Monday, June 16, 2008

IMANI, UVUMILIVU, NGUZO YA MAISHA

MARA nyingi mambo mazuri ya kushangaza hutokea kwa watu wanaoamini kuwa wanaweza kufanya mambo makubwa katika maisha yao.
Unaweza ukawa mgonjwa, mdhaifu, mwenye dhambi, mwenye moyo mpweke au uliyeshindwa. Haijalishi kwa lolote utakalokutana nalo kama utakuwa wa kuamini ushindi.
Imani inabadili hali yoyote ile inayoonekana kuwa haiwezekani. Pia inafunga milango ya mawazo yetu potofu. Mambo yote yanawezekana endapo utaamini na kufanya juhudi.
Imani inatoa mwangaza kwa maisha yetu juu ya yote yanayowezekana. Pia ni mwanzo wa mafanikio yetu. Inawezesha kuwa na nguvu zaidi ya ulivyo sasa. Kila mmoja kati yetu anatakiwa kuamini juu ya mafanikio binafsi.
Mama mmoja, alikuwa akieleza juu ya kukata tamaa kwa ajili ya mtoto wake wa kiume ambaye wakati wote alikuwa mgomvi na kusababisha mashitaka mara kwa mara.
Ikawa kila mara mtoto huyo anamsononesha mama yake, hivyo alimwomba rafiki yake amshauri juu ya mtoto wake huyo.
Rafiki, alimwambia kuwa jambo la muhimu analotakiwa kufanya ni kumpenda mtoto wake na kumwamini zaidi.
Alimweleza kuwa, jambo la kufanya ni kuonyesha upendo kwa mtoto wake na kumwamini zaidi ingawa watu wengi wanashindwa kufanya hivyo.
Kama unataka kuwa na maisha mazuri, kuwa mshindi na kuondoa hali ya ubinafsi, unatakiwa kufanya kazi kwa bidii na malengo.
Pamoja na yote tufanyayo, kumwamini Mungu aliyekuumba ni jambo la msingi.
Mtu mmoja aliyejulikana kwa jina la Jim, alikuwa ni mchapakazi na mwenye bidii. Ilitokea siku moja akajikuta yuko katikati ya matatizo.
Jambo alilolifanya, alikwenda kwa kiongozi wake wa dini na kumtaka amwombee kwa kuwa Jumatatu ya wiki iliyopita alipata ajali iliyoharibu gari lake kabisa.
Jumanne, alipokwenda kazini alikuta ameachishwa kazi, Jumatano kitengo cha kodi walimpigia simu na kumwambia kuwa anadaiwa kodi ya miaka minne iliyopita na kama hatailipa ndani ya siku kumi, watakwenda na kuuza nyumba yake.
Kwa kipindi chote Jim alichomweleza kiongozi wake wa dini matatizo yaliyomkabili, ndani ya wiki mmoja alikuwa mwenye uso wa furaha.
Kiongozi huyo alisema, kuwa ilimchukua dakika chache kuona ukubwa wa matatizo yanayomkabili Jim. Aligundua kuwa Jim anahitaji msaada wa Mungu ili aweze kumsaidia. Jim, alitabasamu tena na kumwambia kiongozi wa dini awe na siku njema kisha aliondoka.
Tunaona Jim alikuwa na imani iliyomfanya kuyaona matatizo yaliyo mbele yake kuwa yatapata ufumbuzi, ndiyo maana alikuwa na uso wa tabasamu.
Usiache kuamini juu ya mambo mazuri yajayo mbele yako. Kuwa mstahimilivu, mwenye kuamini mambo yote yatafanikiwa, kushinda, kupata tuzo, yote hayo yanatokana na uvumilivu.
Vuta subira ili kufikia malengo yako. Ruhusu nafsi yako kuwa na subira, utapata mafanikio. Tuzikumbushe nafsi zetu mara kwa mara kuwa na subira kwani chochote chenye thamani kinachukua muda.
Binti fulani aliajiriwa kwenye kampuni ya mabasi. Kazi yake ilikuwa ni kupokea simu siku nzima na kuchukua maoni na malalamiko ya wateja.
