Friday, December 19, 2008

FAHAMU NJIA SAHIHI YA KUKOSOA ILI MTU ASIKUCHUKIE

KARIBUNI wapenzi wasomaji katika safu hii inayokujia kila Alhamisi. Ninamshukuru kila mmoja aliyekuwa mstari wa mbele katika kufuatilia mada mbalimbali. Wapo waliotoa ushauri, pongezi, lakini pale nilipokosolewa nilikubali kwani nia ni kuelimisha.
Leo tutaangalia mifano mbalimbali katika maisha yetu tunayoweza kuitumia pale tunapotaka kumkosoa mtu yeyote aliyefanya jambo kwa makusudi au kwa kutokujua bila kumfanya ajisikie vibaya.
Kwa kuanza, tumuangalie mkurugenzi mmoja aliyekuwa na viwanda mbalimbali vya kutengeneza nguo. Lakini siku moja aliamua kufanya ziara ya ghafla katika kiwanda chake kimoja.
Alipofika kiwandani aliwakuta baadhi ya wafanyakazi wake wakivuta sigara karibu kabisa na kibao kinachokataza uvutaji sigara sehemu hiyo.
Mkurugenzi huyo akakisogelea kibao hicho na kuwaonyesha wafanyakazi hao huku akiwauliza, ‘hamjasoma hapa?’ Wafanyakazi wote wakataharuki, wakashindwa kujieleza.
“Vijana ningefurahi kama mngevuta sigara nje ya eneo hili au niseme hata nje ya kiwanda.” Wafanyakazi hao walielewa kwamba bosi wao anatambua kuwa wamevunja sheria, lakini walimfurahia kwa sababu hakuzungumza nao kwa ukali, bali alizungumza kwa upendo na kuwafanya wajisikie kwamba wao ni wa muhimu katika kiwanda kile.
Hilo lilikuwa ni fundisho kubwa kwao, kwani tokea hapo hawakurudia kosa hilo tena. Hivyo unaposhughulika na watu mbalimbali jaribu kuwa na busara katika kuwaeleza jambo.
Mfano mwingine ni kwa ofisa mmoja aliyejulikana kwa jina la Robby. Alikuwa na biashara zake na kila siku alikuwa akitembelea mojawapo ya biashara hizo.
Ilifika siku moja akaenda kwenye ghala lake la vinywaji na kumwona mteja amekaa anasubiri huduma, lakini kulikuwa hakuna mtu wa kumhudumia kwa kipindi hicho.
Aligundua kuwa kwa wakati huo, wafanyakazi wake hawakuwa tayari kumsikiliza mteja huyo, bali walikuwa wamekaa kaunta, wakicheka na kuzungumza habari zao zinazowahusu bila kujali kuwa eneo lile ni eneo la kazi.
Robby hakuzungumza lolote, taratibu akanyata kando ya kaunta na kumhudumia mteja yule mwenyewe na kukabidhi pesa kwa wauzaji hao wakati alipokuwa anaondoka.
Hapo tunaona kwamba Robby alitumia njia ya busara ya kuishi na wafanyakazi wale. Angeweza kutumia ukali au kuchukua hatua ya kuwafuta kazi mara moja, lakini kwa kuwa alikuwa ni mtu mwenye hekima na busara, aliamua kumhudumia mteja yule aliyemkuta na hilo lilikuwa fundisho kubwa kwa wafanyakazi wake.
Aliwapa somo kwa njia ya vitendo kwamba kazi si mahali pa mchezo, bali panahitaji kuheshimiwa na kumheshimu kila anayehitaji huduma.
Vilevile tunaona kwamba viongozi wa umma mara nyingi wamekuwa wakipingwa kutokana na kutokuonekana katika majimbo yao. Mara zote wanasongwa na kazi, wamekuwa katika hali ya ulinzi muda wote na wasaidizi wao ambao hawapendi watu wawabugudhi mabosi, kwa kuruhusu wageni wazungumze nao.
Lakini kuna mbunge mmoja ambaye mara zote amekuwa akiwaasa wafanyakazi wake kuwaruhusu watu wamuone. Amekuwa akisema kwamba sera zake zipo wazi kwa kila mmoja, lakini wasaidizi wake wamekuwa wagumu kumuelewa, na kuendelea kuwazuia wananchi wasiweze kumuona kwa urahisi ili waeleze matatizo yao yanayowakabili.
Baada ya kuona somo hilo halieleweki kwa wasaidizi wake, mbunge huyo mwishoni alipata suluhu kwa kuamua kuondoa mlango wa ofisi yake. Kitendo hicho kilitoa ujumbe kwa urahisi kwa wasaidizi wake, kwamba mbunge huyo yuko wazi na yuko tayari kumsikiliza kila mmoja.
Hapo inamaanisha kwamba si lazima kila mara ukawa unazungumza na watu ambao hawakuelewi, wakati mwingine unaweza kuzungumza kwa vitendo, utaeleweka.
Kwa kawaida unapobadilisha maneno mawili au matatu inaweza kuleta tofauti kati ya kushindwa na mafanikio katika kuwabadilisha watu wasiweze kuwa na uchungu.
Unapotumia njia ya busara katika kumrekebisha mtu aliyekosa, inamfanya mtu yule asiyekuwa na uvumilivu katika kuwasahihisha wengine kwa kuwakosoa katika njia ya uwazi, kujifunza kitu.
Mfano mwingine upo kwa familia mmoja, iliyokuwa inakarabati nyumba yao, kwa kutumia mafundi ujenzi, familia hiyo ilifikia mahala ikaamua kuwashawishi mafundi kufanya usafi mara tu wamalizapo kazi yao.
Kwa siku za mwanzoni mwa ujenzi huo, mama mwenye nyumba alipokuwa akirudi nyumbani baada ya kazi, alibaini kuwa eneo la nyumbani kwake lilikuwa chafu, lenye kuonekana vipande vya mbao na uchafu mwingine. Mama huyo hakutaka kuzungumza na mafundi hao, kwa sababu walikuwa wamefanya kazi nzuri.
Kwa hiyo baada ya mafundi hao, kuondoka, yeye na watoto wake waliokota vipande hivyo vya mbao na kusafisha eneo hilo la ujenzi. siku iliyofuata alimwita kiongozi wa mafundi waliokuwa wakijenga na kumwambia kuwa, “Nimefurahishwa na jinsi mlivyoacha eneo hili jana usiku, lilikuwa zuri na safi, na halikuweza kuleta usumbufu kwa jirani.” Tangu siku ile na kuendelea, wafanyakazi wale baada ya kazi walikuwa wakikusanya takataka zote na kuacha eneo lile safi. Na kiongozi yule alikuwa akihakikisha kama wafanyakazi wake wameacha eneo walilofanyia kazi likiwa safi.
Katika mfano mwingine tunaweza kuuona kwa askari. Kati ya eneo linalotatanisha askari wanapokuwa kwenye mafunzo yao ni suala la ukataji wa nywele. Kwa kuwa wengi wao wanajiona kwamba kama bado ni raia wa kawaida, na ghafla wanajikuta wanatakiwa kukata nywele zao na kuwa fupi.
Kiongozi wao mmoja alilibaini hilo, na kusema kuwa awali kabla ya kugundua njia ya kutatua tatizo hilo, alikuwa akiwatisha askari hao bila mafanikio.
Lakini alipobaini tatizo lake, siku hiyo akaanza kwa kuwaambia maaskari hao: “Ndugu zangu, nyie ni viongozi. Na mnakuwa viongozi bora pale mnapofundisha kwa mifano. Mnatakiwa kuwa mfano ili wengine wafuate. Je, mwajua masharti ya jeshi kuhusu kukata nywele? Ninakwenda kukata nywele zangu leo, ingawa bado ni fupi kuliko baadhi yenu. Mnaweza kujiangalia wenyewe kwenye kioo, na mwone kama mnapaswa kukata nywele ili muwe mfano bora, tutapanga muda kwenu wa kwenda kwa kinyozi.”
Matokeo yake yakawa mazuri, kwani maaskari hao wanafunzi walijiangalia kwenye kioo na kwenda kwa kinyozi mchana ule na wakawa wamepokea masharti hayo ya kuwa na nywele fupi.

NJIA SAHIHI YA KUSHUGHULIKA NA MALALAMIKO

WATU wengi wamejaribu kuwashawishi wengine jinsi wanavyofikiri kufanya kwa kuzungumzia zaidi kuhusu mambo yao. Waache na wengine wazungumze.
Kwani wanajua zaidi kuhusu shughuli zao na matatizo kuliko unavyodhani. Kwa hiyo ni vema uendelee kuwauliza maswali ili waweze kukwambia mambo machache wanayoyajua.
Watu wengi hujikuta wakiingilia kati pale ambapo hawakubaliani na mazungumzo ya mwingine. Lakini wewe usifanye hivyo. Ni hatari. Hawatakusikiliza wakati bado wana mawazo yao mengi ya kueleza.
Hivyo ni vema kusikiliza kwa utulivu na kuweka kumbukumbu kile kinachozungumzwa. Kuwa mtulivu katika hilo. Watie moyo kuelezea mawazo yao yote.
Je, unafikiri utaratibu huo ni mzuri? Hebu tumuangalie mfanyabiashara. Kulikuwa na mfanyabiashara moja ambaye alikuwa akitafuta soko kwa ajili ya biashara yake, kabla ya kumwona mhusika mkuu wa ofisi aliyokuwa anakwenda, alipata tatizo la kukaukiwa na sauti yake.
Alipopata nafasi ya kuonana na Mkurugenzi huyo wa kampuni aliyokwenda, aliandika kwenye karatasi kumweleza kuwa sauti yake imekauka na kumuuliza kama wanaweza kuendelea katika hali hiyo aliyonayo na mhusika yule akamwambia kwamba wanaweza kuendelea na mazungumzo yao.
Hivyo, alitoa nyaraka mbalimbali za uthibitisho wa bidhaa zake, ambapo Mkurugenzi yule alipokuwa akizipitia alikuwa akitabasamu kwa kuonyesha kuwa anakubaliana na bidhaa hizo.
Alimpongeza mfanyabiashara huyo kwa kuwa na bidhaa nzuri na kuamua kusaini naye mkataba. Baada ya kutiliana saini, mfanyabiashara alisema tangu aanze biashara yake hiyo hajawahi kupata kazi yenye mkataba wa fedha nyingi kama ulivyo huo.
“Ninajua kuwa ningepoteza mkataba huu kama sauti yangu isingekauka, kwa sababu nilikuwa na mawazo tofauti katika mazungumzo yote tuliyoyafanya.
“Nimegundua kuwa kukauka sauti kwangu kwa bahati mbaya, kumenipatia utajiri mkubwa, hivyo wakati mwingine ni vyema kuwaacha watu wengine wazungumze,” anasema mfanyabiashara huyo.
Kuwaacha watu wengine wazungumze kunasaidia katika mazingira ya familia pia kwenye biashara. Mfano mwingine ni wa mama mmoja na mtoto wake Lilly ambao walikuwa hawana mahusiano mazuri.
Lily alikuwa ni mtoto mkimya asiyependa kuzungumza, lakini alikuwa hana uhusiano mzuri na mama yake wakati wa ukuaji wake, kwa kuwa mama yake alikuwa akimtishia na kumwadhibu pasipo sababu za msingi.
Kutokana na adhabu hizo mtoto huyo alikuwa akimwangalia tu mama yake, na mama huyo alipokuwa akimgombeza mtoto huyo alimwangalia tu na kuondoka eneo hilo.
Siku moja mama huyo aliwaambia wenzake kuwa mtoto wake amemshinda hivyo amenawa mikono juu yake. ” Mtoto huyu amenishinda amekuwa akiondoka nyumbani na kwenda kwa rafiki yake wa kike bila kuaga, lakini aliporudi nilikosa nguvu ya kumwadhibu tena, nilimwangalia kwa huzuni na kumuuliza kwa nini Lilly unafanya hivi?,” anasema mama huyo.
Kwa maelezo ya mama huyo, mtoto wake alimwangalia kwa upole na kumuuliza, “Je ni kweli unataka kujua?,” mama huyo anasema kwanza alimwangalia mtoto wake na kuanza kupatwa na wasiwasi, baada ya muda wasiwasi huo ukatoweka. Hakuwa tayari kumsikiliza, japo amekuwa mara nyingi akimwambia mtoto huyo kufanya kile na kile.
Mama huyo anasema wakati mtoto Lilly alipokuwa anamweleza mawazo na hisia zake, aliingilia kati na kutoa mamlaka nyingi kumzuia asiendelee kuzungumza.
Lakini mama anasema aliaza kutambua kuwa mtoto huyo alimhitaji, si kwamba awe kama mama ambaye anajiona ni bosi, lakini mwenye ujasiri na hayo ndiyo matokeo ya kumchanganya katika makuzi yake. Na mtoto huyo alipokuwa akijaribu kuzungumza na mama yake, mama huyo hakuwa tayari kumsikiliza.
Baada ya kukaa na kutathmini mama huyo alijiona kuwa ana makosa katika malezi ya mtoto wake, kwani mtoto huyo alihitaji kusikilizwa na kuheshimiwa mawazo yake. Tokea siku hiyo mama huyo alimwacha mtoto wake kumweleza hisia zake na aliweza kumsikiliza.
“Tangu wakati huo na kuendelea nimekuwa nikimwacha mtoto wangu azungumze kile anachotaka. Ananishirikisha mambo yake na uhusiano wetu umeanza kuwa mzuri, amerudi kuwa mtu wenye ushirikiano,” anasema mama huyo.
Hivyo, ni jambo zuri kwa wazazi kuwa karibu na watoto wao, kujua nini wanapenda, upungufu wao na jinsi gani anaweza kumrekebisha kwa hekima pasipo kutumia jazba wala kujionyesha kuwa yeye ni bosi hivyo mtoto anapaswa kumsikiliza kwa kila jambo.
Malezi bora ni pale wazazi na watoto wanapoelezana jambo kwa uwazi, hekima na kusikilizana hata kufikia mwisho wa jambo lenyewe. Ni vema kutoa nafasi kwa wengine nao waweze kutoa mawazo yao.

