Wednesday, April 29, 2009

BOSI WAKO ANAPOKUVUNJA MOYO USIKATE TAMAA

KWA mara nyingine tena, ninapenda kuwakaribisha wasomaji wangu katika safu hii inayokujia kila alhamisi, ili uweze kuelimika kwa kupata mawazo mbalimbali.
Leo tutaenda kuangalia njia mbadala za kufanya baada ya kukumbana na misukosuko mbalimbali kutoka kwa bosi, mkuu wa kitengo au mkurugenzi wako.
Watu wengi wamekuwa wakivunjika moyo na wengine wao kuamua kuacha kazi eti kwa sababu bosi wake hampendi, lakini ikumbukwe kuwa hiyo siyo suluhu kwako kwani kuna hatua mbalimbali za kufuata kabla ya kuchukua uamuzi wako ulioukusudia.
Je umeshoka? Umekata tamaa? Huna furaha? au Hupati hamasa katika kazi yako? Pia inawezekana kwamba mawasiliano yako na bosi wako yanakufanya uwe mnyonge, kwa kuwa ni mwonevu, mkatili na mkandamizaji. Anaingilia faragha yako, anakudhibiti, mchokonoaji au kukuona huna maana.
Lakini bosi huyo huyo hupata sifa kupitia kazi zako nzuri unazozifanya, kwa kuwa hakujali wala kukuthamini, kamwe hawezi kukupa habari nzuri kuhusu utendaji wako. Badala yake anakutia katika msukosuko kikazi, pia anashindwa kukusaidia ili uweze kukamilisha kazi yako.
Huyo ni bosi ambaye siye mtendaji mzuri, mara zote hupenda kuchongea wafanyakazi wake na kuwatafutia sababu ya kuwapa onyo. Kutokana na hali hiyo anakuwa ni bosi mwenye upungufu katika kazi yake, hana sifa ya kuwa kiongozi bora. Uwepo wa mameneja au mabosi kama hao ni mkubwa na hiyo ndiyo changamoto kubwa waliyonayo waajiri wengi. Haijalishi ni tabia gani mbaya ya bosi wako, unapojua hali hiyo usikate tamaa endelea kufanya kazi yako kwa bidii na utayaona matokeo.
Sasa basi, unapokabiliana na hali kama hiyo, anza kufanya kampeni ya kufanya bosi wako atambue kuwa yeye ni kikwazo katika utendaji wako.
Kumbuka kuwa mabosi wengi hawatambui kuwa kushindwa kutoa maelekezo au kukupa taarifa za utendaji wako inamfanya yeye kuonekana kuwa hawezi kuongoza. Mara nyingine anaweza kufikiri kuwa ana mamlaka zaidi ya wafanyakazi wake. Kwani bosi au meneja ambaye amekuwa akitoa maelekezo mengi ambayo hushindwa kuyasimamia, hujihisi kuwa hayuko salama.
Mara nyingine hali hiyo hutokea kwa kuwa bosi huyo amekuwa hana elimu ya kuwa bosi, au ni makusudi yake tu. Matokeo yake wafanyakazi mara zote humcheka na kumdharau kutokana na tabia yake mbaya.
Huyo bosi ambaye si mtetezi wa wafanyakazi wake au mbaguzi kwa baadhi ya wafanyakazi, hawezi kuona thamani yako. Hata kama utatumia muda wako wa mapumziko na kuongeza bidii katika kazi.
Hivyo njia ambazo unaweza kuzifanya ili bosi wako ajue kuwa umebaini hali hiyo, ni vema kumfuata na kuzungumza naye, na umwambie unahitaji kwake kupata maelekezo, kuhusu utendaji wako na msaada wake.
Kuwa mpole na ulenge kwenye hitaji lako, ili bosi huyo aweze kujijua na kuamua kubadilika.
Muulize ni jinsi gani unaweza kumsaidia kufikia malengo yake. Hakikisha unamsikiliza vizuri na kutoa msaada unaohitajika.
Tafuta busara nyingine kutoka kwa mabosi wengine au watu wenye ujuzi wao, ili uwe na elimu nzuri ya kuzungumza na bosi huyo, na kuongeza nafasi ya ujuzi wako.
Kama utachukua hatua hizi na hazijafanya kazi, nenda kwa bosi aliye juu ya huyo na kuomba msaada. Au unaweza kwenda kwa mkuu anayehusika na masuala ya wafanyakazi kabla hujafika kwa mkurugenzi mtendaji, uzungumzae naye na kupata ushauri zaidi. Uelewe wazi kuwa bosi wako wa awali hatakusamehe, hivyo hakikisha unafanya kile unachoweza, kabla hujafikisha jambo hilo juu zaidi.
Endapo hutaweza kupata msaada kutoka kwa mabosi wako uliowaeleza, ya kutatua tabia mbaya za bosi wako, iwe ni siri kwako, na kuamua kufanya maamuzi mengine ya busara ambayo yataleta matokea mazuri kwako.
Kama hakuna mabadiliko yoyote, pamoja na jitihada zako binafsi, na kuona kuwa tatizo ni kwamba hawakuamini, unganeni wafanyakazi wote ambao wamepatwa na tatizo hilo, muende tena kwa bosi wa juu zaidi ili aweze kuliangalia tatizo hilo na kulishughulikia kwa ukubwa wake.
Kama unafikiri tatizo ni kwamba bosi wako hawezi au hataki kubadilika, omba uhamisho katika kitengo kingine katika ofisi hiyo hiyo.
Endapo uhamisho wako hautakubalika, anza kutafuta kazi nyingine. Ni vema kutafuta kazi hiyo kwa siri, lakini ukiwa na matumaini kuwa ipo siku moja utaondoka eneo hilo.
Hivyo basi ni muhimu kwa watendaji waliopewa madaraka ya kuwaongoza wengine kuwa makini katika mawasiliano na wafanyakazi wao, pia wapende kujifunza kwa kusoma na kutoka kwa viongozi wengine waliofanikiwa zaidi.

