Sunday, December 27, 2009

KUBALI TATIZO LAKO ULITATUE

MPENZI msomaji, nakukaribisha tena katika safu hii ya Maisha Yetu. Leo tutaangalia njia mbalimbali za kukusaidia unapopatwa na matatizo.
Mara nyingi mtu anapopatwa na matatizo hubabaika na kujikuta hana msaada wowote.
Mtu huyo huwa anashindwa kujikubali kama yupo salama na lipo tumaini jipya baada ya matatizo hayo anayokabiliana nayo.
Ni watu wachache wanaojikubali kuwa wana matatizo na kutafuta njia ya kukabiliana nayo.
Wengi walio na misukosuko hukosa furaha na kujiona kuwa ni wanyonge, waliokataliwa na jamii inayowazunguka.
Hali hiyo huwafanya afya zao kuzorota na kukabiliwa na magonjwa mbalimbali kama ya moyo na vidonda vya tumbo.
Kutokana na hali hiyo inayomkabili mtu huyo, jamii, ndugu na hata marafiki zake huwa mbali naye na kuacha kutoa ushirikiano wa karibu kwake.
Ni vizuri kuelewa kuwa, kila mmoja wetu ana matatizo, hivyo njia ya kuyatatua anayo yeye mwenyewe.
Unaporuhusu hali ya kukata tamaa kujengeka katika maisha yako, ndipo unapoona kuwa matatizo hayatatuliki na ni mzigo mkubwa usiobebeka.
Pili inakupasa kujua kuwa, matatizo ni kitu kisichoepukika katika maisha, japo yanaumiza sana kwa wakati huo.
Lakini faida yake ni kwamba yanakujenga sana imani yako na hata kuwajua watu wa kweli kwako, iwe ndugu ama marafiki.
Na huu ndiyo wakati muafaka wa kujenga maisha yako na kuimarisha ujasiri. Hakuna mtu mwenye akili na jasiri kama mtu mwenye matatizo, kwani fikra zake siku zote ni kutatua hali hiyo inayomkabili. Wakati wale wasio na matatizo hujibweteka kiakili hata kiafya.
Tatu, ni vema kuelewa kuwa njia ya kutatua matatizo yako unayo mwenyewe na lipo tumaini.
Hetu tuangalie mfano wa mtu anayekabiliwa na matatizo ya kuuguliwa na mtoto, baba mzazi na wakati huo huo anakuwa na madeni yaliyomwelemea na kumfanya ashindwe kuelewa anaanzia wapi.
Kumbuka kipindi kama hiki wapo baadhi ya ndugu na marafiki wanaokucheka, wakisubiri waone mwisho wa kushindwa kwako.
Njia sahihi za kufuata ni kuepuka sana kuwa karibu na watu kama hao. Kama unadaiwa na unakwenda kumueleza mtu asiye na madeni akusaidie shida yako, hatakuwa na moyo, atakucheka na wengine hufika mbali kwa kukutangaza.
Ni vizuri ukawa na watu walio na utayari wa kukusaidia, pata muda mzuri wa kupumzika ukiwa peke yako ili uwe na akili tulivu, utafakari uanze na tatizo lipi ili kukabiliana na hali uliyo nayo.
Si vizuri kumwambia kila mtu matatizo yako, kwani walio wengi hawawezi kukuzungumzia mambo mema kwa kuwa midomo yao imejaa hila.
Uwaone viongozi wako wa dini kwa ajili ya ushauri zaidi.
Pia kila unapokutana na watu wa aina mbalimbali jifunze kuongea nao vizuri na penda kuongelea zaidi mafanikio yako kuliko matatizo.
Hii inasaidia wale wasiopenda mafanikio yako, wasijue undani wako ulivyo.
Siku zote za maisha yako uwe na ndoto za mafanikio, hii itakufanya siku moja uketi pamoja na wakuu wa nchi. Kubali kupokea baraka kutoka kwa wengine na uwe mtu wa shukrani. Hiyo ni siri tosha ya kuondoa matatizo.
Tumia muda wako vizuri kupanga mambo ya kimaendeleo. Pia fanya mazoezi ya viungo na si kunywa pombe ukidhani kuwa utatuliza mawazo.
Kumbuka watu waliokabiliana na matatizo makubwa ndio walioweza kufikia mafanikio makubwa kiroho, kiuchumi na kisiasa, kwa kuwa wanazikubali changamoto katika maisha.

USIKUBALI KUKATISHWA TAMAA

MSOMAJI, katika mfululizo wa makala hizi za maisha yetu, nimedhamiria kukuletea kitu kipya kila Alhamisi. Leo tutaangalia jinsi ya kutokufuata mawazo ya wale wanaotaka kukurudisha nyuma kimaendeleo.
Miongoni mwa jamii tunazoishi, huwa kuna baadhi ya watu ambao hufurahia wenzao wanaposhindwa kutimiza malengo waliojiwekea.
Ama huwa na tabia ya kuwakatisha tamaa wanaopenda kujikwamua kutoka katika hatua moja na kuelekea hatua nyingine.
Watu hao mara zote huwakatisha tamaa wenzao kwa jambo fulani, kwa kuwaambia kuwa, wasijaribu kulifanya kwa kuwa hawatafanikiwa.
Kumbe watu hao, ilitakiwa kuwatia moyo wale wanaotaka kujikwamua kiuchumi kwa kuwaambia kuwa, wajaribu kufanya jambo walilolikusudia.
“Mawazo ya watu kama hao wasiopenda mafanikio ya wengine mara zote ni sumu ya maendeleo”.
Hivyo unapokutana na watu kama hao, unachotakiwa kukifanya, ni kujiwekea mazingira ya kujikinga pale wanapokujia na kutaka kukulisha sumu hiyo.
Lakini kwa upande mwingine, wewe unayependa kupiga hatua kimaisha, unaweza kuyapokea mawazo ya wale wanaowakatisha tamaa wenzao, kama ni njia mojawapo ya kukutoa hapo ulipo na kupiga hatua zaidi.
Kamwe usiruhusu watu hao wasiopenda maendeleo yako kukukatisha tamaa kiasi cha kuharibu ratiba na mipango yako ya kimaendeleo uliyojiwekea.
Kwa kuwa, watu wa namna hiyo wapo kila mahali, na kazi yao ni kuharibu mipango mizuri ya maendeleo ya wengine.
Huweza kutumia wengine kuyabeza mafanikio yako, kukucheka, na pengine huweza kukukopa baadhi ya bidhaa zako na kukuletea usumbufu katika malipo, ili mradi wewe uchukie na kuamua kuacha kufanya biashara uliyoianza.
Hizo ni changamoto zilizopo katika maisha yetu ya kila siku cha msingi, ni kusonga mbele na kufanya kile ulichokusudia bila kuangalia wengine wanasemaje juu yako ya kukurudisha nyuma.
Wapinzani wa maendeleo ya wengine wapo kila mahali. Wengi wao ni wavivu hivyo wanashindwa kukabiliana na ugumu wa maisha, hupenda kuwakatisha tamaa wengine ambao wamekuwa wakikabiliana na changamoto mbalimbali katika kufikia mafanikio wanayoyataka.
Usifanye makosa katika malengo yako. Kwa kuwa hata katika eneo lako la kazi, iwe ni ofisini ama kwenye biashara wapo wanaokukatisha tamaa ya kuendelea na mipango yako.
Kwa kuwa, katika hali halisi tumetofautiana kifikra na kimaendeleo. Miongoni mwetu wapo wale wenye mipango ya kupenda kupiga hatua kila wakati za kimaisha, na wapo wale ambao hupenda kuangalia wengine wanafanya nini na kuwabeza.
Katika hilo, usikate tamaa. Piga hatua zaidi katika kufanikisha malengo yako kwa kuwa na mkakati wa kujiwekea kanuni ya kutafuta ushauri kutoka kwa watu wenye mafanikio zaidi yako.
Ukijijengea tabia ya kuuliza maswali pale unaposhindwa, ni sawa na kutibu ugonjwa wa kansa unaokusumbua.
Vile vile ujue kuwa, katika maisha mafanikio yako pia yanategemea msaada wa kimawazo kutoka kwa wengine.
Huwezi ukawa na mipango yako mwenyewe na mawazo yako mwenyewe ukafanikiwa bila kuomba ushauri kwa wengine walio mbali zaidi yako kimaendeleo, wale unaoweza kuonana nao na kuongea nao bila matatizo.
Changamoto za mafanikioKufanya kazi kwa bidii kunaleta mafanikio. Bila kufanya kazi kwa bidii ni vigumu kupata mafanikio katika maisha.
Njia mojawapo ya kufikia mafanikio hayo ni kuainisha malengo yako unayotaka kuyafikia.
Tukutane Alhamisi ijayo.

