NI kitu gani ambacho dunia inahitaji kwa sasa? Ina malighafi, uelewa na ina matokeo ya kufurahisha kutokana na uvumbuzi wa mambo ya kisayansi. Hata hivyo kila mtu anaamini kuwa kuna kitu kilichokosekana katika dunia.
Hivyo inaonekana dunia imeegemea kwenye uharibifu na linahitajika jambo lenye nguvu litakaloondoa uharibifu huo na chuki. Dunia ya leo yenye kukatisha tamaa inahitaji upendo.
Ni kitu gani dunia inachokihitaji sasa? Ni upendo. Upendo ni dawa ya maradhi yaliyoikumba dunia yetu. Kwa hiyo, tumaini na faraja katika hayo, lililo kuu ni upendo. Ukikosa upendo unakuwa mtu asiyekamilika haijalishi ni kitu gani kingine ulichonacho.
Ni nani anayehitaji upendo? Hakuna maswali yoyote kuwa watoto wanahitaji upendo. Watoto wanajifunza upendo kwa kupendwa. Wazazi wanahitaji kupokea upendo kutoka kwa watoto wao. Babu na bibi wanahitaji upendo. Mwajiri na mwajiriwa wanahitaji kuwa na upendo. Marafiki wanahitaji upendo. Hata viongozi wa dini nao wanahitaji upendo pia.
Nani anahitaji upendo? Kila mtu anahitaji, ninahitaji. Watu wanakwenda mpaka pembezoni mwa nchi kutafuta upendo. Katika hali halisi kila mmoja anahitaji upendo. Upendo ni dawa katika maisha yetu ndiyo maana dunia nzima inautafuta.
Waliovunjika moyo na kukata tamaa nao wanahitaji upendo wa vitendo. Wakati mwingine unapoonyesha upendo kwa mwenzako inakuwa ni zawadi kwake.
Siku mmoja mtu na mkewe walikwenda katika kituo cha kulelea watoto yatima kwa ajili ya kuwafariji. Katika mahojiano waliyokuwa wakiyafanya na mmoja wa watoto hao, ambao waliwakabidhi zawadi mbalimbali walipowatembelea, kwa mshangao kijana huyo aliwaambia pamoja na zawadi alizopewa anahitaji mtu wa kumjali na kumpenda. Hivyo tunaona kuwa zawadi si kitu ila upendo ni burudisho na faraja ya moyo.
Pasipo upendo tunaangamia. Watu wengi sik`u hizi mioyo yao inaugua kwa kukosa upendo. Binadamu hatuugui miili na akili peke yake, lakini pia roho. Bila upendo tunaangamia.
Wivu, husuda, ghadhabu, hasira, chuki, kinyongo na vyote vinavyofanana na hivyo, vinazalisha magonjwa. Kutokana na hali hiyo hatuwezi kuwafanya wengine waugue kwa ajili yetu, lakini hisia hizo zinatufanya tuugue ndani ya miili yetu.
Hisia zote hizi binafsi naziita hasi, zinaweza kuwa chanzo cha matatizo pasipo na upendo hakuna mahusiano mema.
Tuangalie mfano mwingine wa mtoto ayemwambia mama yake kuwa ana rafiki ambaye anataka kumpeleka nyumbani kwao. Mama yake akamkubalia mtoto huyo amkaribishe rafiki yake kwa siku chache nyumbani kwao.
Mtoto alimwambia mama yake kuwa rafiki huyo ni mlemavu, ana mguu mmoja, mkono mmoja, jicho moja na uso wake hauko kwenye mpangilio uliozoeleka. “Ni sahihi nikimleta nyumbani?” aliuliza mtoto.
Mama alimwambia amkaribishe rafiki huyo kwa siku chache, lakini mtoto wake akahoji tena kwa mama yake “Mama hujanielewa?, ninahitaji kumleta rafiki yangu tuishi naye hapa siku zote!” majibu ya mama yalikuwa ni jinsi gani watakavyodharaulika na jamii na kutoa sababu nyingi endapo watampokea na kuishi na rafiki huyo mlemavu wa mtoto wake. Mtoto yule akahuzunika na kwenda kupumzika.
