WIKI iliyopita tuliweza kuona tabia za mtu anayependa kutawala. Leo tutaangalia tabia ya mtu anayependa kuhamasisha.
Mhamasishaji hupenda watu. Hupenda kuongea nao, pia huwa na mvuto kwa watu wanaomsikiliza.
Ni mwenye furaha kila wakati. Kwa kuwa hupenda kuwahamasisha wengine mara zote hujitahidi kuwa mwenye furaha.
Pia ni mshawishi. Hupenda kushawishi watu wengine. Mtu huyu hupenda kuwashawishi watu wengine ili wafuate vile alivyokusudia. Kama kuna kazi ya kufanya huwahamasisha wenzake wasiione ile kazi kama ni ngumu bali ni nyepesi.
Mfano katika matukio ya misiba huwahamasisha waombolezaji waimbe wasiwe wanyonge na kuifanya familia ya wafiwa kujihisi upweke zaidi. Kama ni matukio ya harusi huwahamasisha washerekeaji kuchangamka na kuifanya sherehe hiyo kuwa ya furaha.
Anapenda kuzungumza, kusalimu. Mara nyingi mtu huyo hupenda kuzungumza na watu wote. Ndivyo alivyo, huwezi kumbadilisha ili mradi aweze kujijengea mazingira bora zaidi katika uhamasishaji wake.
Mtu huyu hupenda kusalimu watu. Mara zote hupenda kuwa karibu na watu na kuzoeana na watu, hii huchangia kujipatia marafiki wengi na kujulikana zaidi kutokana na alivyo. Ndivyo alivyo, huwezi kumbadilisha.
Hupenda wengine wajisikie vizuri. Watu wenye tabia hii hupenda wenzao wajisikie vizuri. Hawapendi kuwaona watu wakiwa katika hali ya masikitiko, huzuni, na kukata tamaa ya maisha, hutumia fursa hiyo kuwahamasisha ili waweze kuwa na changamoto mbalimbali za maisha na jinsi ya kukabiliana na hali walizonazo.
Anajali sana shida na matatizo ya watu. Ni kweli watu hawa hujali wenzao na hawapendi kumwona yeyote akiwa katika shida au matatizo. Inapotokea anakutana na mtu mwenye shida au matatizo Fulani, hujitahidi kuwa karibu naye ili aweze kumsaidia kwa kumwondoa katika hali hiyo.
Msaada huo unaweza kuwa wa kumpa ushauri kwa kumwelekeza njia sahihi za kutatua matatizo yake na mara nyingine humsaidia uhitaji wake kwa matendo pale anapoweza.
Hupenda sana kusaidia watu. Tabia yake ya kuwa mhamasishaji inamfanya awe na moyo wa kuwasaidia wengine wenye uhitaji.
Mwepesi wa kusisimuka (kuumia). Mwenye tabia hiyo huwa mwepesi wa kupata hisia. Inaweza kuwa hisia nzuri kama furaha. Pia anapopatwa na jambo la kumuumiza huonyesha hisia zake kwa haraka.
Ni mnenaji mzuri. Hupenda kuongea na watu mbalimbali wa rika zote. Mara zote anapokuwa anazungumza na watu hao kulingana na rika zao, hujitahidi kusoma mawazo yao na kuitumia saikolojia hiyo kuwafikishia ujumbe kwa hoja zenye mvuto chanya unaoweza kubadili misimamo yao na kukubaliana naye.
Huepuka kufanya kazi kama hajisikii. Kwa kuwa hupanga kutekeleza mipango yake kwa ufanisi, daima hufanya kazi zake kwa juhudi, maarifa na kujituma zaidi. Hata kama kuna jambo lina mkwaza, hujitahidi kuliondoa bila visingizio na manung’uniko.
Kwa kuwa hupenda kuwa mhamasishaji mzuri, anapokuwa na uchovu au anapoona hawezi kufanya kazi fulani kwa wakati huo, huepuka kufanya kazi hiyo ili asionekane tofauti na tabia yake ilivyo.
Endapo atajilazimisha kufanya kazi hiyo, inapoharibika hujisikia vibaya, ndiyo maana huepuka kufanya kazi kama hajisikii kufanya hivyo.
