IPE nafsi yako raha kwa kuota ndoto. Si ndoto yoyote bali ndoto ya kuwa na malengo makubwa.
Binafsi ninaamini katika malengo hayo kuwa kuna mafanikio endapo utamaanisha.
Wakati mtu anapoanza kuwa na malengo makubwa anaanza kwa kufikiri jinsi Mungu alivyomwezesha mtu kufikiri jambo hata kufikia uamuzi wa kuchukua hatua na kufanikiwa.
Mtu mmoja aliandika barua na kusema kuwa wana mpango wa kuwa na mashindano maalumu ya michezo.
Aliendelea kusema kuwa wamepanga kushinda mashindano ya kitaifa ya mpira wa kikapu, kama siyo mwaka huu itakuwa mwaka ujao, au vyoyote itakavyokuwa ili mradi wafikie lengo hilo.
Kocha wa timu hiyo alijua nia hiyo hivyo alikuwa akiwatia moyo wachezaji wake kwamba watashinda.
Mashindano hayo yalipofika kweli walishinda hivyo ndoto ya ushindi iliyokuwepo ilitimia.
Ndoto haina gharama. Kumbuka ukiwa na malengo ya mafanikio haitakugharimu chochote.
Unaweza ukawa na malengo ya kuanzisha mradi mkubwa pasipokuwa na fedha, inabakia kuwa ni ndoto tu.
Mungu alianza kuumba dunia ikiwa haina kitu. Tunaweza kuwa na malengo makubwa ya mafanikio katika maisha yetu haijalishi ni ya aina gani.
Endelea mbele ukiachia fikira zako kufikiri. Kama moyo wako umevunjika au upo katika hali ya kukata tamaa au umejaa wasiwasi, unatakiwa kuwa na ndoto mpya mapema iwezekanavyo.
Unapohitaji muujiza unatakiwa kuwa na maono mapya katika maisha yako.
Kumbuka hata wewe unaweza ukawa na maono makubwa ya ajabu. Haijalishi ni mtu wa aina gani, au umetoka wapi, au umepatwa na jambo gani?
Katika hali uliyonayo unaweza kuwa na maono mapya. Malengo makubwa si kwa wale waliofanikiwa, bali ni kwa wale wanaotaka kufanikiwa.
Inawezekana ukawa una fikra kama za mwanamke mmoja niliyekutana naye siku za karibuni ambaye alikuwa ameachwa na mumewe, ndoto yake ilikuwa ipo siku atakutana na mtu ambaye kwa pamoja watatengeneza na kujenga nyumba yenye upendo na mafanikio.
Vyovyote uwazavyo, ndoto inainua, inaweka kitu kipya katika maisha yetu, inatutengeneza na kutusogeza mbele, inatuwezesha kufikia malengo makubwa tofauti na ilivyokuwa awali.
Inatuwezesha kufanya kitu kikubwa ambacho hujawahi kukifanya tena kabla ya hapo.
Je, wataka kuwa fulani? Kusimama nje ya kusanyiko kubwa? Kukumbukwa? Hali hiyo inakuwepo ndani ya mioyo yetu inayodunda na kutaka kupata siri ya mafanikio.
Tunataka kuwa fulani. Inawezekana ndiyo inawezekana. Mungu ametoa kwa kila mtu uwezo na vipaji mbalimbali.
Wakati Mungu anakuumba alikupa kipaji na akasema kama utatumia kipaji ulichonacho atakiongeza, na kama hutatumia kipaji ulichonacho utakipoteza. Kukitumia kipaji chako au kukiachia ni juu yako wewe!
Dunia yetu imejaa vipaji vingi na uwezo ambao hautumiwi. Unatakiwa kulima kwa bidii, kupalilia ili upate mavuno bora. Tumia kipaji chako kabla hujakipoteza.
Unaweza kudhani kuwa hauna kipaji chochote si kweli labda inawezekana ujagundua kipaji chako. Inawezekana umekiweka kipaji chako kabatini. Amini kuwa kila mmoja anacho kipaji chake alichopewa na Mungu.