Kazi ya kusikiliza shida na malalamiko ya watu ni ngumu na wengi hawaipendi. Lakini, kwa sababu binti yule aliipenda kazi yake, hivyo aliifanya kwa upole na kuwa rafiki wa kila aliyeeleza matatizo yake.
Kumbuka, wakati mwingine watu walimtukana, kumfokea na kumsemea mambo ya uongo, lakini alifanya kazi hiyo kwa upendo, hakulipiza neno baya.
Alipoulizwa anawezaje kufanya kazi hiyo na watu wa aina mbalimbali, jibu lake lilikuwa rahisi, anaipenda kazi yake. Hivyo anajitahidi kuifanya kwa bidii ili asipoteze sifa.
Unapokuwa na malengo makubwa, ndivyo unavyofanya kazi kwa bidii, matokeo yake unapata mafanikio makubwa. Subira ni jambo gumu, lakini unaposubiri, mambo mazuri hutokea.
Je, unakutana na kipindi kigumu katika maisha yako? Usiache kuamini, usikate tamaa. Jizoeze kuwa mstahimilivu, kumbuka kuwa kipindi hiki kuna matukio mbalimbali katika dunia hii.
Fanya hivi, kadiri miezi inavyoendelea na miaka, utapata majibu ya matatizo yanayokukabili. Mambo mazuri yanakuja, endelea kuwa mstahimilivu.
Kuna baadhi ya watu wanasema, watu wengine hawana matumaini. Hapana, hawako sahihi. Hakuna mtu anayeishi bila matumaini.
Wataalamu wa magonjwa ya akili wamegundua kuwa haijalishi ni kwa jinsi gani mtu anakuwa na mfadhaiko au kukata tamaa, kama watu wanaingiza mwangaza wa matumaini katika fikra za watu, hupata tumaini jipya.
Kuna wakati mwingine baadhi ya watu husema kuwa fulani hana tumaini, kama mtu huyo anakuwa na tumaini katika maisha yake na kuacha kuamini yanayosemwa na watu juu yake, lazima atakuwa mshindi katika maisha yake.
Watu wengi katika jamii yetu siku za leo wamekosa tumaini kutokana na sababu moja ama nyingine. Kamwe usiwe katika historia ya dunia ambayo watu wanateseka kwa msongo wa mawazo.
Mtu mwenye matumaini kamwe hatashindwa. Wakati mipira ya kucheza gofu ilipotengenezwa kwa mara ya kwanza, ilifunikwa na ngozi laini.
Kulikuwa na kijana mmoja aliyekuwa na tatizo la kifedha, alipenda kucheza gofu. Hakutaka kufikiria kuwa alikuwa na mpira uliochakaa katika akili yake.
Aliendelea kuuchezea mpira ule katika hali ya uchakavu wake. Marafiki aliocheza nao waligundua kuwa mpira wa mwenzao umechakaa, lakini waliendelea kucheza. Siku za leo mipira yote ya gofu inatengenezwa ikiwa na vibonyo bonyo vidogo. Kwa jinsi ilivyotengenezwa, ndivyo unavyochezeka vizuri.
Hali hiyo ni sawa na maisha tunayoyaishi, yanakuwa kama mpira wa kuchezea gofu uliochoka, ambao unaweza kuruka mbali.
Ili kufanya maisha yawe mazuri, ni jukumu lako kubadili stahili ya kuishi kwa kufanya kazi kwa bidii na malengo.
Ukiulizwa, je unaamini waweza kufanikiwa katika maisha yako? Kila mtu atasema ndiyo. Inasaidia watu wengi wanaoteseka, inainua mioyo ya watu wengi.
Unapokuwa na matumaini, yanaponya maumivu yako, yanakupa matumaini ya kuwa na maisha mazuri, furaha inazidi na unakuwa na ndoto njema.
Tukutane wiki ijayo.
lcyngowi@yahoo.com0713 3314550733 331455

0 Maoni:

Twitter Facebook