KAMA UMEKOSEA KUBALI KOSA

KARIBUNI wapenzi wasomaji katika safu hii. Tunamshukuru Mungu kwa kutufikisha tena Alhamisi ya kwanza ya Desemba. Nafikiri kupitia safu hii umepata elimu na maarifa mbalimbali. Leo, tutaangalia jinsi inavyokupasa kukubali kosa endapo utakosea.
Katika maisha yetu ya kila siku, ni vema kutambua kuwa unaweza kukosea kwa kufanya jambo makusudi au kwa kutokukusudia. Hivyo basi, endapo utakosea jambo, ni vizuri kukiri kosa pasipo kubisha hiyo ndiyo njia sahihi ya kuishi katika ulimwengu huu.
Iwapo umetenda kosa lolote, ukaulizwa na kukiri kukosea, ni rahisi kwa mtu anayekuuliza kuelewa kwamba umetambua kosa lako na kulijutia, hivyo hautarudia tena, tofauti kama ungekataa na kusema hujakosea.
Asilimia kubwa ya watu wanapokosea hunyamaza hadi wanapoulizwa. Lakini njia nzuri, unapokosea kujitambua mara moja na kukiri kosa kabla hujaulizwa, hiyo itamfanya yeyote kufikiria njia ya kukusamehe kama umemkosea.
Kijana mmoja aliyekuwa kiongozi katika idara yake, alisema kuna wakati hakutoa stahili ya fedha kwa wafanyakazi wake kiasi kwamba jambo hilo lilimgharimu na kuonekana hawezi kuongoza wenzake.
Alilitambua hilo mapema kabla bosi wake hajamuuliza, alimfuata na kumueleza kilichotokea, alikiri kuwa hali hiyo ameisababisha yeye.
Kijana huyo aliingia ofisini kwa bosi wake na kumueleza juu ya jambo hilo na kukiri kuwa amekosea. Kwa maelezo ya kijana huyo, baada ya kukiri kwa bosi wake kwamba jambo hilo ni yeye alilisababisha, anasema bosi wake alimwangalia na kumwambia “Sawa, ni kosa lako, lakini inakubidi kurekebisha jambo hilo.
“Makosa huwa yanarekebishika, kila mmoja anakosea,” anasema. Kijana anabainisha kwamba baada ya kuambiwa hivyo na bosi wake, alipata nguvu mpya na kufarijika zaidi, tangu siku hiyo bosi wake alimwamini kwa kila jambo.
Mtu asiye na busara, mara nyingi hujaribu kujitetea anapofanya makosa badala ya kukiri na kujirekebisha. Hali hii ipo kwa watu wengi katika maisha yetu ya kila siku. Wengi wetu hufanya makosa, badala ya kukiri huamua kukaa kimya mambo yanapoharibika ndiyo hukumbuka kuomba msamaha.
Mara nyingine mtu wa aina hiyo hupoteza uaminifu kwa wenzake na hata kufukuzwa kazi, kwa tabia ya kutokuwa tayari kukiri kosa. Hebu tuangalie mfano wa mwalimu aliyekuwa hana uhusiano mzuri na mtoto wake. Siku moja katika kipindi chake asubuhi, aliwaeleza wanafunzi wake jinsi alivyotofautiana na mtoto wake, hata kushindwa kuwaona wajukuu zake.
Mzazi huyo alihisi kuwa, kijana wake anapaswa kuwaheshimu babu zake, kukubali kila jambo atakaloambiwa liwe zuri au baya, kwamba hapaswi kuwa na maamuzi yake.
Mwisho, mwalimu alilieleza darasa lake kuwa amekuwa akiwaza tatizo hilo na kuona kuwa kuna umuhimu wa kumuomba mtoto wake msamaha. Anaeleza, mwanafalsafa anasema kama umekosea ni vema kukiri kosa haraka; kwa msisitizo. “Kwangu ilichukua muda mrefu kukiri kwa haraka, lakini nimeweza kukubali katika hali ya kumaanisha”.
Inawezekana niliona aibu kumuomba msamaha kijana mdogo, lakini nilikuwa nimekosea na lilikuwa ni jukumu langu kufanya hivyo.
Baada ya kusema hayo darasa lake lilishangilia kwa kupiga makofi, na kumpongeza. Kipindi kilichofuata mwalimu huyo aliwaeleza wanafunzi wake jinsi alivyokwenda nyumbani kwa mtoto wake, kuomba na kupewa msamaha, kwa sasa wamejenga uhusiano mpya na mtoto wake, mkwewe na watoto wao.
Hivyo basi, tumekuwa tukishuhudia watu mbalimbali wenye uwezo wa kukabiliana na watu ambao walikuwa ni maadui na kujenga urafiki mpya.
Je, waweza kusemaje kwa mtu anayekutendea jambo kama hilo? Pale tunapokuwa sahihi tuchukuliane na watu kwa upendo, tunapokosea, tukubali makosa yetu, hali hii itazidisha upendo kuliko kubakia kila wakati unajitetea

JARIBU KUWA JASIRI KUKIRI KOSA

KARIBUNI wapenzi wasomaji katika safu hii ya Maisha Yetu inayokujia kila Alhamisi. Safu hii imekuwa ikielimisha, ikikosoa na hata kutoa muongozo wa maisha ya kila siku.
Leo katika safu hii tutaangalia jinsi unavyoweza kujiepusha usiwe na maadui katika maeneo mbalimbali uliyopo. Kuna wakati unaweza kuona umeelemewa na mawazo pasipo kukumbana na tatizo lolote, lakini mtu anapokuambia umekosea, hilo linaweza kukufanya uwe na huzuni katika moyo wako.
Hivyo basi, unaweza kumueleza mtu kwamba amekosea kwa kumwangalia, kumwambia au kutumia ishara kama njia ya kumshawishi mtu akuelewe kama vile unavyoweza kuzungumza kwa maneno.
Elewa kuwa utapomwambia mtu ana makosa, unafikiri utamfanya akuamini? Hapana. Hiyo si njia sahihi, kwani unaweza kulitatua tatizo hilo kwa busara, maarifa, hekima na staha. Ukitumia njia za busara itamuwezesha yule mwenye tatizo kujutia makosa yake, japo haitamfanya kubadili mtazamo wake.
Unapojishughulisha na mtu yeyote huku ukitaka kufanikiwa, kamwe usianze kwa kueleza: “Ninakwenda kuhakikisha jambo hili na hili kwako” kufanya hivyo si jambo zuri, hiyo ni sawa kusema “Mimi ni bora kuliko wewe”.
Badala ya kutumia njia hiyo ni vyema kumueleza mtu unayetaka kumchunguza, mambo ambayo unafikiri yatabadili fikra zake, na kuweza kumsaidia.
Hiyo ni changamoto kwa kila mmoja kwani inaweza kuleta kutokuelewana na kumfanya yule uliyekusudia kumuonyesha kuwa wewe ni bora kuliko yeye, kupambana nawe kabla hujaamua kuanza. Kwa mtazamo huo, ni vigumu kubadili fikra za watu, ambao unadhani kuwa, wanaenda kinyume.
Hivyo ni busara unapotaka kwenda kuthibitisha jambo lolote, usilifanye kwa uwazi kila mmoja akatambua unalotaka kulifanya. “Fanya kwa werevu, ustadi, asiwepo yeyote atakayeweza kuhisi kwamba kuna jambo unalifanya”. Ili usije kujijengea uadui usiokuwa na lazima.
Mtu mmoja aliweza kumwambia mtoto wake kwamba awe na busara kuliko watu wengine kama anaweza, lakini asiwe mwepesi wa kuzungumza na kuwaeleza udhaifu wao ulipo.
“Ni kweli, ni vyema ukaiambia nafsi yako kuwa huwezi kuwa bora kuliko mwingine, kwa hiyo inakupasa kutokuwahukumu”.
Endapo mtu atakwambia maneno ambayo unafikiri si sahihi, nawe unajua hivyo, si vema kusema “Vizuri, sasa, tazama. Ninafikiri kuwa lakini ninaweza kuwa nimekosea mara kwa mara na kama nimekosea, nataka kujiweka sawa, tuweze kuujua ukweli”.
Huo ni muujiza, unasema “ninaweza kuwa nimekosea, imenitokea mara kwa mara, acha tujue ukweli,”. Hakuna mtu yeyote chini ya mbingu au chini ya ardhi atakayekubaliana na maneno hayo.
Kuna baadhi ya watu wamekuwa wakitumia maneno hayo pale wanapokumbana na misukosuko ya wateja au wafanyakazi wenzao. Kutokana na misukosuko hiyo ya mara kwa mara hupatwa na hasira anapokuwa na wakati mgumu wa kushughulika na matatizo ya wateja wake, hali inayomsababishia hasira, kukosana na watu na kutokukubalika.
Lakini unapokuwa jasiri na kukabiliana na hali hiyo kwa kuwaambia watu unaoshughulika nao, kuwa upo tayari kurekebisha upungufu unaoonekana kwao, na kusema kuwa uko tayari kushughulikia matatizo hayo, utakuwa na imani kwa wateja hao.
Unapokuwa jasiri wa namna hiyo inapunguza hasira kwa wale unaowatumikia na wataondoa hisia walizokuwa nazo juu yako na kampuni yako, ni vyema kuwa makini unaposhughulikia jambo lolote.
Ni vyema kuonyesha heshima kwa wateja, wafanyakazi wote bila kubagua, kwa kuwashauri na kuwajali itasaidia kuendelea kuwa shujaa katika ushindani wa biashara uliyonayo.
Kamwe hutaingia matatizoni pale utakapokubali kuwa umekosea, kwani itakuondolea maswali, kukupa moyo na itakufanya kuwa wazi pamoja na kupata uelewa mkubwa kuliko ulivyokuwa awali.
Unapokuwa umekosea ni vyema kukiri makosa hayo na endapo utakiri kwa unyenyekevu, utawafanya na wengine wajivune kupitia wewe.

JINSI UNAVYOWEZA KUJENGA URAFIKI

KILA mmoja hapa duniani ana jukumu la kuwa kiongozi mahali popote alipo - iwe nyumbani, kazini ama shuleni - ili kuwawezesha wengine kufanya kazi kwa kufuata kanuni na sheria zilizopo.
Mfano wewe ni kiongozi katika kampuni, shirika au ofisi yoyote, ni jukumu lako kuwaangalia wafanyakazi wenzako kama wanafanyakazi zao kwa kufuata sheria na taratibu za kazi zilizopo.
Kama utashindwa kuwasimamia vizuri, ikatokea mmoja wao akapatwa na madhara, jukumu hilo utalibeba wewe kama kiongozi wao. Hivyo basi, kama wewe ni kiongozi katika kampuni ya uhandisi ni vyema kuhakikisha kuwa wafanyakazi unaowasimamia wanatimiza wajibu wao, kwa kuvaa kofia za kufanyia kazi wakati wote wawapo kazini.
Inawezekana wakati mwingine wafanyakazi hao wakafanya mazoea na kuacha kuvaa kofia hizo au wakadharau kufuata sheria unazowaelekeza kama kiongozi wao, na kuamua kuzivunja unapoondoka katika eneo hilo la kazi na kufanya vile wapendavyo.
Kama utagundua kwamba maelekezo unayoyatoa kwa wafanyakazi hao hayatekelezeki ni vyema kujaribu njia nyingine ya kuwafikishia ujumbe huo, ili waweze kufanyakazi zao kwa kufuata sheria zilizopo, kuepuka na madhara yanayoweza kuwapata.
Ikitokea utawakuta wafanyakazi hawajavaa kofia wakiwa kazini, ni vema kutumia mbinu na kuanza kuwauliza, wanajisikiaje pale wanapovaa kofia hizo, je, wanakuwa huru au haziwakai vizuri ili uweze kujua tatizo lipo wapi.
Unapopata majibu kutoka kwao, ni vema kuwakumbusha kwa upole, umuhimu wa kofia hizo za kazi wanazopaswa kuvaa, kwamba zimetengenezwa kwa ajili yao wanapokuwa kazini tu, ili kuwakinga na hatari, endapo vitu vizito vitadondoka kwa bahati mbaya wawapo kazini.
Utakapofanya hivyo itakuwa rahisi kwa wafanyakazi hao kuelewa umuhimu huo na kuutekeleza, tofauti kama ungetumia sauti ya ukali na kuamrisha. Huo ni mfano mojawapo wa kujishughulisha na watu wanaokuzunguka katika mazingira mbalimbali. Unapokuwa mwenye busara na hekima katika kuzungumza, unakubalika na wale wanaokuzunguka kinyume cha hapo hata upige mbiu hautasikilizwa.
Ni vema kukumbuka kuwa, unapojishughulisha na watu, unajishughulisha na viumbe vyenye hisia, hivyo uamuzi mkali utasababisha hisia mbalimbali kwao.
Kiongozi asiye na busara anaweza kutumia muda wake mwingi kukosoa, kulaumu na kulalamika. Hivyo ndivyo wafanyavyo viongozi wote wasiotumia nafasi yao vizuri. Lakini ni vyema kiongozi akawa na tabia ya kujitawala na kuwa mwelewa, mwenye busara na kusamehe.
Kumbuka kuwa kuna siri kubwa ya kushughulika na watu. Pia kuna njia moja ya kumfanya yeyote kufanya chochote anachotaka, itategemea ni jinsi gani utakavyozungumza naye.
Unaweza kumlazimisha mtoto wako afanye kile unachotaka kwa kumchapa au kumtishia. Unaweza ukawalazimisha wafanyakazi wako kukupa ushirikiano, pale unapowatishia kuwafukuza. Lakini kumbuka hiyo siyo njia nzuri ya kujishughulisha na watu wanaokuzunguka.
Kuna msemo unaosema kama hutakuwa na uso wa tabasamu, huwezi kuuza duka. Tabasamu lako ndio mwongozo wa kufanya mambo mema. Pia inatoa mwanga wa maisha kwa wote wanaokutazama.
Hivyo endapo utakutana na watu wenye matatizo mbalimbali yanayowafanya wachukie wakati wote au kukunja nyuso zao kwa kukosa furaha, kumbuka tabasamu yako pekee ndiyo itakuwa dawa kwa wote walioumizwa.
Kwani watu hao hufikia hatua ya kukata tamaa baada ya kupata mashinikizo mbalimbali kutoka kwa mabosi, wateja, walimu, wazazi au watoto wao, tabasamu pekee ndilo linaloweza kuwasaidia kujua kwamba huo si mwisho wa maisha bali kuna furaha katika dunia.
Katika maisha tunayoishi ni vema ukajifunza njia mbalimbali za kuishi na watu ambazo zitakujengea heshima popote utakapokuwa. Njia hizo ni kupenda kujua majina ya kila unayekutana naye, kujitahidi kumwita kwa jina lake kila unapomwona.
Utakapofanya hivyo utajijengea heshima kwa jamii inayokuzunguka iwe ni nyumbani, shuleni na hata ofisini. Baadhi ya watu wamekuwa na tabia nzuri ambazo hupendwa na jamii. Tabia hizi ni pamoja na kutumia muda wao na kumsikiliza kila anayezungumza naye bila kumpinga.
Hali hii humfanya kupata njia sahihi ya kumsaidia mtu huyo endapo anahitaji msaada, ushauri au mara nyingine kumwelekeza. Baada ya kutumia muda wake kusikiliza kwa makini, huzungumza kwa sauti ya upole na unyenyekevu, akionyesha hisia za kweli. Mtu wa aina hii hukubalika na watu wengi, kwa kuwa hutoa muda wake kumsikiliza hata mtu asiye na busara au mropokaji.
Kama kiongozi alikuwa na tabia ya kujisifu, kukatisha mazungumzo wakati wa chini yake anapomweleza shida zake, kutokuwa msikivu, kuingilia mazungumzo yasiyomuhusu na mengune yanayofanana na hayo, basi ajue kuwa ameshajijengea mpaka kati yake na wa chini yake.
Ni kweli watu wa namna hii wanaudhi. “Watu ambao huzungumza mambo yao tu, na wale ambao hufikiria mambo yao tu, wanakuwa hawana maana, tena hawajaelimika,” Dk. Nich Muron, anasema.
Hivyo basi kama unapenda kuwa mzungumzaji mzuri uwe msikilizaji mzuri, unayevutia na unayevutiwa na mazungumzo ya wengine. Penda kuuliza maswali ambayo wengine watafurahia kuyajibu. Watie moyo kuzungumzia mambo yao na mafanikio yao.
Ni muhimu kukumbuka kwamba wakati unapoanza mazungumzo ni vyema kuwa msikilizaji mzuri, uwatie moyo wengine wazungumzie mafanikio yao kuliko kubaki unajisifu wewe mwenyewe.