Muda mchache ulipopita mama yule akapata simu inayoeleza kuwa mtoto mwenye mguu mmoja, mkono mmoja, jicho moja na uso ambao hauko kwenye mpangilio amekutwa amejiua baada ya kujipiga risasi kichwani.
Hivyo tunaona na kujifunza kuwa watu wote wanahitaji upendo. Mtu anapokosa upendo hali inakuwa mbaya na kuwaza mambo mengi yasiyo na majibu.
Kila kitu kinakuwa kizuri upendo unapotawala. Kila kitu kinakuwa kizuri kwa jinsi yake kwa mfano mhandisi anaposimamia daraja na kukamilika linapendeza. Bwana afya anaposimamia usafi wa mazingira yakawa safi, kukufanya upumue hewa safi inapendeza.
Daktari naye anaposimamia upasuaji na kufanikiwa inapendeza, naye mtunza bustani anapoisimamia bustani yake maua yakachanua vizuri inapendeza na mwanamuziki anapoimba vizuri inapendeza pia. Hivyo kila jambo unalolifanya linakuwa zuri kwa jinsi yake.
Vyovyote iwavyo, popote utakapokuwa katika dunia hii jambo zuri ni upendo. Kumbuka upendo wa Mungu ni mkubwa kwa kuwa hauna mipaka, unatosheleza, unajitegemea, ni wa siku zote.Unapita maovu yote tuliyonayo.
Unapokuwa mtu wa upendo unapata afya katika maisha yako hali inayokuletea furaha ya kudumu. Bila upendo, mwanadamu anafanana na mnyama anayetafuta maisha yake mwenyewe. Ni wewe ndiye unayeweza kuwa na upendo au la.
Tunapotaabika, kusumbuka, kuwa na msongo wa mawazo tunakuwa kama chungu kilicho na ukoko. Lakini Mungu anataka tuondoke katika hali hiyo, kuwa huru na kuwa na upendo usio na mipaka.
Si kazi yetu kubadili tabia za watu wengine, bali ni kazi yetu kuwapenda. Hakuna nguvu yeyote inayoweza kutubadili maisha yetu isipokuwa upendo. Usiruhusu nafsi yako kuwa kama sufuria yenye ukoko. Fungua moyo wako na ongeza upendo tena na tena hata kwa wanaojaribu kuweka vikwazo katika harakati za maisha yao.
Upendo unabadili tabia. Unapoutoa upendo wako kwa wengine unakuwa msaada kwao na kukupa uponyaji. Tunavyozidi kuwa na upendo tunaishi maisha mazuri.
Ufanye upendo kuwa nguzo yako kuu katika maisha ya kila siku. Uache ukuongoze. Lengo lako kuu litafanya maisha kuwa na maana leo kuliko siku ya kesho ni upendo. Haijalishi ni jambo gani linalosababisha uufanye upendo kuwa lengo lako kuu. Kumbuka upendo ni nguzo ya kwanza.
Utakapotimiza lengo lako, maisha yatakuwa na mafanikio. Moyo wako utajaa furaha na amani kwa kubadilishana mawazo na wengine na kuwasaidia wasioweza kuwa na upendo, kujifunza kutoka kwako.
Kumbuka hakuna jambo kubwa zaidi ya upendo, hakuna jambo lenye nguvu zaidi ya upendo, hakuna uponyaji mwingine zaidi ya upendo, hakuna uzuri mwingine zaidi ya kuwa na upendo, hakuna utoshelevu katika maisha zaidi ya upendo. Kwa kuwa na upendo siyo kwamba utashinda, bali utaendelea kushinda siku zote.
Tukutane wiki ijayo.
lcyngowi@yahoo.com0713 3314550733 331455
Monday, June 16, 2008
UPENDO TIBA KWA MOYO MPWEKE
Posted in:
0 Maoni:
Post a Comment