Wengi wa mabosi wa aina hiyo ni wale ambao elimu yao ya darasani huwa ni ndogo hivyo wanakuwa hawana mpanuko wa mawazo, na mara nyingi husababisha makundi katika ofisi.

Japo pia wapo mabosi ambao wamekwenda shule, ila kunyanyasa inakuwa ni tabia yao ambayo pia wakiambiwa wanaweza kuibadili.

Kwa upande wa wafanyakazi wanaokabiliana na hali hiyo ngumu, wasichoke kumwomba Mungu kwani yeye ndiye muweza wa mambo yote, pia wajitahidi kupata elimu zaidi ili wawe na uwezo wa kufanya kazi yoyote iliyo mbele yao.

0713 331455/0733 331455
www.lngowi.blogspot.com
lcyngowi@yahoo.com

TUNAWEZAJE KUEPUKA MIGONGANO?

KARIBUNI wapenzi wasomaji katika safu hii ya Maisha Yetu. Leo tutaangalia ni jinsi unavyoweza kuepuka migongano isiyokuwa ya lazima.
Ni jambo jema na la busara kuchagua nini cha kusema kuliko kusema kile unachochagua. Kwa kufanya hivyo utajiepusha na migogoro.
Mara kadhaa wanandoa wamekuwa wakitengana, marafiki kufarakana na wafanyakazi kukosa ushirikiano. Je, unafahamu ni nini kinasababisha hali hii ya huzuni? Sababu kubwa kuliko zote ni kutokuwa na mawasiliano mazuri. Tumeshashuhudia watu wazuri wakitengana kwa sababu ya kutokuelewana. Walifikiri walikuwa na mawasiliano, kumbe sivyo.
Tatizo ni kwamba watu wengi hawawezi kutofautisha kati ya kuzungumza na kuwasiliana, hali inayochangia migogoro. Mawasiliano yana sehemu mbili ya kuzungumza na kusikiliza. Mzizi wa neno mawasiliano maana yake ni kushirikishana. Ni jinsi gani tunaweza kushirikishana mawazo na hisia? ni mpaka pale wahusika katika mazungumzo watakaposikiliza kwa uelewa kama vile katika kuzungumza.
Ni jinsi gani tutakavyowaambia wapenzi wetu tunawapenda? Si kwa maneno, ni kwa kuwasikiliza kile wanachokisema. Tunasikia, lakini hatusikilizi, hatufyonzi ule ujumbe uliotolewa. Nini kinasababisha haya mawasiliano mabaya? Ni kwa kuwa tumetoka katika maeneo tofauti, uzoefu na historia tofauti. Jinsi tunavyoiangalia dunia na matukio mbalimbali tunatofautiana na kusababisha migongano.
Hasira inapopanda ni kwamba tumezungumza kile tulichochagua badala ya kuchagua kile cha kusema. Migongano hiyo husababisha kutokuelewana na hatimaye kutengana. Ukweli, kama tunashirikiana mawazo kwa pamoja, kutakuwa hakuna kutokukubaliana, bali kuishi kama vile dunia ilivyo.
Hatua ya kwanza itakayoondoa kutokuelewana ni kukubali kwamba wote hatufanani. Kwa sababu ya utofauti wa uasilia wetu na mawazo yetu. Yamkini, tunafanana katika hili, kwamba tunahitaji kueleweka na kukubalika.
Kuna wakati mwingine waweza kujihisi kutokukubaliana na fulani, ni vema kutulia na kujiuliza ni jinsi gani watu wanavyotofautiana na wewe. Unaweza kuelewa jambo lakini bado ukawa hukubaliani nalo. Kama mawazo yako ni tofauti, usipende wengine wakubaliane na mawazo yako.
Je, ni jinsi gani unaweza kuwafanya wengine wakubaliane nawe? Ni pale utakapowaheshimu. Unaweza kuwaeleza kuwa ‘siwezi kusema kuwa nakubaliana nanyi, lakini naheshimu kwa kuwa na mawazo tofauti,’ mara nyingi kutokuelewana kunaibuka kwa sababu tunaangalia maneno yanayozungumzwa badala ya kumwangalia mzungumzaji.
Viungo, joto, baridi, utajiri, umaskini, uhuru na amani, ingawa tunaelewa maneno haya tunayatafsiri tofauti. Kwa hiyo usiweke msisitizo kwenye maneno, lakini kwenye moyo wa mtu. Jaribu kumwelewa mtu na siyo maneno. Mara nyingine, licha ya jitihada zetu, migogoro hutokea. Kama ndivyo, hakuna haja ya kukata tamaa.
Jumla ya yote, migongano ni nafasi ya kukua. Tumia hali hiyo kujifunza pale ulipokosea na kujirekebisha. Kwa kuwa tunajifunza kutokana na makosa yetu, tunanafasi ya kusonga mbele.
Tutakapo mwelewa anayezungumza na kutoa nafasi ya kueleweka tutajiepusha na mengi. Pia, kila mmoja anapomwelewa mwenzake, hakuna haja ya kuombana msamaha. Kama tutafanikiwa kujiepusha kutokuelewana na migongano tunafikisha ujumbe wa amani.