IMANI HULETA MAFANIKIO

NAKUKARIBISHA, katika mfululizo wa makala hizi za maisha yetu, zinazokujia kila Alhamisi.
Ili kuwa mtu wa mafanikio ni vema kutumia mbinu ya kufikiri kwa ubunifu kile unachotaka kukifanya.
Ni vizuri kuwa na imani, unaweza kufanya jambo lako na likafanikiwa, kwani unapoamini litafanikiwa, akili yako itazidi kutafuta njia ya kulifanikisha zaidi.
Kuamini kuwa unaweza kufanya jambo kubwa, kunafungua njia ya mafanikio. Kamwe usiseme ama kufikiri kuwa huwezi kufanya jambo fulani katika maisha yako, badala yake, jaribu kufanya kile unachofikiri kuwa huwezi.
Usiruhusu mambo ya mila na desturi ama utamaduni uliouzoea kutawala akili yako.
Kuwa mtu wa kupokea mambo na mawazo mapya kila wakati, kisha uyafanyie kazi.
Kila wakati jaribu njia mpya katika kufanikisha mambo yako, pamoja na kuwa mfuatiliaji wa shughuli zako unazozifanya.
Iulize nafsi yako, inakupasa kufanya nini ili kuweza kufanya vizuri zaidi? Wakati unajiuliza swali hilo, unakuwa tayari umeshapata jibu, cha msingi ni kulifanyia kazi jibu hilo ulilolipata bila kuchelewa.
Pia jiulize ni kwa vipi unaweza kufanya vizuri zaidi? Pia ni vema ukawa na mazoea ya kusikiliza na kuuliza kwa wengine, kuhusu mambo unayotaka kuyafanya kwani utapata mawazo mengi usiyoyajua kutoka kwa wengine.
Yapanue mawazo yako, kwa kujichanganya na watu mbalimbali wakiwamo wenye ujuzi wanaoweza kukupa mawazo na njia mpya za kufanya mambo.
Moja ya kanuni ya mtu anayependa au mwenye mafanikio ni kuwa na muonekano mzuri mbele ya jamii, kuanzia anavyozungumza hadi mavazi yake.
Unaweza usikubaliane nami, lakini ukweli ni kuwa, kama wewe ni mfanyabiashara wa nguo, jinsi unavyokuwa mtanashati mbele za watu, ndivyo watakavyopenda kuja katika duka lako na kununua bidhaa zako hizo.
Lakini, kama utakuwa haujijali kwa upande wa mavazi, halafu ukawa mfanyabiashara wa bidhaa hiyo, utapata wateja wale wasiokujua na wanaokujua wachache.
Utanashati unavutia biashara yako, si tu kwa biashara ya nguo, bali hata katika shughuli zako nyingine unazozifanya, uwe ni mwanasheria, mwalimu ama mpishi wa chakula, vile unavyoonekana ndivyo unavyozidi kuimarisha biashara yako.
Kumbuka watu wanakutathmini kutokana na muonekana ulio nao.
Hebu tuangalie mfano huu kuwa, mtu anafanya biashara ya nyanya, anazipanga mafungu mafungu na kuziuza.
Mwingine anafanya biashara hiyo hiyo, na kuziweka nyanya zile katika mfuko wenye kuonyesha bidhaa iliyopo ndani yake na kufunga vizuri.
Biashara hizo zikiwa katika eneo moja, watu wengi watanunua zile zilizofungwa vizuri kwenye mfuko wakiamini kuwa ni salama zaidi.
Mfano huo ni sawa na muonekana ama utanashati wako kwa watu katika shughuli yoyote ile unayoifanya.
Uvaaji mzuri na wa heshima kwenye jamii, unakufanya uheshimike na kuaminika kuwa unaweza kufanya mambo makubwa unayoyapanga.
Ni vizuri kuboresha mawazo yako kila siku, kama watu maarufu wanavyokuwa.
Kuboresha mawazo, kufikiri na utendaji wako kutakuletea mafanikio katika mipango yako yote.
Hivyo ni vema, kula vizuri ili uweze kufikiri vizuri katika mambo unayoyafanya.
Endapo hautakula mlo kamili, akili yako haitakuwa na uwezo wa kufikiri vizuri, utabakia kuwa mtu wa kushindwa.
Kama mtu anakula vizuri, anajilinda na magonjwa mbalimbali, mwili wake unakuwa na afya pamoja na akili yake kuwaza mambo makubwa.
Akili yako huwezi kuilisha chakula unachokula, bali chakula chake ni mazingira yanayokuzunguka.
Mtu yeyote anayetembea katika nchi ama mikoa mbalimbali, huwa na mazingira ya tofauti, kila anapokwenda hujifunza kitu kitakachomsaidia.
Mazingira ya eneo ulilopo yanaifanya akili yako ifikiri zaidi ufanye kitu gani cha mafanikio katika eneo hilo ulilopo kitachokupatia maendeleo.
Ukubwa wa jinsi unavyowaza, malengo yako, mazingira yako au vile unavyoonekana, ni kutokana na mazingira uliyopo.
Unapokuwa na watu wenye mawazo ya kuchelewa kufanikisha mambo, nawe utakuwa mtu wa kuchelewa kufikia malengo uliyojiwekea.
Kwa maana nyingine, kushirikiana na watu wenye mawazo makubwa kunakufanya uwaze mambo makubwa ya maendeleo.
Pia kukaa karibu na watu wenye malengo ama maono ya mafanikio, kunakufanya nawe uwe katika hali hiyo.
Katika jamii tunayoishi, kumekuwa na watu wenye tabia zilizogawanyika katika makundi matatu.
Kundi la kwanza, ni la watu wale ambao wameona kuwa hawawezi kufanya jambo likafanikiwa kabisa.
Wamekuwa na ujuzi na kukubali ujuzi huo katika eneo moja, yaani wameridhika na hali hiyo.
Kama, Mungu amekupa ujuzi wako mzuri na ukabahatika kupata kazi sehemu nzuri, pamoja na kufanya kazi ile, utumie ujuzi wako katika maeneo mengine.
Unaweza kufungua ofisi yako na kuanzisha kitu chako mwenyewe huku ukiendelea na kazi yako.
Kamwe usijikatishe tamaa kwa kuona kuwa huwezi kufanya hivyo, kudhani kuwa, wewe umeumbwa kwa ajili ya kufanya kazi za wengine tu.
Kuna watu wenye malengo makubwa na waliopanga kuyatimiza lakini kutokana na ushindani uliopo hufika mahali na kushindwa kuendelea na mikakati waliyojiwekea.
Tunaweza kusema, wamekata tamaa na kuacha kuyafanyia kazi malengo yao, mwishoni hupoteza mwelekeo kabisa.
Kundi hili, wamejijengea tabia ya hofu, hofu ya kushindwa kutimiza malengo yao, hofu ya ulinzi, hofu katika jamii inayomzunguka na kupoteza kila wanalicho nacho.
Kundi la watu hawa, kamwe hawatafanikiwa kwani wameshajiweka kwenye kundi la kushindwa ingawa lina watu wenye akili, vipaji walivyojaliwa na Mwenyezi Mungu.
Kundi la tatu ni la watu wale ambao hawako tayari kukatishwa tamaa, hawa ni asilimia ndogo sana katika jamii.
Kundi hili pamoja na kukatishwa tamaa, katika mipango yao, wamekuwa wakijitahidi kufanya jitihada mbalimbali ili wajikwamue katika hali hiyo waliyonayo na kuwa katika hatua nyingine.
Mara zote hupumua mafanikio katika maisha yao. Kundi hili pia lina furaha kwa kuwa limeshakamilisha baadhi ya malengo waliyojiwekea.
Wamekuwa wakipitia changamoto mbalimbali, lakini wamezishinda, wamekuwa wakiangalia siku mpya ikianza na jambo jipya.
Ni ukweli usiopingika kuwa, kila mmoja wetu anapenda kuwa katika kundi la tatu, ambalo kila mwaka wanapata mafanikio, wanaofanya mambo mbalimbali na matokeo yake yanaonekana.
Tukutane Alhamisi ijayo.
Makala hii imeandaliwa kwa msaada wa kitabu cha 'The Magic of Thinking Big,’ kilichotungwa na David Schwartz pamoja na mitandao mbalimbali.

