KARIBUNI wapenzi wasomaji wetu katika safu hii tena leo, kwa wiki mbili zilizopita tumeona tabia ya mtu anayependa kutawala na mhamasishaji.
Leo tutaangalia tabia ya mtu asiyeyumbishwa katika maisha, mwenye misimamo yake binafsi na jinsi ya kuchukuliana na mtu mwenye tabia hii.
Mtu asiyeyumbishwa ni mfuasi mzuri na daima hutafakari sana kabla ya kufanya jambo lolote hata kama ni zito ambalo linahitaji maamuzi ya haraka.
Huwa makini katika kutenda, kuzungumza na kuachukua uamuzi katika mambo yake binafsi, yanayowahusu wengine katika sehemu yake ya kazi na katika jamii inayomzunguka.
Anapenda kukaa kimya kwa sababu anapenda kufahamu mambo ya wengine hata pasipo kuambiwa. Lengo likiwa ni kujifunza tabia, maisha ya watu na hufikiria jinsi ya kutatua matatizo ya wengine.
Anatunza mambo moyoni (msiri) na wakati mwingi hata kama akiwa na tatizo linalohitaji msaada si mwepesi wa kusema kwa wengine.
Huweza kusema au kueleza matatizo yake kwa wengine pindi hali inapokuwa mbaya, yaani anapokuwa ameshindwa kutatua tatizo lake.
Vilevile kwa sababu ya usiri wake, watu humwamini na kumuona kuwa ana hekima, hivyo huwa tayari kumuomba ushauri.
Si mwepesi kutoa siri za watu wanao kuwa wazi kumweleza matatizo yao.
Ni mwoga wa kuzungumza kutokana na tabia yake ya usiri na ukimya, hali inayosababisha asiweze kuzungumza mbele ya watu hata kama jambo linalozungumzwa analifahamu.
Kutokana na tabia yake ya ukimya na usiri, mtu wa aina hii huogopa kuzungumza kwa kuhofia kuwa huenda ataleta matatizo kwa mtu au kundi husika.
Anapenda sana kukaa na familia yake kwani huamini kuwa familia yake ndilo kundi pekee analoweza kuzungumza nalo kwa uwazi zaidi.
Anapenda sana kufanya kazi kwenye shirika kubwa kwa mafanikio, kwakuwa anapenda kazi anayoifanya itambulike, iheshimike na yeye apate malipo mazuri kutokana na kazi hiyo.
Hupenda kuuliza vizuri vizazi vya ukoo au familia yake kwani huwa na silika ya kutaka kufahamu ukoo wake na asili yake kwa ujumla.
Anajali usalama wake na familia. Kwa kuwa huwa na misimamo isiyoyumbishwa hupenda kujali usalama wake binafsi na familia yake.
Anaamini kuwa huweza kupanga taratibu na ratiba za maisha yake bila kumbughudhi yeyote yule.
Hapendi mabadiliko ya mambo yasije yakaharibika. Hupenda kusimamia katika maamuzi ya awali. Pia hapendi anapopanga jambo yawepo mabadiliko ya mara kwa mara kwa sababu ana msimamo na kujiamini katika mambo mbalimbali.
Watu wenye tabia hii mara nyingine huwa sahihi japo kuna wakati inabidi alegeze kamba kwa manufaa ya wengine. Ni vizuri kumwelewa mtu wa aina hii ili usipate shida ya kuishi naye, kushauriana naye hata kufikia muafaka wa pamoja.
Hupenda kila kitu kiende salama. Kwa kuwa ni mtu mwenye misimamo thabiti hupenda mambo yote yaende kama yalivyopangwa.
Hafurahii mabadiliko yanayojitokeza ya mara kwa mara katika mipangilio inayopangwa na yeye, familia au jamii inayomzunguka.
Mara nyingi kwenye makusanyiko ya watu wengi huwa hakosekani mtu mwenye tabia hii.
Huepuka sana magomvi, migongano au kukosana na wengine.
Mara nyingi huepuka tabia ya ugomvi au migongano inayoweza kujitokeza. Hivyo hutafuta njia ya kutatua tatizo kabla halijawa kubwa.
Hujitahidi sana kuficha mambo yanayo muumiza moyoni. Kwa kuwa hapendi kuonekana mtu asiyeyumbishwa. Mara nyingine huficha maumivu yanayompata kwa kuwa anaona kikundi fulani au jamii inayomzunguka inapingana na maamuzi ya awali. Kwa kuepusha shari hujitahidi kutokujulisha hali aliyonayo kwa wakati huo.
Si vigumu sana kwake kusamehe makosa. Ni mtu mwenye kuachilia jambo kwa haraka moyoni kwake. Hupenda kuwa na amani na watu wote mara zote. Hupenda kuchangia hoja na kujenga hoja thabiti, hivyo atakapokuwa si mwepesi wa kusamehe itakuwa vigumu kutoa msimamo wake.
Anapenda sana kufahamu matokeo ya kila jambo kabla ya kutolewa kutokana na tabia yake ya ukimya na kutafakari kwa kila jambo, tabia hii husababisha awe mdadisi wa mambo yaliyofichika na hupenda kuyafahamu kabla hayajatokea.
Ni mtu mwenye msimamo, ana uhakika na kile anachokisema kutokana na umakini wake wa kufanya mambo baada ya kutafakari.
Hawezi kuyumbishwa na mtu au au jambo lolote linalohusu maamuzi binafsi au maamuzi ya jumla.
Ni mtu ambaye ni rahisi kufanya kazi na watu wengine wenye tabia mbalimbali. Kutokana na tabia yake ya ukimya, mtu wa aina hii anaweza kuchanganyikana na watu wa tabia mbalimbali.
Kazini mwake ni mfanyakazi mzuri kwa kuwa ana penda kufanikiwa katika kila kazi anayofanya, hufanya kazi kwa bidii, juhudi na maarifa na kuonyesha ufanisi mkubwa wa kazi ama ya kuajiriwa au kujiajiri mwenyewe.
Ana moyo wa kujitolea kwenye shirika. Mtu wa aina hii mbali na tabia yake ya ukimya, anawajali wengine na hupenda kutoa mchango wake kwa shirika kwa faida ya jamii.
Pia anapenda kusaidia wenye shida mbalimbali na husononeka anapoona mtu ananyanyaswa na kubaguliwa katika jamii.
Mara nyingi mtu wa aina hii anapokuwa na uwezo kifedha, huwa na moyo wa kusaidia wasiojiweza kama vile walemavu, yatima, wajane nk. Pia huwa na moyo wa kuwaendeleza wengine kielimu na hufurahi anapo ona wengine wanafanikiwa katika maisha yao.
Anafanya kazi kwa utaratibu na utulivu. Kutokana na tabia yake ya kujiridhisha kwa kila kazi anayoifanya, huweza kufanya kazi kwa utaratibu na utulivu, hali inayosababisha afanikiwe katika utendaji kazi wake.
Hupenda kufanya kazi kwa kufuata taratibu zilizopo katika eneo lake la kazi na hupenda kukamilisha kazi anazopanga kufanya kwa siku.
Ni mwangalifu sana anapofanya mambo. Anaogopa na hujisikia vibaya pale mambo yanapokwenda kombo, hivyo hufanya kazi kwa uangalifu mkubwa ili kuhakikisha kuwa mambo yanakwenda vizuri.
Tafadhali jua tabia yako.
Tukuatane wiki ijayo.
ngowi2001@yahoo.com0713 331455
Sunday, June 15, 2008
USIYUMBISHWE KATIKA MAISHA
Posted in:
0 Maoni:
Post a Comment