Monday, June 16, 2008

EPUKA KUJIHURUMIA UPATAPO MATATIZO

“HAKUNA anayenipenda, kila mtu ananichukia, utafikiri nimekula kitu kibaya, na kwa sasa sifanyi mzaha”
Msemo huo husemwa na watu ambao wanaonyesha jinsi gani wanajihurumia kutokana na maumivu waliyoyapata kwa kumpoteza mtu ambaye alikuwa muhimu kwake. Mfano mke au mtoto wake.
Ukiwa katika hali hiyo, hakuna mtu ambaye anaweza akajua maumivu unayoyapata. Na wala hawezi kujali kutokana na kwamba hajui kilichokusibu au kinachokusumbua.
Kumbuka unapokuwa na matatizo adui wako wa kwanza ni ile hali ya wewe mwenyewe kujisikitikia.
Kujisikitikia ni ile hali unayojisikia baada ya kupatwa na janga ambalo hukulitarajia.
Kujihurumia ni ile hali ya kukumbana na majaribu ya mara kwa mara ambayo hukuyatarajia wala kuyazoea kama vile kumpoteza umpendaye, kuachishwa kazi, kukabiliana na hali mbaya ya kiuchumi, kuvunjika kwa ndoa yako, watoto wako kuondoka nyumbani, wakati daktari anapokuambia kuwa una ugonjwa hatari usiotibika katika kipindi hicho mtu huwa katika hali ya kujihurumia, ukubali ukweli huo au ukatae, hiyo ndiyo hali halisi itakayokutokea.
Hali hiyo usipoigundua itachukua muda mrefu kwisha katika maisha yako zaidi ya vitu ambavyo vimekutokea.
Kutokana na hali hiyo iliyokutokea unaweza ukaepukana nayo endapo utakubali kuondokana nayo.
Hali hiyo haiwezi kukujengea heshima bali kuiondoa. Pia haiwezi kukuweka huru kutokana na hali ya kutokuwa na furaha ya kipindi kilichopita bali hukuweka katika hali ya utumwa.
Hali hiyo huvunja moyo. Hivyo usikubali kuwa katika hali hiyo ambayo itakusababisha kukupa maumivu ya moyo.
Mfano, mtu anapokuwa na matarajio makubwa ya kufanya biashara, kuwa na maisha mazuri na kujenga nyumba nzuri, kutokana na matarajio hayo akafanikiwa.
Kwa bahati mbaya mambo yakabadilika baada ya biashara zake kwenda mrama hivyo akapatwa na mfadhaiko. Kila mara akawa ni mtu wa kujisikitikia.
Je, wajua ni kwanini hali hiyo ilimtokea? Ni baada ya kujionea huruma nafsi yake na kushindwa kuendelea mbele katika hali ya kupambana na maisha.
Kwa hiyo unachotakiwa kufanya ni kusimama imara na kukabiliana na hali hiyo, hivyo utajikuta hali ya huzuni inaondoka.
Hali ya kujionea huruma inakuletea mfadhaiko. Yakupasa uondokane na hali hiyo uweze kushinda.
Unapokuwa na matatizo usifikirie kufanya jambo ambalo hukutarajia. Mfano baba yako amefariki dunia mkabaki na mama ambaye baada ya kufiwa na mumewe anaamua kuuza nyumba.
Kumbuka kwa wakati huo hali hiyo haitokani na maamuzi yake binafsi ila ni katika ile hali ya kujisikitikia na kuona kuwa hataweza kuimudu familia peke yake.
Hali hiyo inachangia kuvunjika kwa mahusiano yako na watu wengine. Kwa mfano unapokuwa na masikitiko kila wakati kunakusababishia unakuwa mtu wa kulalamika kila wakati, kitu ambacho kinasababisha kukimbiwa na marafiki zako.
Hali hiyo pia inakurudisha nyuma kimaendeleo.
Unaporuhusu hali hiyo kuondoka, mafanikio yako yataonekana. Kumbuka kila mara unapojionea huruma hakuna chochote utakachoweza kukifanya. Kusikitika si njia ya kukufanya ujisikie vizuri.
Je, wataka mambo yako yawe mazuri? Chukua hatua zifuatazo. Jiulize mwenyewe hali hiyo imefanya jambo lolote zuri kwako?
Je, imebadilisha mambo yaliyokutokea? Hapana. Je, hali hiyo imebadilisha mambo mabaya yaliyokutokea kuwa mazuri? Hapana. Je, hali hiyo imekufanya ujisikie vizuri?
Je, hali hiyo imekufanya kupendwa? Je, hali hiyo imekujengea mapenzi na heshima? Je, hali hii imeniletea mafanikio na uhodari? Je, hali hiyo imekuweka karibu na wengine? Je, hali hiyo imekuongezea kupendwa na wengine? Je, hali hiyo imekujengea uwezo? Je hali hiyo imekuponyesha majeraha uliyoyapata? Je, hali hiyo imekuwezesha kuelewana na wenzako?
