Friday, June 27, 2008

HATA WEWE UNAWEZA KUFANIKIWA

MAFANIKIO hutokana na jitihada katika maisha tunayoyaishi. Watu wengi wanaopenda kufanikiwa mara zote hutafuta mbinu mbalimbali ili kutimiza ndoto zao. Hivyo basi unatakiwa kuota ndoto ya mafanikio yenye malengo makubwa.
Binafsi ninaamini katika malengo hayo kuwa kuna mafanikio endapo utamaanisha. Wakati mtu anapoanza kuwa na malengo makubwa, anaanza kwa kufikiri jinsi Mungu alivyomwezesha katika jambo hata kufikia hatua na kufanikiwa.
Ndoto hiyo ya mafanikio haina gharama, ni jinsi ya unavyoweza kujipangia muda na ratiba zako. Kumbuka ukiwa na malengo ya mafanikio haitakugharimu chochote.
Unaweza ukawa na malengo ya kuanzisha mradi mkubwa pasipokuwa na fedha, inabakia kuwa ni ndoto tu. Mungu alianza kuumba dunia ikiwa haina kitu. Tunaweza kuwa na malengo makubwa ya mafanikio katika maisha yetu, haijalishi ni ya aina gani.
Unapokuwa na ndoto hiyo ya kutaka kufanikiwa, kamwe usiruhusu moyo wako kuvunjika au kuwa katika hali ya kukata tamaa na wasiwasi. Kwani hali hiyo itakudhoofisha na kukufanya usisonge mbele, bali urudi nyuma.
Unapohitaji jambo kubwa kutokea katika maisha yako unatakiwa kuwa na maono mapya. Kumbuka hata wewe unaweza ukawa na maono makubwa ya ajabu.
Haijalishi ni mtu wa aina gani, umetoka wapi au umepatwa na jambo gani, katika hali uliyonayo unaweza kuwa na maono mapya. Kumbuka malengo makubwa hayawi kwa watu waliofanikiwa, bali ni kwa wale wanaotaka kufanikiwa.
Vyovyote uwazavyo, ndoto inainua na kuweka kitu kipya katika maisha yetu, inatutengeneza na kutusogeza mbele, inatuwezesha kufikia malengo makubwa tofauti na ilivyokuwa awali. Inatuwezesha kufanya kitu kikubwa ambacho hatujawahi kukifanya tena kabla ya hapo.
Je, wataka kuwa fulani? Kusimama nje ya kusanyiko kubwa? Kukumbukwa? Hali hiyo inakuwepo ndani ya mioyo yetu inayodunda na kutaka kupata siri ya mafanikio.
Tunataka kuwa fulani. Inawezekana, ndiyo inawezekana. Mungu ametoa kwa kila mtu uwezo na vipaji mbalimbali. Wakati Mungu anakuumba alikupa kipaji na akasema kama utatumia kipaji ulichonacho atakiongeza, na kama hutatumia kipaji ulichonacho utakipoteza. Kukitumia kipaji chako au kukiachia ni juu yako wewe!
Dunia yetu imejaa vipaji vingi na uwezo ambao hautumiwi. Unatakiwa kulima kwa bidii, na kupalilia ili upate mavuno bora. Tumia kipaji chako kabla hujakipoteza.
Unaweza kudhani kuwa hauna kipaji chochote, si kweli, labda inawezekana haujagundua kipaji chako. Inawezekana umekiweka kipaji chako kabatini. Amini kuwa kila mmoja anacho kipaji chake alichopewa na Mungu.
Waweza kutumia kipaji ulichonacho au kukipoteza. Maisha yetu yamejengwa katika kanuni hiyo. Kuna mifano mingi ya kupoteza au kupata, hiyo ni kanuni ya kawaida.
Chukua hatua ambazo zitaifanya ndoto yako kuwa kweli. Ota ndoto yenye thamani katika maisha yako. Kama hauna malengo, haitawezekana matarajio yako kutimia. Ndoto inaanza unapokuwa na wazo. Kumbuka watu huvutiwa na wenye maono makubwa.
Chagua maono yenye matarajio. Baadhi ya watu wanapoteza muda wao kwa kuwa na malengo ambayo hayatawasaidia. Mfano, kuna kijana katika miaka iliyopita alisaidiwa kupewa ushauri baada ya kupoteza muda wake mwingi akifikiria ni jinsi gani ataweza kumpata mke wa jirani yake na kumfanya awe wake. Ndoto yake hiyo haikuwa ya thamani ya muda mrefu.