Wednesday, April 8, 2009

MPE MWENZA WAKO NAFASI YA KUZUNGUMZA

KARIBU mpenzi msomaji katika safu hii inayokujia kila Alhamisi, kwa lengo ya kukufanya wewe ujue mbinu mbalimbali zitazokufanya ufanikiwe katika maisha yako.
Katika maisha yako unayoishi, kamwe usiwadhalilishe wengine kwa jambo lolote lile.
Nasema hivyo kwa sababu rafiki yangu aliniambia kuwa hajawahi kujisikia vibaya kama siku moja aliyoalikwa kwenye chakula cha jioni na rafiki yake.
Alisema rafiki yake huyo, kila mara alikuwa akimdhalilisha mkewe alipokuwa akitaka kuchangia mada yoyote ambayo walikuwa wakiichangia.
“Mke wangu hana akili kwenye kichwa chake,” alisema mtu huyo aliyekuwa ameandaa chakula kwa ajili ya rafiki zake.
Baadhi ya wanaume wanafurahia kuwakosoa na kuwavunja moyo wake zao, au rafiki zao. Hali hiyo inaweza kuwafanya wakajisikia kana kwamba ni washindi kwa wakati huo, lakini sivyo walivyo, hiyo ni tabia mbaya inayoonyesha wazi mtu huyo alivyo.
Kunyamazisha uhuru wa kujieleza wa wengine ni kuonyesha hali ya ubinafsi, kutopevuka na dhambi, inafaa kuepukwa na watu wote wanaotamani kuwa na hali hiyo.
Ni vema kumpa nafasi mke wako ya kuzungumza neno lile analotaka kulizungumza. Mpe sifa mbele ya watu, muongoze katika mazungumzo na mpe moyo wa kuzungumza yale aliyonayo.
Pengine anaweza kusema jambo litakalowafanya wasonge mbele au kuwatahadharisha na mawazo mabaya yanayoweza kuwaingiza kwenye kuharibikiwa badala ya kusonga mbele.
Kumbuka kuwa kila mwanamke hupenda kuonyesha shukrani zake kwa mumewe. Mwache mke wako ajisikie wewe ndiye furaha yake zaidi sana mbele ya wengine.
Kwa kuwa ndoa inakuwa nzuri pale wawili wanaopendana wanapeana moyo badala ya kuvunjana moyo, hivyo utakaposhinda katika hilo, katika masuala yenu ya ndani mtaweza kuwa na ndoa yenye mafanikio kwa kupanga mipango mizuri ya familia, kinyume cha hapo hakutakuwa na maelewano, kwani kila mmoja anapenda kufarijiwa na kusikilizwa na mwenzake.
Katika hali hiyo kumbuka kuwa kila mmoja ni tajiri kulingana na vipaji mbalimbali Mungu alivyomjalia, ambavyo ni tofauti na wengine. Kila mmoja ana mambo yake mazuri aliyojaliwa na muumba, yawezekana ni busara, ushauri au mawazo mbalimbali ya kumtoa mtu kwenye hali ya umaskini na kumpa fikra ambazo zitamfanya afikirie mawazo ya kuwa na maendeleo.
Kila unachofikiri kinakuwa, kwani mtu mwenye mafanikio hufikiri njia za kuzidi kupata mafanikio, pia anakuwa na mawazo mapana ya kumpatia maendeleo.
Endapo mtu hutapenda kujishughulisha, wakati mwingine utajikuta ukipata magonjwa ya aina mbalimbali yanayotokana na hofu uliyonayo katika maisha yako.
Madaktari wengi hujua kuwa, asilimia 85 ya magonjwa yanayokupata yanatokana na msongo wa mawazo.
Wakati akili yako ina afya, moyo wako huwa na furaha. Wale wanaotaabika na magonjwa ya akili wanaweza kupata nafuu ya muda kutoka kwa daktari, lakini njia nzuri ni kuamua kukabiliana na hali ngumu ya maisha inayokupata kwa kufanya jitihada kwa mambo mazuri unayoyawaza ili uwe na maisha bora.
Shinda hofu ili utoke kwenye kifungo katika akili yako. Kwani hujazaliwa ili uwe mtu wa tabia ya hofu, ila uweze kukabiliana nayo. Mara nyingi wasiwasi ni ugonjwa unaoharibu maisha ya mwanadamu.
Magonjwa mengi ya hisia yanasababishwa na mtu kuchanganyikiwa kisaikolojia, woga na wasiwasi ambavyo huletwa na hofu na umaskini.
Mtu ambaye amejawa na hofu ni mfungwa katika akili yake. “Mateso mengi katika dunia hii kwa baadhi ya watu ni kufikiri,” anasema Luther.
Watu ambao hawajajifunza jinsi ya kufikiri wanaruhusu mawazo hasi yatakayokuwa muongozo wa maisha yao na baadaye kuwa waathirika wa pombe na dawa za kulevya.
Lakini uelewe kuwa, dawa za kulevya na pombe haviwezi kutatua tatizo. Hivyo basi unaweza kutoka kwenye kifungo cha hofu, wasiwasi, kuchanganyikiwa kwa kutumia akili yako kwa busara.