TAFUTA NJIA SAHIHI YA KUTATUA MIGOGORO

JINSI jamii inavyokuwa na mfumo wa aina fulani ya maisha, kuna kila uwezekano wa kujenga mizizi inayoweza kusababisha mikwaruzano mbalimbali.
Ni vema kuelewa kuwa, kila jamii ina mfumo wake, hivyo wengine kuona kuwa, hawatendewi haki kama wenzao, hali ambayo itaweza kuchangia kutokuelewana au migongano.
Hali hiyo ya kutokuelewana hutokea hasa pale kiongozi wa nchi, wilaya, kijiji, mtaa, kwenye maeneo ya kazi au katika shughuli yoyote inayowashirikisha watu wengi, kiongozi huyo, anaposhindwa kuwawakilisha wote kwa usawa.
hali hiyo huwa hutokea kwa kiongozi yeyote ambaye hayuko makini katika utendaji wake, kwani kila mwanadamu ana mahitaji muhimu, hupenda kuwa salama na kutambulika. Sasa basi, ikiwa mahitaji yake hayafikii malengo iliyokusudia, husababisha maamuzi mabovu kutolewa, amani kutoweka na pengine kutokuelewana. Kuna vyanzo mbalimbali vinavyosababisha migongano katika jamii tunayoishi, ambavyo huweza kuwa vya kisiasa au kujamii. Mara nyingi tunaona kuwa kutokuelewana hutokea pale watu wanapokosa kuelewana katika jambo linalofanana. Endapo kunakosekana usawa katika mojawapo ya mambo, kwa mfano, utofauti wa kipato unaosababisha mifarakano kutokana na rasilimali za nchi kama vile ardhi na maji. Pia tunaona hali ya kutokuelewana huibuka pale watu wanapokuwa hawana furaha kutokana na watawala wanaowaongoza.
Mara nyingi tumeshuhudia kuwa migongano ya mara kwa mara hutokea wakati kikundi fulani kinapotaka kuwa huru kutokana na utawala uliopo madarakani, madai yao yanaposhindwa kuwasilishwa serikalini, serikali inapowadharau, kutowaheshimu wananchi wake au kuwapatia mahitaji yao ya muhimu.Migongano mingine yaweza kusababishwa na masuala ya dini na siasa. Wakati mwingine husababishwa na kikundi cha dini au siasa kilichohujumiwa. Hata hivyo, migongano yoyote inaibuka wakati watu wanapoumizwa.
Ingawa mara nyingi migongano hiyo huonekana ni kinyume, inaweza kufikiwa muafaka kama utatuzi utapatikana. Pia katika maeneo ya kazi mara nyingi kumekuwa na mifarakano ya mahitaji. Wafanyakazi wanapozidiana katika rasilimali na kutambuliwa kazini, migongano hutokea.
Kwa mfano, utakuta kuwa mkuu wa idara amekuwa akiwapendelea baadhi ya wafanyakazi kwa kuwapa motisha zaidi, hali inayowavunja moyo wafanyakazi wengine na kusababisha migongano. Pia ufahari au jinsi ya kuishi na watu maeneo ya kazi huleta kutokuelewana kama tu hutajishusha na kuishi maisha ya kawaida katika jamii inayokuzunguka. Kumbuka kila mtu ana tabia zake binafsi, kunakuwa na tofauti katika kuwafikia watu na matatizo yao. Kama kiongozi jihusishe nao kuelewa mitindo yao ya maisha na jifunze jinsi ya kuepuka migongano inayoweza kusababishwa na hali hiyo.Kwa mfano, inapotokea mfanyakazi mmoja akawa anafanya kazi katika mazingira bora na mazuri wakati mfanyakazi mwingine anafanya kazi katika mazingira yasiyoridhisha, na ilhali wapo katika kampuni au shirika moja, wafanyakazi hao wawili ni rahisi kukorofishana na kutokuelewana, kwa vile mmoja wao ataona kuwa hatendewi haki kwa hilo.
Matatizo mengine huchangiwa pale mtu asipoweza kufikia lengo alilokusudia kutokana na kutowezeshwa na mwajiri wake. Mfano katika suala la vitendea kazi, hali inayochangia kuchelewa kutekeleza majukumu yake.
Wakati mwingine mwajiri wako anaweza kukulaumu kutokana na kuchelewa kufanya kazi zako kwa ufanisi, kumbe ucheleweshwaji huo, huchangiwa na mwajiri huyo, kwa kutoona umuhimu wa kuweka vitendea kazi vya kutosha, hali inayoleta mvutano baina ya wafanyakazi wenyewe wakigombea vitendea kazi vichache vilivyopo.Na wakati mwingine idara mojawapo hupewa vitendea kazi na nyingine kukosa. Hiyo huleta hali ya mvutano na kutokuelewana katika maeneo ya kazi.
Shinikizo kutoka kwa viongozi wa kazi huchangia migongano. Kwa kuwa inaweza kutokea watu wawili au zaidi katika kitengo kimoja wanapokuwa na majukumu tofauti yanayotakiwa na bosi wao kwa wakati mmoja.Kwa mfano, kiongozi wa kazi anapotaka taarifa kamili ikamilike saa tisa alasiri - muda anaotakiwa mfanyakazi mwingine kukamilisha taarifa yake - ambapo wote kwa pamoja wanahitaji kutumia mashine moja kwa kuwa mashine nyingine ni mbovu, kipi ni suluhu? Matokeo yake mgongano unatokea.
Migongano mingine husababishwa na hali ya upendeleo kwa baadhi ya wafanyakazi. Utakuta bosi bila uficho wowote anaonyesha hali ya kuwathamini baadhi ya wafanyakazi na kuwadharau wengine. Ubaguzi katika maeneo ya kazi unasababisha minong’ono, tuhuma, na hatimaye migongano. Hivyo ili kuondoa hali hiyo, kiongozi mkuu wa kampuni anatakiwa kuwa thabiti katika kuhakikisha kampuni yake haiwi na mgawanyiko wowote na kuwafanya wafanyakazi wake wafanye kazi zao kama timu moja imara.Mingine husababishwa na sera mpya ambazo hazikutarajiwa. Popote sera za kampuni zinapobadilika, kutokuelewana kunatokea, wafanyakazi wanahitaji kufahamishwa sheria na sera za kampuni, pale mabadiliko mapya yanapotokea hawatakiwi kubahatisha. Vinginevyo vitu visivyotarajiwa vitatokea kama kupeana taarifa potofu.Njia mbalimbali zinazoweza kumsaidia mkurugenzi wa kampuni, mkuu wa idara au yeyote mwenye dhamana ya kuwaongoza wenzake, jinsi ya kutatua migogoro katika maeneo ya kazi, ni pale atakapotambua na kusuluhisha kwa umakini mkubwa.Kwani baadhi ya migogoro ikitatuliwa kwa umakini matokeo yake, hujenga mahusiano bora zaidi tofauti na ilivyokuwa mwanzo. Ukumbuke kuwa migongano katika sehemu za kazi ni sehemu ya maisha na haiepukiki, lakini ni jinsi gani tunaishughulikia inapotokea kama bosi bila kuathiri biashara na shughuli za uzalishaji katika kampuni yako. Kama viongozi kunakuwepo na majukumu imara ya kusuluhisha migogoro kwa haraka. Viongozi wa kisasa hawatakiwi kuwa ‘wanyapara’, bali wawe viongozi wanaodhihirisha fani zao, heshima na usawa katika mazingira yoyote na zaidi wanaposhughulikia migongano.
Kwanza yampasa kiongozi atathmini chanzo cha tatizo. Mafanikio ya kutatua tatizo la kutokuelewana kwa kikundi au jamii yanatokana na kuelewa chanzo halisi cha mgongano huo. Ni muhimu sana kuangalia mgogoro kutokana na mtazamo wa kila mmoja unaomhusu. Kutokuelewa chanzo cha tatizo kutafanya utatuaji wa tatizo hilo kuchukua muda mrefu kutambua aliyehusika na sababu za kuhusika kwake, na sababu zinazofanya tatizo hilo kuwa gumu. Kutegemeana na hali ya tatizo lilivyo, unaweza kuzungumza ‘chemba’ na kila mmoja aliyehusika katika mgongano huo au unaweza kuzungumza nao wote kama kikundi. Kusikiliza ni silaha mojawapo muhimu itakayoweza kukusaidia na kulielewa tatizo. Pia katika utatuaji wa tatizo unatakiwa kuwa makini na kujua kwa undani chanzo. Kuwa mkweli katika kulishughulikia tatizo. Kusikiliza kwa umakini kutakuwezesha kutoa mawazo yasiyopendelea upande wowote na kukuwezesha kutatua tatizo. Mruhusu kila mmoja kuwa mhusika katika hatua hizo na hakikisha uko wazi, mkweli na kutenda kwa usawa kama unavyozungumza na mtu binafsi. Ainisha njia bora zaidi ya kutatua matatizo. Mara unapokuwa na vielelezo vya uhakika mbele yako ni kazi yako kuongoza kikundi katika kufikia suluhu au kuainisha njia bora ya utatuzi. Mafanikio ya utatuzi wa matatizo mbalimbali mara zote inahusisha pande zote katika kutathmini tatizo na kipindi cha kutafuta utatuzi. Muulize mtu binafsi kama anaweza kutoa mawazo ya jinsi ya kutatua tatizo. Kama hawatakuwa na uwezo wa kufanya hivyo, unaweza kutumia njia bora ya kutatua tatizo. Malengo yako ni kuhakikisha unapatikana mwafaka wa usawa na utatuzi wa tatizo lililokuwepo ambalo litaleta utatuzi thabiti katika kampuni yako au kwa mtu binafsi.
Wakati mwingine linapotokea tatizo, chukua muda na kujiuliza maswali yafuatayo: Nini kinachosababisha migongano katika kampuni yako? Kwa nini wewe au mwingine anahitaji vitendea kazi? Je, mtindo wa mfanyakazi fulani ni tofauti na mtindo wako uliouzowea?0713 3314550733
lcyngowi@yahoo.com, www.lngowi.blogspot.com

ZAWADI SI LAZIMA IWE PESA

KARIBUNI wapenzi wasomaji katika safu hii ya Maisha Yetu kila Alhamisi. Leo tutakwenda kuangalia jinsi unavyoweza kuonyesha zawadi ya upendo kwa watu, hata kama huna fedha.
Kila mtu anapenda kupendwa, yakupasa kuwa na rafiki wa karibu atakayekushirikisha katika mambo mbalimbali unayokabiliana nayo.
Hivyo ni vema kuwa na rafiki mzuri na kuonyesha upendo wako kwake, kwa sababu wakati mwingine unajikuta hata familia yako inakuwa mbali nawe, hivyo kipindi hicho unakuwa unahitaji mtu wa kuongea naye.
Pia ni muhimu kuwa rafiki mzuri kwa sababu unajifunza ni jinsi gani ya kukutana na watu wapya na unajifunza kutokana na makosa yako.
Tafuta watu ambao unapenda wawe rafiki zako, kwa kujitambulisha, kumwacha mtu mwingine kukueleza juu ya mambo anayoyapendelea.
Mwonyeshe mtu huyo kuwa unamwamini, mwache ajue kuwa ni sawa kupendana, mwache ajue kuwa uko pale kwa ajili yake na atakuwa rafiki yako wa kudumu.
Mara zote mfanye atabasamu hata kama ana huzuni. Pia mwache ajue kuwa upo tayari kusikiliza chochote atakachosema.
Je? Unawezaje kuonyesha upendo bila kutumia fedha? Wakati mwingine tunajitahidi kwa bidii kutafuta zawadi ambayo ni sahihi tunayofikiria kuwa ina maana kwa yule unayempelekea.
Au, tunaishikilia zawadi hiyo, tukifikiria kama kuna sababu maalumu ya kutoa zawadi hiyo. Ninakutia moyo kutoa zawadi yako kwa uhuru na iwe ni mara kwa mara, kumbuka kuwa utoaji ni shughuli ambayo inamnufaisha mtu kila mara anapofanya hivyo.
Tuangalie zawadi 10 ambazo zinafaa kwa siku ya kawaida na maalumu. Pia, ni zawadi ambazo mtu yeyote anaweza kutoa kwa sababu halazimishwi ila ni kwa nia ya kuleta ushirikiano.
Zawadi ya kwanza ni muda. Kumbuka kuutoa muda wako na kushirikiana na wenzako ni moja ya zawadi kubwa unayoweza kuitoa.
Kama unatoa dakika 10 kwa kupiga hadithi na mtoto wako, kupata chakula cha mchana na rafiki yako au kutumia muda wa mchana kwa shughuli za nyumbani, shambani au nyinginezo, ukiwa na mume au mke wako, unakuwa unajitolea nafsi yako na kujenga uhusiano mzuri kwa muda huo.
Zawadi nyingine ni kukiri kwa uaminifu. Tumekuwa tukisikia watu wachache wakisema kuwa wamepokea shukrani nyingi au pongezi nyingi.
Wote tunajisikia vizuri wakati tunapata taarifa nzuri na shukrani kwa vile tulivyo au tunayoyafanya.
Anza kuzingatia kuimarika katika hilo na kutoa sifa nzuri kwa wengine na kujenga tabia ya kukiri jambo zuri linalofanywa na wengine kwa kile unachokiona.
Nyingine ni Msamaha. Hii ni zawadi nzuri mno yenye nguvu. Wakati tunasamehe wengine, tunaacha kuwaadhibu. Tunawaruhusu ili wajisikie hatia au kuona aibu ili waweze kugundua makosa yao.
Msamaha pia ni zawadi ya kutuweka huru kutoka kwenye uzoefu ulioupata wakati ulipoumizwa moyo wako au maumivu katika matukio yaliyopita.
Vile vile upendo. Wakati unapotaka kuuonyesha upendo wako kwa wengine, usiwahukumu wengine, na uwaone kama ni watu wa muhimu kwako, watakatifu na wa thamani, hiyo ni zawadi kubwa.
Tunaposhiriki kwa uwazi upendo wetu na wengine inasaidia kuponya majeraha, kujenga uhusiano mzuri na kumsaidia mtu katika kupitia changamoto za maisha pia kuwa na maisha mapya ya uhakika.
Usiugawe usikivu wako. Ingawa tunatoa muda wetu kwa ajili ya wengine, akili zetu zinaweza kuwa popote kutokana na uzoefu.
Jiruhusu nafsi yako kuwa kwa mtu mwingine, kupanga naye shughuli nyingine, mawazo au ajenda mpaka utakapofikia malengo yako uliyokusudia.
Kama utafanya hivyo, watu watakuona unastahili kupata asilimia zote, kwa usikivu wako na kwa upande mwingine inawezekana ukawa hujafikia kiwango hicho ila kutokana na hali hiyo uliyojiwekea kwa watu.
Heshima. Mara kwa mara tunakuwa na shughuli nyingi au tunajishughulisha sana katika maisha yetu ambayo yamekuwa na matukio mfululizo ya kuvutia ambapo tunasahau kama kuna watu wengine wanaotuzunguka. Iache nafsi yako ipumue na kutoa heshima kwa watu ambao unakutana nao kila siku.
Yapo mambo madogo madogo ambayo yanaweza kufungua milango kwa watu wengine kuthamini mambo ambayo unawafanyia kama kumpa lifti kwenye gari yako, kumbebea gazeti lake mpaka mlangoni pake au kusimamisha gari lako mbele ya mtu unayemfahamu na kumpa lifti kipindi cha msongamano wa abiria kituoni.
Mambo yote hayo yataonyesha hali ya kujali kwa mtu ingawa wakati mwingine mtu hawezi kuelewa wema wako na kukushukuru.
Shtukiza. Zawadi za aina hii zinamfanya mtu kuwa mbunifu wa hali ya juu. Je, unataka kumpa dada yako kadi ambayo inasema unampenda? Unajisikiaje unapomtumia mumeo maua?
Je, ni kweli utamshtusha? Au labda umechagua kujitolea kumpa mfanyakazi mwenzako kigari cha kusukuma cha watoto ili aweze kufurahia jioni anapokuwa matembezi na rafiki zake?
Zawadi kama hizo zinakuwa tukio kubwa kwa yule unayempelekea katika siku yake ya kawaida kwa sababu hakutarajia kufanyiwa jambo kama hilo kwa siku hiyo.
Shukrani ni zawadi pekee kwa yule unayempa, kwani inasababisha mtu huyo kujua kuwa umekuwa makini kwa lile alilokufanyia. Kama ukiri wa dhati, na neno jingine ni kusema asante, linaonekana ni jambo ambalo si la kawaida.
Endapo utachagua kusema au kuandika shukrani zako, hii ni zawadi ambayo inakwenda ndani ya moyo wa mpewa shukrani.
Tabasamu katika dunia ya kisasa, mara nyingi tunaona tabasamu chache na nyuso zenye furaha ya kweli. Kinyume cha mwelekeo kwa kujivisha tabasamu kama sehemu yako ya kila siku.
Tabasamu linajulisha moyo mkunjufu, mapokezi na urafiki. Pia inafanya kuonekana kwa urahisi kwa wote wenye nyuso za tabasamu. Iache zawadi hii ya tabasamu itoe ujumbe. Mfano “Nina furaha uko hapa”.
Maombi ya kimya kimya. Wote tunakuwa na maombi ya ziada na ya baraka katika maisha yetu. Hata kama hufahamu, mtu mwingine anaweza kukubariki wakati unampa zawadi ya maombi yenye nguvu.
Kama unajua au la, mazingira ya mtu au dini yake, unaweza kuuliza kwa msaada au usikivu. Maombi rahisi unaweza kumwombea kwa kutumia “Mungu/Allah, ninakuomba umbariki mtu huyu na ukutane na mahitaji yake yoyote ambayo anayo katika maisha yake, asante”.
Tukutane Alhamisi ijayo!
0713 3314550733 331455www.lngowi.blogspot.comlcyngowi@yahoo.com