Wakati wazo linapokujia katika ufahamu wako, iulize nafsi yako maswali matatu. Je, jambo hilo litampendeza Mungu? Litawasaidia watu wanaoteseka? Kwa maneno mengine litakuwa msaada kwa watu? Litaleta mafanikio mazuri kwako? Kama jibu lako ni ndiyo katika maswali yote, utakuwa na maono yenye mafanikio.
Unapoamua kufanya jambo fulani, usijiulize ulize kuwa hii ni njia nyepesi ya mafanikio? Au ni njia rahisi? Inaweza kuwa na usalama? Haitakuwa na vikwazo? Hakuna utakachoshindwa utakapofanya bidii. Hakuna mwenye nguvu ya kuua ndoto yako, isipokuwa wewe mwenyewe.
Panga mipango vizuri kwa kuwa huwezi kujenga bila ramani. Huwezi kufanikiwa matarajio yako pasipokuwa na malengo makubwa. Ninamfahamu mtu aliyekuwa na maono makubwa lakini yalikuwa hayafiki mbali. Ni kwa sababu alikuwa hana ramani ya maono yake.
Hakikisha unatimiza ndoto uliyojiwekea. Malengo yako hayawezi kufanikiwa kama hujajitoa kufanya hivyo. Ili kufanikiwa katika mipango yako unahitaji juhudi na kufanya kazi kwa bidii ili upate mafanikio.
Amua pa kuanzia. Fanya uamuzi sahihi. Panga muda wa kuanza. Usitafute sababu ya kuacha kufanya malengo yako kwa muda ulioupanga. Katika dunia yetu kuna watu wengi wenye mipango mingi lakini hawaifanikishi. Jiondoe katika kundi hilo. Fanya kitu. Andika barua, piga simu. Anza hatua ya mafanikio.
Jiamini waweza kutimiza ndoto zako. Wakati unajaribu kupata mafanikio utaona kuwa ni kipindi kigumu kwako. Hali ya kukata tamaa inakuwepo katika moyo wako, ikisema jiondoe katika hatua ambayo unataka kuianza ya kupata mafanikio katika maisha yako, kataa.
Kama unakutana na kipindi cha majaribio katika biashara, ndoa, mambo yako binafsi, kwenye wingi wa watu au hali ya maisha uliyoizoea na uko tayari kukabiliana nayo, songa mbele usikate tamaa.
Unachofanya ni kujaribu kupata mafanikio, tena mafanikio makubwa. Katika kila mafanikio unayoyapata, kuna gharama ya kulipa. Kumbuka huwezi kupata ushindi bila kulipa gharama.
www.ngowil.blogspot.comlcyngowi@yahoo.com0713 3314550733 331455

JINSI YA KUDHIBITI HASIRA


WAKATI mwingine, hasira na kuchanganyikiwa kwetu kunasababishwa na matatizo yasiyozuilika katika maisha yetu ya kila siku.
Si kila hasira haina mpangilio, na mara nyingi inatokana na mambo ya kiafya, ni hali ya asili inayojitokeza katika mambo tunayokutana nayo.
Njia sahihi ya kukabiliana na tatizo linalokukabili, ambalo linakusababishia hasira, si tu kulenga katika kutafuta muafaka, lakini zaidi ni jinsi gani ya kulichukua na kukabiliana nalo.
Kutatua matatizo yanayokusababishia hasira kutaleta matokeo mazuri, lakini pia si kujiadhibu mwenyewe kama jibu halitakuja kama ulivyotarajia.
Watu wenye hasira mara nyingi hurukia jambo na kulifanyia maamuzi, lakini baadhi ya maamuzi hayo yanaweza yasiwe sahihi.
Kitu cha kwanza cha kufanya kama upo kwenye majadiliano makali ni kupunguza hasira na kufikiri juu ya majibu yako unayoyatoa.
Katika majadiliano hayo, kamwe usiseme kitu cha kwanza kinachokujia kichwani pako, bali tuliza hasira na fikiri kwa uangalifu juu ya kile unachotaka kukisema. Wakati huo huo, sikiliza kwa makini mtu mwingine anachokisema na jipatie muda kabla ya kujibu.
Pia sikiliza kwa makini, jambo lile linalokusababishia hasira. Kwa mfano, wakati mwingine unahitaji uhuru wako binafsi, wakati huo mke au mume wako anahitaji mawasiliano ya karibu na wewe.
Kama ataanza kulalamika kuhusu tabia zako, usilipize kisasi kwa kumfananisha na mfano usio mzuri, kwani hali hiyo italeta uharibifu katika uhusiano wenu.
