MWANAFUNZI mmoja alimuuliza mwalimu wake ni ‘nini kinachompata mtu anayeamua kukaidi utendaji kazi wa kanuni ya dhahabu ‘Golden Rule”, mwalimu alikuwa na jibu rahisi tu kwa mwanafunzi huo.
Kama unataka kufahamu kile kinachotokea kwa mtu ambaye huamua kukaidi msingi ambao kanuni ya dhahabu inafanya kazi, chagua mtu mmoja katika jamii unayoishi anayeishi kwa lengo moja tu la kujikusanyia mali lakini akiwa hana ufahamu wowote wa jinsi mali hiyo inavyokusanywa.
Mchunguze mtu huyo na utagundua kuwa hakuna uchangamfu, hakuna ukarimu hakuna neno karibu katika mazungumzo yake. Kwa hakika amekuwa mtumwa kwa hitaji lake la fedha; amekuwa mbinafsi mkubwa pale linapokuja suala la kuwashirikisha wenzake ili nao wafurahie utajiri wake.
Itakuwa ni upumbavu wa hali ya juu kulinganisha mafanikio na mtu wa jinsi hiyo. Kwa hakika hakuwezi kuwa na mafanikio bila ya kuwapo furaha na hakuna mtu anayeweza kuwa na furaha bila ya kuwafanya watu wengine kuwa na furaha.
Ingawa utumiaji wa nguvu unaweza kuleta mafanikio katika maeneo mengi bado haiwezi kusababisha kuwapo uhusiano wa kudumu. Wakati mtu mwingine anapokupenda, anapocheka nawe, anapokubaliana nawe, hapo ndipo unapoweza kuwa na hakika kuwa mtu huyo atafikiri nawe atakusaidia na atashirikiana nawe. Haiba yenye mvuto ni moja ya kati ya nyenzo muhimu za kijamii.
Lakini ni nini siri ya kuwa na haiba yenye mvuto. Naamini tunawafahamu watu ambao huonekana kuwavutia wengine, marafiki, wateja au watu ambao wanakutana nao katika shughuli za kimaisha.
Mara nyingi huwa tunaishia kusema kuwa watu hawa wana mvuto au bahati na watu hao wanaowavutia kiasi cha kufikiri kuwa huenda kuna nguvu ya asili inayosababisha hali hiyo. Dhana ya jinsi hii si sahihi kabisa kwani huwezi kumlazimisha mtu fulani anapenda au kuvutiwa na mtu mwingine.
Lakini kinyume cha dhana hiyo unaweza kuwavuta watu kwa kukidhi njaa katika mahitaji ya msingi yaliyo katika maisha ya mwanadamu. Kisa hiki kinafunua siri ya dhana hii.
Mfanyabiashara mmoja nchini Marekani amabaye alikuwa wa asili ya Afrika aliwasili ofisini kwake mapema ikiwa ni saa kadhaa kuliko ilivyokuwa kawaida yake. Siku hiyo alikuwa na shughuli ambazo alihitaji kuzikamilisha kabla ya wafanyakazi wake hawajawasili kazini.
Kwa muda huo aliowasili hakukuwa na mtu mwingine isipokuwa kijana mmoja aliyejulikana kwa jina la George aliyekuwa ni mwangalizi wa ofisi. George alikuwa mfanyakazi mwaminifu aliyekuwa akitoa huduma kwa kampuni ile. Wakati ule bosi wake alipokuwa akiingia ofisni , george alikuwa katika shughuli ya kuzoa taka na kufuta vumbi katika samani za ofisi.
Bosi alipogundua hilo alimwambia maneneo haya: “George, unajua ninapoangalia jengo hili nashindwa hata kufikiri na kueleza jinsi ambavyo umekuwa rasilimali muhimu katika kampuni kwa miaka yote hii ambayo umekuwa mtumishi hapa. Umefanya eneo hili kuwa safi na la kuvutia kwa wafanyakazi pamoja na wateja wetu jambo ambalo limewafanya wafurahie.
“George,” bosi aliendelea “Wewe ni sehemu muhimu katika kampuni hii na ningependa utambue kuwa ninathamini yote ambayo umekuwa ukifanya.”
George alisita kidogo na kisha akajibu kwa kusema: “Asante bosi” kisha akatoka nje huku akiwa ameshikilia kitambaa ambacho alikuwa anakitumia kufuta vumbi.
