Sunday, June 15, 2008

EPUKA KUINGILIA MAMBO YASIYOKUHUSU

KARIBUNI tena wapenzi wasomaji wa safu hii ya kila Alhamisi. Wiki iliyopita tuliendelea kuzungumzia kanuni au mbinu mbalimbali za kuishi na watu vizuri, leo tunafikia tamati ya mada hii. Mpaka kufikia hapa tutakuwa tumeona kanuni au mbinu 56 za kuishi vizuri na watu.
Epuka tabia ya kuaibisha wengine. Unapomwona ndugu yako, rafiki yako, mfanyakazi mwenzako au jirani yako ametenda jambo ambalo halijakupendeza, mwite pembeni na kumjulisha kuhusu jambo hilo.
Usipende kumwaibisha ndugu, rafiki, jirani au mfanyakazi mwenzako kwani tabia hiyo haijengi bali inabomoa kwa kuwa hata wewe ukifanyiwa hivyo hutafurahia. Kumbuka tabia nzuri inaleta mahusiano mazuri.
Mtu mstaarabu anapochukia tabia fulani iliyofanywa na mtu fulani, humwita na kumrekebisha na si vinginevyo. Hatapiga mbiu na kuwakusanya watu ili asimulie tabia hiyo mbaya ya mwenzake kwa kuwa anajua kufanya hivyo si kumwelimisha huyo anayestahili kurekebishwa bali ni kumwaribu zaidi.
Jifunze kuamini watu. Tabia ya kutomwamini mwenzako si nzuri, japo kuna wakati unatakiwa kuwa mwangalifu katika kumwamini kila mtu. Pima jambo lenyewe na uzito wake, kisha chukua hatua za tahadhari mapema ambazo hazitakuharibia.
Usionyeshe kwamba huna imani na wenzako, jitahidi kuwa makini katika mambo yako yote na kuwa mwangalifu.
Jitahidi kujua tabia za watu wanaokuzunguka na mienendo yao kwa ujumla. Uaminifu wao kwako na mambo yanayofanana na hayo.
Kwa kufanya hivyo, utagundua hata yule mtu asiye mwaminifu hatatenda jambo baya alilokusudia kutokana na hali ya kumwamini uliyoionyesha kwake.
Jifunze kujali na kusikiliza shida na matatizo ya wengine. Hapa duniani huwa hatufanani kwa kila kitu. Kuna weupe kwa weusi, warefu kwa wafupi, wembamba kwa wanene, matajiri kwa maskini, pia wengine wana uwezo wa kustahimili shida walizo nazo, wengine huogopa shida na matatizo wanayokumbana nayo, ili mradi tuko katika viwango tofauti tofauti vya maisha.
Hivyo basi, mtu anapokuja kwako na kukueleza shida yake, kwanza jua amekuheshimu na anahitaji msaada kutoka kwako. Ni vizuri ukampokea kwa upendo na kusikiliza shida yake na kumpa msaada anaohitaji.
Yamkini anahitaji msaada wa faraja, hali na mali hilo lisikutie shaka. Msikilize pale unapoweza kumsaidia fanya hivyo, pale unaposhindwa jitahidi kumpatia msaada huo kwa kumwelekeza maeneo ambayo ataridhika kuwa atafanikiwa.
Usitoe siri za shida na matatizo ya watu wanaokujia kukueleza.
Jifunze kutunza siri za watu wengine. Tukiangalia katika maandiko matakatifu katika kitabu cha Mika 7:5 kinasema kuwa “msimwamini rafiki, msimwekee kiongozi tumaini, ilinde milango ya midomo ya kinywa chako ili mkeo alalaye kifuani mwako asijue habari.”
Katika maandiko hayo, inaonyesha ni jinsi gani unatakiwa kuwa mtunza siri, yaani hata mtu wako wa karibu kabisa hatakiwi kujua isipokuwa kwa sababu maalumu.