Ni jambo la kawaida kwa mtu yeyote kujilinda wakati anapokosolewa, lakini akumbuke kuwa makini, asiruhusu hali ya kupigana.
Badala yake asikilize kinachojili juu yake. Ujumbe wa mtu huyo unaweza ukaudharau na kutoupenda.
Utahitaji uvumilivu kwa upande wako, na inahitaji kuvuta pumzi, lakini usiruhusu hasira yako au ya mshirika wako aache majadiliano yawe katika udhibiti. Kutulia kutaifanya hali kutokuwa ya uharibifu.
Wakati mwingine, ni vizuri kutumia ‘vichekesho’ kwani vinaweza kukusaidia kupunguza hasira katika njia mbalimbali. Kwa jambo moja la uhakika, ni kwamba vinaweza kukusaidia kuwa na mawazo yaliyo sawa.
Hivyo, wakati unapokuwa na hasira halafu unamwita mtu fulani jina au kumfananisha na kitu fulani, acha na ufikirie neno hilo linafananaje.
Fanya hivi pale jina linapokujia kwenye kichwa chako kuhusu mtu mwingine. kama unaweza, fikiria picha ya kitu halisi kinavyokuwa.
Hali hii itakuondolea hasira uliyokuwa nayo, na vichekesho mara zote vinakuondolea hali ile ya ghadhabu uliyonayo.
Ujumbe muhimu kwa watu wenye hasira kali, Dk. Deffenbacher anasema, watu wenye hasira wana tabia ya kujihisi kuwa wana haki, lakini mwisho wao hujikuta wakiwa wamejishushia heshima mbele ya jamii, lakini hawakutakiwa kutaabika kwa njia hiyo.
Labda watu wengine wangeweza kufanya hivyo lakini si wao.
Wakati unahisi kuwa unataka kuwa na hasira, mtaalamu huyo anashauri, jifikirie mwenyewe kama ungekuwa ni Mungu au kiongozi mwenye mamlaka ya juu, ambaye unamiliki mitaa, maduka na maeneo ya ofisi, mwenye maendeleo ya haraka na kuwa na taratibu zako katika hali zote wakati wengine wanatofautiana nawe.
Jambo unaloweza kulijua zaidi katika mawazo yako, unajiona kuwa wewe si mtu wa maana, unaanza kuona vitu ulivyonavyo havina umuhimu hivyo unakuwa na hasira kutokana na ukweli huo.
Kuna tahadhari mbili za kutumia vichekesho. Kwanza, usijaribu kuondoa aibu yako kwa kucheka, badala yake tumia kichekesho ili kujisaidia kukabiliana na hali hiyo. Pili, usifanye jambo lisilopendeza, kichekesho cha kejeli, hiyo ni aina nyingine ya mwonekano wa hasira isiyo na afya.
Hasira ni hisia ya kuiangalia kwa umakini, lakini mara nyingine inakwenda na wazo kuwa kama utaichunguza, itakuwezesha ucheke.
Wakati mwingine hasira Inabadilisha mazingira yako. Kwa mfano mazingira yetu yanatufanya kuwe na misuguano pamoja na ghadhabu. Matatizo na majukumu yanaweza kukuongezea uzito na kukufanya upatwe na hasira.
Ipe nafsi yako mapumziko. Hakikisha una muda wako binafsi na ratiba inayokuongoza kwa siku nzima. Mfano moja ni kwa mama anayefanya kazi, ambaye amekuwa na sheria yake kwamba, wakati anarudi nyumbani kutoka kazini, kwa dakika 15 za kwanza hakuna yeyote atakayezungumza naye, baada ya muda huo mfupi wa mapumziko anajisikia vizuri na kuanza kuwaandalia watoto wake mahitaji yao kwa furaha.
Njia nyingine za kukupa ahueni katika maisha yako, ni kuwapo matukio tofauti tofauti ambayo yatakuondolea tatizo la hasira ulilonalo.
Muda - Kama wewe na mke au mume wako mmekuwa na tabia ya kutofautiana wakati mnajadili mambo mbalimbali muda wa usiku, Inawezekana mnakuwa mmechoka, au mna mawazo, au labda ni tabia yenu halisi, jaribu kubadilisha muda wakati mnaongea mambo muhimu, badala ya usiku iwe asubuhi au mchana.
Epuka - kama watoto wako wanaonekana wana fujo kwenye chumba chao, hali ambayo itakufanya ukasirike, inabidi ulifanyie kazi suala hilo kwa kukaa kimya na kufunga mlango wa chumbani kwako.
