Monday, June 16, 2008

ELEWA MSONGO WA MAWAZO

Si vibaya nikianza kumshukuru Mungu kwa kunifikisha siku na wakati kama huu. Naamini hata wewe msomaji wangu una kila sababu ya kumshukuru Muumba wetu, kwa kukumbushia tu, leo tunaendelea na mada yetu ambayo ilianza wiki iliyopita inayozungumzia msongo wa mawazo ambao humpata mtu kutokana na mambo mbali mbali anayokumbana nayo katika maisha. Tutaangalia maana, dalili, vitu vinavyosababisha, matokeo na jinsi ya kutatua hali hiyo, endelea.
WOTE tunakabiliana na changamoto na vikwazo mbalimbali, hata wakati mwingine tatizo linakuwa kubwa kukabiliana nalo. Inafikia mahali tunajihisi kuzidiwa, au kuwa chini ya mtutu wa bunduki, au kutokuwa na uhakika wa jinsi tutakavyotimiza mahitaji ambayo yako juu yetu, hapo huwa tunakuwa na msongo.
Iwapo utakuwa katika kiwango kidogo, msongo unaweza kuwa kitu kizuri. Msongo unaweza kukupa msukumo wa kile unachokihitaji, unaweza kukupa motisha wa kufanya vizuri zaidi na kuwa mtu mwenye malengo siku zote.
Msongo unaweza kukufanya uwe makini kwa mfano kama unasoma, unaweza kukufanya uwe makini na masomo wakati wa likizo badala ya kukaa ukiangalia Tv. Lakini mambo yanapokuwa magumu na mahitaji ya maisha yakazidi uwezo wako wa kuyatimiza, hapo ndipo msongo huwa tishio kwako kimwili na kihisia pia.
Wiki iliyopita tuliona baadhi ya sababu zinazosababisha msongo wa mawazo, leo tutaangalia sababu nyingine zaidi zinazochangia tatizo hilo.
Mojawapo ya sababu hizo ni pamoja na maisha yasiyo na uhakika 'maisha kamari.' Wataalamu wengi wanaamini kuwa kutokuwa na maisha ya uhakika ni moja ya sababu za msongo.
Wengi tumekuwa watumwa wa maisha ya kisasa tukitaka kuishi katika daraja ambalo si letu. "Wote tunataka kuwa maarufu, matajiri, washindi wa bahati nasibu," anasem mwanasaikolojia Patrick Whiteside, mtunzi wa kitabu kijulikanacho kama 'little Book of Bliss'.
Aina hii ya utamaduni unatuweka katika shinikizo. Watu wanajishurutisha ili waweze kuwa na mafanikio na pesa, wanataka kuwa na nyumba kubwa, televisheni kubwa na magari ya thamani kubwa, lakini wanasahau umuhimu wa kuwa wenzi wazuri katika familia zao," anasema.
Mara nyingi, mtu anajikuta hana uchaguzi ila kuendelea na hali ya mawazo. Lakini ni muhimu ukathubutu kujaribu na kurudi nyuma huku ukifikiria juu ya uchaguzi ulioufanya awali. Kufikiria juu ya mabadiliko unayoweza kuyafanya kulingana na aina ya maisha unayoishi.
Kama hali ya mawazo inaendelea, inaweza kuleta matatizo makubwa katika kutekeleza majukumu ya kitaalamu kulingana na fani yako au maisha, au hata kuathiri afya yako.
Sababu nyingine ni matatizo ya kiuchumi. Kama mtu hana fedha za kukidhi mahitaji ya muhimu atajikuta katika hali mbaya ya kuwaza ambayo inaweza kumsababishia msongo.
Mtu huyo atajikuta katika lindi la mawazo , akijaribu kufikiri jinsi atakavyopata fedha kwa ajili ya kufanya biashara, au kusomesha mtoto au hata itakayomwezesha kuishi maisha mazuri.
Mwingine unaweza kukuta akiwaza juu ya nyumba na anataka kuishi katika nyumba ya hadhi fulani lakini hana uwezo wa kufanya hivyo, au pengine kuharakishwa kutoka katika nyumba katika kipindi ambacho alikuwa hajawa tayari kufanya hivyo, hayo pia yanaweza kuwa matatizo ambayo yanaweza kuleta msongo.
Sababu za msongo zina wigo mkubwa, wakati mwingine unaweza kukuta mtu anapata shinikizo kutoka kwa bosi wake, au hata ndugu anaoishi nao kama vile shemeji au wifi, au wakati mwingine kuachishwa kazi au kustaafu akiwa hajajiandaa.
Kwa wale wanaostaafu hupatwa na msongo pale ambapo hujikuta wakitakiwa kuachia nyadhifa zao wakati hawajajiandaa kwa ajili ya maisha mapya nje ya kazi. Wengine hujikuta hawajaweza kujenga nyumba au kuwa na biashara yoyote ya kuwaingizia fedha kwa ajili ya kuendeleza maisha yao yaliyobaki.
Msongo hutuathiri sote. Hivyo basi iwapo unaweza kutambua dalili basi unaweza kuudhibiti.
Mbali na sababu tulizoziona hapo juu, zipo sababu nyingine ambazo ni za kawaida kabisa, ambazo husababisha msongo kama kitisho, hofu na shaka.