BUNI NJIA ZA MAFANIKIO

MSOMAJI wangu, katika mfululizo wa makala hii ya maisha yetu, nimedhamiria kukuletea kitu kipya kila Alhamisi.
Leo tutaangalia ujasiri unavyomfanya mtu kubuni njia mbalimbali za mafanikio.
Kila mmoja anapenda kuwa na mafanikio katika maisha yake, lakini mafanikio hayaji tu bila kufanya juhudi ama jitihada za dhati.
Mojawapo ya njia inayoweza kukutoa hapo ulipo na kukupeleka katika hatua nyingine nzuri zaidi ni ubunifu.
Mtu yeyote anayependa kuwa na mafanikio maishani, inambidi awe mbunifu katika nyanja mbalimbali ili kama yeye ni mfanyabiashara aweze kuteka soko kubwa.
Unaweza kuwa mbunifu katika fani yoyote ile uliyonayo, ama kipaji ulichopewa na Mungu, kitakachokufanya uwe mtu tofauti katika maisha yako.
Kama wewe ni mwalimu ambaye ni mbunifu wa kufundisha, maisha yako yatakuwa mazuri kwa sababu utasifika kwenye shule yako na sifa zako zitafika mbali hadi shule nyingine.
Hali hiyo itakufanya utafutwe na shule nyingi, hivyo ni uamuzi wako kuchagua uende wapi.
Ama utatafutwa na wanafunzi kutoka shule mbalimbali uweze kuwasaidia katika masomo yao ili waweze kufaulu mtihani, hapo wewe si yule wa zamani bali umekuwa mtu mwingine wa tofauti, kutokana na ubunifu wako.
Kama wewe, una ofisi ya ushonaji na ukawa mbunifu mzuri wa mavazi, sifa zako zitafika mbali zaidi na watu wengi watakutafuta kwa ajili ya kuwabunia mavazi yao.
Tayari utakuwa umeshajijengea jina, cha msingi ni kuongeza jitihada ili wale wateja wako usiwapoteze.
Kama wewe ni mbunifu wa kupika chakula ama vitafunwa mbalimbali, utajulikana mtaani, kwenye ofisi ama kampuni mbalimbali na hata kutafutwa na watu kwa ajili ya shughuli zao za sherehe.
Hiyo ni mifano michache sana, ambayo unaweza kujifunza. Si hiyo tu, bali unaweza kutumia uhandisi wako kwa kujenga nyumba nzuri, ukatumia uandishi wako kwa kuandika habari nzuri, ukatumia udaktari wako kutoa ushauri na kutibu vizuri wagonjwa unaowaoona.
Tumia akili yako uliyopewa na Mungu, kwa kuwa mbunifu ili uweze kuwa na maisha mazuri.
Binafsi ninaamini kuwa kila mmoja Mungu amempa kipaji ama akili kwa ajili ya kuwa mbunifu.
Tatizo lililopo kwa watu wengi ni kukata tamaa. Wengi wamekuwa wakikatishwa tamaa na ndugu, jamaa ama marafiki zao.
Na mara nyingi, wanaweza kufanya jambo na lisifanikiwe kama walivyofikiri matokeo yake, badala ya kutafuta ufumbuzi kwa nini hali hiyo imetokea, hukata tamaa na kuamini kuwa hawezi kufanya jambo lolote likafanikiwa labda aajiriwe tu.
Inabidi tubadilike kimtazamo, kiakili na kifikra ili kila mmoja afurahie maisha yake aliyopangiwa na Mwenyezi Mungu hapa duniani.
Hivyo, endapo unaamini jambo fulani haliwezekani, ndivyo itakavyokuwa.
Lakini endapo unaamini kuwa jambo fulani linawezekana, akili yako italifanyia kazi na kutafuta njia ya kulifanikisha.
Kuamini kuwa unaweza kufanya jambo, kunakufungulia milango zaidi ya kuwa mbunifu katika shughuli na maisha yako.
Akili yako, itafungua njia ya mafanikio kama utaitumia vema.
Na pia, kama unataka kuona njia ya kukutoa hapo ulipo, ondoa ukuta wa kuona kuwa haiwezekani, ndipo mafanikio yako yatakapoonekana.
Mafanikio makubwa yanakwenda kwa mtu anayefikiri kuwa na maisha ya viwango kwa ajili yake na wengine.
Ni vizuri pia kuboresha biashara zako ama shughuli zako unazozifanya kwa ajili ya kukupatia riziki, ili wengine waweze kufurahia huduma zako na kukutafuta.
Pia unaweza kujijengea tabia ya kuwa na mazoea ya kufikiri mbinu mbalimbali za maendeleo kwa dakika 10 kila siku, kabla hujaanza kazi yoyote.
Zoezi hilo, ni rahisi na kama utalizingatia utaona matokeo yake mazuri, ni vema kulizingatia.
Kwa upande mwingine, utagundua kuwa, watu wote waliofanikiwa, hupenda kujishughulisha, si wavivu.
Penda kujiuliza unatakiwa kufanya nini ili uzalishe zaidi? Ama uwe na maisha bora zaidi? Majibu ya maswali hayo ndiyo yatakayokufanya uongeze bidii zaidi.
Na kwamba, ili uweze kuzalisha kitu chochote, unatakiwa uwe na malighafi.
Katika kufikia uamuzi makini, malighafi ni mawazo na mapendekezo ya watu wengine.
Kuwa makini, usipende sana kuhitimisha jambo lako, kwa mawazo ya wengine. Kwani mawazo ya wengine yanakusaidia kuchekecha mawazo yako mwenyewe kwa kuwa akili yako ina ubunifu.
Ili ufanikiwe katika kampuni yako ama kiwanda chako, inakupasa ufanye utafiti wa kujua ubora wa bidhaa zako kwa wengine.
Uliza maswali kuhusu ubora wa bidhaa zako, ukubwa wake, bei yake ama mwonekano wake kwa jamii uko vipi ili uweze kufanya maboresho pale inapotakiwa.
Kuwasikiliza wengine, kunakufanya kukuwezesha kuboresha pale penye upungufu.
Tukutane wiki ijayo.
Makala hii imeandaliwa kwa msaada wa kitabu cha ‘The Magic of Thinking Big’, kilichotungwa na David Schwartz pamoja na mitandao mbalimbali.

