Monday, June 16, 2008

ELEWA JINSI YA KUUKABILI MSONGO

KARIBUNI wapenzi wasomaji katika safu hii tena leo.
Kwa wiki saba mfululizo tulikuwa tukiangalia maana ya msongo wa mawazo, vyanzo vyake, dalili zake na jinsi ya kutatua tatizo hilo linapokukabili.
Leo tumefikia tamati katika mada hii, tutamalizia kwa kujibu swali moja kati ya mengi tuliyotumiwa kwenye safu hii.
Swali hilo ni kwamba, baba mmoja alipatwa na msongo wa mawazo ambao ulimsababishia kupooza, lakini kwa bahati nzuri ametibiwa, anaendelea vizuri. Kwa maelezo ya baba huyo, hali hiyo imempata kutokana na mkewe kumsababishia msongo kwa makusudi, kutokana na kumnyima unyumba, kutotimiza wajibu wake ama kumfanyia jeuri tu.
Anauliza, afanye nini ili kuepuka hali hiyo ambayo inahatarisha uhai wake? Anasema anafikiria kuvunja ndoa lakini anakumbuka athari zake zitaathiri watoto na yeye bado anahitaji msaada kutoka kwa mkewe.
Pole sana ndugu yangu kwa yanayokusibu. Kumbuka hali unayokabiliana nayo wewe si wa kwanza kukutana nayo, ila kinachotakiwa, uwe jasiri katika hali hiyo bila kusahau kumshirikisha Mungu.
Kwani wengi waliochukua uamuzi wa haraka bila kuwashirikisha ndugu, jamaa au rafiki zao wamejikuta wakijutia uamuzi huo.
Vile vile njia nyingine nzuri ni kuzungumza na ndugu, rafiki, kiongozi wa dini au daktari wako juu ya matatizo yanayokusibu. Hali hiyo itakusaidia kupunguza msongo unaokukabili.
Kwa kufanya hivyo itakusaidia, kwani marafiki na familia yako wanaweza wasijue kuwa unakabiliana na kipindi kigumu, watakapoelewa watafanya jitihada za kukusaidia.
Pia si vibaya ukisoma vitabu mbalimbali vinavyoweza kukusaidia, tazama filamu, video na kuhudhuria kozi mbalimbali juu ya hali uliyonayo.
Soma vitabu vizuri vya siasa, literature, jamii, historia pamoja na vitabu vinavyoelezea matatizo mbalimbali ya kijamii.
Lakini waweza kuishi maisha ya kawaida bila kuwaza mambo makubwa, hasira, au hali ya hofu. Usimdharau mke wako pamoja na yote anayokutenda. Atajisikia aibu na kubadilika.
Jitahidi kuwa na uhusiano mzuri wa kirafiki na mke wako, itakuongezea furaha na maisha mazuri katika familia, mke wako na wewe mwenyewe.
Katika kipindi unachokipitia, unaweza tu kujaribu kwa kudhibiti mihemko pamoja na hisia zako. Kitu muhimu ni kukuza ‘hobby’ yako na kutumia muda wako mwingi katika hiyo. Kuwa mbunifu wa kazi kama usanii, muziki, dansi, ushonaji, ufundishaji na kuelekeza nguvu zako zote na vipaji katika mambo hayo.
Hata kama hutaweza kufanya kitu kingine chochote, utaisikia nafsi yako ikikuelekeza katika kazi za jamii. Kuwa na kusudi sahihi na malengo katika maisha yako. Fanya baadhi ya mabadiliko katika aina yako ya maisha uliyozoea kuishi.
Kula vyakula vyenye chumvi kidogo visivyokuwa na joto kali, pamoja na viungo vingi. Kataa kitu chochote kitakachokufanya usisimke au kukupa mhemko. Usitazame picha za x, pamoja na kusoma vitabu vitakavyo kusababishia msisimko katika mwili wako.
Idadi kubwa ya barua zinazoandikwa kwa washauri mbalimbali wa saikolojia katika magazeti ni kutoka kwa wanawake ambao hawapendelei matendo ya kimapenzi wanapokuwa na waume zao, kutokana na mahusiano mapya na watu wengine ambapo kwa sasa wanalipa gharama kwa ajili yao. Wanatafuta muafaka katika mambo magumu wanayopitia, kuwa njia panda katika maamuzi, kuwa na hatia ambayo matokeo yake ni kutokana na mahusiano mapya ya kimapenzi na mtu mwingine.
Wanasaikolojia wanachambua mabadiliko yanayowapata waume zao kuwa katika kadhia na kuhisi uadui, kudhamiria jambo baya, huzuni, wasiwasi au hasira kwa wake zao katika hali iliyofichika katika akili zao. Hisia hizo zinakuwa na mizizi ya siku nyingi, wakati waume zao wamekuwa na uchungu juu ya wake zao, na hali hiyo inakuwa haijawekwa wazi.
Wanawake wengine walio na uhusiano nje ya ndoa zao, wanakuwa hawana ari ya kutenda jambo na waume zao.
Kama mke atakuwa hana hamu na tendo la ndoa, waume zao huanzisha uhusiano mwingine. Katika jamii zetu sheria haziwi kali kwa wanaume kama zinavyokuwa kwa wanawake wanapotoka nje ya ndoa zao.
Kamwe usimdharau mumeo endapo itatokea ongezeko la kazi katika kampuni aliyoko hata kukosa muda wa kuwa na familia yake kama ilivyokuwa awali, anapopatwa na mawazo, udhaifu, ugonjwa au hali yake kubadilika kutokana na ratiba yake ya ofisini kubana, hivyo kushindwa, kuwa na mkewe katika matukio mbalimbali, kumridhisha mkewe kimapenzi, kamwe usithubutu kumdharau kutokana na hali hiyo au umri mkubwa.
Kwa maelezo mengine, mtie moyo mume wako ili aweze kukushirikisha hisia na mawazo yake ili aweze kukufikiria kama rafiki wake wa karibu anayemtegemea katika maisha yake.
Hivyo basi, si vema wala busara kuivunja ndoa yako kutokana na hali ya kukuvunja moyo katika familia yako unayokutana nayo.
Jitahidi kumuenzi mkeo, familia yako na kuiokoa ndoa yako kwa gharama zozote. Kamwe usilipize kisasi kwa mkeo hata kama anakufanyia mambo mabaya ili umuache.
Ijenge familia yako kwa kuwa na muda wa kutosha na watoto wako katika kipindi kigumu unachopitia. Kama ni watoto wenye upeo wataweza kukupa furaha zaidi kwa kujifunza kushirikishana matatizo yanayowakabili na wewe baba kuwaeleza yale matatizo yanayokukabili juu ya kazi na masomo hivyo wote mtatafuta njia nzuri ya kurekebisha mambo.
Ushirika wa baba, mama na watoto katika familia ni muhimu. Unazilinda nyumba nyingi zilizoanza kuweka nyufa.
Tukutane wiki ijayo katika mada mpya.
lcyngowi@yahoo.comwww.ngowil.blogspot.com0713 331455

0 Maoni:

Twitter Facebook