KUWA JASIRI KATIKA MAAMUZI YAKO

KWA mara nyingine wapenzi wasomaji tunakutana katika safu hii ya maisha yetu inayokujia kila Alhamisi kwa ajili ya kukuelimisha pamoja na kukuongezea maarifa kwa namna moja ama nyingine katika kukupatia maendeleo.
Leo tutaangalia jinsi ambavyo maamuzi mazuri unayoyaamua katika maisha yako yanavyokupa ujasiri wa kusonga mbele katika kufikia malengo uliyojiwekea.
Kumbuka kama unataka kuwa mtu fulani katika jamii au kuwa kiongozi, ni vema ukawa jasiri wa maamuzi yatayokufikisha kwenye mafanikio.
Pia wapo watu wanaokuwa thabiti katika kufanya maamuzi, lakini pia, kutekeleza inakuwa shida. “Ni jambo moja kuwa thabiti kufanya maamuzi, lakini ni jambo Jingine kutendea kazi.”
Unapothubutu kufanya jambo lolote ambalo unaona kuwa baadaye litakuletea mafanikio, wewe ni jasiri. Tofauti na hapo unajimaliza mwenyewe, unakuwa mtu ambaye mipango unayopanga inaishia kwenye mikoba.
Yeyote anayewekeza kwenye mradi wowote, anayenunua gari au kufanya uamuzi wa kubadili kazi, anajiwekea mkanganyiko katika maisha yake, lakini mwisho wa yote anavuna furaha na maendeleo kwa kuwa anakuwa amepiga hatua nyingine katika maisha yake, ambayo hakuwahi kuwa nayo.
Kwa upande wa watu ambao hawapendi mabadiliko katika fikra zao kwa jambo lolote, huwa wanakosa kila kitu. Hata kuwa na mafanikio makubwa katika maisha inakuwa ni vigumu.
Kuwa mtu wa kupenda kuthubutu kufanya jambo lolote lenye mafanikio katika maisha.
Unapotaka kusonga mbele, usichukie mawazo ya wengine wenye busara wanaokushauri, japo wapo wengine ambao mara zote hawapendi kuona wenzao wanasonga mbele, jiepushe nao. “ Kuwa na chuki ya kupata maoni kutoka kwa wengine, ni jambo baya ambalo halitakufanya uendelee mbele,” inakupasa uchukue maoni ya kila mmoja na kuyapima. Kamwe usipoteze muda na nguvu zako kutafakari maoni yasiyo na maana.
Mara zote penda kujifunza kutokana na makosa. Kuna msemo mmoja unaosema kuwa, kama umekosea ni vema kukiri kosa lako. Wala usichukie unapoambiwa kuwa umekosea, jifunze kutokana na makosa yako.
Kila tatizo lina utatuzi wake. Kwani hakuna jambo lolote katika sura ya dunia ambalo halina utatuzi. Kila tatizo linalojulikana kwa mwanadamu linapatiwa ufumbuzi.
Japo wakati mwingine tatizo lako linaweza kuonekana ni la kipekee, jua kuwa wengine wameshakabiliana nalo na kulitafutia ufumbuzi.
Matatizo yote yanayompata mwanadamu, ufumbuzi wake unapatikana, kwani kila tatizo lina mlango wake wa kutokea.
Acha kufikiria matatizo unayokutana nayo, hata kama ni mazito kiasi gani, kadiri unavyoruhusu akili yako kufikiria matatizo yanayokukabili ndivyo yanavyozaliwa mengine ambayo hayakuwepo.
Jaribu kupata ufumbuzi wa kila tatizo lililopo mbele yako ili uweze kusonga mbele.
Jipe nafasi ya kufikiri, jipe nafasi hiyo pale unapokuwa na jambo zito linalokutatiza. “Jipe nafasi ya kutulia nyumbani kwako, unapokuwa umekaa kwenye kiti chako, wakati huo utakuwa unapata ufumbuzi wa tatizo linalokukabili.” Wakati huo ni vizuri ukawa na furaha na ushindi wa majibu ya matatizo yanayokukabili.
Ondoa hofu, kwa kuwa mara zote ndiyo inayoharibu uwezo wako wa kuwa na maamuzi ya busara. Kwani hofu inatokana na uamuzi mbaya wa matatizo yako. “Hofu ni adui mkubwa wa matatizo yako.” Inafikia hatua watu wengine huogopa kifo, kutokana na hofu waliyonayo.
Mara nyingine hofu inatokea kwa sababu ya kutokujua ukweli wa jambo, usipoteze nguvu zako kufikiria kitu ambacho haukijui.

