Monday, June 16, 2008

MAKOSA 10 YA KUACHANA NAYO KATIKA MATUMIZI YA PESA

SI jambo la ajabu kumsikia mtu akisema fulani ana matumizi mabaya ya pesa au yule akipata pesa zinamtawala.
Hata hivyo, tunashindwa kutambua kuwa hiyo si njia ya kumsaidia mtu wa aina hiyo kwani hawezi kubadilika.
Mtu huyo tunamuona mfujaji wa pesa kutokana na ukweli kuwa hajui jinsi ya kushughulikia tatizo alilonalo.
Ni vema ukatambua kuwa, kamwe huwezi kubadilisha mwenendo wako kuhusu hali ya kifedha, isipokuwa unaweza kushughulikia baadhi ya matatizo.
Hii inahusu tabia ya kufanya au kutofanya mambo fulani. Tabia zetu nyingi kuhusu pesa huundwa bila ya sisi kujitambua au kutojali katika kipindi kirefu.
Hakuna hata mmoja wetu ambaye hukaa chini na baada ya kufikiri kwa muda mrefu, akatoka na jibu kwamba, kuwa na uwiano katika kitabu cha hundi ni jambo la kijinga. Badala yake tabia huibuka yenyewe baada ya muda mrefu.
Tabia yetu kuhusu pesa husababishwa na namna tunavyotunza pesa, tunavyotumia, tunavyothamini na tunavyofikiri kuhusu mustakabali wetu. Hivyo kile tutakachojifunza kuhusu pesa, kinaweza kufanya tuwe na mwenendo mzuri au mbaya wa pesa zetu.
Ni vema ukakumbuka kuwa, unapogundua juu ya jambo fulani ambalo limekosa mwenendo mzuri, basi utafute namna ya kuachana nalo.
Acha kurudia makosa yale yale kila mwaka na ujiulize ni kwa nini huweki akiba kutokana na kipato chako? Njia pekee ya kuepekuna na tabia hiyo ni kufuta mfululizo wa makosa hayo yenye tabia ya kujirudia na udhamirie kubadili maisha yako.
Baadhi ya watu huishi huku wakiendelea kurudia makosa katika sekta ya kiuchumi. Bila shaka hutakiwi kuwa mmoja wa watu wa aina hiyo.
Ili uepukane na mkosaji anayerudia kosa, unapaswa kuhakikisha kuwa hufanyi kosa lolote miongoni mwa makosa haya kumi ambayo wengi wetu huyafanya kuhusu pesa.
Hata hivyo unapaswa kuhakikisha kuwa unaitambua vyema hali halisi ya gharama duniani, huku ukichagua njia muafaka ya kukabiliana na kila hali.
1. Kutumia pesa bila ya bajeti
Mara nyingi watu hufikiri juu ya mipango mbalimbali ya kuwaingizia fedha, mfano wapo wanaofikiri ni jinsi gani watawekeza ili kuifanya pesa hiyo iongezeke, lakini ni wachache sana ambao hufikiri juu ya kuandaa bajeti, hasa kwa kuzingatia uwezo wao kifedha.
Mshauri mmoja wa masuala ya kifedha kutoka nchini Marekani, John Ritter, aliwahi kusema iwapo una kipato na Ankara, unahitaji pia kuwa na bajeti.
“Mara nyingi kuna kikubwa kinachotoka kuliko kipato,” anasema.
Je, kutumia pesa bila bajeti kunaweza kukugharimu nini? Wengi wetu wanaweza wasikubaliane na hili kwa kuamua kutokubaliana nalo, au wamekuwa wakisumbuka bila ya kuelewa kinachowasumbua.
Jambo hili si jingine, isipokuwa kukosa utulivu wa akili na mawazo kuhusu pesa pamoja na uwezo wa kuandaa bajeti ya muda mrefu.
Mwisho wa hali kama hii ni kushindwa kuwa sahihi juu ya kile ulichotumia kuwa ni asilimia 15 au 20 au zaidi katika chakula au afya.
Namna ya kuepukana na athari hiyo, hakikisha unaweka utaratibu wa kutambua kila aina ya matumizi unayoyafanya ili kung’amua ni wapi pesa zako zinakwenda.
Njia nzuri ya kumudu jambo hilo ni kuhakikisha unaorodhesha mahitaji yote ambayo hayalipwi kwa utaratibu wa ankara, mfano vinywaji, burudani mbalimbali, kuchangia sherehe miongoni na mengine mengi.
