Monday, December 8, 2014

Kipozi: Uhuru wa habari si upotoshaji



Na Mwandishi Wetu
MKUU wa Wilaya ya Bagamoyo ambaye pia ni mwanahabari, Ahmed Kipozi amesema kuwa uhuru wa vyombo vya habari maana yake si upotoshaji wa habari.
Kipozi ambaye pia ni mtangazaji mkongwe enzi za iliyokuwa redio Tanzania, televisheni ya ITV pamoja na redio Uhuru, alisema hayo katika mkutano mkuu wa Watangazaji kwa mwaka huu, ulioandaliwa na Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), Jijini Dar es Salaam.
Alisema hivi sasa sekta ya habari imekuwa, na kwamba utangazaji unabeba utaifa na uzalendo hivyo lugha zinazotumika kwa miaka ya sasa zimebadilika tofauti na ilivyokuwa zamani.
“Uhuru wa habari maana yake si upotoshaji, lugha, nidhamu ya utangazaji vimebadilika. Ukumbuke kuwa mtangazaji unapotangaza unajibeba mwenyewe pia unabeba taifa,” alisema Kipozi.
Aliongeza kuwa, hivi sasa watangazaji wengi wanaweza kutangaza lakini hawafikishi ujumbe uliokusudiwa tofauti na ilivyokuwa miaka ile ya zamani.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa TCRA Profesa John Nkoma alisema kuwa mabadiliko makubwa ambayo yametokea katika karne hii ni utangazaji wa kutumia teknolojia ya kidijiti.
Na kwamba mfumo huo wa kidijiti umeleta mabadiliko makubwa kwenye maisha ya kila siku kwa sasa unaweza kupata matangazo ya televisheni mahali popote kwa kutumia vifaa mbalimbali kama vile kompyuta, simu za mkononi na kompyuta ndogo za mkononi kwa kupitia mfumo wa intaneti.
Aliongeza kuwa kwa kipindi c ha miaka 20 iliyopita sekta ya utangazaji imekuwa kwa kiwango cha haraka hadi kufikia mwaka huu kuna vituo vya televisheni 28 na redio 94.
mwisho

watumiaji wa simu kudhibitiwa

Na Mwandishi Wetu
WAZIRI wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia Profesa Makame Mbarawa ameagiza wataalamu  kutayarisha mwongozo kwa ajili ya kampuni za simu, utakaoelekeza jinsi ya kutuma meseji katika kipindi cha kuelekea uchaguzi mkuu mwakani.
Mbarawa alisema jana alipokuwa akifungua mkutano wa kuadhimisha siku ya  Teknolojia ya Habari na Mawasiliano ya Jumuiya ya Mawasiliano Afrika, Jijini Dar es Salaam, ulioandaliwa na Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA).
Waziri Mbarawa alisema, mwakani ni kipindi cha uchaguzi hivyo kuna baadhi ya watu wamekuwa wakitumia simu kutuma meseji ambazo zinaweza kuhatarisha usalama wa raia.
“Watu wanatuma meseji hizo, nimeshawaagiza wataalamu kutoka wizarani na TCRA kwa ajili ya kuandaa mwongozo huo kwa ajili ya kutuma meseji kwa sababu teknolojia imekuwa, watu wanaweza kuitumia vibaya,” alisema.
Vile vile alivitaka vyombo vya habari vitumike kuwaelimisha wananchi vizuri kuhusu masuala ya uchaguzi kwa kutahadharisha kuwa mwongozo walioupata usiwe kwenye makaratasi tu bali wautekeleze.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa TCRA Profesa John Nkoma alisema kuwa, hivi sasa Tanzania imepiga hatua kubwa kwa kuwa wanaotumia kadi za simu ni milioni 28, mtandao wa mawasiliano ni milioni tisa ikiwa na pamoja na ukuaji wa huduma za simu ambazo zimewezesha kutuma na kupokea fedha.
Pia alisema serikali imewekeza dola milioni 200 katika mkongo wa taifa kwa ajili ya maboresho kwenye upande wa utangazaji.
mwisho