MALENGO NI MUHIMU KATIKA MAISHA

KARIBUNI wapenzi wasomaji wa safu hii ya Maisha Yetu. Leo ni siku nyingine mpya tunayoangalia ili tufanikiwe katika maisha yatupasa kufanya mambo gani.
Kama unataka kufanikiwa katika maisha yako, inakupasa uwe wazi kwa kile unachohitaji kukifanya. Kwa mfano, unaweza kumuuliza kijana mdogo anatarajia kuwa nani katika maisha yake, hapo utapata jibu kutoka kwake. Kijana huyo anaweza kukwambia, anataka kuwa mwana anga, rubani, daktari, muigizaji au askari. Watoto hueleza kwa uwazi kile wanachohitaji.
Kwa upande mwingine swali hilo hilo ukimuuliza mtu mzima kile anachokitarajia katika maisha yake, mara nyingi huwa hayuko wazi kuelezea matarajio yake ni yapi. Hapa inaonyesha kuwa watu wengi wanashindwa kufikia matarajio waliyonayo kwa kuwa hawana malengo thabiti ya maisha yao.
Ni nini unachokihitaji katika maisha yako? Je, unakijua? Umeweka wazi malengo yako kwa kipindi hiki? Katika maisha ni muhimu kujua kile unachotaka kukifanya na kuandika malengo katika kutimiza kile unachokihitaji. Ni vema kuandika, kuwa wazi kwa kile unachotaka kukifanya.
Fahamu kile unachotaka kufanya katika kutengeneza maisha yako, vitu unavyotarajia kuvikamilisha kama ni afya njema, ndoa yenye mafanikio, amani, kazi nzuri, nyumba mpya, safari ya kwenda nje ya nchi au pesa nzuri.
Kila jambo huwa na mpangilio, ili ufikie maisha mazuri inakupasa uwe na malengo na kujituma katika kazi. Kama unajua ni nini unachohitaji na kuwa na malengo sahihi, utakuwa na bidii katika shughuli zako. Kwa kuwa unapokuwa na mipango katika maisha yako, kunakufanya kusonga mbele.
Kumbuka kuwa mafanikio huja kutokana na malengo, kinyume na hapo utashindwa. Malengo ni kiongozi katika safari yako ya maisha, tofauti na hapo safari hiyo itakuwa na vikwazo vingi. Unapokuwa na biashara yako, ni vema ukawa na ripoti inayoonyesha maendeleo yako ya kila siku. Usivunjike moyo kama malengo yako hayatafanikiwa.
Songa mbele. Ona kama kushindwa ni kwa muda tu, hivyo yakupasa uongeze bidii. Kila jambo linakwenda kwa mzunguko. Jipe moyo kwa kujua kuwa, uwezo na utayari ulionao unaondoa vikwazo vyovyote vinavyo kukwamisha.
Kwa upande mwingine unapopata wazo lolote la maendeleo usilidharau, kwani linaweza kukutoa hapo ulipo na kukufanya kuwa na mafanikio zaidi.
Wazo linapokujia katika akili yako,liandike, lifikirie kwa umakini, likuze zaidi, kuwa na shauku nalo, halafu chukua hatua kuhusiana na wazo hilo.
Wazo unalolipata ni kitu cha thamani kinachoweza kukuzwa na kuendelezwa na kuchukua hatua ili kiwe kitu halisi.
Ni kama vile kupanda mbegu, ambazo hukua na kuleta mazao mazuri. Mawazo ni mbegu, ambayo yakitumiwa vizuri yataleta matokeo mazuri. Ni jinsi gani unaweza kupata wazo la kukuinua kimaisha? Mawazo hupatikana kwa kuangalia, kuuliza, kufikiri, kuangalia matatizo unayokabiliana nayo na kutafuta njia ya kuyatatua.
Pamoja na kusoma vijarida vinavyoweza kukupatia mawazo mapya na maendeleo, kujadiliana na wengine. Jifunze kuwa na utaratibu wa kuandika kila wazo linakujia na kulipanua zaidi.
Mara nyingi mawazo huja yenyewe. Yanaweza kukujia kwa kusoma magazeti, unapokuwa kwenye matembezi, unapotembelea madukani, unapoangalia picha na kuwasikiliza watangazaji wa vipindi mbalimbali vya kwenye redio au televisheni.
Unaweza kupata mawazo toka kwenye vyanzo mbalimbali, inakupasa uchukue mawazo mazuri pekee yatayokuletea mafanikio katika maisha yako.