USIIGE FANYA BIASHARA UNAYOIMUDU

HABARI wapenzi wasomaji wetu. Tunamshukuru Mungu kwa siku nyingine ya leo kutuamsha tukiwa wenye afya njema. Kama kawaida leo tutakwenda kuangalia Maisha Yetu ambayo huchapishwa kila Alhamisi.
Je, wajua kuwa bahati yako ipo mikononi mwako? Na kama utafanya bidii kwa kutumia mikono yako Mungu aliyokupa ni lazima utaiona.
Ninamaanisha kuwa mtu yeyote anayependa mafanikio na kuamua kupambana ili kufikia malengo yake, ni lazima atafanikiwa. Mafanikio hayo yatatokana na jitihada pamoja na bidii anayoionyesha mtu huyo.
Mtu yeyote ambaye hatataka kujikwamua kutoka katika hali ya dhiki aliyonayo, atabakia kuwa maskini na tegemezi. Utajiri wa watu wale wanaofanya jitihada na hata kufanikiwa hautamsaidia mtu ambaye hapendi kujishughulisha.
Kama hautapenda kujikwamua kutoka katika hali ya dhiki uliyonayo, kuendelea na ujinga wa kutotaka kujifunza ili kuondoka katika tabu yako, wenye akili watatumia juhudi na maarifa yao na kukuzidi katika hali ya kuwa na mafanikio.
Kama utakuwa mwenye upumbavu, busara za wengine hazitakuongoza. Kama utapoteza muda na pesa zako, uchumi wa wengine utafikia kikomo na kukufedhehesha.
Unapokuwa na mafanikio binafsi unakuwa na nguvu katika kufanikisha mambo mbalimbali unayotarajia, ndiyo maana kila mtu peke yake anafanya jitihada za kutaka kujikwamua kutoka kwenye umaskini.
Katika jamii tunayoishi, kila mmoja wetu ni mjasiriamali. Kila mmoja ni rais katika shirika lake. Hivyo atawajibika katika mafanikio na kushindwa ambako kutaweza kutokea katika ofisi yake.
Wewe na familia yako ni wadau katika shirika lako, na ni jukumu lako kuhakikisha kuwa thamani ya mahitaji ya biashara zako yanakuwepo kwa miaka yote.
Wakati unaendelea kuendesha biashara yako inayoendelea kukua, inawezekana kabisa kama utaamua kupunguza mahitaji makubwa uliyonayo, ili uweze kusimamia vizuri pesa ulizonazo, kusimamia vizuri suala la uzalishaji, mauzo na kufanya utafiti.
Pasipokuwa na mtaji wa kutosha, hakuna uzalishaji. Bila uzalishaji, biashara yako itakuwa haina kitu cha kuuza. Bila bidhaa, shirika lako litasimamisha uzalishaji. Na bila utafiti, washirika wako hawatakuwa na imani ya kuendelea kuwepo katika kampuni hiyo kwa siku zijazo.
Suala la kutumia akili yako ya kuzaliwa ni la muhimu sana. Utafiti unaonyesha kuwa mara nyingi mtu anayefanikiwa ni yule ambaye anatumia akili yake katika kumpatia faida.
Mfano, mtu alikopa pesa benki na kuweka dhamana kwa kutumia samani zake za nyumbani. Na alitumia akili yake kuwaza biashara atakayoifanya kutokana na mkopo ule. Alianzisha biashara ya kuuza nafaka kwa jumla na sasa hivi mtu huyo ana malori ambayo yanapeleka mizigo nje ya nchi.
Kufanikiwa kwa mtu huyo kusikufanye na wewe ukaanzisha biashara kama yake, kwani unaweza kukwama. Kinachotakiwa ni kuchekecha akili yako na kuamua kufanya biashara ambayo utaimudu.
Mafanikio katika biashara yako ya kifedha yanakuja kutokana na uongozi mzuri katika biashara yako unayoisimamia. Hakuna milango iliyo wazi katika suala la mafanikio, ni lazima ufanye utafiti, uweke malengo na kutimiza ndoto yako uliyoipanga. Japo kuna misuko suko mbalimbali katika kufikia mafanikio hayo.
Ukosefu wa nafasi isiwe sababu ya kutoa udhuru katika mipango yako inayoshindikana kutokana na kuwepo kwa vikwazo mbalimbali unavyoviruhusu wewe mwenyewe.
Kila maisha unayoyaishi yana nafasi nzuri ya mafanikio. George anasema tunaishi katika dunia ambayo wakati wote ina uwezekano wa kuwa na utajiri mwingi.
Maisha ni somo, na kila somo, linapokujia ni nafasi kwako ya kujifunza. Kila biashara unayoipitia ni nafasi kwako ya kujifunza. Unapowaza juu ya watu unaowafahamu waliofanikiwa, hiyo ni nafasi nzuri kwako ya kujifunza kutoka kwao.
Uwepo wako ni upendeleo wa pekee wa kukufanya uongeze bidii katika mipango yako, na pale unapopata bahati hiyo, nafasi yako ya mafanikio inakuja kwa haraka.
Watu wenye mafanikio, wavumbuzi na waasisi ni wale wenye ujasiri na wanaweza kusema, “Ndiyo, ninaweza! Njia ipo pale na nitaitafuta”. Wote hao ambao binafsi wameyakubali maisha na changamoto zake na kuzifanyia kazi changamoto hizo katika mafanikio.
Acha kulalamika kutokana na bahati mbaya uliyokumbana nayo au jambo baya lililokupata, amua kuwa na nafasi ya kubadilika.
Kuna kitu ambacho unaweza kukifanya vyema zaidi ya mtu mwingine. Ni nini hicho? Tafuta mpaka pale utakapopata eneo lako ambalo utafanya vizuri na kuzidi wengine. Halafu upange mipango yako ukinuia kuwa utafanikiwa.
Kamwe usipende kuwa mtu wa kushindwa ila wewe ndiye unayeweza kupata mafanikio. Inawezekana kabisa mtu aliyezaliwa katika familia maskini, akakua katika hali ya umaskini, akasoma kwa shida na matatizo mengi, hatimaye mtu huyo akaja kuwa tajiri mkubwa.
Mifano mingi tunayokutana nayo ni ya watu walioishi katika hali duni, kutokana na hali ile wakaamua kubadilika na kuwa watu tofauti katika dunia tunayoiishi na wengi wao wamefanikiwa, ni matajiri wanaishi maisha ya raha.
Watu hao mara zote wamekuwa wakiwausia watoto wao kuishi maisha ya kujituma na kufanya bidii ili watakapokua waweze kuwa na mafanikio, pia wasitegemee utajiri wa wazazi wao.
Kamwe usikate tamaa, wala kuvunjika moyo. Utavuna kesho kile ulichokipanda leo. Kila siku unatakiwa kujiuliza: “Siku hii ya leo kwangu ina maana gani?”
Utakapofanya maamuzi juu ya siku hiyo, utakuwa tayari kwa kutumia uzoefu ulionao wa kufanya jambo lile ambalo umelipanga.
Umepewa saa 24 kwa siku, siku saba kwa wiki, unatakiwa kuwajibika katika siku hizo. Uko huru kufanya kazi katika muda uliojipangia kutokana na uchaguzi wako.
Uamuzi wa mafanikio upo kwako, hivyo usivunjike moyo katika hatua unayoichukua ya kufanikisha malengo yako.
Tukutane alhamisi ijayo!
www.lngowi.blogspot.com, lcyngowi@yahoo.com, 0733 331455

KUJIAMINI KUNASTAWISHA MAISHA YAKO

UTAKUWA na tofauti gani katika maisha yako endapo utakuwa mtu wa kujiamini? Ni nini zaidi utakachokipata? Hilo ni swali ambalo sote tunaweza kujiuliza.
Ni ukweli usiopingika, kwamba hali ya kujiamini inasitawisha maisha yako. Hivyo unapokuwa na afya nzuri inakufanya ufikie malengo yako kwa urahisi zaidi.
Unapojiamini katika maisha yako na shughuli zako za kila siku, utaweza kuwasaidia na wengine ambao unawasiliana nao katika maeneo mbalimbali iwe ni nyumbani au kazini. Vile vile endapo unakutana na mambo ya kustaajabisha, ya kushtusha au ya mshangao huna haja ya kuogopa, kwa kuwa tayari umeshajijengea hali ya kujiamini, utaikabili hali hiyo kwa urahisi.
Ni vizuri kujijengea hali ya kujiamini katika maisha yako kwani watu wote walio na hali hiyo wamekuwa na viwango vya tofauti ambavyo kila moja anavifurahia. Kumbuka kuwa hali ya kujiamini na kuwa jasiri, ni muhimu sana katika kila hatua ya maisha yetu, hivyo watu wengi wanajitahidi kuitafuta.
Kwa mtazamo mwingine watu waliokosa hali ya kujiamini inakuwa ni vigumu kwao kupata mafanikio. Kwa upande mwingine, unaweza kushawishika na mtu anayezungumza kwa ufasaha, anayejibu maswali yake kwa kujiamini na anayekuwa tayari kukubali kwamba jambo fulani halifahamu.
Mtu huyo ni rahisi kujifunza jambo jipya ambalo litamwongezea mafanikio zaidi katika maisha yake kwa kuwa yuko tayari. Watu wanaojiamini huambukiza hali hiyo kwa wengine. Hadhira anayokutana nayo, wanachama wenzake, bosi wake, wateja wake na rafiki zake.
Kupata ujasiri wa wengine ni njia mojawapo ambayo mtu anayejiamini huitafuta kwa ajili ya kupata mafanikio zaidi. Habari njema ni kwamba hali hiyo unaweza kujifunza na kuijenga katika maisha yako.
Na endapo unafanya kazi kwa kujiamini au kuwajengea ujasiri watu wanaokuzunguka, unakuwa umefanya jambo jema. Mambo mengine yote yanakuwa sawa kutokana na kujiamini kwako, na yeyote anayejiamini huwa na mafanikio katika maisha yake tofauti na yule mtu ambaye hajiamini. Kiwango chako cha kujiamini kinaweza kuonekana katika njia nyingi. Mfano kutokana na tabia yako, lugha yako, jinsi unavyoongea, kile unachozungumza na mambo mengine mbalimbali. Unawezaje kujijengea hali ya kujiamini?
Ni kwa kufanya kazi ya kutoa ushauri katika mazingira ya kushughulika na watu wa aina mbalimbali, wenye tabia mbalimbali waliovunjika moyo na wanaohitaji msaada zaidi wa kukabiliana na ugumu wa maisha. Unapofanya kazi hiyo ya kutoa ushauri unatakiwa kujua njia sahihi ya kukabiliana na mtu mwenye msongo wa mawazo na kujua ni jinsi gani utaanza mazungumzo naye kutokana na hali aliyokuwa nayo.
“Wakati nilipokuwa naanza kuangalia jinsi ya kuwa na hali yangu mwenyewe ya kujiamini, nilijaribu kuangalia maeneo mbalimbali yatakayonifanya nijijengee uwezo wa kujiamini. Japo kwa mara ya kwanza ilikuwa ni vigumu, lakini ilichukua muda mrefu na niliweza kufanikiwa,” alisema John Robert.
Jambo jingine ambalo linaweza kukusaidia ni kupunguza kumbukumbu za maumivu yatokanayo na mambo yaliyopita katika maisha yako. Hivyo, kama unataka kusonga mbele usikumbuke mambo yaliyopita ambayo yatakurudisha nyuma. Japo ni vizuri kujifunza kutokana na mambo yaliyopita lakini huhitaji kuendelea kuwa na kumbukumbu zinazoumiza.
Ni vyema kama hautafikiria yaliyopita. Hivyo, unaweza ukawa umejifunza wewe mwenyewe mbinu za kujiamini, unapoamua kubadilika na kuwa jasiri, ni kwamba pale unapoanza, utaendelea kukua na kukua.
Unaweza kuendelea kuhisi kwamba pengine unaweza kujiamini zaidi, maisha yanaweza kuwa mazuri kutokana na hali hiyo. Hivyo, mwishoni unafikia ndoto zako kama vile kupata kazi kubwa, kuwa na mahusiano mazuri, kununua nyumba na mambo mengineyo. Unajisikia vizuri wewe mwenyewe na kuwa na furaha kutokana na kile unachokipata. Zipo njia mbalimbali zinazoweza kukufanya ujiamini. Baadhi ya njia hizo zinafanikiwa na nyingine zinashindwa kutokana na mtu mwenyewe.
Wakati mwingine unaweza kujisikia kuwa unahitaji msaada, mtu wa kuongea naye, au kutafuta njia rahisi na kutoa ushauri bila kulipa pesa nyingi. Ni njia ya muda mrefu kuweza kuwa na hali hiyo ya kujiamini lakini inaweza kuwa ni safari nzuri kwa sababu inabadilisha maisha yako. Pia inashangaza kwa sababu unaweza kunufaika zaidi katika kila hatua unavyoongea.
Je, uko tayari kujijengea hali ya kujiamini? Kwanza inakupasa kufanya shughuli mbalimbali ambazo zitakujengea uwezo huo.
“Fanya shughuli za kukujengea ujasiri kila siku na kuwa na mawazo yanayoipanua akili yako,” anasema Mike Bonny. Pia unaweza kujiuliza ni kwa kiasi gani una ujasiri? Hali hiyo inaweza kuwepo kutokana na afya katika akili yako. Kwa mfano, kama unajisikia uchovu muda wote, itakuwa ngumu kuwa jasiri.
Ujasiri katika kufikiri ni jinsi gani mawazo yako yanaweza kuyabadilisha maisha yako. Unapokuwa jasiri katika kufikiri ni sababu ya kuyabadili mawazo tunayoyawaza. Vilevile, ujasiri katika mahusiano mara nyingine unaweza kuona ni kitu cha kukupa changamoto.
Sasa basi, unaweza ukaangalia ulinganisho wa tabia ya kujiamini na ile ya kutojiamini. Ni hatua gani unazoweza kuzichukua kwako binafsi na kwa watu wanaokuzunguka? Unapokuwa mtu wa kujiamini unafanya kile unachofikiri ni sawa, ingawa wengine watakukosoa.
Pia utakuwa tayari kwa lolote ili uweze kupata vitu vizuri. Vile vile unakuwa ni mtu wa kukubali makosa yako na kujifunza. Mtu asiyejiamini anakuwa ameegemea upande wa wengine wanavyofikiri. Unabakia kukaa sehemu moja ukiogopa kushindwa na kukwepa kubahatisha au kuthubutu kufanya jambo fulani. Anakuwa mgumu kukubali kosa.
Kama ulivyoona katika mifano hiyo hapo, hali ya kutojiamini inakuletea uharibifu, bali inakujenga. Jifunze kujiamini, kuwa jasiri katika kila jambo unalolifanya, usitetereke utafanikiwa.
www.lngowi.blogspot.comlcyngowi@yahoo.com0713 331455 au 0733 331455

