Sunday, June 15, 2008

TABIA ZA WATU WANAOPENDA KUTAWALA

ZIPO aina kuu nne za watu ambazo zimegawanyika kutokana na tabia walizo nazo.
Tabia hizo ni kutawala (Choleric – Dominance), mhamasishaji (Sanguine - infuluencing), asiyeyumbishwa (Phlegmatic (steadiness) na mstaarabu (Melancholy - compliane). Ukiweza kujua tabia hizo, utaona ni rahisi kuishi na watu kwa kuwa tayari utakuwa umeshazifahamu tabia hizo.
Leo tutaanza kuangalia tabia ya kutawala. Utawala ni namna ya kuendesha shughuli za kutawala au ni hali ya kupenda enzi.
Kutawala ni tabia kuu ya kwanza ambayo mtu hupenda kutawala au kuongoza wengine. Ni shupavu, si mwoga na si mwepesi wa kukata tamaa. Mtu huyu anajiamini sana katika maamuzi yake na hajali maoni ya watu wengine hata yakiwa bora kuliko ya kwake. Anapenda kubadilisha mambo bila kushauriana na mtu yeyote.
Mara chache huomba ushauri kwa wengine. Anao uwezo mkubwa wa kushawishi ili kufikia lengo alilokusudia; hivyo kumpa fursa ya kuweza kushinda upinzani wowote kinyume na mipango yake. Ana uwezo wa kusimamia watu. Kama ana tatizo na mtu husema waziwazi bila aibu.
Mtu wa tabia hii hupenda matendo kuliko maneno. Hapendi maelezo mengi, hupenda mambo ya haraka haraka, na wala hajali mambo madogo madogo. Hutegemea mambo yake kufaulu. Hapendi wengine wanufaike kupitia mgongo wake. Si rahisi kumsifu mtu hata kama amefanya vema.
Ni vigumu kukubali kama ana shida hata akiwa na shida. Haonyeshi kuhuzunika au kushituka hata akipokea taarifa mbaya. Hata hivyo, mtu huyu si mvumilivu, ni mwepesi wa kukasirika na ni vigumu kumpendeza.
Kama tulivyoona mtu wa tabia hii anapenda kuongoza na kutawala wengine. Huwa hapendi kuongozwa mara kwa mara linapotokea jambo huwa mstari wa mbele kutoa maelekezo. Ndivyo alivyo, hivyo mara nyingine huweza akapendwa na watu kutokana na namna anavyotawala wenzake au akachukiwa.
Huweza kuchukiwa kama akiwa ni mtu anayependa kuamrisha na kuonekana kuwa yeye ni mjuaji kuliko wengine.
Wakati mwingine hupenda kubadilisha mambo bila kushauriwa. Hapa ina maanisha kuwa huwa anajali mtazamo wake binafsi bila kushirikisha wengine. Ni vizuri kupata ushauri wa wengine, kwani wakati mwingine mtu wa tabia hii atabadilisha jambo bila kupata ushauri ambalo litampa wakati mgumu.
Ana uwezo wa kushinda upinzani wa mipango yake. Mtu huyu kwa kuwa anapenda kutawala huwa amejaliwa uwezo wa kuweza kushinda upinzani wowote anaokutana nao katika maisha. Kwa kuwa anajiamini kuwa anaweza.
Hupenda kushawishi ili kufikia lengo. Kama anahitaji jambo fulani liweze kufanikiwa atatumia muda wake kushawishi wengine ili mradi afikie lengo alilokusudia.
Anajiamini katika uamuzi wake na hajali maoni ya wengine. Si vibaya kujiamini katika maisha, ila ni vizuri katika kujiamini kwako wakati mwingine ukasikiliza na maoni ya wengine, kwani waweza kuharibikiwa katika maamuzi yako.
Mtu wa tabia hii akumbuke kuwa pamoja na kujiamini kwake, wako watu wengine wenye maoni ambayo yanaweza kumsaidia. Kwani moja ya sifa za mtawala yoyote awe mtu anayependa kusikiliza maoni ya watu wengine na kuyatendea kazi kwa kuyapima. Katika maoni hayo yapo yanayoweza kumsaidia na mengine yanaweza kumpotosha.
Ni vigumu kumpendeza. Mtu anayependa kutawala huwa ni vigumu kufanya jambo lolote likampendeza kwa kuwa anajiamini kuwa hata yeye anaweza kulifanya. Hivyo kama tuishivyo katika mazingira mbalimbali unapomgundua mtu wa namna hii, usipate shida kutaka akusifu kwa kufanya jambo zuri kwake.
Mtu mwenye tabia hiyo ya kutawala huwa si mwoga ni shupavu katika mambo yake, hivyo hutegemea mambo yake yote kufanikiwa na si kushindwa.
Ni mwepesi wa kukasirika na si mwepesi wa kukata tamaa. Jihadhari kumkasirisha mtu huyo, jitahidi kumwelewa. Hakati tamaa kwa kuwa anapenda kuonekana kuwa ana uwezo wa kutawala.
Tatizo lingine la watu wa aina hii huwa hajali mambo madogo madogo wala hawapendi kutoa maelezo mengi inapotakiwa afanye hivyo huwa ni mtekelezaji zaidi kuliko kuzungumza.
Kwa kuwa hupenda kutawala, hupenda vitendo zaidi kuliko maneno. Hupenda kufanya mambo yake haraka haraka. Mara nyingi hupenda kufanya mabadiliko bila kujali maoni ya wengine.
Kufanya mabadiliko katika jambo fulani si vibaya, lakini ushauri ni muhimu sana kutoka kwa watu unaofanya nao kazi.
Mtu mwenye tabia hii huwa hapendi wengine wanufaike kwa ajili yake. Pia wanapokuwa na tatizo na mtu husema waziwazi hana tabia ya unafiki.
Hutokea mara chache sana huomba ushauri kwa wengine kwa kuwa anajiamini. Pia hapendi kukubali kama ana shida hata akiwa na shida si mvumilivu. Mwenye kupenda kutawala huwa haonyeshi huzuni au kushtuka awapo na shida.
Kwa kuwa mwenye tabia hii hupenda kutawala huwa na uwezo wa kusimamia watu. Inapotokea kuna jambo ambalo linataka usimamizi huweza kulisimamia vizuri.
Kutokana na tabia yake hiyo, si rahisi kukusifu, hata kama umefanya jambo zuri. Hivyo kufahamu tabia za mtu anayependa kutawala kutasaidia kumwelewa na kuweza kuishi naye bila matatizo.
Tukutane wiki ijayo.
0713 331 455

0 Maoni:

Twitter Facebook