KARIBUNI wapenzi wasomaji katika safu hii ya Maisha Yetu inayokujia kila wiki. Ninawatakia heri ya mwaka mpya 2008 uwe wa mafanikio.
Wiki iliyopita tuliangalia maana ya upendo, leo tutaangalia vitu vinavyosababisha kukosekana kwa upendo kwa watu wapendanao.
Kijana Jerry Bright anasema kuwa, utafiti wake alioufanya amegundua kuwa kwa watu wapendanao wanapokosa muda wa kuwa pamoja, hali hiyo huchangia sana upendo wao kuvunjika au kuhitilafiana. Kwa kuwa inaonyesha kuwa lazima kutakuwa na chanzo cha hali hiyo kuwepo, aidha mmoja wa marafiki kuamua kujipa shughuli nyingi ilimradi amvunje moyo rafiki yake kwa makusudi yake maalum.
Pamoja na suala hilo la kukosa muda wa kuwa pamoja, Bright anaeleza kuwa wakati mwingine heshima hukosekana kwa watu wapendanao, si lazima kwa wapenzi ambao hutarajia kuoana hata kwa wale ambao ni marafiki wa kawaida kama mwanamke kwa mwanamke mwenzake au mwanaume kwa mwanaume mwenzake au marafiki wa jinsia tofauti.
Anasema heshima ni kitu cha bure na si cha kulazimishwa. Hivyo basi, ni vizuri kwa mtu awaye yote kumheshimu mkubwa wake, au mdogo au hata kama mtu huyo unalingana naye, kwani huchochea upendo wa kweli kati yao.
Endapo heshima itakosekana lazima kutakuwa na mpasuko mkubwa wa upendo. Hata kama kama kuna jambo la kutatiza likiwa limejitokeza kwa watu wapendanao, ni vizuri likatafutiwa utatuzi wa haraka kwani hali hiyo uchangia kuongezeka kwa upendo kwa kuwa mmoja wao ameonyesha hali ya kujali.
Pia kama mmoja wa wapendanao hataonyesha hali ya kujali kwa mwenzake endapo anaugua, amefiwa, au amepatwa na jambo lililomvunja moyo na kumkatisha tamaa, hali hiyo itachangia pendo lililokuwepo kati yao kutoweka mara moja kwa kuwa si hali ya kiubinadamu.
Hivyo kama hayo yote yatakosekana kwa watu wapendanao, itajitokeza hali ambayo itasababisha mawasiliano kupungua, ugomvi kuwepo, na hali ya kutokujali kama kuna mtu ambaye unaweza kumshirikisha jambo lako upatapo na msuko suko.
Hali nyingine itakayojitokeza ni kukosa uangalifu kwa wapendanao, kutokuelewana, kutokuheshimiana. Pia ukosefu wa kusimamia mambo mbalimbali kwa wapendanao.
Kumbuka suala la talaka linapojitokeza na matatizo katika mahusiano ni chanzo cha kukosa upendo.
Kijana Benson anasema kuwa yeye na mke wake wameishi katika ndoa miaka 9, wamebahatika kupata watoto wawili. Mke wake amewahi kumwambia kuwa hana furaha na anafikiri kuwa wangeachana. Anasema kuwa hakushangaa sana kusikia maneno hayo kutoka kwa mkewe kwa sababu alimwona hana furaha kabla na kuna wakati hali hiyo ilikuwa ikimtokea.
Alikuwa akilalamika kuwa kila kitu ninachomfanyia si kitu, na hajisikii kumpenda. Anasema kuwa anajutia kuolewa naye. Anasema kuwa alifikiri kuwa mambo yangekwenda vizuri kila wakati kuwa na matukio makubwa katika maisha kama kuoana, watoto n.k. Benson anasema wamekuwa wakienda kwa washauri ili apatiwe msaada na amekuwa akichanganyikiwa afanye nini. Anasema yeye anampenda mkewe kutoka ndani ya moyo wake na hapendi kuachana naye. Pia anaogopa madhara yatakayowatokea watoto wao ambao bado ni wadogo. Anasema na ushirika mzuri katika mambo yote isipokuwa eneo la upendo. Amekuwa mbali na hana uamuzi katika kujamiiana, amekuwa wa kulaumu na kusema kuwa hamvutii.
Watu wengi wanakosana kutokana na amri. Mara nyingi wanaume ndio wamekuwa watoa amri katika familia zao, japo pia wapo baadhi ya wanawake ambao hupenda kuwa watu wa amri kila wawapo nyumbani kwao.
Mary anasema, alifikiri mume wake hana kasoro, atakuwa na njia nyingi za kumpa furaha, atamtimizia mahitaji yake, mwenye uwezo wa kiuchumi na mtafutaji, mtoaji, lakini yale yote aliyokuwa akiyatarajia kwa mumewe yamekuwa tofauti, amekuwa mtu wa kutoa amri, si wa kuaminika, mfano: "Ninakupa dakika kumi na tano ya kubadili nguo zako na kutengeneza nywele zako, hakikisha chakula cha jioni kinakuwa tayari kabla sijarudi nyumbani."
Kwa maelezo ya Mary, ana mambo mengi ya kuzungumza na mumewe, lakini mara zote amekuwa akielezea matukio ya siku nzima anayoyafanya awapo kazini kwake, na hana nafasi ya kumsikiliza. Mary amechoka pia kutokana na amri za mumewe na anataka kuwa huru.
Lakini Mary kwa upande mwingine anakosea. Anatakiwa awe wazi kwa mume wake na kumweleza yale asiyoyapenda ambayo mumewe huyo huyafanya aidha kwa kujua au kutokujua. Endapo angemshirikisha mumewe hali anayojisikia, ninafikiri kuwa asingekuwa na uamuzi wa kutaka kuwa huru, ili hali hiyo imsimtokee tena.
Kiongozi mmoja wa dini anasema kuwa hali kama hiyo kwa wapendanao ni kosa. Anahoji kuwa mtu anawezaje kumfanya mke wake kama mtumwa? Anasema hata kwa watu ambao hawajasoma hawawezi kuwa na tabia hiyo kwa wake zao. Anasema kuwa mume anatakiwa kumsikiliza mke wake kama mkewe anavyomsikiliza ndipo maisha yao yatakapokuwa na furaha.
Kuna wanaume wengi wenye tabia kama hizo, wanapenda kutoa amri na wanapenda mambo yafanyike kama wanavyotaka wao. Mara zote ndio wanaotoa maamuzi ya mwisho.
Kama mwenzako hatakuwa na mawasiliano mazuri nawe ni hakika utajisikia vibaya. Hali hiyo inamfanya mwanamke kukata tamaa na kuvunjika moyo. Ni vizuri ukamweleza ajirekebishe kwani wewe ni mke wake na anatakiwa akujali.
Inaonekana kuwa kama mwanamke ni mtumwa wa sheria za mumewe. Jaribu kuzungumza naye kuhusu hali hiyo ili irekebishike. Kama kusipokuwa na masikilizano ni hakika uhusiano huo utavunjika.
Kama ilivyoelezwa hapo juu, usiache kuongea naye kuhusu tatizo hilo juu ya tabia hiyo, inawezekana ana msongo wa mawazo katika kazi yake na hajielewi kama yuko hivyo.
Tukutane wiki ijayo.
lcyngowi@yahoo.comwww.ngowil.blogspot.com0713 3314550733 331455
Monday, June 16, 2008
VITU VINAVYOSABABISHA KUKOSEKANA KWA UPENDO
Posted in:
0 Maoni:
Post a Comment