JINSI YA KUPANGA MALENGO YAKO

MSOMAJI wangu, nakukaribisha tena katika mfululizo wa makala hizi za maisha yetu, zinzokujia kila Alhamisi.
Leo tutaangalia jinsi unavyoweza kupanga malengo makubwa katika maisha yako.
Watu wengi hushindwa kufikia malengo makubwa kwa kuwa, mara zote hujikatisha tamaa kuwa hawawezi kufanya jambo kubwa la kimaendeleo, kabla ya kujaribu kulifanya.
Tabia ya baadhi ya watu hao wanaokuwa na malengo madogo katika mazingira wanayoishi, ina maanisha eneo hilo hakuna ushindani wa kimaendeleo, ama wao wenyewe hawana jitihada za dhati za kupiga hatua zaidi mbele.
Lakini ikimbukwe kuwa, katika kutafuta mafanikio hayo ili uwe na maisha bora, usimwangalie mtu jinsi alivyo, kwamba ana urefu gani, ana pesa kiasi gani, digrii aliyonayo ama kuangalia historia ya maisha yake, bali hupimwa kwa uwezo wa kufikiri kwake.
Watu wengi wanaofikiria kuwa na malengo makubwa ya mafanikio, katika maisha yao ni kutokana na matarajio waliyonayo.
Inakupasa kila mara ujitahidi kupanua mawazo yako na kubuni mbinu mpya za kukutoa hapo ulipo na kukuweka katika hatua nyingine nzuri zaidi kimaendeleo.
Hivyo utambue kuwa, unapotaka kufanya mambo makubwa inakupasa ujijue wewe ni nani na una thamani gani.
Kwa maelezo mengine usijishushe hadhi yako kwa kuona kuwa huwezi kufanya mambo makubwa ya kimaendeleo ambayo yatakutoa hapo ulipo na kukuweka katika hatua nyingine nzuri zaidi.
Tuangalie mfano wa kijana mmoja aliyeshindwa kupiga hatua mbele baada ya kujishusha hadhi yake na kujiona hawezi.
Kijana huyo, aliona tangazo la kazi katika gazeti. Kazi aliyokuwa anapenda kuifanya na pia ameisomea.
Lakini hakufanya jitihada za dhati za kuomba nafasi ile, kwa kuwa alijiona hawezi kuipata hata kama angeomba.
Aliona kuliko ajitaabishe ni heri aache kuomba nafasi hiyo. Mfano huo si mzuri kwa mtu anayetaka kupiga hatua kimaisha.
Usijishushe hadhi yako ama usikatishwe tamaa kwa hali yoyote ile. Ni vema kujaribu kile unachokipenda na unachokihitaji katika maisha yako, kuliko kuacha kujaribu kwa kuogopa kuwa hautafanikiwa.
Kwani matokeo huja baadaye, hata utakaposhindwa, utakuwa na nguvu ya kujaribu tena sehemu nyingine.
Wengi wetu, tumekuwa tukijikatisha tamaa katika shughuli mbalimbali tuzifanyazo ama tunazotaka kuzifanya.
Yawezekana umeanzisha biashara kwa lengo la kukuinua kiuchumi, lakini matokeo yake, biashara hiyo haiendi kama vile ulivyotarajia.
Jambo la msingi, inakupasa kukaa chini na kujitathmini, kuangalia ni sehemu gani unayokosea.
Ama kuangalia, kama una washindani wengi katika eneo hilo, ili uweze kufanya vizuri zaidi yao, kwa kuweka vitu vingi tofauti na kuboresha eneo la biashara yako.
Kuwa mbunifu katika biashara yako kutakupa wateja wengi, na utafanikiwa zaidi. Cha msingi usikate tamaa katika kufikia malengo unayoyakusudia.
Kutokana na hali ya kujikatisha tamaa, miongoni mwa watu wengi, wanasaikolojia mbalimbali wamekuwa wakishauri ni vema, watu wajijue vile walivyo ili waweze kujirekebisha pale penye upungufu na kusonga mbele kimaisha.
Hali ya kujikatisha tamaa ni mbaya sana, ni sawa na ugonjwa usiopona katika mwili wako. Ili kuutibu ugonjwa huo, inakupasa ujielewe wewe ni nani, na una upungufu gani, pamoja na kukubali mabadiliko.
Tatizo kubwa lililopo kwa watu wengi, hawajui kuwa, wao wana uwezo mkubwa tofauti na wanavyojifikiria.
Hivyo ni vema kuweka mawazo yako kwenye kipimo halisi, uyachuje na kuchukua yale yaliyo na thamani.
Penda kufikiri mambo makubwa. Usijishushe hadhi yako kwa kujiwekea au kufikiri malengo madogo. Anza sasa kuwaza mambo makubwa ili uwe mtu mwenye ndoto njema ya maendeleo.
Kutokana na hali hiyo ya watu kujikatisha tamaa, wale ambao wamewahi kufanya biashara na kufilisika, wengi wao wamekuwa wakisema kuwa hawatarudia tena kufanya biashara hiyo.
Lakini kumbe, haikuwapasa kukata tamaa, bali kujipa moyo, na kuelewa kuwa pamoja na hali hiyo ya kushindwa inawapasa kujaribu tena.
Kamwe usikate tamaa katika jambo lolote unaloliwaza ama kulifanya. Kwa kuwa, upo msemo mmoja unaosema, penye nia pana njia.
Tukutane wiki ijayo.
Makala hii imeandaliwa kwa msaada wa kitabu cha ‘The Magic of Thinking Big’, kilichotungwa na David Schwartz pamoja na mitandao mbalimbali.