Waweza kutumia kipaji ulichonacho au kukipoteza. Maisha yetu yamejengwa katika kanuni hiyo. Kuna mifano mingi ya kupoteza au kupata hiyo ni kanuni ya kawaida.
Chukua hatua tano ambazo zitaifanya ndoto yako kuwa ya kweli.
Ota ndoto yenye thamani katika maisha yako. Kama hauna malengo, haitawezekana matarajio yako kutimia.
Ndoto inaanza unapokuwa na wazo. Kumbuka watu huvutiwa na wenye maono makubwa.
Chagua maono yale yenye matarajio. Baadhi ya watu wanapoteza muda wao kwa kuwa na malengo ambayo hayatawasaidia.
Mfano kuna kijana mmoja miaka iliyopita alisaidiwa kupewa ushauri baada ya kupoteza muda wake mwingi akifikiria ni jinsi gani ataweza kumpata mke wa jirani yake na kumfanya awe mke wake. Ndoto yake hiyo haikuwa ya thamani, ya muda mrefu.
Wakati wazo linapokujia katika ufahamu wako, iulize nafsi yako maswali matatu. Jambo hilo litampendeza Mungu? Litawasaidia watu wanaoteseka?
Kwa maneno mengine litakuwa msaada kwa watu? Litaleta mafanikio mazuri kwangu?
Kama jibu lako ni ndiyo katika maswali hayo yote matatu, utakuwa umekuwa na maono yenye mafanikio.
Unapoamua kufanya jambo fulani usijiulize ulize kuwa hii ni njia nyepesi ya mafanikio? Au ni njia rahisi?
Inaweza kuwa na usalama? Haitakuwa na vikwazo? Hakuna utakachoshindwa utakapofanya bidii. Hakuna mwenye nguvu ya kuua ndoto yako isipokuwa ni wewe mwenyewe.
Panga mipango. Huwezi kujenga jengo bila kuwa na ramani. Huwezi kufanikiwa matarajio yako pasipokuwa na malengo makubwa.
Ninamfahamu mtu mmoja aliyekuwa na maono makubwa lakini yalikuwa hayafiki mbali. Ni kwa sababu alikuwa hana ramani ya maono yake.
Hakikisha unatimiza ndoto uliyojiwekea. Malengo yako hayawezi kufanikiwa kama hujajitoa kufanya hivyo.
Ili kufanikiwa katika mipango yako kunahitaji juhudi na kufanya kazi kwa bidii. Ili upate mafanikio, endelea kufanya bidii.
Amua pa kuanzia. Fanya uamuzi. Panga muda wa kuanza. Usitafute sababu ya kuacha kuanza malengo yako kwa muda ulioupanga.
Katika dunia yetu kuna watu wengi ambao hupanga mipango mingi lakini hawaifanikishi. Jiondoe katika kundi hilo. Fanya kitu. Andika barua, piga simu. Anza hatua ya mafanikio.
Jiamini, waweza kutimiza ndoto zako. Wakati unajaribu kupata mafanikio utaona kuwa ni kipindi kigumu kwako.
Hali ya kukata tamaa inakuwepo katika moyo wako, ikisema jiondoe katika hatua ambayo unataka kuianza ya kupata mafanikio katika maisha yako.
Kama unakutana na kipindi cha majaribio katika biashara yako, ndoa yako, katika mambo yako binafsi, kwenye wingi wa watu, hali yako au hali ya maisha uliyoizoea na uko tayari kukabiliana nayo, songa mbele usikate tamaa.
Unachofanya ni kujaribu kupata mafanikio, tena mafanikio makubwa. Katika kila mafanikio unayoyapata, kuna gharama ya kulipa. Kumbuka huwezi kupata ushindi bila kulipa gharama.
lcyngowi@yahoo.com0713 3314550733 331455
Monday, June 16, 2008
OTA NDOTO MPYA YA MAFANIKIO
Posted in:
0 Maoni:
Post a Comment