Monday, June 16, 2008

UMUHIMU WA NENO SAMAHANI

SAMAHANI hutumika kama njia ya kuomba kusamehewa, lakini siku hizi neno hilo hutumika katika maana ya vitu vingi.
“Mara zote inaonekana kwangu neno samahani kama neno gumu kulitamka,” anasema Elton John.
Lakini katika miaka ya sasa, neno hilo huwa ni jepesi kulitamka kwa kuwa limepoteza thamani yake ya awali.
Mara nyingi baadhi ya watu huamua kutenda jambo la kumsikitisha mtu kwa kudhamiria na kisha kukimbilia kusema samahani kwa hilo alilolitenda.
Samahani ni neno la kiasili ambalo hutumika kuelezea masikitiko kwa kufanya jambo lisilopendeza.
Siku hizi, tunatumia neno samahani si tu kuelezea masikitiko yetu kutokana na mazoea, lakini pia hutumika neno hilo kama kumwomba mtu arudie maneno aliyokuwa akikueleza.
Mfano ‘samahani, sijakupata vizuri ulichosema.’ Inaonyesha kuwa katika Bara la Ulaya neno hili hutumika mara nyingi zaidi kuliko katika Bara la Afrika.
Asilimia 86 ya watu wanaotumia neno hili hulitumia kwa mzaha, kama neno rahisi kulitamka na kama njia inayofaa ya kuomba samahani kwa tabia mbaya wanayoifanya.
Tuangalie sababu tano kuu zinazomaanisha neno samahani: Sababu ya kwanza ni pale tunapokuwa hatuna muda wa kuzungumza na mtu au kufanya kitu. Mfano (samahani, sitakuwa na muda wa kuzungumza kwa sasa).
Ya pili ni kuomba radhi kwa niaba ya mtu mwingine, kama kwa watoto wetu, kwa rafiki zetu au kwa wafanyakazi wenzetu. (samahani, Jimmy mara zote ni mtu wa vurugu).
Ya tatu ni pale ambapo hujaweza kumsikia mtu akiwa anazungumza kwa ufasaha, hivyo unamwomba arudie. (samahani, unaweza kurudia?).
Nne, ni pale unapotaka jambo fulani lirudiwe kuelezwa kwako (samahani, sina uhakika na kile ulichomaanisha).
Mwisho ni wakati pale tunapojihisi kuwa tunahitaji kuomba radhi kwa kumsaliti mtu, na kumfanya mwingine asifanikiwe, hatuna budi kuomba radhi. (nimekosa).
Pia tunatakiwa kusema samahani kwa wabia wetu, kama vile unavyosema kwa mkuu wako wa kazi.
Utafiti uliofanywa umebaini kuwa, asilimia 27 ya matumizi yetu kwa neno samahani tunatumia kusema hivyo kwa wabia wetu, asilimia 19 linasemwa kwa wageni, asilimia 14 kwa watoto wetu, asilimia 14 kwa wafanyakazi wenzetu, asilimia nane kwa rafiki zetu, asilimia tano kwa wazazi wetu, asilimia tatu kwa ndugu zetu na kama asilimia moja kwa wakuu wetu wa kazi (bosi).
Inaonyesha kuwa Waingereza wamekuwa ni watumiaji wazuri wa neno hilo. Hujulikana kama taifa la sorry-sayers.
Inaelezwa kuwa Waingereza wamekuwa wakitumia neno hilo katika mazingira mbalimbali, kwa mfano ‘samahani, ninaweza kusema chochote?’ Au samahani umenipa pungufu ya fedha uliyostahili kunirudishia.
Tunaona ni kwa jinsi gani neno samahani linakuwa ni rahisi kulitamka, kwa kuwa linatumika kama mhimili, pia njia ya kukiri makosa uliyoyatenda.
“Kusema samahani mara kwa mara ni tabia iliyojengeka kwa Wazungu, neno samahani linatamkwa kwa adabu, liko pale kwa ajili ya mshikamano wa kijamii.”
“Pia tunasema samahani mara nyingi kama tunahisi kuwa tunalaumiwa kwa kitu fulani - ambayo hali hiyo inakusababishia ‘maumivu ya ndani.’
Wakati mwingine tunafikiri kuwa neno hilo linaonyesha kuwa tuna tabia nzuri, lakini inaweza kuwa tofauti na fikra zetu ila ni hali tu ya kuonyesha kuwa unajali.
Peter Carvin, anasema kuwa, baba yake alimweleza kuwa neno samahani linamaanisha kutorudia kosa lile lile, tofauti na miaka ya sasa limeonekana kuzoeleka vinywani mwa watu wengi na pengine unakuta mtu hamaanishi kutoka ndani ya moyo wake.
Laura anasema kuwa anachukia tabia ya baadhi ya watu ambao wanatenda ukatili wa kukusudia kwa wenzao kwa nia ya kuomba samahani baada ya tendo hilo. Ni vizuri wakafikiria kwa upya tabia hiyo isiyopendeza.
Hivyo ushauri mzuri ni kwamba pamoja na neno hilo kuelezwa katika maana nyingi, lakini ile iliyozoeleka hasa ni pale unapotenda jambo halafu ukajisikia kuwa na hatia katika moyo wako, hivyo basi hali hiyo inapokutokea ni bora ukaomba msamaha kwa yule uliyemtendea isivyostahili.
Unapokuwa mtu wa kukubali kuwa umekosea na kuomba samahani kwa yule uliyemuumiza, aidha kwa maneno yako au matendo yako, itakuwa faraja kwake na kuona kuwa unajali kutokana na hali ile ya kukubali kushuka na kusema neno samahani, hivyo naye ataonyesha hali ya kupokea msamaha wako.
Inakuwa haipendezi endapo utamuudhi mtu halafu ukatamka kwake neno la msamaha kisha akagoma kukusamehe, ninaamini vitabu vyote vya dini vinasisitiza neno msamaha. Hivyo basi kama mhusika uliyemuudhi hajakubali ombi lako, inategemea umelitoa vipi.
Yawezekana kabisa umelitoa kwa kejeli, mzaha au dharau ndiyo maana mhusika hakulikubali ombi lako hilo, hivyo ni vizuri ukalitoa neno hilo kwa kuonyesha hali ya kujali na kujutia kile ulichokitenda.
Tukumbuke tuwapo majumbani mwetu, shuleni, vyuoni na kazini mara zote vikombe viwili vikikaa pamoja ni lazima vigongane, hivyo ni vyema pale unapogundua umemfanya mtu akaumia katika nafsi yake kutokana na matendo au maneno yako, usiache kusema neno hilo ili liwe faraja kwake.
lcyngowi@yahoo.comwww.ngowil.blogspot.com0713 3314550733 331455

0 Maoni:

Twitter Facebook