KARIBUNI wapenzi wasomaji katika siku nyingine tena. Leo tunaendelea na mfululizo wetu wa kuangalia jinsi ya kukabiliana na hali ya msongo wa mawazo uliyonayo.
Kwa kuwa kila mmoja wetu ni tofauti na mwenzake, hakuna njia moja ya kuweza kukabili msongo wa mawazo. Hata hivyo, kuna idadi ya vitu mbalimbali ambavyo vinaweza kuondoa mawazo hayo yanayompata mtu. Ambavyo vinaweza kuchukua muda mrefu au muda mfupi, kupunguza msongo unaokukabili.
Kwanza ni vizuri ukajua matatizo yako yanayokukabili. Kama ni kazi yako, uhusiano wako na mtu fulani, au masuala ya kiuchumi yanayokufanya kuwa na mawazo. Pale unapojua uhakika wa tatizo lako, unaweza kufanya kitu cha kukusaidia ili kuondokana nalo.
Tatua matatizo yako kwa kuanza kufikiria jinsi ya kuyapatia muafaka. Utafanya nini kama utakuwa na msongo juu ya hitaji la kazi, au ushauri katika ndoa yako, au unahitaji ushauri wa mtaalamu wa uchumi aweze kukueleza jinsi ya kutumia fedha zako? Nini kitatokea kama hautafanya chochote? Kama utafuta njia za kuondoa tatizo hili, utakuwa na uwezo wa kufanya baadhi ya mabadiliko ya kuondoa mawazo na hali ile ya wasiwasi inayokukabili. Njia hii ndefu ya kupunguza mawazo katika maisha yako kwa kila mmoja, mapema au kwa haraka, itafanikiwa.
Zungumza kuhusu matatizo yako. Utakuta inakusaidia kuzungumza kuhusu msongo wako. Marafiki na familia yako wanaweza wasijue kuwa unakabiliana na kipindi kigumu. Mara watakapoelewa, wanaweza kukusaidia katika njia mbili. Kwanza, kwa kukusikiliza na pili kwa kuangalia uwezekano wa kutatua matatizo yako. Kama utahitaji kuzungumza na mtu mwingine aliye nje ya marafiki na ndugu zako, daktari wa familia yenu anaweza kukusaidia kwa kukuelekeza kwa mshauri wa afya katika masuala ya akili.
Jifunze jinsi ya kutawala msongo. Kuna vitabu vingi vinavyosaidia, filamu, video na kozi mbalimbali ambazo zitakuwezesha kukabiliana na hali uliyonayo. Pia wapo washauri ambao wamebobea katika masuala ya msongo wa mawazo, muulize daktari wako wa familia kwa maelekezo zaidi. Pia kuna kozi katika vyuo vingi vya jumuiya na jinsi ya kutawala msongo unaokukabili, katika jamii inayokuzunguka.
Punguza hali ya wasiwasi inayokukabili. Shughuli mbalimbali unazozifanya zinaweza kuwa msaada mkubwa kwako wa kupunguza msongo. Fanya matembezi, cheza michezo mbalimbali, lima bustani, fanya usafi ndani ya nyumba. Utakuta inakusaidia sana katika kuuweka mwili wako katika hali ya kuchangamka. Pia hali ya kupumua taratibu (kuvuta pumzi kutoka ndani ya tumbo), bila kuruhusu pua zako kuvuta hewa halafu kuitoa pumzi kwa nguvu kupitia mdomoni. Mazoezi mengine ni kujinyosha na kupumzika katika kila kiungo katika mwili wako, kwa kuanzia shingo yako na kuishusha chini.
Kama utakuwa na tabia la kupuuza hali mbalimbali zinazokusababishia msongo, kwa kujiongoza mwenyewe vile unavyotaka, utajikuta huna tatizo la msongo na mwepesi wa kutatua hali hiyo ambayo mwanzoni bila kufahamu ilikusababishia kupata msongo.
