Sunday, June 15, 2008

UAMINIFU NI KITU MUHIMU KATIKA MAISHA

KARIBUNI tena wapenzi wasomaji wa safu hii ya kila Alhamisi. Wiki iliyopita tuliendelea kuzungumzia kanuni au mbinu nyingine za kuishi na watu vizuri, leo ni mwendelezo wa pale tulipoishia.
Mara zote jifunze kuwa mwaminifu katika mambo yote, hasa mambo madogo madogo. Kuna watu wengine neno uaminifu katika maisha yao halipo kabisa.
Kumbuka kuwa uaminifu si katika mambo makubwa tu, hata kwa jambo dogo unapokuwa mwaminifu unajijengea heshima katika jamii.
Epukana na upendeleo wa namna yoyote kama ukabila, ukoo, udini au jinsia. Upendeleo wa namna yoyote unaozingatia mambo yaliyo hapo juu, haufai katika jamii yetu ya sasa.
Hebu fikiria katika ofisi, waajiriwa mnakuwa wote ni kabila moja, ukoo mmoja au jinsia moja, mara nyingi hali hiyo haipendezi kwa kuwa kutakuwa na hali ya upendeleo.
Epuka tabia ya kusema uongo au kumsingizia mtu. Watu waongo ni kama wauaji, huwa hupenda kuchongea wenzao, ili wao waonekane wema au ni bora kuliko wenzao.
Tabia hiyo inaweza ikakusababisha ukagombana na familia yako, majirani zako, wanafunzi wenzako au wafanyakazi wenzako. Uongo si mzuri katika maisha, jifunze kusema kweli daima.
Jifunze kuheshimu mamlaka ya dini na serikali mradi hazipingani na amri za Mungu. Heshima ni jambo zuri katika maisha.
Mtu yeyote anayeheshimu viongozi wake wa dini au serikali, huyo ni mwadilifu. Japo mara nyingine viongozi hao wanaweza kukosea, omba ushauri kabla hujatenda lolote.
Tunza mwonekano, jenga tabia ya usafi. Hapa ndugu zanguni unadhifu umewashinda watu wengi, japo wapo wengi walio nadhifu sana. Baadhi ya watu wamejijengea tabia ya uchafu katika maisha yao yote.
Ukimfuatilia mtu huyo utakuta kuanzia nyumbani kwake ni mchafu, mazingira yanayomzunguka pamoja na mwili wake anashindwa kabisa kuhudumia. Usafi si fedha, kwa hicho kidogo ulichojaliwa waweza kuwa msafi.
Katika eneo hili la usafi, mara nyingi wanawake wanahusika moja kwa moja, kwani wao ndio kioo cha familia. Mwanamke anapokuwa msafi na familia yake, nyumba yake vyote vitakuwa safi. Lakini, atakapokuwa mchafu, hata wote wanaomzunguka wasipokuwa makini watakuwa wachafu.
Lakini cha kushangaza kuna baadhi ya wanawake wanajihusisha na biashara ya maandazi, chapatti, vitumbua, samaki na vitu kama hivyo, lakini ukifuatilia kwa umakini utagundua kuwa walio wengi hawazingatii kanuni za afya. Kumbuka mwanamke ni kioo cha jamii, hivyo kuwa mwangalifu katika maeneo yote yanayokuzunguka.
Katika maongezi yako na watu, usionyeshe kuwa unajua kila kitu. Hali ya kuwa msikilizaji na kuchangia hoja inapobidi itakujengea hali ya kuheshimika, lakini unapoonyesha hali ya kujua kila kitu unapokuwa unazungumza na wenzako, italeta mushkeli kidogo.
Yawezekana kweli unajua kila mnachozungumzia unapokuwa na wenzako, toa nafasi kwao nao waweze kuzungumza na kuwaonyesha kuwa nao wanauelewe na jambo hilo.
Epuka tabia ya kuchafua majina ya watu. Watu wengine hupenda kuchafua majina ya wenzao kwa kuwasema vibaya. Si nzuri tabia hiyo iache, kwani inaepukika.