Tafuta njia muafaka - kama kila siku asubuhi unakutana na msongamano wa foleni, hali inayokusababishia hasira, ipe nafsi yako kazi ya kusoma ramani ya kujua barabara nyingine zisizokuwa na foleni. Au tafuta njia nyingine muafaka.
Kuna njia mbalimbali za kukuonyesha kuwa una hasira. Mwili wako utakujulisha kuwa una hasira, kwa kuhema kwa nguvu, kubadilika uso wako, kukaza kwa misuli yako pamoja na kuonekana unaongea kama unanguruma, hata kwa mtu unayempenda.
Watu wengine wanazika hasira zao ndani. Kama unafanya hivi, utapata maumivu ya kichwa au tumbo. Na mara nyingine unaweza kuanza kulia peke yako.
Si vizuri kuficha hasira yako, inakubidi utafute njia ya kuitoa pasipo kujiumiza mwenyewe au kuwaumiza wengine.
Kuna njia za kufanya endapo utajikuta kuwa umepatwa na hasira. Njia hizo ni kuongea na rafiki yako unayemwamini, kufanya mazoezi, kucheza michezo mbalimbali, kuimba, kupalilia bustani yako pamoja na kufikiria mawazo mazuri.
Kwa mtu yeyote mwenye afya, haiwezekani asipatwe na hasira. Badala yake ukumbuke kuwa, unapatwa na hali gani unapokuwa na hasira.
Je, inafanya mazingira yako kuwa mazuri au mabaya? Usiruhusu hasira iwe bosi wako. Fanyia kazi jambo hilo.
lcyngowi@yahoo.comhttp://www.ngowil.blogspot.com/0713 3314550733 331455

KABILIANA NA CHANGAMOTO KATIKA MAISHA


KUNA wakati maisha yako yanaporomoka kutokana na kupatwa na misukosuko ya maisha kama vile kufiwa na mke, mume au mtoto wako, kusalitiwa na marafiki uliowategemea maishani mwako, kukimbiwa na mke au mume wako, kufilisika, kupoteza kazi uliyokuwa ukiitegemea, au daktari kukuambia kuwa ugonjwa unaokusumbua si rahisi kupona.
Hali hiyo inapokutokea, unajikuta unakata tamaa ya maisha na kujiona kuwa hustahili kuishi katika dunia hii inayokuzunguka, lakini kumbuka hiyo ni njia ya kupitia katika maisha haya tunayoishi.
Hivyo ni vizuri kumtafuta rafiki yako wa karibu au kiongozi wako wa dini kwa msaada zaidi. Kwani viongozi wa dini mara nyingi wamekuwa washauri wazuri katika maisha yetu ya kila siku.
Pia ukubaliane na hali ile ambayo huwezi kuibadilisha katika maisha yako. Na kukataa kuendekeza nafsi yako katika hali ya kujisikitikia kwani hali ya kujihurumia ni ugonjwa, kama vile acid.
Hali hiyo itakuondolea hadhi yako, itakuongezea sononeko na kukata tamaa. Itakuharibia uhusiano wako na wengine. Itakusababishia hali ya kuwa na chuki. Hakuna jambo zuri litakalokujia katika maisha yako kutokana na hali hiyo ya kujisikitikia.
Usichukue maumivu yako kwa wengine. Unaporuhusu maumivu huumizi watu wengine bali unajiumiza wewe mwenyewe. Iambie nafsi yako kuwa unahusika na vitendo au tabia zako mwenyewe. Hakuna atakayeiumiza nafsi yako ila wewe mwenyewe.
Usifanye ukaidi. Kubaliana na ukweli. Si wakati wote maisha yanakuwa sawa na ya kuridhisha. Haijalishi hali inayokutokea katika maisha yako, hali ya kukata tamaa, ndoto zako hazikutimia bado kuna tumaini katika maisha yako.
Baada ya usiku inakuja siku mpya, baada ya kipindi cha baridi huja kipupwe, baada ya mvua kubwa huja jua, baada ya dhambi huja msamaha, baada ya maangamizo nafasi nyingine hutokea.
Tuangalie mfano wa kijana mmoja wa miaka 15 ambaye alidondoka kutoka juu ya mti na kuvunjika mgongo. Kwa bahati aliokolewa akiwa mzima, lakini tokea kipindi hicho hakuweza kutembea tena. Alitembelea kiti cha watu wenye ulemavu, katika maisha yake yote.