Usiruhusu akili yako kushikilia matatizo uliyonayo. Unaweza kuondoa hali hiyo kwa kujishughulisha. Kama unajihusisha na michezo mbalimbali au kazi, unaweza kuipa akili yako mapumziko kutoka kwenye msongo uliokuwa nao. Kutokufikiria matatizo yako kwa muda kunaweza kukupa wepesi katika kutatua hali hiyo kwa mapema.
Jinsi ya kuzuia msongo.
Mara utakapofanikiwa kupunguza hali ya msongo uliyokuwa nayo, ni busara kuangalia njia za kuzuia msongo usijirudie tena. Njia rahisi ya kukabiliana nayo ni kuzuia. Baadhi ya njia nzuri za kufanya hivyo ni:
Kufanya maamuzi. Maamuzi hayo yasikuletee hofu na baadaye msongo.
Epuka kudharau baadhi ya vitu vyako. Unatakiwa kuwa na ratiba yako ya wiki, ambayo itajumuisha shughuli za starehe pia kusikiliza nyimbo mbalimbali.
Ushirikiano. Waachie wengine wafanye shughuli zile uzifanyazo ili kuepuka hali ya kufanya kila shughuli wewe mwenyewe.
Kumbuka, haiwezekani kuwa na maisha yasiyo na msongo. Malengo yako lazima yaepuke kuwa katika daraja la msongo ambapo nguvu yako uliyonayo inanyonywa.
Je, unahitaji msaada zaidi? Kama kuna mtu unayemfahamu na ambaye ameathirika sana kwa msongo wa mawazo, wasiliana na jamii inayokuzunguka kama kikundi cha afya ambacho kitaweza kukusaidia kukutafutia msaada zaidi.
Mara zote jitahidi kuondoa hali hiyo inapokupata. Utafanyaje endapo utakabiliana na hali hiyo? Njia muhimu itakayoweza kukusaidia kuondokana na hali hiyo, ni kujifunza jinsi ya kuidhibiti hali hiyo ambayo inakuja katika changamoto mpya, kwa uzuri au kwa ubaya.
Usijione kama wewe umekamilika katika kila kitu kwani hakuna aliye kamili. Na unapowatarajia wengine kuwa ni bora kuliko wewe, inakuongezea hali ya msongo, kama unahitaji msaada wa kitu chochote omba msaada kwa wengine.
Jitahidi kupata usingizi mzuri. Kuwa na muda mzuri wa kulala, kunaufanya mwili na akili yako kutulia, kuwa na maamuzi thabiti pamoja na kudharau misongo inayokuletea madhara. Kama utakaa muda mrefu usiku bila kulala na unahitajika kuamka asubuhi kuwahi kazini au shuleni, huwezi kupata muda mzuri wa kulala unaotakiwa, hivyo itakuletea athari.
Jifunze kupata muda wa kupumzika. Muda huo uwe unasoma kitabu, unasikiliza muziki, unaangalia luninga au unaoga na kuupumzisha mwili wako baada ya shughuli za siku.
Utunze mwili wako vizuri. Wataalam wanaamini kuwa kupata mazoezi ya kawaida kunasaidia watu kupunguza mawazo. Pamoja na kula vizuri kuwezesha mwili wako kufanya kazi yake vizuri. Kumbuka mwili unahitaji virutubisho mbalimbali. Ingawa vileo au dawa za kulevya zinaelezwa kuwa zinapunguza msongo kwa muda, ukweli ni kwamba zinazidisha tatizo kwa sababu zinaufanya mwili uchoke na kushindwa kufanya kazi yake vizuri.
Mara zote jitahidi kutatua matatizo ya kila siku ambayo unaweza kuyakabili, lakini kuyaepuka kutakusababishia hali ya kujiona unashindwa na hatimaye kuibuka tatizo kubwa zaidi.
Tukutane tena Alhamisi ijayo .
lcyngowi@yahoo.comwww.ngowil.blogspot.com 0713 3314550733 331455
Monday, June 16, 2008
VITU VINAVYOWEZA KUBADILISHA MSONGO WA MAWAZO
Posted in:
0 Maoni:
Post a Comment