Hupenda kukaa upweke nyumbani, jambo linalosababisha achukue muda mwingi akiwaza namna ya kubuni mikakati mbalimbali ya kumsaidia kutekeleza kazi zake.
Anapenda kusikiliza (anafuatilia), maoni na ushauri wa watu wengine, hali inayomsababisha awe katika nafasi nzuri ya kujifunza kutoka kwa watu wengine. Pia kutokana na hali hii, mhamasishaji yuko tayari kubadilisha mtazamo na mawazo ya watu kuelekea katika hali bora zaidi juu ya lengo tarajiwa.
Hapendi kuishi mbali na watu ili aweze kusoma mazingira yao na kuyatumia katika kubadilisha msimamo wao kadiri anavyoona inafaa.
Unajisikia huru kuwa naye kwa sababu ni mtu anayependa kuchanganyana na watu wa rika zote, (social), jambo linalosababisha apendwe na kukubalika na wengi.
Hapendi ukimya, hupenda vichekesho na kutokana na tabia hii, basi huvuta hisia za watu anaokutana nao. Hata kwa wale walio na msongo wa mawazo wanapokutana na mtu wa aina hii, hupata faraja na wakikaa naye kwa muda mrefu, hupata ahueni katika matatizo yao.
Hujisikia vibaya sana kunapokuwa na ukimya, kwani kwenye ukimya usiokuwa na tafakari ya jambo lolote la maana hasa katika kundi la watu, mawazo mabaya hujitokeza.
Kwenye mabaraza na mikutano huwa msemaji sana kama nilivyosema hapo awali, kabla ya kusema, mhamasishaji husoma mawazo ya kundi alilopo na kutumia mawazo yao kujenga hoja chanya au hasi kulingana na matakwa yake.
Huwa hajali sana njia za kufanya kazi na kufanya vitu vidogo vidogo, jambo linalosababisha asionekane kuwa mtu aliye mbali na jamii.
Ni mwoga kutopoteza copy right. Vile alivyo, hupenda kuwa hivyo hivyo bila kupoteza asili yake. Hupenda kupendwa na watu wanaomzunguka.
Anapenda atambuliwe, kwa kuwa kutokana na tabia yake, hupenda sana atambuliwe na jamii kutokana na mawazo, ushauri na ushawishi alionao.
Ni mwepesi kuelewa watu wanavyojisikia mbele yake, na huwa tayari kujirekebisha haraka pale anapoona kwamba amepotoka au amekwenda nje ya matarajio ya wale wanaomsikiliza.
Mtu wa aina hii anapotoa mada juu ya jambo fulani hujua kama wasikilizaji wanamsikiliza au wanaendelea na shughuli nyingine.
Hivyo hutumia nafasi hiyo kuichangamsha jamii kwa kutafuta mbinu mbalimbali zitakazowezesha hao wasikilizaji waendelee kumsikiliza na kufurahia mada yake anayotoa. Ni mjanja wa kusoma upepo unavyoelekea.
Mwoga wa kuchukiwa kwa sababu ikitokea hivyo, huhisi kwamba amedharauliwa kutokana na mawazo, ushauri na ushawishi wake kwa jamii.
Anafahamu jinsi ya kupendeza watu na kufanya wampende. Hii inatokana na uwezo wake wa kuwa karibu na watu, upole, ucheshi na uwezo wake wa kuzungumza kwa kujenga hoja.
Anajali sana mwonekano wake kimwili na kimaisha, hii ni kutokana na ukweli kwamba anapenda kuwa mfano.
Watu wengi wanamkubali mtu kulingana na muonekano wake kimwili na kimaisha, hivyo huwa moja ya ushawishi kwao.
Mtu aliye na matumaini na wema wa kufaulu. Kwa kuwa mhamasishaji ni mtu anayependa kujifunza mambo mapya kulingana na wakati na jamii inayomzunguka, huwa na matumaini makubwa ya kufaulu katika maisha yake binafsi na katika yale anayopanga kufanya kwa watu wengine ‘target to others’.
Tukutane wiki ijayo.
0713 331455
Sunday, June 15, 2008
HAMASISHA WATU KWA MAMBO MAZURI
Posted in:
0 Maoni:
Post a Comment