ZUIA HASIRA, HISIA ZINAZOKULETEA MAUMIVU

NI siku nyingine njema ambayo Mwenyezi Mungu ametujalia kuiona tena. Tunayo kila sababu ya kumshukuru kwa pumzi na uhai aliotupa.
Mwanadamu yeyote aliyeumbwa na Mwenyezi Mungu ana hisia mbalimbali ambazo humfanya kuwa hivyo alivyo. Mojawapo ya hisia hizo ni hasira. Lakini ni vema kujitambua na kuitawala hasira yako kabla haijakutawala.
Hivyo basi, kama hupatwi na hasira, ni lazima utakuwa na tatizo. Pia ni vema kutambua kuwa kupatwa na hasira ni hali ya kawaida. Ni suala la hisia za muhimu kwa afya yako. Tatizo linakuwepo pale mtu anaposhindwa kuzuia hasira yake na kuchukua hatua na kuanza kupigana au kugombana na watu pasipo sababu ya msingi.
Hasira isiyo na mipaka inasababisha vurugu zinazoleta uharibifu. Ni sawa na ugonjwa, usipoizuia hasira inaweza kukudhuru na kukukereketa moyoni kwa njia ya fundo, husuda, chuki.
Wakati haya yanatokea, njia pekee ya kuondoa hasira ni msamaha. Kuwa tayari kusamehe na kusahau. Safisha akili na moyo wako. Rudisha chuki kwenye upendo.
Unaporuhusu furaha moyoni mwako unapata afya. Kwa kuwa inakufanya uwe na afya bora. Watu wenye furaha wana afya na watu wenye afya wana furaha.
Vile vile, kicheko ni dawa kubwa, Pia ni afya. Inaondoa hali ya kukata tamaa. Madaktari wanasema ndiyo dawa pekee ya dunia. Inakuletea furaha, amani na utulivu katika akili yako na mwili.
Unaweza kuepuka magonjwa ya akili kwa kujifunza kuwa na furaha pamoja na kucheka.
Pia jambo lingine la kuzingatia, ni kwamba usile chakula wakati una hasira, vinginevyo hakitafanya kazi mwilini au kitakusababishia vidonda vya tumbo.
Ni desturi kwamba, kabla hujakaa na kuanza kula unanawa mikono, vile vile ni vema kusafisha akili yako na kuondoa hasira uliyokuwa nayo, uchungu, uhasama na mawazo mabaya. Endapo unakula ukiwa na hisia hizo, chakula unachokula kinakuwa hakina ladha, pia hakitaweza kufanya kazi vizuri mwilini.
Safisha akili yako vizuri na uondoe mawazo yote mabaya. Kama umekasirishwa na mtu, au jambo lolote au una matatizo sahau wakati unapokula chakula. Kwa kufanya hivyo utafurahia chakula unachokula.
Ni jinsi gani unaweza kuzuia vidonda vya tumbo visikupate? Kwanza utambue kuwa vidonda vya tumbo humpata mtu mmoja kati ya watu kumi. Mara nyingi husababishwa na wasiwasi, hasira, uchungu, uchovu na utumiaji wa sigara pamoja na vinywaji vikali.
Kamwe usiache matatizo yako yakakuzidi, yaachilie kwa kuzungumza na watu unaofikiri kuwa wanaweza kukusaidia. Wakati unapojisikia vibaya, jisogeze taratibu baada ya kuacha kile ulichokuwa ukikifanya ili upate muda wa kupumzika.
Punguza matatizo yako kwa kujishughulisha, usiende nayo nyumbani. Kama utapenda kuwa na furaha na amani moyoni mwako itakufanya usipate vidonda vya tumbo. Kumbuka hali ya furaha ya mara kwa mara inakuondolea hali uliyonayo ya huzuni, majonzi au hasira na kukufanya uwe na afya bora.
Njia nyingine inayoweza kukufanya uepuke kupata maradhi ya moyo ni kuondoa wasiwasi na kula vyakula ambavyo havina mafuta mengi. Wataalamu wa afya wanaamini kuwa maradhi ya moyo yanaweza kuzuilika kuanzia kipindi cha ujana.
Pia wanaamini kuwa vyakula vya mafuta, shinikizo la damu, kukosa mazoezi, uvutaji wa sigara, ulevi, msongo wa mawazo na uchovu unasababisha ugonjwa huo.
Ili kujiepusha ni vema kupata muda mzuri wa kupumzika, kufanya mazoezi, kuondoa hofu, kutokuvuta sigara, kutokunywa pombe, jitahidi kutokuwa na uzito utakaozidi pamoja na kuangalia afya yako mara kwa mara.