Hata iweje, hali hiyo haiwezi kukuongezea kitu zaidi ya kukuzidishia maumivu na kukufanya mnyonge.
Kama unataka kuendelea kuwa na huzuni, kuwa na masononeko, kutokuwa na marafiki, kuwa mgonjwa, kuwa na matatizo ya mara kwa mara, hivyo endelea kujisikitikia lakini kama unataka kujisikia kuwa na maisha mazuri amua kuachana na hali hiyo.
Ili kuondokana na hali hiyo yakubidi ufanye yafuatayo:
Kwanza, yakupasa uigundue hali hiyo haraka na baini kilichosababisha hali hiyo. Hali ya ubinafsi inasababisha kuwa katika hali ya kujisikitikia.
Kuona kila kitu kinakwenda vibaya na hakuna hata kimoja kilicho sahihi. Jitahidi kuondokana na hali hiyo itakuongezea majuto.
Pima uwezo wako kupambana na hali hiyo kwa kuchagua kipi bora zaidi ya hali inayokukabili.
Mfano, kuna kijana mmoja ambaye ni mchezaji bora wa mpira wa miguu, alifiwa na mama yake siku chache kabla ya kuwa na mashindano makubwa.
Kocha wa timu ambayo alikuwa akichezea kijana huyo hakujua afanye nini baada ya tukio hilo, kwa kuwa alikuwa ndiye wanayemtarajia katika mechi iliyokuwa mbele yao, na hakuna mwingine aliyekuwa na uwezo kama wa kijana huyo.
Siku ilipowadia ya mechi hiyo kijana huyo alijitokeza na kuwa miongoni mwa wachezaji wenzake, pamoja na msiba mkubwa aliokuwa nao kijana yule aliondokana na hali ile ya kujisikitikia na kudhamiria kucheza mechi ile. Alicheza vizuri kuliko siku zote na kuipatia timu yake ushindi.
Habari hiyo inaelezea kuwa haijalishi ni hali gani unayokumbana nayo, cha msingi ni kuikataa hali ile inayokufanya kuwa mnyonge au kujisikitikia.
Kama kijana huyo angekaa chini na kuanza kulia, angejisababishia huzuni katika nafsi yake na kuwafanya wenzake wamsikitikie.
Pia angeisababishia timu yake kukosa ushindi. Ni kweli inaumiza katika hali ya kibinadamu, hasa mambo mabaya yanapotupata lakini inabidi kuikataa hali hiyo ya kukuletea huzuni, majonzi na hali ya kujihurumia.
Fanya mazoezi ya viungo. Mazoezi ya viungo yana faida kwa maisha ya mwanadamu. Mfano kuna baba mmoja alifiwa na mke wake. Anasema alikuwa katika hali ya kuchanganyikiwa asijue la kufanya, ndipo alipotokea rafiki yake ambaye alitaka kumsaidia.
Alizungumza naye juu ya kujiunga na sehemu ya kufanyia mazoezi ya viungo ambapo alikuwa akimpitia kwa wiki mara tatu na kumpeleka sehemu hiyo.
Anasema rafiki huyo alimsaidia sana kwa kuwa aliacha kuwaza juu ya matatizo yaliyomkuta. Mwili wake ulianza kuimarika, kubadilika na kujengeka upya. Anasema mazoezi hayo yalimfanya mwili wake uchoke na kupata usingizi usiku alipolala.
Jambo jingine, tarajia maumivu fulani ya moyo wakati wa zoezi hilo. Kumbuka ni juhudi zinazomfanya mtu awe na nguvu. Ni mambo magumu yanayomfanya mtu abadilike. Pia ni vikwazo vinavyomfanya mtu apate changamoto kubwa na fursa nzuri.
Ni vizuri kuwekeza mawazo au malengo yako yote kwa kile ukipendacho, si kwa kile ulichopoteza. Watu wengi hupatwa na maumivu kwa kuwa wamesimamia katika upungufu wao, kupoteza na vikwazo wanavyokutana navyo. Hilo ni tatizo kubwa kwa watu wengi.
Jitolee kuwahudumia wengine. Njia mojawapo ya kuondokana na hali hiyo ni kwenda kuwatembelea ndugu, jamaa na marafiki majumbani kwao. Unapofanya hivyo unajikuta unasahau mambo yaliyokupata.
Usiwe katika hali ya kujihurumia unapopatwa na matatizo ili usiache nafasi ya wengine kukuhurumia.
ngowi2001@yahoo.com0713 331455073 2331455

0 Maoni:

Twitter Facebook