Chuo Kikuu chatoa zawadi kwa wanafunzi

Na Mwandishi Wetu
CHUO Kikuu Ardhi (ARU) kimewazawadia wanafuzi 130 wa masomo mbalimbali zawadi zenye thamani ya zaidi ya shilingi mil. 60 kutokana na ufaulu mzuri katika masomo yao.
Zawadi hizo ni fedha taslimu, mashine za upimaji ardhi na laptop katika hafla fupi iliyofanyika chuoni hapo Jijini Dar es Salaam.
Akikabidhi zawadi hizo, Makamu Mkuu wa chuo hicho Idrissa Mshoro alisema kuwa wanafunzi wa kike wameendelea kufanya vizuri katika masomo yao ambapo wamefikia wastani wa asilimia 40 dhidi ya asilimia 30 kwa wanaume.
Alisema miongoni mwa wanafunzi waliopata zawadi hizo hawakuwa na sifa za kujiunga katika chuo hicho mpaka walipopewa kozi fupi ambapo baada ya usaili walifaulu.
Profesa Mshoro alisema kuwa waliamua kuwa na mfumo huo baada ya kuona wanafunzi wengi wanataka kujiunga na chuo hicho kwa ajili ya elimu ya juu lakini alama zao walizopata katika shule walizokuwa wanasoma haziwawezesha kujiunga.
Kwa upande wake Makamu Mkuu wa Taaluma chuoni hapo, Gabriel Kassenga alisema kuwa matokeo ya mwaka huu yameendelea kufuta dhana kuwa wanawake sio wazuri katika masomo ya sayansi.
“Wameonyesha uwezo mkubwa kwa kutwaa zawadi nyingi kuliko wanaume na hiyo ni dalili kuwa sayansi sio ya wanaume pekee” aisema na kuongeza kuwa hata mwaka jana wanawake waliongoza kwa kupata tuzo nyingi za kitaaluma kuliko wanaume.
Mwisho………………

ARU kudahili wanafunzi zaidi ya 7000

Na mwandishi wetu 
Chuo Kikuu Ardhi (ARU) kinatarajia kudahili wanafunzi 7700 ifikapo 2016/17.
Mwenyekiti wa Baraka la Chuo Kiki Ardhi Tabitha Siwale alisema hayo kwenye mahafali ya nane yaliyofanyika jijini Dar es Salaam. 
Alisema ili mpango huo utekelezwe chuo hakina budi kuongeza idadi ya wahadhiri na wafanyakazi wengine, kupanua miundombinu pamoja na kuongeza vifaa vya kujifunzia na kufundishia. 
"Chuo bado kinakabiliwa na changa moto mbalimbali zikiwemo idadi ya wahadhiri, uchakavu wa miundombinu, upungufu wa vyumba vya miha dhara, maabara, malazi kwa wanafunzi na nyumba za wafanyakazi, "alisema. 
Siwale alisema ili mpango huo utekelezwe zinahitajika shilingi bil 44 katika miaka mitatu ijayo. 
Kwa upande wake Makamu Mkuu Wa ARU, Profesa Idrissa Mshoro alisema kuwa katika mahafali hiyo wanafunzi 964 walihitimu ikilinganishwa na 483 wa mwaka jana. 
Alisema mafanikio hayo yanatokana na ongezeko la udahiliwa wanafunzi ambalo lilianza kukua kwa kasi zaidi mwaka 2010/11. 
Alisema ili kufikia malengo waliojiwekea mwaka wa masomo 2015/16 wanatarajia kuongeza udahili na kufikia 7741. 
Mwisho

NHC kutatua matatizo ya wananchi



Na Mwandishi Wetu
MKURUGENZI Mkuu wa Shirika la Nyumba  nchini (NHC), Nehemia Mchechu, amesema kuwa wanaiangalia miradi waliyonayo ni jinsi gani inaweza kutatua matatizo waliyonayo wananchi.
Mchechu alisema hayo jjijini Dar es Salaam, alipokuwa akizungumza katika mjadala ulioandaliwa na Chuo Kikuu Ardhi (ARU), wakati akiwasilisha mada yake.
Alisema NHC inaangalia ni jinsi gani watengeneze vitovu vya miji ambavyo kutakuwa na makazi ya watu, biashara mbalimbali pamoja na ofisi ili kumpunguzia mwananchi usumbufu wa kutembea muda mrefu.
“Je NHC katika miradi yao wanafanya nini ili wananchi waishi vizuri? Tunachoangalia miradi yetu tuliyonayo ni jinsi gani inaweza kutatua matatizo na kurahisisha huduma kwa wananchi,” alisema Mchechu.
Mchechu alisema kuna miradi Kawe ‘apartment’ iliyopo Dar es Salaam ambayo itawezesha watu kupata mahitaji yote kwa pamoja.
“Ukimfanya mtu akaishi na kufanya kazi karibu na ofisi, ataongeza kipato na kupunguza matumizi kwa kuwa hatasafiri tena mwendo mrefu kwa ajili ya kuwahi kazini, pia itafanya awe na afya bora kwa kupunguza msongo unaotokana na foleni,” alisema Mkurugenzi huyo.
Naye Profesa Lusugga Kironde ambaye anashughulika na masuala ya Maendeleo ya Ardhi na Uthamini (ARU),alisema kuwa siku hizi watu wanakuja mjini kuishi siyo kuondoka tofauti na zamani, hivyo wanaangalia masuala ya kazi, makazi na jinsi wanavyojitambua ili kuwezesha waishi vizuri.
Pia alishangazwa na kitendo cha kuvunja majengo ya zamani na kuwekwa mapya kwa kuwa kinadhoofisha fursa za utalii.
mwisho

Twitter Facebook