ILI UFANIKIWE KAMILISHA JAMBO MOJA NDIPO UANZE LINGINE

NI siku nyingine tena ambayo Mwenyezi Mungu ametuamsha tukiwa wazima na wenye afya njema. Karibu mpenzi msomaji katika safu hii ya Maisha Yetu inayokujia kila alhamisi kwa lengo la kukuelimisha na kukuadilisha.
Kumbuka, katika maisha hakuna njia ya mkato ya mafanikio. Mafanikio yoyote yana gharama kubwa. Uwezekano wa kufanikiwa upo, thawabu ipo lakini mpaka uwe na uhitaji huo. Ili ufanikiwe, yakupasa ufanye kazi kwa bidii, kwani ni muhimu kujishughulisha na kitu unachokipenda na kuongeza ujuzi wa kufanya kazi yako kwa ubora unaotakiwa.
Siri nyingine ya mafanikio katika maisha ni uaminifu, kwa maneno mengine tunasema, uaminifu ni siri ya mafanikio. Kama utakuwa mwaminifu, utaaminiwa. Ina maana utakuwa mwaminifu katika shughuli zako zote unazozifanya.
Hata katika maeneo ya kazi, kila mwajiri hupenda kujua tabia za wafanyakazi wake, kila mmoja uaminifu wake ulivyo. Ina maana kuwa mwajiriwa yeyote asiyekuwa mwaminifu hatapata nafasi ya kupandishwa daraja katika eneo lake la kazi.
Hata marafiki zako watakapogundua wewe siyo mwadilifu, hawatakuwa tayari kufanya kazi nawe. Utaheshimika na wenzako pale tu watapogundua kuwa ni mtu uliyemwadilifu. Watu wengi wamekuwa na tabia mbaya na kuwasababishia uharibifu katika maisha yao kwa kukosa uaminifu.
Wanaibua matumaini kwa wengine kwa ahadi huku wakijua kuwa hawawezi kuzitimiza. Kufanya hivi ni kutenda kosa lisilosameheka na kutokuwa na adabu kwa wenzako. Mtu mwenye busara huelewa tokea mwanzo kuwa, uaminifu ni sera nzuri katika maisha. Na unaweza kufanya mambo mengi mazuri kutokana na uaminifu huo, tofauti na mtu asiyemwaminifu.
Kumbuka kuwa mtu aliyefanikiwa amepata digrii ya uaminifu katika maisha yake. Mbali na uaminifu suala la kuzingatia ni nidhamu. Hiyo ni moja ya tabia muhimu katika kupata mafanikio yako.
Mwimbaji mmoja aliwahi kuimba – ‘nidhamu ya kazi ni msingi wa mafanikio mema kazini’. Mtu binafsi anapaswa kuwa na nidhamu vile vile taifa zima. Pasipo nidhamu dunia inaweza kutetereka.
Kipindi cha vita kuu ya dunia, Uingereza isingeweza kustahimili mabomu ya kila siku kama watu wake wasingekuwa na nidhamu. Wakazi wake walikwenda kujihifadhi kwenye makazi ya muda wakati wa usiku bila kujua kuwa nyumba zao zitasalimika asubuhi inayofuata. Lakini waliendelea kuishi. Hiyo ni nidhamu. Hakuna vita itakayoweza kufanikiwa mpaka kuwepo na nidhamu.
Hakuna kampuni itakayofanya vizuri hadi pale wafanyakazi wake watakapokuwa na nidhamu. Nidhamu inaleta Umoja, nguvu, ushupavu na mafanikio. Katika kufikia mafanikio yako ni vema kufanya kitu kimoja kwa wakati. Baadhi ya watu wamekuwa hawawezi kukamilisha jambo lolote wanalolianza.
Kwa sababu wamekuwa wakijihusisha na miradi mingi lakini yote imekuwa haikamiliki. Hii ni kwa sababu hawashikamani na jambo moja kwa wakati na kulikamilisha. Huu ni ukosefu wa nidhamu. Ukamilifu wa malengo huleta furaha. Kukamilisha mipango yako kunakupa ujasiri wa kufanya kitu kingine kikubwa zaidi, ambacho ni kizuri.
