Friday, June 27, 2008

TAFUTA NJIA YA KUTATUA MATATIZO YAKO


NI jambo la kawaida kuchukua jukumu endapo kitu chochote kitakwenda vibaya, ambacho umekisababisha mwenyewe, lakini unapojenga tabia ya kujilaumu mwenyewe kwa kila jambo, unaweza kuwa na wakati mgumu katika hilo.
Unapojikuta ukijilaumu eti kwa kuwa watu wengine wana furaha katika familia zao au maisha yao, wana mafanikio kutokana na kufanya kazi zao kwa bidii, hali ya mahusiano katika familia zao imeimarika wakati kwako inasuasua, jaribu kutafuta njia nyingine ya kukuondolea hali hiyo inayokutesa.
Njia hizo ni pamoja na kuzungumza na familia yako, wazazi wako, watoto wako, wafanyakazi wenzako wale ambao wanaweza kukupa neno la busara, kiongozi wako wa dini, daktari wako pamoja na kusoma maandiko matakatifu.
Utakuta kuwa watu wengi hupenda kujilaumu kwa makosa mbalimbali wanayoyafanya ambayo hushindwa kuizuia hali hiyo na kumuathiri kisaikolojia. Kwa mfano, wazazi wanaweza kuwa imara na kuwashawishi watoto wao katika masuala ya elimu, lakini hawawezi kudhibiti mapungufu waliyonayo watoto wao. Unaweza kuwa imara kumdhibiti mume/mke au rafiki yako kuwa katika wakati mzuri, lakini huwezi kujihusisha katika jambo hilo moja kwa moja.
Lawama zilizopitiliza zinasababisha kukupokonya majukumu yako uliyonayo labda nyumbani, kazini au shuleni. Kuwa imara katika kudhibiti hali hiyo ili uweze kuondokana nayo. Kwani ikiendelea itakusababishia kukata tamaa, kuvunjika moyo na mwishowe kupatwa na msongo wa mawazo.
Kumbuka hali hiyo ukiiendeleza ni sawa na kujiongezea mzigo wa matatizo juu ya mabega yako. Jifunze kujisamehe hata kwa makosa yaliyokwisha kupita ambayo yanaumiza ufahamu wako.
Wengi wetu huwa mahakimu au washitaki juu ya makosa yao wenyewe, wakiendelea kujilaumu wenyewe. Unapokumbuka mambo ya aibu au ya kushindwa yaliyokupata zamani unazidi kuvunjika moyo na kujiona kuwa hustahili machoni pa watu. Hali hii itakuongezea machungu, wasiwasi, msongo wa mawazo pia inakuondolea ujasiri ulionao. Suluhisho ni kusahau yaliyopita na kuanza upya.
Ingawa inaweza kuwa ngumu kuzuia kumbukumbu za kushindwa kwako kukurudia, usizipe nafasi katika ufahamu wako. Kama Mungu au watu waweza kukusamehe si zaidi wewe mwenyewe kujisamehe? Achana na maamuzi mabaya uliyokwisha kuyafanya ya kibinafsi yaliyosababisha kuwaangusha marafiki zako, jamii au wewe mwenyewe.
Kabiliana na siku mpya kwani wewe si yule wa jana bali ni wa leo.
Pia usipende kuwalaumu watu wengine kwani ni sawa na kujiweka kwenye nafasi ya Mungu au hakimu, nafasi ambayo hata mmoja wetu haistahili. Tunapowalaumu wengine wakati mwingine tunataka kufunika mapungufu yetu wenyewe ambayo hatuko tayari kuyakabili.
Mfano utamkuta mwanamke akisema kwa ujasiri kuwa mumewe anatoka nje ya ndoa kwa sababu tu huchelewa kurudi nyumbani au kutumia pesa zake za mapato visivyo. Bila kujali kuwa mumewe anafanya kazi saa za ziada au anahifadhi fedha zake ili aweze kumnunulia mkewe zawadi nk. Yawezekana kuwa mwanamama huyu amekuwa akibeba hisia hizo za shutuma juu ya mumewe kwa muda mrefu kiasi cha kuweza kusababisha hata uhusiano wao kuyumba au ndoa yao kuvunjika. Lakini ukichunguza undani wa shutuma hizo huweza kukuta ni hitimisho iliyojaa hisia potofu.