Wednesday, July 23, 2008

WAZA MAMBO MAZURI


KARIBUNI wapenzi wasomaji katika safu ya ‘Maisha Yetu’. Kwa zaidi ya mwaka sasa nimeandika mambo mbalimbali yanayohusu mafanikio, jinsi ya kuishi na watu mbalimbali, kujua tabia za watu, kujijua mwenyewe na jinsi ya kupambana na maisha katika hali yoyote.
Kwa kweli safu yetu imepongezwa sana na tulipokosea tulikubali ushauri kutoka kwa wasomaji wetu. Naamini mtaendelea kutuungana mkono kwa kusoma na kuendelea kutoa ushauri wa kuboresha safu hii.
Wiki iliyopita niliishia sehemu inayosema; kumbuka unapoanza kuwa na hofu ya vitu vilivyopita ni kama unajaribu kupanda mazao yako kwenye vumbi.
Maana yake ni kwamba yale yaliyopita usiyasumbukie, bali ugange yajayo. Ukiendelea kuyasumbukia, utajisababishia mikunjo katika paji la uso wako na vidonda vya tumbo.
Hivyo, endapo una tatizo la kukumbuka mambo yaliyopita, iambie nafsi yako kwamba huishi kwa ajili ya mambo hayo. Badala yake unaweza kuwa na mipango mizuri zaidi kwa ajili ya maisha yako.
Unaweza kujishughulisha kwa kuandaa mashindano mbalimbali kama vile muziki, soka au uchoraji. Lengo ni kujishughulisha kila mara ili usiwe na nafasi ya kufikiria mambo yaliyopita ambayo yamekusababishia hasara na hofu maishani mwako.
“Miaka michache iliyopita nilitakiwa kujibu swali moja ambalo lilikuwa likiuliza, je, ni somo gani kubwa ambalo nimejifunza.
“…Jibu lake lilikuwa ni jepesi kwamba somo nililowahi kujifunza na kulifurahia ni juu ya umuhimu wa vile tunavyofikiri.
“Kwani endapo mimi ningejua kile unachokifikiri ningejua wewe ni nani na wewe ungejua kile ninachofikiri, ungejua mimi ni nani - kwani mawazo yetu yanatufanya tujue sisi ni nani”.
Sasa tunaweza kujua matatizo makubwa tunayokuwa nayo mimi na wewe, kwamba tatizo tunalohangaika nalo ni jinsi ya kuchagua mawazo sahihi. Kama tutafanikiwa katika hili, tutakuwa kwenye njia sahihi ya kutatua mawazo yetu yote.
Ni ukweli usiopingika kuwa endapo unafikiria mawazo ya furaha utakuwa na furaha maishani mwako, vile vile endapo unafikiria mawazo ya umaskini, utakuwa hivyo.
Kama unawaza mawazo ya hofu, utaishi kwa hofu. Iwapo mawazo yako ni kuumwa, kuna uwezekano wa kupata maradhi. Kama unafikiria kushindwa, utashindwa kweli kwenye mipango yako.
Kama unatabika na kujionea huruma, kila mmoja atakuepuka na kujitenga nawe. Huko vile unavyofikiri, bali kile unachofikiri, ndivyo kilivyo.
Mtu mmoja alikuwa na maisha mazuri, lakini ghafla alifilisika, ingawa mtu huyo alijikuta na madeni makubwa, alijishughulisha hakuwa na hofu kwa kuwa alijua endapo ataruhusu hali hiyo imvunje moyo, atakosa kuthaminiwa, pamoja na mdai wake.
Hivyo alijipa matumaini kwa kuwaza mambo ya mafanikio, mawazo ya kutia moyo na kukataa kuiruhusu hali ya kushindwa.
Hali hiyo ilimfanya atulize akili yake na kupanga mambo ya mafanikio katika maisha yake. Alijitathmini na kuangalia upungufu uliokuwapo hadi hali ile ikamtokea, alimwomba Mungu, pia alijitahidi kufanya kazi yoyote iliyokuwa mbele yake kwa malengo.
Tuangalie mfano uliotolewa na Mwalimu John uliomhusu mwanafunzi wake ambaye alivunjika moyo kutokana na hofu iliyomwandama.
Kwa maelezo ya Mwalimu John, mwanafunzi huyo alikuwa wazi kwake hivyo alimweleza kuwa hali ya wasiwasi ilikuwa ikimtesa kwa muda mrefu.
Hivyo, alikuwa na wasiwasi wa kila kitu, alikuwa na hofu kutokana na wembamba aliokuwa nao, kwamba alihofia kupata fedha za kuoa, alihofu kumpoteza msichana aliyetaka kufunga naye ndoa.
Alihisi kuwa kamwe hatakaa aishi maisha mazuri, alikuwa na hofu kuwa atapata vidonda vya tumbo. Kutokana na hali hiyo, aliamua kuacha kazi.
Mwanafunzi huyo alisema baada ya kujitathmini alijiona ana kasoro, hivyo alimwomba Mungu ampe nguvu ya kufanya shughuli zake na kuondoa hofu hiyo aliyokuwa nayo.
“Hali hiyo ilikuwa ikinitokea mara kwa mara, hivyo sikuweza kuieleza hata familia yangu,” anasema mwanafunzi huyo. Anasema hakuweza kuidhibiti hali hiyo, kwani alikuwa amejaa hofu.
Kutokana na hali hiyo, alijiepusha na kila mtu. Lakini ufumbuzi ulipatikana baada ya kumwomba Mungu ampe nguvu ya kuikabili hali hiyo na kujishughulisha.
Baada ya kuigundua hali hiyo, ilimbidi abadilike kwa kuondoa mawazo yaliyokuwa yakimsumbua. Alipoamua kukondokana na hali hiyo, alijikuta ameirudia kazi yake aliyokuwa ameiacha, miezi minne baadaye alimwoa binti aliyefikiri kuwa angemkosa kutokana na hofu aliyokuwa nayo, hivyo kujikuta anaishi maisha yenye furaha.
Kumbuka unapokuwa katika hali ya kukata tama, unajikuta huwezi kuendelea wala kuwa na mafanikio yoyote katika maisha yako. Unapoikataa hali hiyo maisha yanakuwa mazuri na kuwa kama ni rafiki yako.
Kumbuka amani tuliyonayo na furaha tunayopata haitegemei wapi tulipo au nini tulichonacho ama sisi ni kina nani, lakini ni kutokana na mawazo tunayoyawaza.
Ni vizuri kuitafuta furaha kwa gharama yoyote ili kuondoa hofu na wasiwasi inayokuandama. Iambie nafsi yako kwa leo utakuwa na furaha. Kumbuka furaha inatoka ndani, si jambo linalotoka nje. Pia uhudumie mwili wako kwa mazoezi na kuupamba, usiudharau.
Pia jifunze kuwa na mawazo yenye nguvu ambayo yatakufanya ujifunze mambo kwa ajili ya manufaa. Usiiruhusu akili yako iwaze masuala yasiyo na nguvu yatakayokufanya ujione huna maana. Jizoeze kusoma vijaridia vya kukuwezesha kuwa na jitihada katika shughuli zako, pamoja na akili.
Anza kuwa na ratiba katika maisha yako ya kila siku, kwa kuandika kwenye kijitabu yale mambo unayotarajia kuyafanya kila saa, si lazima ufuate kama ratiba ilivyo, lakini ni vizuri kuwa na ratiba.
Pia ni vizuri kujipa muda wa kutulia na kupumzika, pamoja na kumwomba Mungu. Iambie nafsi yako kwa siku hiyo hautakuwa na hofu, ila furaha na kufurahia vitu vizuri na kuwapenda wengine.
Tukutane Alhamisi ijayo.
Makala hii imeandaliwa kwa msaada wa mtandaohttp://www.lngowi.blogspot.com/lcyngowi@yahoo.com0713 – 331 455 au0733 – 331 455

ONDOA WASIWASI KATIKA MAISHA USONGE MBELE


KARIBUNI wapenzi wasomaji wa safu hii inayowajia kwa lengo la kufundisha na kubadili maisha yetu. Pia safu hii huweza kumtoa mtu katika hali fulani aliyokuwa nayo na kumweka katika hali nyingine.
Wiki iliyopita tuliishia sehemu iliyoeleza, unapokuwa kwenye wakati mgumu, kama unaweza kuiondoa hali hiyo ni vizuri, lakini kama huwezi usiipe nafasi moyoni mwako.
Endapo utaipa nafasi hali hiyo, itarudisha nyuma maendeleo yako kwa kuwa kila utakapotaka kupiga hatua, hofu ya kufa au kuugua na kuacha mali zako hukujia.
Katika vipindi mbalimbali mtu anavyopitia, amekuwa akikutana na hali isiyo nzuri kutokana na mzunguko wa dunia.
Hivyo, unapojikuta katika hali hiyo, una uamuzi wa kuikubali hali iliyokupata kuwa haiwezi kubadilika na kuwa tayari kukabiliana nayo, endapo hautaikubali hali hiyo utaishia kuwa na hofu kila wakati.
Leo, tutaangalia jinsi ya kukabiliana na hali inayokupata mara tu biashara yako inapokwenda mrama. Unapokutana na hali hiyo ni vema kuweka tamko la kusitisha hasara uliyoipata, kwamba huko tayari kukubali hasara hiyo iendelee, kwani utajitahidi kuweka mikakati zaidi ya kuiboresha na kuomba ushauri wa kimaendeleo kwa wafanyabiashara waliofanikiwa.
Tumwangalie mfanyabiashara John Robert, aliyekuwa amepewa fedha na rafiki zake kiasi cha dola 200,000 za Kimarekani, ili kuwekeza katika soko la hisa.
Baada ya kupewa fedha hizo na kuzifanyia biashara, Robert alifikiri kuwa angepata faida ambayo ingemfanya awe na maendeleo zaidi katika maisha yake, lakini kwa bahati mbaya ilikuwa kinyume na matarajio yake.
Awali, alipoanza biashara hiyo alipata faida ambayo ilimfanya asiwe mbunifu katika biashara yake, lakini matokeo yake ni kwamba baada ya muda mfupi alifilisika.
Mfanyabiashara huyo, baada ya kufilisika alipata hofu kutokana na fedha alizopewa kwa ajili ya kufanyabiashara.
“Sikujali kupoteza pesa zangu mwenyewe,” alisema mfanyabiashara huyo na kwamba kipindi hicho kilikuwa kigumu kwake, kutokana na kupoteza pesa za rafiki zake.
Lakini, mara baada ya kufanikiwa kuishinda hofu iliyokuwa ikimkabili, alijikuta amepata ujasiri mpya na kwenda kuwakabili tena rafiki zake na kuwaeleza kilichomsibu.
Pamoja na maelezo hayo, marafiki wale hawakuonyesha mshangao katika jambo hilo, bali walilichukulia kuwa la kawaida. Lakini kwa upande wake ilionekana halitatibika.
“Nilijua nilikuwa nafanya biashara katika mtindo wa 'pata potea' nikitarajia zaidi bahati na mawazo ya watu. Nilikuwa nikishiriki katika soko la hisa kwa kusikia,” alisema.
Kwa maelezo ya Robert, alianza kufikiria makosa yake na kufanya uamuzi kabla ya kuamua kurudi kwenye soko kwa mara nyingine, alijaribu kutafuta chanzo cha jambo hilo, pia alifikiri na kuamua kuja na mwongozo mpya wa mafanikio.
Baada ya hali hiyo kumtokea, alitafuta ushauri kutoka kwa rafiki zake, kwa kuwauliza ni jinsi gani wameweza kufanikiwa na kuendesha biashara zao, ambazo zinakwenda vizuri.
Mmoja wa marafiki zake, aliyeendesha biashara yake vizuri alimweleza akiweka tamko la kusitisha hasara katika hofu yake kwenye majukumu aliyojipangia.
Hivyo, mtu yeyote anaweza kuondoa tabia ya hofu aliyonayo. Hivyo popote unaposhawishika kuweka pesa zako baada ya kupoteza, ni vizuri kutulia na kujiuliza maswali yafuatayo.
Ni kwa kiasi gani umekuwa na hofu kuhusu jambo fulani juu yako? Ni kwa jinsi gani utaepuka kupata hasara katika hofu inayokukabili na kusahau? Ni kwa jinsi gani utaepuka kupata hasara katika wasiwasi na kusahau?
Kumbuka unapoanza kuwa na hofu ya vitu vilivyopita na kufanyika ni kama unakuwa ukijaribu kupanda mazao yako kwenye vumbi. Maana yake ni kwamba yale yaliyopita usiyasumbukie, bali ugange yajayo. Ukiendelea kuyasumbukia utajisababishia mikunjo katika paji la uso wako na vidonda vya tumbo.
Hivyo, endapo una tatizo la kukumbuka mambo yaliyopita, iambie nafsi yako kwamba huishi kwa ajili ya mambo hayo. Badala yake unaweza kuwa na mipango mizuri zaidi kwa ajili ya maisha yako. Unaweza kujishughulisha kwa kuandaa mashindano mbalimbali kama vile muziki, ngumi au uchoraji.
Lengo ni kuwa unajishughulisha kila mara ili usiwe na nafasi ya kufikiria mambo yaliyopita ambayo yamekusababishia hasara na hofu maishani mwako.
Tukutane Alhamisi ijayo.
Makala hii ni kwa msaada wa mtandao wa mtanadao na kitabu cha Ondoa wasiwasi anza maisha mapya’.
http://www.lngowi.blogspot.com/ lcyngowi@yahoo.com0713 331455 OR 0733 331455

KUBALIANA NA HALI USIYOWEZA KUIBADILI

KARIBUNI wapenzi wasomaji katika Safu ya Maisha Yetu, ambayo huelimisha, huadilisha na kubadilisha mambo mbalimbali tunayokabiliana nayo katika maisha yetu ya kila siku.
Wiki iliyopita tulimwona Steven baada ya kufiwa na watoto wake wawili mfululizo aliishi kwa hofu na kukata tamaa kwa muda mrefu, lakini siku moja mtoto wake wa kiume (5) alimwomba baba yake amtengenezee boti, ambayo ilimchukua muda mrefu kuimaliza.
Kwa maelezo ya Steven, kutengeneza boti hiyo kulichukua muda wa saa tatu, lakini ilipokwisha aligundua muda huo alioutumia katika kazi aliyokuwa akiifanya, uliweza kumpumzisha akili yake na kumpa amani ambayo aliipoteza kwa muda mrefu baada ya kufiwa na watoto wake.
Tokea hapo, aligundua kuwa ni vizuri mtu ajishughulishe katika kipindi kigumu anachopitia kama vile kufiwa na mke, mume, wazazi au watoto. Kwa kuwa mtu anapojishughulisha hukosa muda wa kufikiri hali ile iliyompata huko nyuma na badala yake anafiki kile anachokifanya kwa wakati huo.
Leo tutakwenda kumwangalia George ambaye anasema alipokuwa mtoto alikuwa na wasiwasi. Kwa maelezo yake, kila ilipofikia kipindi cha radi na ngurumo alikuwa akipatwa na hofu kuwa huenda mwanga wa radi utamuua.
Vilevile katika kipindi kigumu cha kutokuwa na mazao shambani mwao, alikuwa akihofu huenda watakosa chakula cha kutosha, na kuwasababisha wakae na njaa.
Hofu yake haikuishia hapo, bali aliendelea kuwaza kuwa endapo atakufa atakwenda motoni. Alikuwa akimwogopa kijana ambaye alimtishia kuwa angemkata masikio yake na kuwaogopa wasichana kuwa wangemcheka endapo angeongea nao. Wasiwasi wake ni kwamba hakuna msichana yeyote atakayekubali kuolewa naye.
Yote hiyo ni hali ya wasiwasi aliyokuwa nayo kijana huyo na kumfanya aishi kwa hofu muda mrefu, mpaka pale alipokuwa mkubwa na kugundua asilimia 90 ya vitu alivyokuwa akiviogopa havikumtokea.
Hivyo unaweza kuona, hofu inapoumbika katika maisha yako inasababisha shida kubwa na kurudisha nyuma maendeleo yako kwa kuwa kila ukitaka kupiga hatua unakuwa na hofu kuwa huenda ukafariki au kuugua.
Hivyo wasiwasi ni mbaya sana. George anasema hali hiyo ilikuwa ikimtesa katika kipindi cha ujana, lakini kadiri alivyokuwa anakuwa aliipuuza kwa kuwa ilimtesa.
Endapo unasumbuliwa na hali hiyo, jitahidi kuiondoa kwa gharama yoyote ili isikuletee uharibifu siku za usoni. Mara nyingi mwishoni mwa wiki, watu wengi hupenda kwenda matembezi mbalimbali kama madukani, sokoni au kutembelea ndugu, jamaa na marafiki.
Safari hiyo itakuwa nzuri kama mtu huyo atatuliza akili yake katika matembezi anayoyafanya. Lakini kinyume chake kama utakuwa haujaishinda huko uliko, utaanza kuwa na wasiwasi labda umeacha pasi inawaka au nyumba yako inaungua.
Unaweza kuwa na wasiwasi, kwamba msichana unayeishi naye ametoroka na kuwaacha watoto wako peke yao au hofu yako wamegongwa na gari na kufariki wakati wakiendesha baiskeli zao.
Hali hiyo itakuondolea raha ya matembezi hivyo usipoidhibiti itakuletea matatizo katika familia na hata ndoa yako. Unapokuwa na hali ya hofu ni vema ukaupumzisha mwili na kufikiri njia ya kuondokana na hali hiyo.
Ni vema ukakubaliana na hali ile ambayo huwezi kuibadili au kuizuia. Unapokutana na jambo linalokuumiza, ni vema ukakubaliana nalo. Mfano unaweza kupata ajali na kukatika vidole vya mguu wa kushoto, kabla ya hapo ulikuwa ukiuona mguu wako ukiwa na vidole vyote vitano, usipokubali hali hiyo, siku zote utakuwa mtu wa hofu na kukata tamaa. Hivyo ni vizuri kukubaliana na hali ile ambayo huwezi kuizuia au kuiepuka.
Katika vipindi mbalimbali tunavyopitia, tumekuwa tukikutana na hali isiyo nzuri katika maisha yetu, na hivyo ndivyo ilivyo. Tuna uamuzi, tunaweza kukubali hali hiyo kuwa haiwezi kubadilika na kuwa tayari kukabiliana nayo, au kutokubaliana na hali hiyo, ambapo mwisho wake ni kuwa na wasiwasi kila wakati.
“Kukubaliana na kile kilichokutokea ni hatua ya kwanza ya kukabiliana na jambo lolote lililo gumu,” anasema Godfrey Johnson. Usiiruhusu nafsi yako kukata tamaa hadi kushindwa kufanya jambo la maendeleo katika maisha yako. Isifikie hatua ukaona kuwa hakuna faida ya kuishi kutokana na misukosuko inayokukabili.
Watu wengine wanapokumbana na hali ngumu katika maisha yao hufikia hatua ya kuidharau kazi anayoifanya na hata kujitenga na marafiki zake. Isifikie hatua ukaachilia kila jambo ulilokuwa ukilifanya kutokana na hali hiyo.
“Nilipopata habari za kunitia hofu niliacha kazi yangu, na kwenda mbali ambako nilijificha nikalia kwa uchungu,” alisema Mary. Kwa maelezo yake alikumbuka wakati alipofiwa na mama yake mzazi alitumiwa ujumbe ambao ulisema kuwa; “Jipe moyo kwa yale yaliyokupata. Zuia huzuni zako kwa tabasamu na kuinuka.”
Alisema maneno hayo alipoyatafakari kwa mara nyingine yalimwinua na kumtia nguvu mpya. Alisahau tabu na huzuni zote zilizomkabili. Baada ya kupata faraja hiyo, aliondoka na kurudi kazini kwake kuendelea na kazi, kwa kuwa, aliikataa hali ile iliyokuwa ikimsononesha, kwa kuiambia nafsi yake kuwa, “imetokea. Siwezi kuibadili hali hiyo.”
Hivyo ni vema kila unapokabiliana na hali hiyo, kukubali kuuchosha mwili wako kwa kuanza masomo ya jioni, kujifunza mambo mapya na kuwa na marafiki wapya. Baada ya kufanikiwa kufanya hivyo utaishi maisha mapya ya furaha yasiyo na huzuni, kwa kuwa hautairuhusu nafsi yako kukumbuka yaliyopita.
Hivyo ni kawaida, mazingira pekee hayawezi kutufanya tuwe na furaha au kutokuwa nayo. Ni kwa jinsi gani tunakabiliana nayo inategemea hisia zetu. Tuangalie mfano wa kijana mmoja ambaye alizoea kusema kuwa, hawezi kuwa na wasiwasi hata kama atapoteza fedha zote alizonazo kwa sababu haoni atakachopata endapo atairuhusu hali hiyo zaidi ya kujipa maumivu.
Ila alisema kitakachofuata baada ya hapo, ni kufanya kzi kwa bidii vile atakavyoweza, na matokeo yake atayaacha mikononi mwa Mungu. Unapokuwa katika wakati mgumu, kama unaweza kuiondoa hali hiyo ni vizuri, kama huwezi usiipe nafasi katika moyo wako hali hiyo.
Makala hii ni kwa msaada wa mtandao wa intanenti na kitabu kijulikanacho kama ‘Ondoa wasiwasi anza maisha mapya’.
Tukutane alhamisi ijayo
www.lngowi.blogspot.comlcyngowi@yahoo.com0713 331455 or 0733 331455