Baada ya kufanya hivyo hakikisha unatenga kiasi fulani cha pesa kwa ajili ya dharura, mfano matengenezo ya gari iwapo umebarikiwa kuwa nalo, au hata pesa ambayo itakuwezesha kusafiri kwenda kuona mgonjwa au kuhudhuria msiba.
Watu wengi hudharau mahitaji ya aina hii na kuyaweka kando ya bajeti kwa sababu hayana umuhimu kwao.
Hata hivyo, mara yanapotokea, umuhimu wake huonekana na hapo ndio hutambua kuwa kumbe katika wakati wote kuna matumizi.
2. Kutembea na kadi inayoruhusu ukope
Hili ni tatizo kubwa kwa nchi za wenzetu walioendelea, na wengi hifikiri kuwa hiyo ni sehemu ya ustaarabu na maendeleo.
Kutembea na kadi inayoruhusu ukope, ni hatari kwani inakufanya kuwa na tamaa ya kupata mahitaji. Sharti la ukopaji wa aina hii ni kukatwa riba kubwa ikilinganishwa na mtu anayenunua moja kwa moja.
Hapa kwetu kuna taasisi na mashirika yanayotoa huduma na vitu kwa njia ya mkopo, lakini iwapo utachunguza vema, utagundua kuwa muda ambao unakaa na deni unakugharimu zaidi, kwani utalazimika kulipa kwa asilimia kadhaa zaidi ya yule aliyenunua kwa kulipia moja kwa moja.
“Mara nyingi watu wanaotaka kulipia huduma au kitu kidogo kidogo hawawezi kufanya chochote na badala yake wanapata hasara kubwa,” anasema John Ritter.
Kwa ujumla kadi za aina hii ni njia mojawapo ya kukufanya uwe mtumwa wa mahitaji yako au madeni.
Ushauri ambao ningependa kukupatia hapa ni kwamba, hakikisha unafanya malipo yanayotakiwa kwa wakati na usikubali kubaki na deni lisilo la lazima.
Baada ya hapo, hatua inayofuata ni kuhakikisha kuwa unadhamiria kwa hali na mali, hata ikiwezekana kwa kujinyima, ili uweze kulipa na kuachana na madeni hayo kabisa, ukianza na moja na baada ya jingine.
Tambua kuwa siku zote deni kubwa ni gumu kulimaliza, lakini hiyo isikukatishe tamaa na badala yake ione kuwa changamoto kwako. Iwapo ulifurahia matunda ya deni hilo, basi uwe tayari kubeba mzigo wake.
Kwa ujumla njia rahisi ya kuepukana na madeni, ni kuhakikisha kuwa unalipia mahitaji yako yote kwa ukamilifu, kila ifikapo mwisho wa mwezi.
Iwapo utahitajika kutumia kadi inayokuruhusu kukopa wakati una dharura, basi hakikisha kuwa unakopa kiasi cha kutosha kukidhi dhahruara hiyo tu (mfano, ugonjwa, ajali au safari).
Baada ya kufanya matumizi hayo, hakikisha kuwa hutumii kadi hiyo hadi utakapokamilisha malipo ya deni hilo.
3. Kudharau riba zitolewazo na benki
Bila ya kujali kiwango cha riba kinachotolewa katika masoko ya hisa, mabenki au kuwekeza katika taasisi zinazotoa mikopo kwa ajili ya ujenzi wa nyumba, ni jambo la muhimu kuweka pesa katika taasisi zinatoa riba.
Unaweza kujenga utaratibu wa kununua hisa katika makampuni, mashirika au hata taasisi za fedha. Jambo la kuzingatia, ni kwamba, hii ni njia ya kuzalisha pesa ambazo huzitumii kwa sababu siku utakapoamua kuuza hisa hizo au kuhitaji pesa zako, hazitarejea kama zilivyokuwa, zitaongezeka.
Ipo faida ya kuwa mwanachama unayechangia katika taasisi zinazotoa mikopo, kwani hupata unafuu wakati wa kurejesha mkopo huo.
Mfano, mwanachama anayekopa kutoka taasisi ambayo hutoa mikopo kwa ajili ya ujenzi wa nyumba, ni wazi kuwa atapata unafuu wakati wa kurejesha mkopo huo kuliko mtu anayekopa wakati si mwanachama, kwani riba ya urejeshaji wa mkopo wake itakuwa ya juu zaidi.
Kwa leo tuishie hapa, juma lijalo tutaendelea na makosa yaliyosalia.

Twitter Facebook