ONDOA HOFU, KUWA JASIRI

KARIBU msomaji wa safu hii ya maisha yetu inayokujia kila siku ya Alhamisi.
Leo tutaangalia jinsi ya kuwa na ujasiri na kuondoa hofu katika maisha yako.
Hofu si jambo zuri katika maisha, lakini ni ukweli usiopingika kuwa, kila mtu hupatwa na hofu kutokana na jambo fulani analokutana nalo.
Hofu hiyo hukaa nayo kwa dakika chache kabla ya kutoweka. Lakini wapo wengine hukaa nayo kwa siku nzima. Kutegemea ni jinsi gani unavyoidhibiti hofu hiyo.
Watu wengi hukabiliwa na hali ya wasiwasi, kutokutulia, kudharauliwa, kuchanganyikiwa au mambo yake kutokuwa katika mpangilio mzuri, pamoja na kuwa na mawazo hasi.
Hali hiyo, isipodhibitiwa kwa haraka huleta usumbufu katika maisha yake. Hivyo ni vema kujijengea hali ya ujasiri na kuondoa hofu, katika jambo lolote lile unalolifanya.
Kwa mfano, kama umeamua kulima ekari tano, utimize lengo lako, usiwe tayari kukatishwa tamaa na maneno kutoka kwa wengine, kuwa hakutakuwa na mvua, ama ardhi haina rutuba nzuri, ng’ang’ana pale ulipojiwekea malengo yako.
Ama umedhamiria kufungua duka eneo fulani, wapo watakaokuunga mkono, pia wapo watakaokukatisha tamaa, cha msingi, fanya kile ulichokusudia kukifanya, mradi kiko kwenye mpangilio wako na umekifanyia maandalizi ya kutosha.
Fahamu kuwa, biashara yoyote haiwafuati wateja, bali wateja ndio wanaoifuata. Hivyo ubunifu wako ndiyo utakaokufanya usonge mbele na kukabiliana na changamoto katika biashara hiyo.
Kamwe usiingize hofu katika uamuzi wako, kutokana na maneno ya watu wengine ya kukuvunja moyo.
Hivyo utaona hofu ni adui namba moja wa maendeleo yako. Pia hurudisha nyuma maendeleo ya watu, kwa kuwazuia kufanya mambo yatakayowafanya wasonge mbele.
Pia humfanya mtu augue, husababisha matatizo ya kimaumbile, hufupisha maisha na hukunyamazisha pale unapotaka kuzungumza. Hivyo ni vizuri ukaondoa hali ya hofu katika maisha yako.
Hofu hukuletea hali ya mashaka, ambayo hukufanya usiwe na uamuzi sahihi. Inakuondolea hali ya kujiamini, ya kuweza kujitathmini kwa nini unakuwa na hali ngumu ya kiuchumi.
Ukweli ni kwamba, hofu ina nguvu katika maisha ya mwanadamu. Kwa njia moja ama nyingine hali hiyo inazuia watu kupata kile wanachokihitaji katika maisha.
Hofu kwa jinsi yoyote ile ni athari za saikolojia. Unaweza kuitibu hali hiyo kama vile unavyotibu magonjwa katika mwili wako.
Kwanza, kuwa na maandalizi wewe mwenyewe ya kuondoa hali hiyo, kwa kuwa na hali ya kujiamini. Kwa kuwa, hakuna yeyote aliyezaliwa katika hali hiyo ya kujiamini, bali wameishinda hali hiyo.
Hata pale unapokabiliwa na hali ngumu katika maisha, usikate tamaa, chukua hatua madhubuti ya kupambana na hali hiyo, njia itaonekana kwako.
Inakupasa kuondoa hali ya hofu uliyonayo ili uweze kupiga hatua zaidi.
Endapo unakabiliwa na hali ya hofu ya kupoteza wateja wako muhimu kulingana na ushindani ulionao, fanya kazi mara mbili zaidi ili kutoa huduma bora zaidi, weka vitu vile vinavyowafanya wateja wako wakukimbie, utafanikiwa.
Ama unakabiliwa na hofu ya kupata ajali wakati ukiendesha gari, ni vema kuwa makini na kuvaa ujasiri ili kuondoa hofu kwa abiria wengine waliopo kwenye gari.
Yamkini unaweza kujikuta unakabiliwa na hofu ya watu wengine hufikiri ama kusema nini juu yako. Inakupasa kuweka mipango yako vizuri na kuikamilisha kama ulivyoipanga ili kutimiza kile ulichokikusudia.
Katika kutibu hali hiyo, iondoe hofu uliyonayo, pamoja na kuchukua hatua madhubuti za kuondoa hali hiyo.
Kadiri unavyoshindwa kuwa na ujasiri, ndivyo unavyoshindwa kujisimamia katika mipango yako.
Akili yako ni kama benki, kila siku unawaza mambo mapya unayoyahifadhi katika benki yako.
Mawazo hayo unapoyaweka katika benki ya akili yako, yanakuwa na kukaa katika kumbukumbu zako.
Pale unapokabiliana na tatizo, unaangalia katika benki yako na kupata jibu sahihi. Benki yako itatoa majibu na kusambaza taarifa mbalimbali zinazohusiana na hali unayokabiliana nayo.
Lakini ili benki yako iwe na manufaa kwako, inakupasa uweke mawazo mazuri yenye kukupatia maendeleo.
Iwapo unakula, ama unaendesha gari wakati ukiwa mwenyewe, ni wakati wako mzuri wa kuhifadhi mawazo mazuri katika benki yako. Pia kabla ya kulala, ni vema kuweka mawazo mazuri katika benki yako.
Waza kuwa na maisha mazuri, familia nzuri, afya njema, elimu nzuri na hali ya kupata mahitaji yote katika utoshelevu.
Pia katika benki yako, unatakiwa kuchukua mawazo mazuri tu. endapo utachukua mawazo mabaya, yatakuletea usumbufu au hali ya kuchanganyikiwa.
Tukutane wiki ijayo.
Makala hii imeandaliwa kwa msaada wa kitabu cha The Magic of Thinking Big, kilichotungwa na David Schwartz.