KUJISHUGHULISHA NI NJIA YA KUONDOA HOFU, WASIWASI



NI vizuri ukakabiliana na hali ya wasiwasi inayokusumbua na kuanza siku mpya. Wasiwasi mara nyingi unasababisha uso wako kuharibika, kukunjika, kupatwa na chunusi, vipele vidogo vidogo, ngozi kukunjamana, nywele kubadilika rangi na wakati mwingine kukatika.
Unaweza kuona hali hiyo kuwa ni ya kawaida, lakini sivyo unavyofikiri, hivyo unaweza kukabiliana nayo kwa kuondoa hali hiyo ya hofu na wasiwasi.
Je, unapenda maisha? Je, unapenda kuishi maisha marefu na kufurahia afya bora? Unatakiwa kuwa na amani ndani ya moyo wako ambayo itakuwezesha kuishi kwa kujiamini.
Tuangalie mfano wa kijana Dave, ambaye alihakikishiwa na daktari wake kuwa ana ugonjwa wa kansa, hivyo tangu wakati huo alijiona kama anakufa taratibu kutokana na ugonjwa huo uliompata.
Kwa kuwa alikuwa bado kijana, hakupenda kufa mapema, hivyo kila mara akawa anasumbuliwa na hofu ya kifo. Hivyo aliamua kumpigia simu daktari wake na kumweleza hali aliyonayo na jinsi anavyojisikia kutokana na hali hiyo.
Daktari yule alimweleza wazi kijana Dave, kwamba, kama ataendelea kuwa na hofu, atakufa, cha msingi akubaliane na hali ile aliyokuwa nayo ya ugonjwa bila kuwa na wasiwasi.
“Ni kweli umepatwa na hali mbaya, cha msingi ikubali hali hiyo,” alisema daktari yule na kumsisitiza zaidi kwa kumwambia aiondoe hali ya hofu aliyonayo.
Tangu hapo Dave aliikubali hali ile na kuiambia nafsi yake hana haja ya kuwa na wasiwasi tena, wala kulia, pia yuko tayari kukabiliana na hali yoyote katika maisha.
“Sitaki kuwa na mawazo kuwa nina kansa, bali ninaamini kuwa akili yenye uchangamfu inausaidia mwili kupigana na magonjwa,” alisema Dave na hapo aliendelea kuwa na afya njema, na kusema kuwa anaufurahia msemo unaosema, ‘kubaliana na ukweli, ondoa wasiwasi, halafu fanyia kazi hali hiyo’.
Ni jinsi gani ya kuchanganua na kutatua matatizo yanayosababisha wasiwasi? Kwanza yakupasa upate uhakika wa jambo linalokusumbua, ulichanganue na kufikia uamuzi ambao utaufanyia kazi.
Unafikiri ni kwanini ni muhimu kupata uhakika? Ni kwa sababu kama una uhakika wa lile unalotaka kulitatua haitakuwa rahisi kupata utatuzi wa busara, kwani bila uhakika yote utakayoyafanya yatakuchanganya zaidi.
Unapoamua kutafuta utatuzi wa tatizo lako kamwe usigeuke nyuma na kuangalia hali uliyokuwa nayo awali, ambayo inaweza kukusababishia hofu nyingine. Pia tuangalie ni jinsi gani unaweza kuondoa hofu inayokukabili katika biashara zako.
Dk. Jarome anasema kuwa, kwa miaka 15 amekuwa akitumia nusu ya muda wake wa kufanya biashara zake kwenye mikutano, kujadili matatizo. Kwamba biashara hiyo inaweza kufanywa hivi au vile au kutokufikia muafaka. Anaeleza mara zote amekuwa akipata wasiwasi yeye na wenzake, kwenye viti walivyokalia vinavyozunguka, kutembea kwenye korido, kujadili na kuangalia ukubwa wa tatizo. Na inapofika usiku tayari amekuwa amechoka.
Anasema anategemea hali hiyo ya kuwa na mambo mengi yanayomkabili itakuwa inaendelea katika maisha yake yote. Anasisitiza amekuwa akifanya hivyo miaka 15 iliyopita, kamwe haitatokea kwake njia nyingine ya kufanya hivyo.
“Hapa kuna siri,” anasema Jarome. “Kwanza nimeacha utaratibu niliokuwa nimejiwekea katika mikutano kwa miaka 15 iliyopita.” Anasema aliamua kubadilisha mfumo huo na kuwashirikisha wengine kwa kuwauliza watafanya nini ili kutatua matatizo.
Pili, anasema alitengeneza sheria mpya ya kwamba kila mmoja atakayetaka kupeleka tatizo kwake, lazima ajiandae na kuandaa taarifa ambayo itampatia majibu katika maswali manne ambayo ni kutaka kujua tatizo haswa ni nini, chanzo chake, njia zinazowezekana kutatua tatizo hilo na njia za kutatua tatizo zitakazofikiwa. Hiyo ndiyo changamoto ya kuondoa wasiwasi kwa asilimia 50.
Ni jinsi gani ya kuondoa hali ya wasiwasi inayokukabili kabla haijakuondoa wewe? Tuangalie mfano wa Steven ambaye alikuwa jasiri na kuwaeleza wenzake aliokuwa akisoma nao kwenye chuo kimoja, jinsi ambavyo alikumbana na msiba mara mbili katika familia yake. Kwa maelezo ya Steven, mara ya kwanza alimpoteza mtoto wake wa miaka mitano ambaye alikuwa ni binti, mtoto aliyempenda mno.
Anasema yeye na mke wake walifikiri kuwa hawataweza kustahimili hali hiyo, lakini Steven anasema, miezi kumi baadaye, Mungu aliwapa mtoto mwingine wa kike ambaye alifariki baada ya siku tano.
Steven alisema yeye na mkewe hawakuwahi kupitia kipindi kigumu kama hicho katika maisha yao. “Sikuweza kuchukuliana na hali hiyo, sikuweza kulala, sikuweza kula, sikuweza kupumzika wala kuburudika. Mishipa yangu ilikuwa ikitetemeka na hali ya kujiamini ikaniaondoka,” anasema baba huyo.
Mwishoni alienda kwa madaktari ambao walimshauri wamchome sindano ya usingizi au atafute matembezi ya mbali kwa ajili ya kupumzisha akili. Anasema alijaribu vyote lakini havikuweza kumsaidia.
Anasema hali hiyo iliendelea kumtesa kwa muda mrefu, akaeleza kuwa kwa yeyote aliyewahi kupooza kutokana na jambo baya lililompata ataelewa ni nini anachokisema.
Lakini anamshukuru Mungu kwa kuwa, alikuwa na mtoto mmoja aliyebakia wa kiume wa miaka mitano. Ambaye alimpa ufumbuzi wa tatizo lake. Siku moja mchana alipokuwa amekaa anajisikitikia, mtoto huyo alimwuliza baba yake kama anaweza kumtengenezea boti.
“Ukweli ni kwamba nilikuwa sijisikii kutengeneza boti hiyo, nilikuwa sijisikii kufanya jambo lolote lile,” alisema na kuongeza kuwa ilimbidi afanye hivyo kwa kuwa mtoto wake huyo huwa abadili msimamo wa kile anachokitaka, hivyo ilimbidi amtengenezee.
Anasema kutengeneza boti hiyo ya kuchezea ilimchukua muda wa saa tatu. Lakini ilipokwisha, aligundua muda huo alioutumia uliweza kumpumzisha akili yake na kumpa amani aliyokuwa nayo kwa muda mrefu.
Hivyo amegundua kuwa unapokuwa na shughuli za kufanya kipindi ambacho umekuwa katika wakati mgumu uliokufanya uwe na wasiwasi, hofu au hali ya kukata tamaa, zinakufanya mtu uwe na nguvu mpya kwa kuwa hupati muda wa kufikiri yaliyopita, bali jinsi ya kufanya kazi hiyo ili ikamilike. Hivyo alifikia uamuzi wa kujishughulisha ili hali aliyokuwa nayo isimrudie tena.
Makala hii imetafsiriwa kutoka kwenye kitabu kijulikanacho kama ‘Ondoa wasiwasi anza maisha mapya’, pamoja msaada wa intaneti.
Tukutane wiki ijayo
lcyngowi@yahoo.com0713 331455 or 0733 331455

ONDOA WASIWASI ANZA MAISHA MAPYA

MWANAFUNZI aliyekuwa akichukua masomo ya udaktari, alikuwa na wasiwasi wa jinsi ya kufaulu mitihani yake ya mwisho ya kumaliza chuo. Na hata atakapomaliza masomo yake na kufaulu atapelekwa wapi kufanya kazi aliyoisomea na jinsi gani ataweza kumudu maisha.
Wakati akitafakari hayo, alijikuta anasoma maneno machache ambayo yalibadilisha mtazamo wake huo, na kumfanya kuwa daktari mmoja maarufu katika kizazi chake, na hata alipofariki kurasa 1,466 ziliandikwa kwa ajili ya kueleza wasifu wake.Maneno hayo ni - “Kazi yetu si kuona kwa upeo mdogo kilicho mbali, bali ni kufanya kile tulichonacho mkononi”.
Hata hivyo, mwanafunzi huyo aliamini kuwa njia inayowezekana kuandaa mambo ya kesho ni kufikiri kwa ufahamu wote, pamoja na kuwa na shauku ya kufanya kazi ya leo vizuri zaidi.
Aligundua kuwa hiyo ndiyo njia pekee inayowezekana mtu anayoweza kuiandaa kwa ajili ya maisha.
Mfano mwingine ni kwa mwanamke mmoja ambaye baada ya kufiwa na mume wake, alianza kujiona mpweke na kuvunjika moyo. Siku moja alipokuwa akitoka shuleni alikokuwa akifundisha, alianza kufikiri na kujisemea moyoni mwake kuwa shule aliyopo ni ya kimaskini, pia barabara anayopita wakati wa kwenda na kurudi nyumbani kwake ni mbaya, hivyo aliamua kuchukua uamuzi wa kujinyonga.
Alifikia hatua hiyo baada ya kuona kila kitu kwake hakiwezekani. “Sioni faida ya kuishi. Ninaamka kila asubuhi, kukabiliana na maisha. Nina hofu ya kila kitu, hofu ya kutoweza kumudu kuliendesha gari langu, hofu ya kushindwa kulipa kodi ya nyumba, hofu ya kutokuwa na chakula cha kutosha. Nina hofu ya afya yangu nami sina fedha ya kumwona daktari.
"Yote hayo yalimfanya kufikiria kujinyonga. Siku moja alisoma kifungu kimoja kilichomuinua kutoka katika ile hali iliyokuwa inamkabili na kumpa moyo wa kuendelea kuishi. Kifungu alichosoma kilisema: "Kila siku ni maisha mapya kwa mtu mwenye busara."
Alikiandika kifungu kile na kukibandika kwenye kioo cha gari yake alipoweza kukiona kila mara alipokuwa akiendesha.
Aligundua kuwa kuishi si jambo gumu kama alivyofikiria awali, alijifunza kusahau yaliyopita na kutokufikiria mambo ya kesho. Kila siku alijisemea moyoni mwake kuwa, ‘leo ni siku mpya’.
Alifanikiwa kuishinda hofu iliyokuwa ikimkabili ya upweke aliyojitakia. Tangu hapo akawa mtu wa furaha, mwenye mafanikio na anayependa kuishi.
Kuanzia hapo alisema kuwa hataogopa tena, bila kujali maisha yatakuwa ya aina gani kwake. Aligundua kuwa hataogopa maisha yajayo na ndiyo maana kila siku ni mpya kwa mtu mwenye busara.
Jinsi ya kuondoa hali hiyo ya wasiwasi
Kumbuka kuwa hali ya wasiwasi inakuondolea uwezo wa kufikiri. Kwani unapokuwa na hofu akili yako 'inaruka' na kufikiri hapa na kule na kila mahali, na unapoteza nguvu yote ya maamuzi. Hata hivyo, wakati unapojilazimisha kufikiria jambo linalokufanya upatwe na hali hiyo na kuikubali katika akili yako, unaiweka katika kupata muafaka wa jambo linalokukwaza.
Unapokuwa na wasiwasi unaweza kupata vidonda vya tumbo, pia uzito wako unaweza kupungua ghafla pamoja na kupata maradhi mbalimbali.Ili kuondokana na hali hiyo, inakupasa kuacha kufikiria na kujipa ujasiri katika kila jambo unalolifanya, pamoja na kuamua kufanikisha mipango yako ya baadaye. Pia unaposafiri maeneo mbalimbali inakusaidia kukutana na watu tofauti na kupata mawazo mapya ya maisha hivyo kujikuta unaondokana na hali uliyokuwa nayo.
Hali hiyo imekusababishia mambo gani
Hali hiyo humfanya mtu akawa mgonjwa na kuanza kuhisi dalili za tumbo kujaa, kuwa na vidonda vya tumbo, mapigo ya moyo kuongezeka, kuumwa na kichwa na mara nyingine kupatwa na hali kama ya kupooza.
"Magonjwa kama haya hutokea. Ninajua ninachokizungumza,” anasema Dk. Gober. "Kwa upande wangu nimesumbuliwa na vidonda vya tumbo kwa muda wa miaka 20.
“Hofu inasababisha wasiwasi. Pia wasiwasi huo, unakufanya uwe katika hali ya kutotulia na ya fadhaa, huathiri misuli ya tumbo lako, hubadili tumbo lako kutoka katika hali ya kawaida, ambayo mara nyingi huchangia kupata vidonda vya tumbo,”.
Naye Dk. Joseph Montague anasema huwezi kupata vidonda vya tumbo kutoka kwenye kile ulacho, bali unapata vidonda hivyo kutoka kwa kile kinachokutafuna.
Hofu, wasiwasi, chuki, ubinafsi na kutokuwa na uwezo wa kukabiliana na ukweli wa mambo katika ulimwengu huu, ni sababu kubwa za maumivu ya tumbo, pamoja na vidonda…vidonda vya tumbo vinaweza kukuua.
Pia utafiti uliofanywa umebaini kuwa wafanyabiashara wengi ambao hawajafikisha miaka 45 hupatwa na magonjwa ya moyo, vidonda vya tumbo na shinikizo la damu, kutokana na kuishi maisha ya wasiwasi.
Mtu anaweza kupata mafanikio katika biashara yake na kujisababishia matatizo makubwa ya afya yake. Itamsaidia nini kupata ulimwengu wote kwa utajiri na kupoteza afya yake? Hata kama amekuwa tajiri wa dunia inambidi alale katika kitanda kimoja kwa wakati na kula mlo mara tatu kwa siku, siyo kujishughulisha kupita kiasi na kusahau muda wake wa kula, pamoja na kulala.
Zaidi ya nusu ya wagonjwa wanaolazwa hospitalini huwa na matatizo yaliyosababishwa na hofu, wasiwasi, mshtuko, dukuduku na hali ya kutofanya lolote la maana. Mtu mmoja alisema kuwa kosa linalofanywa na wataalamu wanakuwa wanajitahidi kuponya mwili, badala ya kuangalia chanzo cha tatizo na kukishughulikia. Ingawa mwili na ufahamu ni mmoja na hautakiwi kutenganishwa.
Wasiwasi unaweza kukuweka kwenye kiti cha walemavu kutokana na ugonjwa wa viungo na ugonjwa wa baridi yabisi. Dk. Russell Cecil ameorodhesha vitu vinne vinavyochangia ugonjwa wa baridi yabisi kuwa ni: kuvunjika kwa ndoa, majanga ya kutokuwa na fedha pamoja na huzuni, upweke na wasiwasi pamoja na hali ya kutaka kupata faraja kuchukua muda mrefu tofauti na matarajio.
Tukutane wiki ijayo.
Makala hii imetafsiriwa kutoka kwenye kitabu kilichoandikwa na Dale Carnegie
lcyngowi@yahoo.com0713 3314550733 331455Mwisho