Watu waliofanikiwa kukamilisha vitu vingi na kupata mafanikio ni wale wanaofanya jambo moja kwa wakati na kulikamilisha halafu wanaanza kufanya jambo lingine. Huu ni mpango mzuri, pia ni nidhamu.
Weka maisha yako katika mpangilio mzuri kwa namna ambayo muda wako utatumika kwa manufaa mazuri. Fanya kazi muhimu sasa, vitu vya kawaida vitasubiri. Kazi unayoianza hakikisha unaifanya mpaka inakamilika. Kwa kufanya hivyo utazuia kuchanganyikiwa. Fanya kitu kimoja kwa wakati na ukifanye sasa.
Unaweza kufanikiwa mara nyingi kadiri unavyoiweka akili yako kufanikiwa. Kila kazi au uzoefu unaoupata ni somo muhimu kwa maisha, kwa kila ujuzi unaoupata ni vema ukautumia kwa mafanikio ili kukamilisha malengo yako.
Ni vyema kuonyesha shukurani. Kamwe usilaumu kila kitu. Maneno mazuri huongeza nguvu na uhai na kukufanya kusonga mbele katika shughuli zako. Toa shukurani kwa ajili ya maisha yanayokuzunguka, shukuru kwa mambo yote unayoyapitia katika maisha yako, shukuru kwa ajili ya kazi uliyonayo na vikwazo vyote unavyovipitia.
Shukuru kwa ajili ya familia yako na marafiki kwani pasipo wao usingeyafurahia maisha yako. Onyesha shukurani kwa vitu vizuri vya asili, kama vile milima, maziwa, miti, maua, ndege na wanyama. Kufanya hivi ni kushukuru kwa maisha yako na vyote vinavyokuzunguka.
Ijaze nyumba yako shukurani, kamwe usizungumzie mambo yanayokurudisha nyuma nyumbani kwako, wakati unazungumzia umaskini na upungufu, unafungulia milango ya vitu hivyo na kuvikaribisha katika maisha yako.
Kuwa na mawazo ya upendo, afya, furaha, mafanikio na shukrani kwa yote unayokabiliana nayo. Kamwe usiseme kuwa fedha ni adimu au maisha ni magumu. Zungumza mafanikio, fikiri mafanikio na toa shukrani kwa mafanikio uliyonayo katika maisha yako.
Kama unataka kufanikiwa, jifunze kuwashukuru wengine. Katika shughuli mbalimbali, mafanikio yanategemea mchango unaoupata kutoka kwa wengine.
Inaweza kutokea kuwa kikwazo pekee katika mafanikio yako ni mtu fulani. Hivyo ni muhimu kujenga tabia ya shukrani kwa wengine. Kila mmoja anapenda shukrani. Endapo unapenda kuwa na mafanikio yasiyokoma ni vema ukajifunza kupenda wengine, kufurahia vipaji walivyonavyo na kuzungumza nao.
Kila mmoja anamwitaji mwenzake katika mafanikio yake. Kila mmoja anahitaji msaada wa mwenzake. Muuzaji anahitaji mnunuzi katika biashara zake. Kama mfanyabiashara hatapata watu watakaonunua bidhaa zake, hatafanikiwa.
Mkurugenzi anahitaji utegemezi wa wafanyakazi wake ili vitu viende vizuri. Bila msaada wao, atashindwa kufanya kazi zake. Wanasiasa wanahitaji msaada kutoka kwa wapigakura wao. Bila msaada wao hawataweza kuchaguliwa. Siri ya mafanikio katika maisha yetu ni kwamba, kila mwanadamu anahitaji kuheshimu wengine na kuheshimiwa. Hili ni la msingi.
Kwa vyovyote vile unaposhughulika na watu wengine, uweke akilini kuwa shukrani ni jambo la msingi. Kwa kujua hili litakuweka katika wakati mzuri unaposhughulika na watu katika shughuli zako.
Wafanye wengine wajisikie wao ni wa maana kwa kukumbuka majina yao, kwa kuwatambulisha kwa heshima na kuomba ushauri kutoka kwao. Watambulishe wengine kwa mavazi yao, vyeo na jinsi wanavyofanya kazi.

Twitter Facebook