JIAMINI UTAFANIKIWA

MSOMAJI wangu, katika mfululizo wa makala hizi za Maisha Yetu, nimedhamiria kukuletea kitu kipya kila Alhamisi.
Leo tutaangalia jinsi ambavyo kila mmoja anapaswa kujijengea uwezo wa kuweza kujiamini ili kupata mafanikio.
Kila mmoja anapaswa kutamani kuwa kiongozi yeye mwenyewe, ili aweze kujenga uwezo wa kuwa na maendeleo binafsi, pasipo kutamani maendeleo ya mtu mwingine.
Kwasababu hakuna mtu atakayemlazimisha mtu mwingine kupata mafanikio.
Lakini kwa upande mwingine, suala la mafanikio ni jambo linalotokana na muda uliopo, kujitoa na kufanyia kazi mambo mbalimbali mtu anayoyapanga.
Hivyo ujue wazi hakuna mtu atakayekulazimisha wewe kupata mafanikio, bali inakupasa kufanya bidii binafsi ili ufikie matarajio ya juu uliyojipangia.
Haya yakizingatiwa, kila mmoja atakuwa na ari ya kujisimamia, kufanya kazi kwa bidii katika mipango mbalimbali ya maendeleo ya ukuaji wa uchumi.
Sasa basi ili uweze kukua na kupata maendeleo, inakupasa kila jambo unalolipanga uweze kulitekeleza.
Ni vema kuanza kufanya jitihada binafsi za kupata maendeleo, pamoja na kufanya tathmini ya hapo ulipo na ulipotoka, taratibu utajikuta unapiga hatua siku baada ya siku.
Kwa kuwa, tayari unayo maabara iliyosheheni kila hitaji la mwanadamu, unayotakiwa kuichunguza na kuifanyia kazi, ni vema kujibidiisha ili uweze kukitumia kila kifaa kilichopo ndani yake, kwa ajili ya maendeleo.
Hakuna kikwazo chochote katika maabara hiyo, kinachoweza kukukwamisha, kama utajitambua kama wewe ni mhusika mkuu katika maabara hiyo ni wazi utapenda kujua kazi ya kila kifaa.
Kwa kuwa, ndani ya maabara hiyo, hakuna kitu cha kununua, kodi ya kulipa, wala ada ya aina yoyote ila unaweza kuitumia vile unavyopenda bila malipo yoyote.
Kama wewe ni msimamizi katika maabara yako mwenyewe, utapenda kufanya vile wanasayansi wengine wanavyofanya.
Unaweza kushangaa kwa nini watu wengi wana uelewa mdogo wa kufikia mafanikio, wakati wanazungukwa na wenye mafanikio makubwa.
Hii ni kwa sababu watu wengi hawafuatilii mambo yanayofanywa na wengine ili kufikia malengo makubwa.
Hivyo basi, Mtunzi David Sachwartz, nia yake ni kukusaidia kwa kuchunguza na kuangalia undani wa mambo yanayofanywa na wengine ambao wameweza kufanikiwa.
Kuna uchaguzi wa aina mbili wa kukusaidia ili uweze kufanikiwa; mojawapo ukiwa ni kupenda kujifunza kwa kuchunguza kila kitu unachokiona na kuamini kuwa kinaweza kukupatia maendeleo.
Pia unaweza kuchagua mifano ya watu wawili ambao unaweza kuwatumia kwa ajili ya kujifunzia katika kupata mafanikio yako.
Unatakiwa kuwachagua watu ambao mmoja wao, amefanikiwa na mwingine ambaye hajafikia mafanikio, ambao unawajua vema.
Anza kufuatilia kila jambo wanalolifanya, utapata somo litalokufumbua macho.
Kila unachojifunza kwa watu hao, kinakuwezesha kupiga hatua zaidi, lengo lako likiwa ni kuangalia kanuni za kufikia mafanikio. Pia kwa kutumia mifano ya watu hao, ndivyo utakavyopata mbinu mpya za kukabiliana na changamoto za maisha kufikia mafanikio.
Ni jambo la kufurahisha unapokuwa na ujasiri, na kufanikiwa kila unachopanga, kujiangalia unavyokuwa siku baada ya siku na mwezi baada ya mwezi.
Makala hii imeandikwa kwa msaada wa kitabu cha ‘The Magic of Thinking Big’, mtunzi wake ni David Schwartz.
Tukutane Alhamisi ijayo.

HUU NDIO UGONJWA WA KUSHINDWA KUFIKIA MALENGO

MSOMAJI wangu, katika mfululizo wa makala hizi za maisha yetu, nimedhamiria kukuletea kitu kipya kila alhamisi.
Leo tutaangalia jinsi ya kukabiliana na ugonjwa wa kushindwa kufikia malengo.
Kila mmoja tayari ana vifaa vya kutosha katika maabara yake ambayo anaweza kuitumia kwa ajili ya kazi na kujifunza.
Maabara ambayo ina kila kitu kinachokuzunguka katika dunia hii. Ambamo hutapata vikwazo, kwa kuwa kila utakachojifunza utajiona kama wewe ni mtaalamu.
Ukiweza kuitumia vizuri maabara hiyo, itakuwezesha kumaliza matatizo yako ya kifamilia kama vile, kulipia kodi ya nyumba, kulipia ada za shule na mambo mengine yanayofanana na hayo. Hivyo unaweza kuitumia maabara hiyo kwa uhuru zaidi jinsi unavyopenda.
Kwa upande mwingine, unaweza kuwaza jinsi ya kuwa na malengo makubwa katika maisha, kwa kupenda kujifunza kwa wengine waliofanikiwa.
Lakini angalizo lililopo, unatakiwa kujifunza kutoka kwa wengine kwa uangalifu. Pale unapopata jambo linalokufaa lifanyie kazi.
Unapoendelea kujifunza kutoka kwa wengine, utaona kuwa, watu wasiokuwa na mafanikio wanataabika katika akili zao kwa ugonjwa wa kufikiri.
Kila mtu asiyefikia malengo ya mafanikio amekuwa na ugonjwa huo kwa kiwango kikubwa.
Na mara zote mtu mwenye malengo makubwa hupenda kujiuliza ni kwanini hapo alipofikia hajafanikiwa, kwa nini hana kitu fulani au kwanini hawezi kufanya jambo fulani, ili aweze kupiga hatua zaidi ya hapo alipo.
Kama ugonjwa mwingine wowote unavyompata mtu, ugonjwa wa kufikiri unakuwa mbaya sana endapo hautatibiwa vizuri.
Muathirika wa ugonjwa huu, anakuwa akiwaza mambo mengi, kama vile ‘najaribu kufanya jambo hili na lile lakini sipati mafanikio’ na kuendelea kuwaza: “ Je, ni afya mbaya niliyonayo” au ni ukosefu wa elimu? Umri mkubwa? Umri mdogo? Bahati mbaya? Ama kutokuwa na bahati ya maisha? Mke? Ama jinsi nilivyolelewa na familia yangu?”
Hivyo mtu huyo aliyeathirika na ugonjwa huo, asipojigundua ataendelea na hali hiyo katika maisha yake.
Ili kukabiliana na hali hiyo, ni vizuri kujizoeza kuwa na mawazo chanya yenye mafanikio, ambayo ndiyo tiba ya ugonjwa wa kushindwa.
watu wenye ugonjwa wa kushindwa huwa na visingizio mbalimbali kama vile ‘afya yangu siyo nzuri’. Hiyo hufanya kila siku anapopata changamoto ya maisha badala ya kutoka hapo alipo, kuwa na jambo lolote la utetezi fulani.
Anakuwa na afya mbaya katika aina tofauti tofauti, ambacho ndicho kisingizio chake anaposhindwa kufanya jambo linalompatia maendeleo.
Wapo watu wengine wamekuwa wakisingizia wana matatizo ya moyo, na wamekwenda kwa daktari zaidi ya mara nne, na kila wanapokwenda ugonjwa hauonekani.
Kuendelea kueleza kuwa, una ugonjwa wa moyo, mwisho wa siku tatizo hilo litakupata kweli. Kinachotakiwa ni kuishinda hali hiyo na kusonga mbele katika kupata maendeleo yako katika maisha, bila kujali unasumbuliwa na kitu gani.
Sasa basi yapo mambo manne ambayo yanaweza kukupa afya njema na kuondokana na hiyo hali inayokufanya ukate tamaa, ama kufikiria kuwa huwezi kila jambo lililopo mbele yako.
Kwanza usikubali kuizungumzia afya yako. Kadiri unavyozungumzia kuhusu ugonjwa unaokusumbua, hata kama ni wa kawaida, ndivyo utakavyozidi kukusumbua.
Kuzungumzia kuhusu afya yako kama ni mbaya ni kama unaweka mbolea kwenye mbegu zilizopandwa.
Kuzungumzia afya yako ni tabia mbaya. Inachosha wengine. Watu waliofanikiwa wana tabia ya kutokuzungumiza afya zao zinapokuwa mbaya.
Pili usiwe na hofu juu ya afya yako. Fanya kile unachokusudia ili kufikia malengo mazuri.
Tatu, jione kuwa afya yako ni njema haina kasoro. Na pia endelea kujikumbusha kuwa, maisha yapo kwa ajili ya kuyafurahia. Usipoteze. Wala usiishi kwa kufikiri juu ya kulazwa hospitali.
Vile vile usipende kuchunguza kwa nini mipango unayoipanga haifanikiwi, bali ichekeche akili yako kuelekea njia ya mafanikio.
Tukutane wiki ijayo.