Jifunze kupenda watu wasiopendeka, mfano watu wenye ulemavu na masikini. Katika imani ya Kikristo tunaona katika maandiko matakatifu kuwa, Yesu alipenda wenye dhambi na watoza ushuru.
Kumbuka watu hao ambao mara nyingi hutengwa na jamii huitaji upendo, hivyo ni vizuri kuwa karibu nao na kuwapenda ili wasijisikie vibaya.
Epukana na tabia ya chuki au fitina na uadui kwa watu. Usimchukie mtu ambaye hajakutenda jambo lolote, na hata kama imetokea akakukosea mwite na kumweleza kuwa jambo alilolitenda si zuri.
Fitina nayo si nzuri, usimfitini ndugu yako, rafiki yako, mfanyakazi mwenzako au mwanafunzi mwenzako kwa jambo lolote lile.
Tabia hiyo ni mbaya. Usipende kujenga uadui, si tabia njema. Jifunze kujenga tabia ya upendo kwa kila mtu kama vitabu vya dini vinavyotusisitiza.
Kumbuka kutimiza ahadi zako zote ama sivyo usitoe ahadi. Unapotoa ahadi yoyote ile jitahidi uitimize, kufanya hivyo kutakuongezea kuaminika katika jamii. Wapo watu mabingwa wa kutoa ahadi, lakini hazitimiziki.
Kama unajua kuwa huna uwezo wa kutimiza ahadi yako ni bora usiitoe kwa kuwa inakuondolea uaminifu. Subiri mpaka utakapoona una uwezo huo ndipo uahidi na kutimiza.
Epuka tabia ya kuchonganisha watu. Kuna watu wao kazi yao ni uchonganishi. Wengi wao hawajitambui kama wako hivyo, lakini kuna wengine wanaojitambua hali hiyo, lakini wanaiendeleza kwa kudhani kuwa wanapendwa.
Tabia ya uchonganishi mara nyingi iko kwa wanawake, japo si wote. Wengi hupenda kudodosadodosa mambo yako na kuyazungumza tofauti. Jihadhari na tabia hiyo inakuvunjia heshima.
Epuka tabia ya uzushi, kamwe usieneze habari ambazo huna uhakika nazo na ukweli wa mambo. Usipende kuzungumzia jambo usilolijua kwani linaweza likamharibia mtu sifa yake.
Jaribu kuzungumza jambo lile ambalo una uhakika nalo, hata utakapoitwa na kuulizwa una uwezo wa kulithibitisha. Tabia njema itakuongezea hali ya kuaminiwa katika jamii inayokuzunguka.
Uwatakie wengine mafanikio na epuka tabia ya kuonea wivu wengine. Penda mafanikio ya watu wengine. Kamwe usiwe na tabia ya kuwaonea wivu wengine. Kila unapopata taarifa ya mafanikio kwa ndugu, jamaa au rafiki yako furahi pamoja naye na ikibidi umpongeze kwa zawadi au kadi.
Jifunze kuwa na kiasi katika mambo yote na epuka tabia ya kuzidisha mambo. Kuwa na kiasi katika mambo yako ni jambo zuri.
Mfano kwa upande wa mavazi ya akina mama kupasua kidogo ni vizuri kuliko kupasua nguo yako hadi kupitiliza na kusababisha kelele zisizo za msingi kutoka kwa vijana walio wahuni. Kama ni kujipodoa ni vizuri ukajipodoa kwa kiasi na si kupitiliza hadi ukatisha.
Hiyo ni mifano michache, lakini iko mifano mingi kwa jinsia zote la muhimu ni kuwa na kiasi katika mambo yote.
Epuka tabia ya kuaibisha wengine. Hapa kama unamwona mwenzako amekosea mwite na kumweleza kwa taratibu, lakini si tabia nzuri kumweleza kwa sauti kubwa na kuwapa faida wale wasiohusika.
Tukutane wiki ijayo.
Kwa maoni, ushauri wasiliana nami kwa simu; 0713 331455 au barua pepe; ngowi2001@yahoo.com

0 Maoni:

Twitter Facebook