Dakika chache baadae mlango wa ofisi ulifunguliwa na alikuwa ni George tena. Macho yake yalionekana kulengwalengwa na machozi, jambo ambalo lilimshangaza bosi wake kiasi cha kuuliza “Je kuna tatizo gani George, je nimesema neno lolote ambalo limekuudhi?”
George alijaribu tabasamu kisha akasema “Hapana bosi, hujaniudhi kwa lolote. Lakini nina jambo ambalo ningependa kushirikiana na wewe.”
Ukimya ulitawala chumba kwa muda mfupi baadae George akasema maneno yafuatayo. “Unajua bosi nimefanya kazi na kampuni hii kwa miaka 17 kati ya hiyo 12 ikiwa ni chini yako na asubuhi hii ya leo ndiyo mara ya kwanza mtu kuniambia kuwa anathamini kile ambacho nimekuwa nikifanya.”
Baadaye George aliendelea kusema hivi. “Ninapenda bosi utambue kuwa ninathamini kile ambacho umekisema kwangu asubuhi hii ya leo kuliko vile ambavyo nimekuwa nikithamini hundi ya mshahara wangu! Nilipenda ujue hilo.” Baada ya kusema maneno hayo George aligeuka na kutoka ndani ya chumba cha bosi wake.
Jambo muhimu katika asili ya mwanadamu ni hitaji la kuthaminiwa. Mtu hawezi kutoa kilicho bora kwa kubadilishana na fedha tu, lakini anaweza kutoa kila kinachowezekana kwa ajili ya kuthaminiwa tu hata kama ni kwa kiasi kidogo kiasi gani.
Pale unapoamua kutokosoa, kulaumu na badala yake ukaamua kuangalia kila uwezekanao wa kutamka kwa dhati japo neno moja tu la kusifia au kuthamini, utagundua kuwa watu wengine watatamani kuandamana na wewe.
Kwa dhati kabisa watataka kuwa jirani na wewe. Kwa kufanya iwe tabia yako kusifia kwa dhati na uaminifu utakuwa umepiga hatua muhimu katika kujenga na kupalilia mafanikio na furaha yako mwenyewe.
Hebu jaribu kujiuliza maswali haya. Je, unapata kusifiwa na watu wengine, je, watu wanakubaliana na kile unachokifanya au kukisema, je, wanathamini mchango wako nyumbani au kazini? Je, ni lini ulimsifia kwa dhati mtu mwingine au kutoa maneno ya dhati katika kuthamini kazi au manen yake? Mambo haya mawili huenda kwa pamoja na ni vigumu kuyatenganisha. Watu wengi hivi leo wanaonekana kuchanganyikiwa.
Huku wakiwa waliozidiwa na shughuli nyingi katika miji na majiji makubwa, wamejikuta wakitawaliwa na hisia na mihemko. Wakati hisia zetu ana mihemko vinaposhindwa kudhibitiwa, tutajikuta tukiwatendea wengine kwa haraka, tukionyesha ishara na kufanya maamuzi ya haraka huku tukitumia maneno ambayo hayakuchaguliwa kwa uangalifu unaostahili.
Jaribu kuweka kando hisia zako za ndani. Na kanuni muhimu ni hii simama, sikiliza, fikiri na utafakari wewe mwenyewe. Kwa namna nyingine ni sawa tungesema kuwa jaribu kuhisi kwa jinsi ambayo watu wengine wanajihisi, na si vile ambavyo wewe unajihisi.
Ni wazi kuwa unapojiangalia katika kioo unachotarajia kukiona ni taswira yako. Vivyo hivyo mtu mwingine angependa kuona taswira yake kutoka katika kioo chako, hisia zake na mtazamo wake.
Jaribu kufikiri juu ya ufahari, hisia na mihemko ya wengine na si kwako tu. Hapo utashangaa kuona jinsi watu wengi watakavyovutiwa nawe na kutaka kuwa jirani nawe wakati wote. Na hapo ndipo utakapogundua thamani na umuhimu wa kuwatendea watu wengine kwa jinsi wanavyojihisi na kujisikia badala ya vile wewe unavyofikiri na kujisikia.
lcngowi@yahoo.com 0713 331455, 0733 33 1455
Monday, June 16, 2008
FIKIRI UWE TAJIRI - 8
Posted in:
0 Maoni:
Post a Comment