Monday, June 16, 2008

ACHA TABIA YA KULALAMIKA

TABIA ya kulaumu watu huanza tokea wakiwa na umri mdogo. Kwa mfano mtoto wa miaka mitatu ameanguka kutoka kwenye kiti chake akiwa anacheza, kwa hasira ananyanyuka kutoka chini na kukilaumu kiti alichokuwa amekikalia.
“Kiti kibaya, kwanini umenisababisha kuanguka?” anasema mtoto huyo. Kwa umri mdogo alionao wa miaka mitatu ameshaanza tabia hiyo ya kulaumu.
Lawama si kitu cha kufurahisha kwani huweza kusababisha hasara zaidi.
Kwa mfano waweza kumwona mtu akigonga gari lake kwa hasira ukafikiria kuwa amechanganyikiwa kumbe analaumu kwa nini limeharibika au kwa nini limemwishia mafuta.
Kila wakati mambo yanapoharibika ni kasumba kwa mwanadamu kutafuta sababu ya lawama au mtu wa kumlaumu.
Mara nyingine tunapomwona kilema, kipofu au kichaa, swali kubwa watu wanalojiuliza ni nani anayestahili kulaumiwa.
Wengine humlaumu Mungu, wengine hulaumu uumbaji na wengine huwalaumu wazazi.
Tunachotakiwa kujiuliza ni jinsi gani ya kumsaidia mtu huyo? Ni namna gani ya kumtoa katika hali ile aliyonayo sasa? Ni namna gani tunaweza kuboresha mazingira yanayomkabili? Ni jinsi gani twaweza kumfanya aanze upya na kwa ubora zaidi.
Ingawa lawama ni mchezo uliozoeleka na watu wengi siku hizi, bado ni mchezo ambao huleta athari kubwa sana.
Siku zote lawama haiponyi bali huumiza moyo, Haijengi uhusiano bali huuvunja, haiunganishi bali hutenganisha, haijengi bali hugawanyisha na haitatui matatizo bali huongeza ukubwa wa matatizo.
Acha kumlaumu Mungu
Mara zote matukio mabaya yanapotutokea tunakimbilia kumlaumu Mungu.
Mfano, baba ambaye amefiwa na kijana wake kwenye ajali mbaya ya gari ambayo imesababishwa na uzembe wa dereva mlevi, kwa uchungu na maumivu atalia na kumlaumu Mungu.
Katika mazingira kama hayo mtu yeyote anatakiwa kujua kwamba mvua huwanyeshea watu walio wema na wasio wema, haijalishi mtu ameishi kwa muda mrefu kiasi gani au ameishi kwa namna gani, thamani ya maisha ndiyo inayohesabika.
Mungu hawezi kusababisha matukio mabaya kututokea maishani. Mara nyingi katika ulimwengu huu tunaoishi, mambo yaweza kwenda kombo au waweza kudhulumiwa haki yako uliyostahili kuipata lakini kamwe usimlaumu Mungu kwa lolote.
Acha kulaumu wengine
Kulaumu wengine ni sawa na kujiweka kwenye nafasi ya Mungu au hakimu- nafasi ambayo hata mmoja wetu haistahili.
Tunapowalaumu wengine wakati mwingine tunataka kufunika mapungufu yetu wenyewe ambayo hatuko tayari kuyakabili. Mfano, utamkuta mwanamke akisema kwa ujasiri kuwa mumewe anatoka nje ya ndoa kwa sababu tu huchelewa kurudi nyumbani au kutumia pesa zake za mapato visivyo.
Bila kujali kuwa mumewe anafanya kazi saa za ziada au anahifadhi fedha zake ili aweze kumnunulia mkewe zawadi nk. Yawezekana kuwa mwana mama huyu amekuwa akibeba hisia hizo za shutuma juu ya mumewe kwa muda mrefu kiasi cha kuweza kusababisha hata uhusiano wao kuyumba au ndoa yao kuvunjika.
Lakini ukichunguza undani wa shutuma hizo huweza kukuta ni hitimisho iliyojaa hisia potofu.
Lawama yaweza kusababisha watu kufikia hitimisho isivyo sahihi hata kubeba uchungu kwa muda mrefu kiasi cha kuvunja ndoa.
Lawama huweza kusababisha hali ya maelewano na masikilizano kuwa ya kutoelewana au kutosikilizana.
Njia mojawapo ya kusaidia ndoa zenye msukosuko ni kumsaidia kila mhuhusika kuacha kumlaumu mwezie au kuacha kumtazama mwenzie kwa jicho la lawama, ila ajitazame mwenyewe na kuona ni wapi alipofanya makosa na nini anaweza kufanya ili kurekebisha ndoa yao.
Njia nyingine ni kumfanya kila mmoja aweze kukiri makosa mbele ya mwingine na kusema samahani, nimekosa. Katika hatua hiyo uhusiano uliovunjika huanza kuimarika tena.
Hata mwanadamu wa kwanza alianza kwa kumlaumu mwanamke kwa kuelezea makosa yake kwa Muumba wake. “Huyu mwanamke ndiye aliyenisababisha. Mwanzo 3:12”. Mwanamke naye alitupa lawama zote kwa nyoka. “Nyoka ndiye aliyenisababishia kufanya hivi. Mwanzo 3:13”.
Tunapowalaumu wengine tunaongeza ukubwa wa tatizo badala ya kulitatua. hii inaonyesha kuwa aliyemwepesi kulaumu wengine ndiye mwenye makosa mengi zaidi.
Waungwana ndio wanaoweza kukiri makosa yao au kushindwa kwao mbele ya jamii. Mtu muungwana ni yule aliyemwepesi kusema nimekosa.
Shinda lawama kwa kukiri makosa yako. Acha kufunika makosa kwani yataongeza ugumu wakati wa kutatua. Kuna njia moja ya kuweza kusafisha dhamira inayokushitaki, nayo ni kukiri makosa.
Acha kutafuta watu wa kulaumu, kabiliana na makosa yako mwenyewe. Kubali makosa yako utapona. Kiri maovu utasamehewa.
Usijilaumu mwenyewe
Tunapojilaumu wenyewe tunajiongezea mzigo wa matatizo juu ya mabega yetu kwa sababu tunajiadhibu wenyewe.
Jifunze kujisamehe hata kwa makosa yaliyokwisha kupita ambayo yanaumiza ufahamu wako.
Watu wengi wanakuwa mahakimu au washitaki juu ya makosa yao wenyewe, wakiendelea kujilaumu wenyewe.
Unapokumbuka mambo ya aibu au ya kushindwa yaliyokupata zamani unazidi kuvunjika moyo na kujiona kuwa hustahili machoni pa watu.
Hali hii itakuongezea machungu, wasiwasi, msongo wa mawazo, pia inakuondolea ujasiri ulionao, suluhisho ni kusahau yaliyopita na kuanza upya.
Ingawa inaweza kuwa ngumu kuzuia kumbukumbu za kushindwa kwako kukurudia, usizipe nafasi katika ufahamu wako.
Kama Mungu au watu waweza kukusamehe, si zaidi wewe mwenyewe kujisamehe?
Achana na maamuzi mabaya uliyokwisha kuyafanya ya kibinafsi yaliyosababisha kuwaangusha marafiki zako, jamii au wewe mwenyewe.
Kabiliana na siku mpya kwani wewe si yule wa jana, bali ni wa leo.
ngowi2001@yahoo.com0713 331455

0 Maoni:

Twitter Facebook