AKILI YAKO NI KIWANDA CHA MAFANIKO

MSOMAJI wangu, katika mfululizo wa makala hizi za maisha yetu, nimedhamiria kukuletea kitu kipya kila Alhamisi. Leo tunazungumzia ili ufanikiwe unatakiwa ufanye nini.
Ni ukweli usiopingika kuwa, ili ufanikiwe katika maisha yako, inakubidi ufanye jitihada ya dhati. Kwa kujiuliza ni wapi uliposhindwa, ili uweze kuongeza bidii.
Vile vile, ni vema kuangalia udhaifu wako ulipo, ili uweze kurekebisha pale unapokosea katika kufikia mafanikio unayoyataka.
Watu wengi hupenda kuwa na mafanikio makubwa, lakini hawaonyeshi jitihada za dhati za kuwatoa pale walipo na kuwasogeza mbele.
Mara zote hukata tamaa kwa kuwaza mambo ambayo huwarudisha nyuma, hawako tayari kukubaliana na ukweli kuwa wanaweza kufanya jambo lolote ili kufikia malengo makubwa, cha msingi kinachotakiwa ni jitihada.
Hivyo basi, ni vizuri kuiambia nafsi yako, kuwa wewe unaweza kufanya jambo fulani kubwa litalokutoa hapo ulipo na kukufikisha sehemu nyingine yenye mafanikio zaidi.
Watu wengi hawaamini kuwa, Mungu amewabariki kwa kuwapa utajiri mwingi katika maisha yao, kwa kuwa, hawajui akili, nguvu, vipaji mbalimbali walivyonavyo ni utajiri tosha Mungu aliowapa katika maisha yao.
Ni vema kujiamini kuwa unaweza kufanya jambo kubwa katika maisha. Jitihada katika jambo lolote linakuleta mafanikio, kwa kukutoa katika hatua moja na kukupeleka katika hatua nyingine.
Vinginevyo utabakia kila siku ukiiambia nafsi yako, kwa nini wengine wanafanikiwa na wewe unabaki katika hali ile ile.
Jione kuwa wewe ni mtu wa thamani na ni mtu wa daraja la kwanza. Pia jenga hali ya kujiamini katika kila jambo unalotaka kulifanya.
Jiamini wewe mwenyewe na mambo mazuri yatatokea kwako, usiwe na hali ya hofu katika mambo uyafanyayo.
Akili yako ni kiwanda cha fikra. Ni kiwanda kilicho na shughuli nyingi. Hivyo itumie kwa busara upate mafanikio mengi.
Utakapoitumia akili yako vizuri utajikuta kila siku unapiga hatua zaidi. Kamwe usiiruhusu akili yako kuwaza kushindwa.
Unapodhamiria kufanya jambo fulani amini kuwa utafanikiwa. Wasiwasi utakufanya ushindwe katika kila unalotaka kulifanya.
Inuka, mlango wa mafanikio uko wazi na ujiweke kwenye kumbukumbu sasa kwamba unajiunga na kundi ambalo linakubali mabadiliko katika maisha.
Na hatua ya kwanza katika maisha yako, ambayo huwezi kuiepuka, amini kuwa unaweza kufanikiwa.
Je, ni jinsi gani, unaweza kuwa katika hali ya kujiamini kwamba unaweza kufanya jambo lolote na ukafanikiwa?
Ni pale tu utapofikiri kuhusu mafanikio yako na siyo kushindwa, uwapo kazini kwako ama nyumbani.
Hata pale utakapoona unapokabiliwa na hali ngumu, jiambie kuwa utashinda. Na kama upo ushindani kati yako na mtu mwingine, fikiri kuwa, una uwezo wa kushinda na si kushindwa.
Na nafasi ya kushinda inapoonekana, fikiri kuwa unaweza na si kwamba huwezi. Akili yako mara zote ifikiri kuwa unaweza kufanya jambo la mafanikio katika maisha.
Hali ya kuwaza mafanikio inakufanya katika akili yako uweke mikakati ya kukufanya upige hatua zaidi. Kinyume na hapo, utakaporuhusu akili yako kuwaza hali ya kushindwa, kamwe hautapiga hatua yoyote, kila mara utabakia pale pale.
Jambo jingine jikumbushe kwamba wewe ni bora kuliko unavyodhani. Watu wenye mafanikio si kwamba wana nguvu zaidi ya wengine.
Wala mafanikio si suala la kuona mtu fulani ana bahati, bali ni hali inayoweza kujengwa na mtu mwenyewe kwa kuongeza bidii.
Panda kuwaza mambo makubwa, ukubwa wa mafanikio yako unategemea jinsi unavyowaza. Kama unawaza malengo madogo, utarajie kupata mafanikio madogo.
Unapofikiri malengo makubwa, unakuwa na mafanikio makubwa pia.
Kumbuka hili, mawazo na malengo makubwa, mara zote yanarahisisha mambo yako na kukufanya usipate vikwazo vingi, tofauti na unavyowaza malengo madogo.
Makala hii imeandaliwa kwa msaada wa kitabu cha ‘The Magic of Thinking Big’ kilichotungwa na David Schwartz.
Tukutane alhamisi ijayo.