Usipende kuingilia mambo ya wengine yasiyokuhusu kwani itakuletea matatizo katika maisha yako. Ukisikia jambo lolote ambalo halikuhusu, usiongeze neno wala kupunguza, waachie wale yanayowahusu wamalize mambo yao.
Mfano mume na mke wanaweza wakagombana na wewe ukajiweka mstari wa mbele kwamba unajua kisa cha ugomvi huo na mwanzilishi wa ugomvi unamjua, hivyo ukawa unatetea upande mmoja. Je, watakapopatana wewe utajisikiaje?
Au wakati mwingine marafiki wanaweza kugombana na wewe ukasimama kidete ukimtetea mmoja wao. Je, wakipatana utajisikiaje? Usiingilie mambo yasiyokuhusu, ili kuepuka kutokuelewana nao watakapopatana.
Fanya hivyo pale unapoombwa kuwapatanisha na si kuonyesha kuwa uko upande fulani. Tumia busara zaidi kuliko kukosoa, kutukana au kumdharau mmoja ya hao wasioelewana.
Kila unapaoandika barua kumbuka usitukane, kulaumu, kumchambua mtu au kumgombeza.
Kumbuka barua ni maandishi yenye ujumbe yanayopelekwa kwa mtu mwingine kwa njia ya mkono au kupitia posta. Ni kama waraka fulani pia watu wamezoea kusema kuwa barua ni nusu ya kuonana.
Sasa basi kama barua ni nusu ya kuonana kwa nini upoteze muda wako wa kuiandika kwa nia ya kutukana, kulaumu, kumchambua mtu au kumgombeza? Kama unataka kufanya hivyo, ni vizuri ukamtafuta mhusika na kumwelimisha kuwa mambo anayoyafanya au unayoyasikia juu yake si mazuri hivyo ajirekebishe, hiyo itamsaidia.
Unapoandika barua ya kumtukana mtu, anaweza kuitumia kukushtaki na kufikishwa mahakamani. Mara zote jifunze kuandika barua za kumsalimia mtu kwa kumpa changamoto mbalimbali za maisha au masomo kwa ujumla.
Usiandike barua ukiwa na msisimko, hasira, upendo au furaha sana, tulia kwanza, kwani kwa kufanya hivyo itakupa upeo wa kufikiri zaidi.
Ukiandika barua ukiwa katika hali ya hasira unaweza ukajikuta barua nzima unaiandika kwa kutukana badala ya kutaka muafaka wa jambo linalokutatiza, ukiandika barua ukiwa na furaha sana pia unaweza ukamaliza barua nzima bila kueleza nia na madhumuni yako.
Unapoandika barua muhimu usitume mara moja, tulia kwanza, pata ushauri. Ni kweli kila unapoandika barua muhimu ni vizuri kutulia na kupata ushauri kwani kama haujatulia, wakati mwingine unaweza ukasahau vitu muhimu ambavyo ulitakiwa kuviandika.
Mfano unaandika barua ya kuomba kazi ni muhimu kutulia na kujiuliza ni kitu gani ulichosahau katika barua hiyo, pia si vibaya kupata ushauri kwani bila kufanya hivyo unaweza ukakosa kazi uliyoiomba kwa kutokuainisha mambo muhimu ambayo ulikuwa haujui kama yanahitajika.
Jifunze kujibu kila barua. Ukiwa mtu wa kujibu kila barua unayoipata, itakuongezea marafiki wengi kwa kuwa wataona kuwa ni mtu unayejali. Hata ukiwa na kampuni yako utakapohitaji wafanyakazi, kila atakayeandika barua ya kuomba kazi kwako, iwe amepata nafasi hiyo au ameikosa, ni vizuri kumjulisha juu ya hilo.
Kama amekosa ni vizuri kumpa matumaini kuwa asikate tamaa ajaribu tena wakati mwingine.
0713 331455
ngowi2001@yahoo.com

0 Maoni:

Twitter Facebook