzako au bosi katika maeneo mbalimbali anapokuwa makini na kukumbuka majina ya watu wanaomzunguka inaleta heshima na faraja. Hivyo ni vizuri ukijifunza kukumbuka majina ya watu unaoweza kukutana nao.
Hapa namaanisha kuwa jifunze kukumbuka majina ya watu wote unaoweza kukutana nao au unaokutana nao.
Ni vizuri kuepuka kumsifu mtu isivyostahili kwani ni kumvika kilemba cha ukoka. Kuna watu wengine hupenda kutoa sifa kwa mtu tofauti na mpewa sifa alivyo. Hivyo basi anayestahili sifa mpe sifa yake na anayestahili heshima mpe heshima yake lakini usithubutu kutoa sifa ya uongo kwani itakuondolea heshima na kumvika kilemba cha ukoka mhusika huyo kiasi kwamba ataweza kudharau wengine.
Mara zote unapozungumza na mtu jaribu kuzungumza naye kulingana na mambo anayoyapenda.
Kwa mfano, unajua mtu huyo hapendi mambo ya mzaha, zungumza naye mada zile anazozipenda au unapogundua mtu unayezungumza naye hapendi masuala ya muziki, siasa au michezo jaribu kuzungumza naye yale anayoyapenda ili muwe na uwiano katika mazungumzo yenu, vinginevyo mara zote mtatofautiana katika mazungumzo yenu.
Epukana na mijadala juu ya hoja zinazoleta ugomvi au mifarakano. Katika jamii inayotuzunguka mara zote mijadala ya siasa ambayo unakuta watu wametofautiana katika vyama, mijadala ya timu za mipira, dini mbalimbali huchangia ugomvi na mara nyingine mifarakano. Hivyo ni vizuri ukaepuka hayo ili kuleta hali ya amani.
Epuka kusengenya au kusema mtu katika udhaifu wake. Mara nyingi tabia mbaya ya masengenyo ipo kwa makundi ya kina mama, naomba mniwie radhi kina mama kwa kuwa huwa na tabia ya kuoneana wivu na kutopenda maendeleo ya wenzao.
Lakini pia wapo wanaume ambao wamejiingiza katika makundi ya wanawake na kushiriki kusengenya ili tu waonekane wema machoni pa wanawake hao.
Unapomwona mwenzako ana udhaifu mathalani katika kujieleza, kuvaa, usafi katika maeneo mbalimbali ni vizuri ukamwita kwa upendo na kumrekebisha. Si ustarabu kusimulia udhaifu wa mwenzako kwa kuwaeleza watu na baada ya kumsengenya ndipo unamwita na kumweleza upungufu wake.
Fanya hivyo kabla ya kumsengenya, utajijengea heshima katika jamii inayokuzunguka hata yule unayemsaidia.
Jifunze kusikiliza shida na matatizo ya watu. Unapokuwa baba au mama wa familia, kiongozi katika ofisi, shule, mtaa, taifa na maeneo mbalimbali yanayotuzunguka penda kusikiliza shida za kila mtu bila kubagua jinsia, kabila, rangi au elimu.
Unapojenga tabia ya kuwa msikilizaji wa shida na matatizo ya watu utakubalika katika jamii na hata kwa taifa. Hali hiyo itakuongezea heshima.
Jifunze kuvumilia na kusamehe pale unapokosewa na watu wengine na toa msaada unaohitajika kwao kila wanapohitaji kutoka kwako. Baadhi ya watu mbalimbali neno uvumilivu huwa ni gumu kwao pamoja na neno kusamehe.
Hivyo ni vizuri kujijengea tabia ya kuwa mvumilivu na mtu wa kusamehe pale unapoumizwa na rafiki, jirani, mwalimu hata bosi wako.
Epukana na tabia ya kujisifu kutokana na mafanikio uliyoyapata. Hii ina maana kuwa hata kama unajua umefanya mambo ambayo yanahitaji usifiwe, ni vyema ukasubiri watu wakusifu kuliko kujisifu, kwani hali ya kujisifu kwako inaweza kusababisha watu wakaona kama unajisikia kumbe sivyo na wakaamua kukujengea chuki.
Kamwe usimfanyie mtu jambo lolote ambalo wewe hutaki utendewe. Angalia katika Biblia, kitabu cha Mathayo 7:12, kinasema kuwa: “Basi, yoyote mtakayo mtendewe na watu, nanyi watendeeni vivyo hivyo”.
Mara nyingi katika maeneo ya mkusanyiko wa watu huwa kuna tabia mbalimbali zinazojitokeza za baadhi ya watu kupenda kuwatendea wenzao mambo ambayo wao hawapendi kutendewa. Kwa mfano, wapo watu wanaopenda kutuma wenzao lakini wao hawapendi kutumwa.
Au wako watu wanaopenda kukosoa wenzao lakini wao hawapendi kukosolewa, pia wengine hupenda kutania wenzao lakini wao hawapendi kutaniwa. Tukutane wiki ijayo
0713 331455Ngowi2001@yahoo.com

0 Maoni:

Twitter Facebook