Thursday, July 10, 2008

Bill Gates


Wengine kufikia mfanikio kama aliyo nayo Bill Gates, huona ni ndoto na jambo lisilowezekana, kabisa, lakini amini inawezekana!

Friday, June 27, 2008

HATA WEWE UNAWEZA KUFANIKIWA

MAFANIKIO hutokana na jitihada katika maisha tunayoyaishi. Watu wengi wanaopenda kufanikiwa mara zote hutafuta mbinu mbalimbali ili kutimiza ndoto zao. Hivyo basi unatakiwa kuota ndoto ya mafanikio yenye malengo makubwa.
Binafsi ninaamini katika malengo hayo kuwa kuna mafanikio endapo utamaanisha. Wakati mtu anapoanza kuwa na malengo makubwa, anaanza kwa kufikiri jinsi Mungu alivyomwezesha katika jambo hata kufikia hatua na kufanikiwa.
Ndoto hiyo ya mafanikio haina gharama, ni jinsi ya unavyoweza kujipangia muda na ratiba zako. Kumbuka ukiwa na malengo ya mafanikio haitakugharimu chochote.
Unaweza ukawa na malengo ya kuanzisha mradi mkubwa pasipokuwa na fedha, inabakia kuwa ni ndoto tu. Mungu alianza kuumba dunia ikiwa haina kitu. Tunaweza kuwa na malengo makubwa ya mafanikio katika maisha yetu, haijalishi ni ya aina gani.
Unapokuwa na ndoto hiyo ya kutaka kufanikiwa, kamwe usiruhusu moyo wako kuvunjika au kuwa katika hali ya kukata tamaa na wasiwasi. Kwani hali hiyo itakudhoofisha na kukufanya usisonge mbele, bali urudi nyuma.
Unapohitaji jambo kubwa kutokea katika maisha yako unatakiwa kuwa na maono mapya. Kumbuka hata wewe unaweza ukawa na maono makubwa ya ajabu.
Haijalishi ni mtu wa aina gani, umetoka wapi au umepatwa na jambo gani, katika hali uliyonayo unaweza kuwa na maono mapya. Kumbuka malengo makubwa hayawi kwa watu waliofanikiwa, bali ni kwa wale wanaotaka kufanikiwa.
Vyovyote uwazavyo, ndoto inainua na kuweka kitu kipya katika maisha yetu, inatutengeneza na kutusogeza mbele, inatuwezesha kufikia malengo makubwa tofauti na ilivyokuwa awali. Inatuwezesha kufanya kitu kikubwa ambacho hatujawahi kukifanya tena kabla ya hapo.
Je, wataka kuwa fulani? Kusimama nje ya kusanyiko kubwa? Kukumbukwa? Hali hiyo inakuwepo ndani ya mioyo yetu inayodunda na kutaka kupata siri ya mafanikio.
Tunataka kuwa fulani. Inawezekana, ndiyo inawezekana. Mungu ametoa kwa kila mtu uwezo na vipaji mbalimbali. Wakati Mungu anakuumba alikupa kipaji na akasema kama utatumia kipaji ulichonacho atakiongeza, na kama hutatumia kipaji ulichonacho utakipoteza. Kukitumia kipaji chako au kukiachia ni juu yako wewe!
Dunia yetu imejaa vipaji vingi na uwezo ambao hautumiwi. Unatakiwa kulima kwa bidii, na kupalilia ili upate mavuno bora. Tumia kipaji chako kabla hujakipoteza.
Unaweza kudhani kuwa hauna kipaji chochote, si kweli, labda inawezekana haujagundua kipaji chako. Inawezekana umekiweka kipaji chako kabatini. Amini kuwa kila mmoja anacho kipaji chake alichopewa na Mungu.
Waweza kutumia kipaji ulichonacho au kukipoteza. Maisha yetu yamejengwa katika kanuni hiyo. Kuna mifano mingi ya kupoteza au kupata, hiyo ni kanuni ya kawaida.
Chukua hatua ambazo zitaifanya ndoto yako kuwa kweli. Ota ndoto yenye thamani katika maisha yako. Kama hauna malengo, haitawezekana matarajio yako kutimia. Ndoto inaanza unapokuwa na wazo. Kumbuka watu huvutiwa na wenye maono makubwa.
Chagua maono yenye matarajio. Baadhi ya watu wanapoteza muda wao kwa kuwa na malengo ambayo hayatawasaidia. Mfano, kuna kijana katika miaka iliyopita alisaidiwa kupewa ushauri baada ya kupoteza muda wake mwingi akifikiria ni jinsi gani ataweza kumpata mke wa jirani yake na kumfanya awe wake. Ndoto yake hiyo haikuwa ya thamani ya muda mrefu.
Wakati wazo linapokujia katika ufahamu wako, iulize nafsi yako maswali matatu. Je, jambo hilo litampendeza Mungu? Litawasaidia watu wanaoteseka? Kwa maneno mengine litakuwa msaada kwa watu? Litaleta mafanikio mazuri kwako? Kama jibu lako ni ndiyo katika maswali yote, utakuwa na maono yenye mafanikio.
Unapoamua kufanya jambo fulani, usijiulize ulize kuwa hii ni njia nyepesi ya mafanikio? Au ni njia rahisi? Inaweza kuwa na usalama? Haitakuwa na vikwazo? Hakuna utakachoshindwa utakapofanya bidii. Hakuna mwenye nguvu ya kuua ndoto yako, isipokuwa wewe mwenyewe.
Panga mipango vizuri kwa kuwa huwezi kujenga bila ramani. Huwezi kufanikiwa matarajio yako pasipokuwa na malengo makubwa. Ninamfahamu mtu aliyekuwa na maono makubwa lakini yalikuwa hayafiki mbali. Ni kwa sababu alikuwa hana ramani ya maono yake.
Hakikisha unatimiza ndoto uliyojiwekea. Malengo yako hayawezi kufanikiwa kama hujajitoa kufanya hivyo. Ili kufanikiwa katika mipango yako unahitaji juhudi na kufanya kazi kwa bidii ili upate mafanikio.
Amua pa kuanzia. Fanya uamuzi sahihi. Panga muda wa kuanza. Usitafute sababu ya kuacha kufanya malengo yako kwa muda ulioupanga. Katika dunia yetu kuna watu wengi wenye mipango mingi lakini hawaifanikishi. Jiondoe katika kundi hilo. Fanya kitu. Andika barua, piga simu. Anza hatua ya mafanikio.
Jiamini waweza kutimiza ndoto zako. Wakati unajaribu kupata mafanikio utaona kuwa ni kipindi kigumu kwako. Hali ya kukata tamaa inakuwepo katika moyo wako, ikisema jiondoe katika hatua ambayo unataka kuianza ya kupata mafanikio katika maisha yako, kataa.
Kama unakutana na kipindi cha majaribio katika biashara, ndoa, mambo yako binafsi, kwenye wingi wa watu au hali ya maisha uliyoizoea na uko tayari kukabiliana nayo, songa mbele usikate tamaa.
Unachofanya ni kujaribu kupata mafanikio, tena mafanikio makubwa. Katika kila mafanikio unayoyapata, kuna gharama ya kulipa. Kumbuka huwezi kupata ushindi bila kulipa gharama.
www.ngowil.blogspot.comlcyngowi@yahoo.com0713 3314550733 331455

JINSI YA KUDHIBITI HASIRA


WAKATI mwingine, hasira na kuchanganyikiwa kwetu kunasababishwa na matatizo yasiyozuilika katika maisha yetu ya kila siku.
Si kila hasira haina mpangilio, na mara nyingi inatokana na mambo ya kiafya, ni hali ya asili inayojitokeza katika mambo tunayokutana nayo.
Njia sahihi ya kukabiliana na tatizo linalokukabili, ambalo linakusababishia hasira, si tu kulenga katika kutafuta muafaka, lakini zaidi ni jinsi gani ya kulichukua na kukabiliana nalo.
Kutatua matatizo yanayokusababishia hasira kutaleta matokeo mazuri, lakini pia si kujiadhibu mwenyewe kama jibu halitakuja kama ulivyotarajia.
Watu wenye hasira mara nyingi hurukia jambo na kulifanyia maamuzi, lakini baadhi ya maamuzi hayo yanaweza yasiwe sahihi.
Kitu cha kwanza cha kufanya kama upo kwenye majadiliano makali ni kupunguza hasira na kufikiri juu ya majibu yako unayoyatoa.
Katika majadiliano hayo, kamwe usiseme kitu cha kwanza kinachokujia kichwani pako, bali tuliza hasira na fikiri kwa uangalifu juu ya kile unachotaka kukisema. Wakati huo huo, sikiliza kwa makini mtu mwingine anachokisema na jipatie muda kabla ya kujibu.
Pia sikiliza kwa makini, jambo lile linalokusababishia hasira. Kwa mfano, wakati mwingine unahitaji uhuru wako binafsi, wakati huo mke au mume wako anahitaji mawasiliano ya karibu na wewe.
Kama ataanza kulalamika kuhusu tabia zako, usilipize kisasi kwa kumfananisha na mfano usio mzuri, kwani hali hiyo italeta uharibifu katika uhusiano wenu.
Ni jambo la kawaida kwa mtu yeyote kujilinda wakati anapokosolewa, lakini akumbuke kuwa makini, asiruhusu hali ya kupigana.
Badala yake asikilize kinachojili juu yake. Ujumbe wa mtu huyo unaweza ukaudharau na kutoupenda.
Utahitaji uvumilivu kwa upande wako, na inahitaji kuvuta pumzi, lakini usiruhusu hasira yako au ya mshirika wako aache majadiliano yawe katika udhibiti. Kutulia kutaifanya hali kutokuwa ya uharibifu.
Wakati mwingine, ni vizuri kutumia ‘vichekesho’ kwani vinaweza kukusaidia kupunguza hasira katika njia mbalimbali. Kwa jambo moja la uhakika, ni kwamba vinaweza kukusaidia kuwa na mawazo yaliyo sawa.
Hivyo, wakati unapokuwa na hasira halafu unamwita mtu fulani jina au kumfananisha na kitu fulani, acha na ufikirie neno hilo linafananaje.
Fanya hivi pale jina linapokujia kwenye kichwa chako kuhusu mtu mwingine. kama unaweza, fikiria picha ya kitu halisi kinavyokuwa.
Hali hii itakuondolea hasira uliyokuwa nayo, na vichekesho mara zote vinakuondolea hali ile ya ghadhabu uliyonayo.
Ujumbe muhimu kwa watu wenye hasira kali, Dk. Deffenbacher anasema, watu wenye hasira wana tabia ya kujihisi kuwa wana haki, lakini mwisho wao hujikuta wakiwa wamejishushia heshima mbele ya jamii, lakini hawakutakiwa kutaabika kwa njia hiyo.
Labda watu wengine wangeweza kufanya hivyo lakini si wao.
Wakati unahisi kuwa unataka kuwa na hasira, mtaalamu huyo anashauri, jifikirie mwenyewe kama ungekuwa ni Mungu au kiongozi mwenye mamlaka ya juu, ambaye unamiliki mitaa, maduka na maeneo ya ofisi, mwenye maendeleo ya haraka na kuwa na taratibu zako katika hali zote wakati wengine wanatofautiana nawe.
Jambo unaloweza kulijua zaidi katika mawazo yako, unajiona kuwa wewe si mtu wa maana, unaanza kuona vitu ulivyonavyo havina umuhimu hivyo unakuwa na hasira kutokana na ukweli huo.
Kuna tahadhari mbili za kutumia vichekesho. Kwanza, usijaribu kuondoa aibu yako kwa kucheka, badala yake tumia kichekesho ili kujisaidia kukabiliana na hali hiyo. Pili, usifanye jambo lisilopendeza, kichekesho cha kejeli, hiyo ni aina nyingine ya mwonekano wa hasira isiyo na afya.
Hasira ni hisia ya kuiangalia kwa umakini, lakini mara nyingine inakwenda na wazo kuwa kama utaichunguza, itakuwezesha ucheke.
Wakati mwingine hasira Inabadilisha mazingira yako. Kwa mfano mazingira yetu yanatufanya kuwe na misuguano pamoja na ghadhabu. Matatizo na majukumu yanaweza kukuongezea uzito na kukufanya upatwe na hasira.
Ipe nafsi yako mapumziko. Hakikisha una muda wako binafsi na ratiba inayokuongoza kwa siku nzima. Mfano moja ni kwa mama anayefanya kazi, ambaye amekuwa na sheria yake kwamba, wakati anarudi nyumbani kutoka kazini, kwa dakika 15 za kwanza hakuna yeyote atakayezungumza naye, baada ya muda huo mfupi wa mapumziko anajisikia vizuri na kuanza kuwaandalia watoto wake mahitaji yao kwa furaha.
Njia nyingine za kukupa ahueni katika maisha yako, ni kuwapo matukio tofauti tofauti ambayo yatakuondolea tatizo la hasira ulilonalo.
Muda - Kama wewe na mke au mume wako mmekuwa na tabia ya kutofautiana wakati mnajadili mambo mbalimbali muda wa usiku, Inawezekana mnakuwa mmechoka, au mna mawazo, au labda ni tabia yenu halisi, jaribu kubadilisha muda wakati mnaongea mambo muhimu, badala ya usiku iwe asubuhi au mchana.
Epuka - kama watoto wako wanaonekana wana fujo kwenye chumba chao, hali ambayo itakufanya ukasirike, inabidi ulifanyie kazi suala hilo kwa kukaa kimya na kufunga mlango wa chumbani kwako.
Tafuta njia muafaka - kama kila siku asubuhi unakutana na msongamano wa foleni, hali inayokusababishia hasira, ipe nafsi yako kazi ya kusoma ramani ya kujua barabara nyingine zisizokuwa na foleni. Au tafuta njia nyingine muafaka.
Kuna njia mbalimbali za kukuonyesha kuwa una hasira. Mwili wako utakujulisha kuwa una hasira, kwa kuhema kwa nguvu, kubadilika uso wako, kukaza kwa misuli yako pamoja na kuonekana unaongea kama unanguruma, hata kwa mtu unayempenda.
Watu wengine wanazika hasira zao ndani. Kama unafanya hivi, utapata maumivu ya kichwa au tumbo. Na mara nyingine unaweza kuanza kulia peke yako.
Si vizuri kuficha hasira yako, inakubidi utafute njia ya kuitoa pasipo kujiumiza mwenyewe au kuwaumiza wengine.
Kuna njia za kufanya endapo utajikuta kuwa umepatwa na hasira. Njia hizo ni kuongea na rafiki yako unayemwamini, kufanya mazoezi, kucheza michezo mbalimbali, kuimba, kupalilia bustani yako pamoja na kufikiria mawazo mazuri.
Kwa mtu yeyote mwenye afya, haiwezekani asipatwe na hasira. Badala yake ukumbuke kuwa, unapatwa na hali gani unapokuwa na hasira.
Je, inafanya mazingira yako kuwa mazuri au mabaya? Usiruhusu hasira iwe bosi wako. Fanyia kazi jambo hilo.
lcyngowi@yahoo.comhttp://www.ngowil.blogspot.com/0713 3314550733 331455