Lawama yaweza kusababisha watu kufikia hitimisho lisilo sahihi hata kubeba uchungu kwa muda mrefu kiasi cha kuvunja ndoa/unyumba. Lawama huweza kusababisha hali ya maelewano na masikilizano kuwa kutoelewana au kutosikilizana.
Njia mojawapo ya kusaidia ndoa zenye msukosuko ni kumsaidia kila mhuhusika kuacha kumlaumu mwenzie au kuacha kumtazama mwenzie kwa jicho la lawama ila ajitazame mwenyewe na kuona ni wapi alipofanya makosa na nini anaweza kufanya ili kurekebisha ndoa yao.
Njia nyingine ni kumfanya kila mmoja aweze kukiri makosa mbele ya mwingine na kusema samahani, nimekosa. Katika hatua hiyo uhusiano uliovunjika unaanza kuimarika tena.
Hata mwanadamu wa kwanza alianza kwa kumlaumu mwanamke kwa kuelezea makosa yake kwa muumba wake. “Huyu mwanamke ndiye aliyenisababisha.” Mwanamke naye alitupa lawama zote kwa nyoka. “Nyoka ndiye aliyenisababishia kufanya hivi.”
Tunapowalaumu wengine tunaongeza ukubwa wa tatizo badala ya kulitatua. Hii inaonyesha kuwa aliye mwepesi kulaumu wengine ndiye mwenye makosa mengi zaidi. Waungwana ndiyo wanaoweza kukiri makosa yao au kushindwa kwao mbele ya jamii. Mtu muungwa ni yule aliye mwepesi kusema nimekosa.
Shinda lawama kwa kukiri makosa yako. Acha kufunika makosa kwani yataongeza ugumu wakati wa kutatua. Kuna njia moja ya kuweza kusafisha dhamira inayokushitaki nayo ni kukiri makosa. Acha kutafuta watu wa kulaumu, kabiliana na makosa yako mwenyewe. “Kubali makosa yako utapona. Kiri maovu utasamehewa.”
Tukumbuke tabia hiyo huanza tokea mtoto anapokuwa na umri mdogo. Kwani anapokimbia na kujigonga mahali hulaumu kile kilichomgonga, mfano kama amejigonga kwenye ukuta husema kuwa ukuta ule mbaya umemwumiza.
Tukumbuke kuwa lawama si kitu cha kufurahisha kwani huweza kusababisha hasara zaidi. Kwa mfano waweza kumwona mtu akigonga gari lake kwa hasira ukafikiria kuwa amechanganyikiwa kumbe analaumu kwa nini limeharibika au kwa nini limemwishia mafuta.
Kila wakati mambo yanapoharibika ni kasumba kwa mwanadamu kutafuta sababu ya lawama au mtu wa kumlaumu.
Mara nyingine tunapomwona kilema, kipofu au kichaa swali kubwa watu wanalojiuliza ni nani anayestahili kulaumiwa. Wengine humlaumu Mungu, wengine hulaumu uumbaji na wengine huwalaumu wazazi. Tunachotakiwa kujiuliza ni jinsi gani ya kumsaidia mtu huyo? Ni namna gani ya kumtoa katika hali ile aliyonayo sasa? Ni namna gani tunaweza kuboresha mazingira yanayomkabili. Ni jinsi gani twaweza kumfanya aanze upya na kwa ubora zaidi?
Ingawa lawama ni mchezo uliozoeleka na watu wengi siku hizi, bado ni mchezo ambao huleta athari kubwa sana. Siku zote lawama haiponyi bali huumiza moyo. Haijengi uhusiano bali huuvunja, haiunganishi bali hutenganisha, haijengi bali hugawanyisha na haitatui matatizo bali huongeza ukubwa wa matatizo.
lcyngowi@yahoo.comhttp://www.ngowil.blogspot.com/0713 331455, 0733 331455

0 Maoni:

Twitter Facebook