AMINI KUWA UNAWEZA KUFANIKIWA

MSOMAJI wangu, katika mfululizo wa makala hizi za maisha yetu, nimedhamiria kukuletea kitu kipya kila Alhamisi. Leo tutaangalia jinsi ya kuwa na malengo makubwa katika maisha.
Kufikiria mambo makubwa katika maisha, kunakuwezesha kuishi maisha mazuri, yenye furaha, utimilifu, kipato kizuri, marafiki na heshima.
Mafanikio maana yake ni kupata mahitaji unayohitaji, kustawi katika maisha, kuwa na nyumba nzuri, kupata safari, kuwa na vitu vipya, fedha zinazotosheleza mahitaji, pamoja na kuwapa watoto wako mahitaji ya muhimu.
Vile vile kwa maelezo mengine mafanikio ni kupandishwa cheo kazini kwako, kuendelea kuwa karibu na watu katika biashara zako na maisha yako kwa ujumla.
Pia kwa maelezo mengine, ni kujiheshimu, kuendelea kuwa na furaha pamoja na kutosheka katika maisha, kuwa na uwezo wa kufanya zaidi kwa wote wanaokutegemea.
Maana yake nyingine ni kushinda ama kufaulu katika maisha.
Kila mwanadamu anapenda kuwa na mafanikio katika maisha yake, hakuna hata mmoja anayefurahia hali ya kutokupiga hatua katika maisha, pia hakuna anayependa kuwa nyuma katika maisha haya tunayoishi.
Hivyo ni vizuri kupenda kujenga imani ya kujiamini kuwa unaweza kufanya jambo fulani ulilokusudia na kufanikiwa.
Kwa kuwa, mtu yeyote anapoweka nia kuwa anaweza jambo fulani, anafanikiwa. Lakini kinyume cha hapo, kamwe hatafanikiwa, atabakia katika hatua ile ile kila siku, ilhali wengine wakiwa wanasonga mbele.
Kila siku ulimwenguni, vijana wanaomaliza vyuo huanza kazi mpya. Kila mmoja anafikiria kuwa siku moja atafurahia mafanikio yatayompandisha juu kwa kumtoa hapo alipo na kumpa nafasi nyingine nzuri zaidi.
Lakini wengi wa vijana hao, hawafikirii kwamba ipo siku wanaweza kufika mbali zaidi ya hapo walipo. Matokeo yake, hawafiki mbali kwa kuwa hawana imani ya kuwatoa hapo walipo.
Matokeo yake, hubakia kuwa watu wa kawaida katika maisha yao.
Lakini kuna baadhi ya vijana wachache, wanaoamini kuwa, katika kipindi kifupi, tokea waanze kazi, watakuwa wameshasonga mbele zaidi.
Wanakuwa wanawaza kufika mbali zaidi na kuamini hivyo kunatokana na imani yao hiyo na kufikia pale walipokusudia.
Vijana hao huwa wajanja kwa kuwatazama wale waliowatangulia, upungufu wao na kufikiria jinsi ya kufanya vizuri zaidi.
Huwa wanawatazama wale waliofanikiwa kwamba wanakabilianaje na vikwazo mbalimbali na kufanya maamuzi ya busara.
Wanakuwa watu wanaokusudia kuwa na mafanikio, hivyo wanafanya jitihada mbalimbali ili kufikia walipokusudia.
Mara nyingi katika maisha yetu ya kawaida, unakuta mtu anakuwa anapenda kufika mbali katika maisha lakini anakatishwa tamaa na wengine.
Cha msingi, unapaswa kufanya kile ulichokusudia. Usiwe mwepesi wa kukata tamaa katika maisha yako. Na matokeo yake utayaona.
Unapokuwa na imani ya kufanya jambo fulani, kamwe usikate tamaa, kinachokupasa ni kufikiri mbinu ya kukutoa hapo ulipo na kusonga mbele.
Unapokuwa jasiri kufanya jambo fulani, kunawafanya na wengine wakuamini kuwa unaweza.
Hivyo unapoamini kuwa unaweza kufanya jambo fulani, utafanikiwa. Kwa wale wasiokuwa na imani ya kufanikiwa hata wanapofanya jambo hukwama njiani, kwa kuwa tokea awali walishaona hawataweza.
Unapokuwa na imani kuwa huwezi kufanya jambo fulani, ama kuwa na wasiwasi wa kufanya jambo, akili yako inapata sababu ya kukubaliana na kile unachokiamini.
Hofu, wasiwasi, kutokuamini kuwa unaweza, vinakufanya ushindwe kufikia malengo uliyojiwekea.
Hivyo ni vema kuwa na mawazo ya ushindi ili uweze kufanikiwa.
Imani ni kipimo chako katika maisha ambacho kitakuongoza. Kama unaamini kuwa kamwe hautakuwa tajiri, hali huwa hivyo hivyo.
Kama unaamini hutaweza kufanya mambo makubwa katika maisha, ndivyo itakavyokuwa. Kama unajiona kuwa wewe si wa muhimu, utaendelea kuonekana hivyo hivyo.
Kwa mtu anayewaza mambo makubwa, anakuwa anaamini kuwa atakuwa na utajiri, ndivyo inavyokuwa kwake.
Anaamini kuwa ataweza kufanya shughuli ngumu ambazo zitaMfikisha mahali pazuri na ndivyo inavyokuwa.
Kila kitu anachokifanya, jinsi anavyochukuliana na watu, tabia yake, mawazo yake, vyote vinamweka katika nafasi nzuri ya kuwa na mafanikio zaidi. Na kuonekana ni mtu wa maana.
Mtu ni bidhaa ya mawazo yake mwenyewe kwa kuamini na kufikiri mambo makubwa.
Tukutane Alhamisi ijayo.

KUWA NA MAWASILIANO MAZURI KAZINI KWAKO

MSOMAJI, katika mfululizo wa makala hizi za maisha yetu, nimedhamiria kukuletea kitu kipya kila Alhamisi. Leo tutaangalia jinsi gani unaweza kuwa na mawasiliano mazuri katika ofisi unayofanyia kazi.
Ni ukweli usiopingika kuwa, wale wote wanaofanya kazi maofisini, hutumia muda mwingi zaidi wakiwa ofisini kuliko nyumbani.
Hivyo ni muhimu kufurahia kazi ile unayoifanya na kuwa karibu na wale wote unaofanya nao kazi kwa muda huo, kwa sababu, wakati mwingine kazi tuzifanyazo husababisha msongo, hivyo kama unapata msaada kutoka kwa wenzako, inakusaidia kuondoa hali hiyo.
Lakini kwa upande mwingine, unaweza ukajikuta kuwa bila sababu ya msingi unapata upinzani katika shughuli zako unazozifanya kutoka kwa wafanyakazi wenzako.
Na kwamba, pasipo sababu ya msingi unakuta watu wanakutendea matendo yanayokuudhi, unachotakiwa kukifanya ni kuwasamehe.
Unaweza ukawa mwema kwao, lakini wakakudharau, endelea kuwa mwema kwao.
Unaweza ukawa mpole, wakatumia nafasi hiyo kukuhadaa, endelea kuwa mpole kwao.
Ukiwa katika shughuli zako, unaweza ukaamua kutafuta furaha lakini wengine wakakuonea wivu, usivunjike moyo, endelea kuwa na furaha hiyo unayoitafuta.
Au unaweza kujikuta kuwa, mambo mazuri unayoyafanya leo, kesho yanaweza yakawa yamesahauliwa, Endelea kufanya vile vile bila kupunguza.
Pamoja na upinzani unaoweza kukutana nao katika ofisi yako, elewa kuwa na mawasiliano ni muhimu katika eneo lolote la kazi.
Kuzungumza na kusikiliza wasimamizi wako na wafanyakazi wenzako ni muhimu, si tu kwa ajili ya mafanikio yako, bali kwa ajili ya mafanikio ya kampuni yako pia.
Jifunze njia sahihi za kuwasiliana na wafanyakazi wenzako kwa njia mbalimbali, pia weka mazingira bora ya kazi kwa kila mmoja.
Penda kujifunza kusikiliza kwa makini, kusikiliza mtu ni jambo la muhimu sana, ni zaidi ya kuzungumza.
Kwa kuwa, kusikiliza kunakufanya kuwaelewa wafanyakazi wenzako, mawazo na thamani yao.
Kuwa na tabia ya kumsikiliza mwenzako na uliza maswali ili uwe na uhakika wa kile anachokizungumza na matarajio yake.
Pili, watendee wenzako vile unavyotaka wakutendee wewe. Kila mmoja mheshimu jinsi alivyo. Usimwingilie anapofanya shughuli zake, usimbughudhi na wala usigombane naye kuhusiana na vifaa vya ofisini.
Unapohitaji kufanya jambo mwombe na ukimaliza mshukuru, usisite kumpa sifa zake pale anapostahili.
Kuwa mwangalifu na ishara za mwili unazotaka kuzitumia. Kamwe hata kama hupendi kusikiliza jambo unaloambiwa na mfanyakazi mwenzako, epuka kushika shika mikono yako, kugonga gonga miguu yako au kuzungusha macho yako.
Kwa kufanya hivyo itaonyesha dhahiri kwamba hauna utayari wa kumsikiliza mtu huyo, na kufanya mawasiliano yenu kuwa magumu kwa siku zinazofuata.
Kuwa na muonekano wa tofauti katika shughuli zako. Pokea simu unazopigiwa, jibu barua pepe unazotumiwa na fanya kazi zako kwa wakati. Utaheshimika na jaribu kujenga mahusiano mazuri na baada ya muda nao watakuwa wema kwako.
Makala hii imeandikwa kwa msaada wa mashirika ya habari.
Tukutane Alhamisi ijayo.

Twitter Facebook