KABILIANA NA CHANGAMOTO KATIKA MAISHA


KUNA wakati maisha yako yanaporomoka kutokana na kupatwa na misukosuko ya maisha kama vile kufiwa na mke, mume au mtoto wako, kusalitiwa na marafiki uliowategemea maishani mwako, kukimbiwa na mke au mume wako, kufilisika, kupoteza kazi uliyokuwa ukiitegemea, au daktari kukuambia kuwa ugonjwa unaokusumbua si rahisi kupona.
Hali hiyo inapokutokea, unajikuta unakata tamaa ya maisha na kujiona kuwa hustahili kuishi katika dunia hii inayokuzunguka, lakini kumbuka hiyo ni njia ya kupitia katika maisha haya tunayoishi.
Hivyo ni vizuri kumtafuta rafiki yako wa karibu au kiongozi wako wa dini kwa msaada zaidi. Kwani viongozi wa dini mara nyingi wamekuwa washauri wazuri katika maisha yetu ya kila siku.
Pia ukubaliane na hali ile ambayo huwezi kuibadilisha katika maisha yako. Na kukataa kuendekeza nafsi yako katika hali ya kujisikitikia kwani hali ya kujihurumia ni ugonjwa, kama vile acid.
Hali hiyo itakuondolea hadhi yako, itakuongezea sononeko na kukata tamaa. Itakuharibia uhusiano wako na wengine. Itakusababishia hali ya kuwa na chuki. Hakuna jambo zuri litakalokujia katika maisha yako kutokana na hali hiyo ya kujisikitikia.
Usichukue maumivu yako kwa wengine. Unaporuhusu maumivu huumizi watu wengine bali unajiumiza wewe mwenyewe. Iambie nafsi yako kuwa unahusika na vitendo au tabia zako mwenyewe. Hakuna atakayeiumiza nafsi yako ila wewe mwenyewe.
Usifanye ukaidi. Kubaliana na ukweli. Si wakati wote maisha yanakuwa sawa na ya kuridhisha. Haijalishi hali inayokutokea katika maisha yako, hali ya kukata tamaa, ndoto zako hazikutimia bado kuna tumaini katika maisha yako.
Baada ya usiku inakuja siku mpya, baada ya kipindi cha baridi huja kipupwe, baada ya mvua kubwa huja jua, baada ya dhambi huja msamaha, baada ya maangamizo nafasi nyingine hutokea.
Tuangalie mfano wa kijana mmoja wa miaka 15 ambaye alidondoka kutoka juu ya mti na kuvunjika mgongo. Kwa bahati aliokolewa akiwa mzima, lakini tokea kipindi hicho hakuweza kutembea tena. Alitembelea kiti cha watu wenye ulemavu, katika maisha yake yote.
Katika kipindi kigumu kama hiki, inakuwa ni rahisi kujihurumia na kujiona huna thamani tena katika maisha yako. Lakini haikuwa hivyo wa kijana huyu ambaye alivunjika mgongo. Kwani hakujiweka katika hali ya unyonge. Alitaka kuondoa hali aliyonayo na kuwa mtu mashuhuri. Kitu cha kwanza alicholenga kukifanya ni kumaliza masomo yake ya kidato cha sita. Alichohitaji ni kupata alama nzuri ili kufikia matarajio yake. Alimwambia mama yake anataka kuchukua masomo ya sanaa na uchoraji.
Kijana huyo ndoto yake ya maisha bora ilianza kung’aa tokea hapo na kufanikiwa katika maisha yake kutokana na kazi yake nzuri aliyoifanya. Kwani alikuwa mchoraji mzuri kiasi kwamba aliweza kupata mialiko mbalimbali kwenye vyuo vikuu vingine kutokana na bidii yake aliyoionyesha kwenye michoro aliyoichora. Baada ya masomo yake, kijana huyo alipata barua ambayo ilimtaka kwenda kufanya kazi ya kuchora katika kiwanda cha nguo.
Kazi hiyo imempatia pesa nzuri na kuweza kuisaidia familia yake. Kazi yake imempatia mahitaji yake yote ambayo alifikiri anahitaji. Anayapenda maisha katika hali ile aliyonayo. Kijana huyo ni mmoja wa watu wenye matarajio makubwa ukiachilia mbali hali aliyonayo ya kuwa mtu maarufu.
Kamwe usiishi maisha ya kushindwa. Unaona njia katika hali ya ugumu unayokabiliana nayo. Siri ya ushindi ni hii, usijione mshindwa, usikubali kushindwa kamwe usiishi katika hali ya kushindwa. Iambie akili yako kuwa hukuumbwa ili uwe mtu wa kushindwa.
Huwezi kuwa mtu wa kushindwa kama hujaruhusu hali hiyo katika maisha yako. Watu siku ya leo wanakata tamaa kutokana na sababu mbalimbali za maisha. Katika mtiririko wa mambo hayo, hakuna haja ya kukata tamaa katika maisha. Mtu ambaye hana kitu kinachofanya ajishughulishe anaona kuwa hana haja ya kuishi. Kila mtu anahitaji kitu cha kushikilia fikra zake na kumpa changamoto ili kufikia malengo anayotarajia.
Kumbuka, hakuna mafanikio pasipo kutaabika. Njia ya mapambano ni njia ambayo inamwezesha mtu binafsi kuongezeka, kukua, kuwa na maendeleo. Kila mtu anapitia maisha magumu kwa jinsi yake. Ni jinsi gani utakabiliana na hali hiyo ili uweze kuondokana nayo? Ni kwa kukataa hali hiyo na kusonga mbele.
Fanya jambo fulani kubwa ambalo hujawahi kulifanya kabla ya hapo. Unaweza kufanya mambo makubwa ambayo hukuwahi kuyafanya kabla ya hapo. Hiyo ni kwa sababu maumivu yako yamegeuka kuwa nyota ya mafanikio, tumia fikra zako, panua akili yako, jenga na tarajia. Uje na wazo kubwa, jambo fulani kubwa kuliko ilivyo kawaida yako. Songa mbele usikate tamaa mpaka pale matarajio yako yatakapotimia.
lcyngowi@yahoo.comhttp://www.ngowil.blogspot.com/0713 3314550733 331455

TAFUTA NJIA YA KUTATUA MATATIZO YAKO


NI jambo la kawaida kuchukua jukumu endapo kitu chochote kitakwenda vibaya, ambacho umekisababisha mwenyewe, lakini unapojenga tabia ya kujilaumu mwenyewe kwa kila jambo, unaweza kuwa na wakati mgumu katika hilo.
Unapojikuta ukijilaumu eti kwa kuwa watu wengine wana furaha katika familia zao au maisha yao, wana mafanikio kutokana na kufanya kazi zao kwa bidii, hali ya mahusiano katika familia zao imeimarika wakati kwako inasuasua, jaribu kutafuta njia nyingine ya kukuondolea hali hiyo inayokutesa.
Njia hizo ni pamoja na kuzungumza na familia yako, wazazi wako, watoto wako, wafanyakazi wenzako wale ambao wanaweza kukupa neno la busara, kiongozi wako wa dini, daktari wako pamoja na kusoma maandiko matakatifu.
Utakuta kuwa watu wengi hupenda kujilaumu kwa makosa mbalimbali wanayoyafanya ambayo hushindwa kuizuia hali hiyo na kumuathiri kisaikolojia. Kwa mfano, wazazi wanaweza kuwa imara na kuwashawishi watoto wao katika masuala ya elimu, lakini hawawezi kudhibiti mapungufu waliyonayo watoto wao. Unaweza kuwa imara kumdhibiti mume/mke au rafiki yako kuwa katika wakati mzuri, lakini huwezi kujihusisha katika jambo hilo moja kwa moja.
Lawama zilizopitiliza zinasababisha kukupokonya majukumu yako uliyonayo labda nyumbani, kazini au shuleni. Kuwa imara katika kudhibiti hali hiyo ili uweze kuondokana nayo. Kwani ikiendelea itakusababishia kukata tamaa, kuvunjika moyo na mwishowe kupatwa na msongo wa mawazo.
Kumbuka hali hiyo ukiiendeleza ni sawa na kujiongezea mzigo wa matatizo juu ya mabega yako. Jifunze kujisamehe hata kwa makosa yaliyokwisha kupita ambayo yanaumiza ufahamu wako.
Wengi wetu huwa mahakimu au washitaki juu ya makosa yao wenyewe, wakiendelea kujilaumu wenyewe. Unapokumbuka mambo ya aibu au ya kushindwa yaliyokupata zamani unazidi kuvunjika moyo na kujiona kuwa hustahili machoni pa watu. Hali hii itakuongezea machungu, wasiwasi, msongo wa mawazo pia inakuondolea ujasiri ulionao. Suluhisho ni kusahau yaliyopita na kuanza upya.
Ingawa inaweza kuwa ngumu kuzuia kumbukumbu za kushindwa kwako kukurudia, usizipe nafasi katika ufahamu wako. Kama Mungu au watu waweza kukusamehe si zaidi wewe mwenyewe kujisamehe? Achana na maamuzi mabaya uliyokwisha kuyafanya ya kibinafsi yaliyosababisha kuwaangusha marafiki zako, jamii au wewe mwenyewe.
Kabiliana na siku mpya kwani wewe si yule wa jana bali ni wa leo.
Pia usipende kuwalaumu watu wengine kwani ni sawa na kujiweka kwenye nafasi ya Mungu au hakimu, nafasi ambayo hata mmoja wetu haistahili. Tunapowalaumu wengine wakati mwingine tunataka kufunika mapungufu yetu wenyewe ambayo hatuko tayari kuyakabili.
Mfano utamkuta mwanamke akisema kwa ujasiri kuwa mumewe anatoka nje ya ndoa kwa sababu tu huchelewa kurudi nyumbani au kutumia pesa zake za mapato visivyo. Bila kujali kuwa mumewe anafanya kazi saa za ziada au anahifadhi fedha zake ili aweze kumnunulia mkewe zawadi nk. Yawezekana kuwa mwanamama huyu amekuwa akibeba hisia hizo za shutuma juu ya mumewe kwa muda mrefu kiasi cha kuweza kusababisha hata uhusiano wao kuyumba au ndoa yao kuvunjika. Lakini ukichunguza undani wa shutuma hizo huweza kukuta ni hitimisho iliyojaa hisia potofu.
Lawama yaweza kusababisha watu kufikia hitimisho lisilo sahihi hata kubeba uchungu kwa muda mrefu kiasi cha kuvunja ndoa/unyumba. Lawama huweza kusababisha hali ya maelewano na masikilizano kuwa kutoelewana au kutosikilizana.
Njia mojawapo ya kusaidia ndoa zenye msukosuko ni kumsaidia kila mhuhusika kuacha kumlaumu mwenzie au kuacha kumtazama mwenzie kwa jicho la lawama ila ajitazame mwenyewe na kuona ni wapi alipofanya makosa na nini anaweza kufanya ili kurekebisha ndoa yao.
Njia nyingine ni kumfanya kila mmoja aweze kukiri makosa mbele ya mwingine na kusema samahani, nimekosa. Katika hatua hiyo uhusiano uliovunjika unaanza kuimarika tena.
Hata mwanadamu wa kwanza alianza kwa kumlaumu mwanamke kwa kuelezea makosa yake kwa muumba wake. “Huyu mwanamke ndiye aliyenisababisha.” Mwanamke naye alitupa lawama zote kwa nyoka. “Nyoka ndiye aliyenisababishia kufanya hivi.”
Tunapowalaumu wengine tunaongeza ukubwa wa tatizo badala ya kulitatua. Hii inaonyesha kuwa aliye mwepesi kulaumu wengine ndiye mwenye makosa mengi zaidi. Waungwana ndiyo wanaoweza kukiri makosa yao au kushindwa kwao mbele ya jamii. Mtu muungwa ni yule aliye mwepesi kusema nimekosa.
Shinda lawama kwa kukiri makosa yako. Acha kufunika makosa kwani yataongeza ugumu wakati wa kutatua. Kuna njia moja ya kuweza kusafisha dhamira inayokushitaki nayo ni kukiri makosa. Acha kutafuta watu wa kulaumu, kabiliana na makosa yako mwenyewe. “Kubali makosa yako utapona. Kiri maovu utasamehewa.”
Tukumbuke tabia hiyo huanza tokea mtoto anapokuwa na umri mdogo. Kwani anapokimbia na kujigonga mahali hulaumu kile kilichomgonga, mfano kama amejigonga kwenye ukuta husema kuwa ukuta ule mbaya umemwumiza.
Tukumbuke kuwa lawama si kitu cha kufurahisha kwani huweza kusababisha hasara zaidi. Kwa mfano waweza kumwona mtu akigonga gari lake kwa hasira ukafikiria kuwa amechanganyikiwa kumbe analaumu kwa nini limeharibika au kwa nini limemwishia mafuta.
Kila wakati mambo yanapoharibika ni kasumba kwa mwanadamu kutafuta sababu ya lawama au mtu wa kumlaumu.
Mara nyingine tunapomwona kilema, kipofu au kichaa swali kubwa watu wanalojiuliza ni nani anayestahili kulaumiwa. Wengine humlaumu Mungu, wengine hulaumu uumbaji na wengine huwalaumu wazazi. Tunachotakiwa kujiuliza ni jinsi gani ya kumsaidia mtu huyo? Ni namna gani ya kumtoa katika hali ile aliyonayo sasa? Ni namna gani tunaweza kuboresha mazingira yanayomkabili. Ni jinsi gani twaweza kumfanya aanze upya na kwa ubora zaidi?
Ingawa lawama ni mchezo uliozoeleka na watu wengi siku hizi, bado ni mchezo ambao huleta athari kubwa sana. Siku zote lawama haiponyi bali huumiza moyo. Haijengi uhusiano bali huuvunja, haiunganishi bali hutenganisha, haijengi bali hugawanyisha na haitatui matatizo bali huongeza ukubwa wa matatizo.
lcyngowi@yahoo.comhttp://www.ngowil.blogspot.com/0713 331455, 0733 331455

Twitter Facebook