Hofu inasababisha mtu kupatwa na msongo. Hii inajumuisha hofu ya kimaumbile, hofu ya kijamii, hofu ya kifedha na mengineyo. Katika hali ya kawaida, hali inakuwa mbaya wakati mtu anapohisi hakuna namna ya kupunguza vitisho, hiyo huathiri hisia na hivyo huwa vigumu kuzidhibiti.
Kiujumla tishio lolote katika mahitaji linaweza likasababisha msongo.
Hali yoyote ya utisho inasababisha hofu, ambayo huleta msongo. Hofu inaongoza kufikiria matokeo, ambayo ni chanzo halisi cha mawazo.
Wakati ambapo tuna shaka, hatuna uimara katika kutabiri, na wakati tunahisi hofu au tishio hali hiyo husababisha shaka.
Tabia ya utambuzi
Kunapokuwa na pengo kati ya kile tunachofanya na kile tunachofikiri, hapo tunashuhudia tabia ya utambuzi ambayo inahisiwa kama shinikizo, kwa hiyo kama ninafikiri kuwa mimi ni mtu halafu nikafanya kitu ambacho kitamuumiza mtu mwingine, hapo nitakuwa ninajiweka katika hali itakayonisababishia shinikizo.
Pengo hilo linaweza kutokea pale ambapo hatuwezi kufikia malengo yetu. Tunaamini kuwa waaminifu na tumejitoa kikamilifu lakini inapotokea jambo la kutukwamisha tusifikie malengo yetu hayo tunakumbana na mazingira yanayotufanya tuonekane kuwa si waaminifu au wenye uwezo wa kile tulichopanga kukifanya.
Mfano ni pale ambapo tunakumbana na tishio la kijamii, kwamba tusipofanya kitu Fulani, jamii haitatuelewa au tutataabika.
Chanzo kitokanacho na maisha
Kuna vyanzo mbalimbali vya msongo wa mawazo katika maisha ikiwa ni pamoja na kifo cha mume, mke, ndugu katika familia au rafiki wa karibu. Afya pia inaweza kuwa chanzo, hasa pale ambapo unahisi hali si nzuri katika mwili wako, ama kwa ugonjwa na ujauzito kwa mwanamke.
Uhalifu pia ni mojawapo ya mambo yanayoweza kusababisha msongo. Uhalifu kama vile kudhalilisha wengine kijinsia, kuvunja na kuiba, kudokoa au wizi wa mifukoni.
Kutumia dawa za kulevya
Katika ulimwengu wa sasa, watu wengi na hasa vijana, wamejikuta wakikumbwa na msongo kutokana na kujiingiza katika matumizi ya dawa za kulevya, hali ambayo inawafanya kutojithamini au kukata tamaa ya maisha.
Dawa za kulevya na ulevi wa kupindukia humfanya mtu ashindwe kujikinga na hatimaye kujikuta akijeruhiwa.
Mambo mengine ni mabadiliko ya ghafla katika familia kama vile mume na mke kutengana, kupata mtoto bila ya kutarajia hasa kwa wanawake walio katika ndoa.
Matatizo ya kimahusiano
Kila mtu hupenda kuwa na mahusiano ili kuoyesha ni jinsi gani anapendwa au kupenda.
Inapotokea kuwa hitaji la mtu katika mahusiano halikufikiwa, basi mtu hujikuta katika msongo ambao huathiri zaidi hisia, hili linaweza kuwa pia katika upande wa mahusiano mabaya na mpenzi wako, mwenzi wako, rafiki au ndugu katika familia, hata mfanyakazi mwenzako au bosi katika maeneo ya kazi.
Mabadiliko ya kimaumbile; kama kukosa usingizi na kuongezewa muda zaidi kazini, mtu kuwa mnene au mwembaba au hata kurefuka au kuwa mfupi isivyo kawaida, ni baadhi ya mambo yanayochangia msongo.
Mabadiliko ya kimazingira kama vile kuhamishwa eneo la kazi au makazi, mfano kutoka mjini kwenda maeneo ya shambani, kuhama shule na kwenda katika shule ambayo hupendezwi nayo huweza kumfanya mtu awe katika hatari ya kukumbwa na msongo.
Jambo jingine ni kuzidiwa na majukumu kama vile kuongeza ukubwa wa familia huku kipato kikiwa kidogo au kujikuta wategemezi wako wakiongezeka kwa ghafla, mfano watoto wa ndugu yako kuhamia kwako baada ya ndugu huyo kufariki yeye na mwenzake.
Msongo katika maeneo ya kazi
Nchini Uingereza, Idara ya Afya na Usalama inaorodhesha mambo sita makubwa ambayo yanachangia msongo katika maeneo ya kazi.
Hitaji la kazi: Udhibi walio nao wafanyakazi juu ya kazi wanazofanya na jinsi wanavyopaswa kuzifanya.
Uungwaji mkono unaoupata kutoka kwa wenzako na wakubwa wako. Mahusiano baina ya mtu na mwenzake, iwapo watu wanatambua wajibu wako na majukumu uliyonayo, na pia ni kwa kiasi gani kampuni inashauriana na wafanyakazi kuhusiana na mabadiliko ya maeneo ya kazi.
Tukutane wiki ijayo.
lcyngowi@yahoo.com0713 331455; 0733 331455

0 Maoni:

Twitter Facebook