Monday, June 16, 2008

TABIA YA MTU ANAYEPENDA KUTAWALA

KWA mara nyingine tunawakaribisha katika safu hii wapenzi wasomaji wetu. Kwa wiki tatu mfululizo tumekuwa tukiangalia tabia mbalimbali za watu.
Siku zote tabia za kawaida za mtu ni za kupenda kutawala, kuhamasisha, kutoyumbishwa na ustaarabu.
Kwa kawaida, saikolojia inaangukia kwenye imani kuwa mtu anazaliwa akiwa mkamilifu lakini anapokua hubadilika polepole na wakati mwingine si rahisi kubadili tabia zake.
Mungu pekee ndiye anaweza kumbadili yeyote. (Wagalatia 5: 22 - 26). Nina amini kuwa unaweza kutumia tabia yako ya asili kwa faida yako na kuwa zawadi kwa wengine .
Ustaarabu wako unaweza kukusaidia kubadilishana mawazo, kipaji na matarajio ya wenzako.
Tumeshaona tabia ya mtu anayependa kutawala, kuhamasisha, asiyeyumbishwa na leo tunakwenda kuangalia tabia ya mtu mstaarabu.
Ni mtu mzuri na mwenye kujali wengine, hujisikia vibaya anapoona wenzake wana matatizo. Anapenda maisha yenye mafanikio na akifanikiwa mara nyingi huwa tayari kutoa msaada kwa wenye shida.
Ana tabia ya kutoa ushauri kwa wenye shida na matatizo mbalimbali, na mtu akikosea humrekebisha na si kumcheka kama wafanyavyo watu wengine wasio wastaarabu.
Ni mkweli na ni mwepesi wa kukosoa anapoona mambo yanaharibika. Haogopi kusema ukweli bila kujali anayemweleza ni mkubwa au mdogo.
Ana tabia ya kuepuka unafiki na uongo, mara nyingi huwa wazi zaidi na huwa hashikilii mambo au kero kwa muda mrefu. Ni mwepesi wa kusamehe.
Huwaonyesha wema watu anaokuwa nao karibu, hali hii husababisha aonekane mwenye hadhi na heshima kwa jamii.
Anachukizwa anapoona baadhi ya watu wananyanyasa wengine na wakati mwingi hujitahidi kuwatetea wanyonge.
Si mbinafsi, anajali sana masilahi yake na ya wengine. Hupenda watu wote wafanikiwe.
Ni vizuri kwa mtu mstaarabu kujitathmini mwenyewe uwezo wake na mapungufu yake ili aweze kujirekebisha palipo na kasoro.
Hali itakayosababisha aweze kujipambanua katika jamii inayomzunguka na kuendelea kulinda heshima na hadhi yake.
Mwenye tabia hii hapaswi kujaribu kutoa kisingizio au kuruhusu kufanya jambo lisilo la kistaarabu na kimaadili kwa kuwa jamii inayomzunguka inamwangalia yeye kama mfano na kioo kwa jamii.
Mtu mstaarabu huheshimiwa na jamii kutokana na tabia yake. Hivyo akifanya makosa yasiyotarajiwa na jamii inayomzunguka anaweza kupoteza heshima na hadhi aliyonayo kwa jamii.
Mwenye tabia hii huwa na mipangilio mizuri kwa kuhakikisha mipango anayoipanga inakwenda kama ilivyopangwa, japokuwa wakati mwingine mipango inaweza kuwa kinyume cha matarajio.
Mara nyingi huwa wakamilifu katika mambo yao. Mwenendo wa tabia zao huhuhusisha katika kufikiria, kutathmini, kuorodhesha na kutathmini matokeo hasi na chanya kwa ujumla.
Pia hupenda kazi zisizo na kasoro kwa kuwa ni mtu makini kwa kila jambo. Huona kuwa kama kazi zake zitakuwa na kasoro zitamshushia hadhi yake.
Ni vigumu kusahau jambo lililomuumiza kutokana na ukweli kuwa ustaarabu anaoonyesha kwa wengine humfanya aamini kuwa kila anachokifanya ni sahihi, hivyo anapoumizwa na jambo lolote hujiona kuwa hajatendewa haki.
Huhitaji maelekezo zaidi ili afanye kazi iliyo kamili. Kwa kuwa hupenda kazi zake zisiwe na kasoro kabla ya kufanya jambo lolote ambalo hana uhakika nalo hupenda kupata maelezo ya kina ili asiiharibu kazi yake.
Anafikiri sana, hali inayosababisha afanye mambo yake kwa uangalifu na tahadhari ili kuepusha kuvunja heshima yake na hadhi aliyonayo kwa jamii.
Hapendi kuanza kazi nyingine kwa haraka mpaka ameelewa. Hii humwezesha kufanya kazi zake kwa mafanikio zaidi.
Anapenda kusifiwa kutokana na tabia yake ya ustaarabu na matendo mema anayoonyesha kwa jamii. Hujisikia vibaya asipofikia lengo lake.
Kwa kuwa hujiamini katika shughuli zake mbalimbali azifanyazo, hujisikia vibaya asipofikia lengo lake. Kutokana na kupenda kusifiwa kwa shughuli azifanyazo.
Ni mwepesi kujitoa mhanga kwa faida yake na wengine. Huwa na tabia ya kujaribu kufanya mambo mbalimbali yenye manufaa.
Hapendi kitu cha ghafla. Mfano safari au taarifa. Hupenda shughuli zake ziwe katika mipangilio aliyoipanga. Hupenda kuweka ratiba zake katika utaratibu unaoeleweka ambao hautetereki.
Ni mtu wa kufuata ratiba katika maisha yake na si wa kukurupuka. Labda itokee dharura ambayo ni kawaida kutokea kwa kila binadamu.
Hapendi lawama, havumilii kazi zilizo kombo. Ni mtu asiyependa lawama, pia havumilii kazi zinazokwenda shaghalabaghala.
Anapenda awe nadhifu na safi, ikiwa ni sehemu ya mambo yanayoonyesha ustaarabu na heshima, hali mbayo humuongezea hadhi kwa jamii na hufurahi zaidi anapokuwa hivyo.
Anapenda kila kitu kiwe katika utaratibu na hapendi njia za mkato katika shughuli mbalimbali anazofanya.
Hupenda kazi yake iwe safi. Mtu mkimya mara nyingi huangalia upande wa kushindwa. Yuko tayari kufa, kujitoa, haogopi kudhuriwa.
Anafaa kuokoa, anapenda kushukuru wengine, huogopa wengine wanavyomfikiria. Ana hasira zilizojificha, aweza kufanya uamuzi mzito usio tegemewa, aweza kujinyonga.
Tukutane wiki ijayo tutakapoanza mada nyingine.
0713 331455ngowi2001@yahoo.com

0 Maoni:

Twitter Facebook