Tuesday, October 28, 2014

TCRA KUTOA MWONGOZO KWA WATANGAZAJI KWENYE UCHAGUZI


MAMLAKA ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), imeandaa rasimu ya mwongozo utakaofuatwa na vituo vya utangazaji katika kipindi cha uchaguzi wa serikali za mitaa, wabunge na raisi lengo likiwa kuweka usawa na uwazi katika kipindi cha uchaguzi, wakati wa uchaguzi na baada ya uchaguzi kufanyika.
Mwenyekiti wa Kamati ya Maudhui ya mamlaka hiyo Margaret Munyagi alisema hayo katika mkutano wa kupokea maoni ya wadau juu ya utaratibu wa kuandaa na kurusha vipindi vinavyohusu vyama vya siasa wakati wa uchaguzi.
Alisema kuingia kwa mfumo wa vyama vingi vya siasa nchini 1993, kulienda sambamba na kuanzishwa kwa vituo binafsi vya utangazaji, hivyo ongezeko la vituo hivyo limekuwa ni kichocheo cha kukuza demokrasia, kuboresha amani, kudumisha umoja na mshikamano wa taifa.
“Kama mnavyojua nchi yetu inategemea kuingia kwenye kipindi cha uchaguzi wa serikali za mitaa, wabunge na rais ifikapo 2015. Uchaguzi ni mchakato muhimu sana katika kukuza na kuimarisha demokrasia ya n chi husika,” alisema.
Munyagi alisema kuwa, vipindi vinavyotangaza masuala ya uchaguzi vinahitaji umakini mkubwa pamoja na uwepo wa mizani katika muda wanaopewa vyama vya siasa, kuwepo kwa uwazi, kufuata sheria na kanuni husika.
Alisisitiza kuwa, kukamilika kwa mwongozo huo kutawasaidia watangazaji na waandaaji wa vipindi kuepuka kufanya makosa ambayo kama yasipodhibitiwa yanaweza kusababisha uchochezi na kuleta mifarakano miongoni mwa jamii.
Alisema, tofauti na mategemeo hayo baadhi ya vyombo vya utangazaji vimekuwa vikikiuka sheria na kanuni kwa kuwa maudhui yanayotangazwa hayazingatii maadili ya kitanzania badala yake vimechangia kuharibu utamaduni wetu.
Pia vingine vimesahau madhumuni ya kuanzishwa kwao na wajibu wao katika jamii, hivyo kujiingiza katika masuala ya uchochezi pamoja na uvunjifu wa amani na utulivu.
Awali Mkurugenzi wa Utangazaji TCRA, Habbi Gunze alisema kuwa mpaka sasa kuna vituo vya redio 95, pamoja na  vya televisheni 28 nchini, hivyo ni bora vikapata mwongozo maalum wa namna ya kuandika habari za uchaguzi.


mwisho

Twitter Facebook