Katika kipindi kigumu kama hiki, inakuwa ni rahisi kujihurumia na kujiona huna thamani tena katika maisha yako. Lakini haikuwa hivyo wa kijana huyu ambaye alivunjika mgongo. Kwani hakujiweka katika hali ya unyonge. Alitaka kuondoa hali aliyonayo na kuwa mtu mashuhuri. Kitu cha kwanza alicholenga kukifanya ni kumaliza masomo yake ya kidato cha sita. Alichohitaji ni kupata alama nzuri ili kufikia matarajio yake. Alimwambia mama yake anataka kuchukua masomo ya sanaa na uchoraji.
Kijana huyo ndoto yake ya maisha bora ilianza kung’aa tokea hapo na kufanikiwa katika maisha yake kutokana na kazi yake nzuri aliyoifanya. Kwani alikuwa mchoraji mzuri kiasi kwamba aliweza kupata mialiko mbalimbali kwenye vyuo vikuu vingine kutokana na bidii yake aliyoionyesha kwenye michoro aliyoichora. Baada ya masomo yake, kijana huyo alipata barua ambayo ilimtaka kwenda kufanya kazi ya kuchora katika kiwanda cha nguo.
Kazi hiyo imempatia pesa nzuri na kuweza kuisaidia familia yake. Kazi yake imempatia mahitaji yake yote ambayo alifikiri anahitaji. Anayapenda maisha katika hali ile aliyonayo. Kijana huyo ni mmoja wa watu wenye matarajio makubwa ukiachilia mbali hali aliyonayo ya kuwa mtu maarufu.
Kamwe usiishi maisha ya kushindwa. Unaona njia katika hali ya ugumu unayokabiliana nayo. Siri ya ushindi ni hii, usijione mshindwa, usikubali kushindwa kamwe usiishi katika hali ya kushindwa. Iambie akili yako kuwa hukuumbwa ili uwe mtu wa kushindwa.
Huwezi kuwa mtu wa kushindwa kama hujaruhusu hali hiyo katika maisha yako. Watu siku ya leo wanakata tamaa kutokana na sababu mbalimbali za maisha. Katika mtiririko wa mambo hayo, hakuna haja ya kukata tamaa katika maisha. Mtu ambaye hana kitu kinachofanya ajishughulishe anaona kuwa hana haja ya kuishi. Kila mtu anahitaji kitu cha kushikilia fikra zake na kumpa changamoto ili kufikia malengo anayotarajia.
Kumbuka, hakuna mafanikio pasipo kutaabika. Njia ya mapambano ni njia ambayo inamwezesha mtu binafsi kuongezeka, kukua, kuwa na maendeleo. Kila mtu anapitia maisha magumu kwa jinsi yake. Ni jinsi gani utakabiliana na hali hiyo ili uweze kuondokana nayo? Ni kwa kukataa hali hiyo na kusonga mbele.
Fanya jambo fulani kubwa ambalo hujawahi kulifanya kabla ya hapo. Unaweza kufanya mambo makubwa ambayo hukuwahi kuyafanya kabla ya hapo. Hiyo ni kwa sababu maumivu yako yamegeuka kuwa nyota ya mafanikio, tumia fikra zako, panua akili yako, jenga na tarajia. Uje na wazo kubwa, jambo fulani kubwa kuliko ilivyo kawaida yako. Songa mbele usikate tamaa mpaka pale matarajio yako yatakapotimia.
lcyngowi@yahoo.comhttp://www.ngowil.blogspot.com/0713 3314550733 331455

TAFUTA NJIA YA KUTATUA MATATIZO YAKO


NI jambo la kawaida kuchukua jukumu endapo kitu chochote kitakwenda vibaya, ambacho umekisababisha mwenyewe, lakini unapojenga tabia ya kujilaumu mwenyewe kwa kila jambo, unaweza kuwa na wakati mgumu katika hilo.
Unapojikuta ukijilaumu eti kwa kuwa watu wengine wana furaha katika familia zao au maisha yao, wana mafanikio kutokana na kufanya kazi zao kwa bidii, hali ya mahusiano katika familia zao imeimarika wakati kwako inasuasua, jaribu kutafuta njia nyingine ya kukuondolea hali hiyo inayokutesa.
Njia hizo ni pamoja na kuzungumza na familia yako, wazazi wako, watoto wako, wafanyakazi wenzako wale ambao wanaweza kukupa neno la busara, kiongozi wako wa dini, daktari wako pamoja na kusoma maandiko matakatifu.
Utakuta kuwa watu wengi hupenda kujilaumu kwa makosa mbalimbali wanayoyafanya ambayo hushindwa kuizuia hali hiyo na kumuathiri kisaikolojia. Kwa mfano, wazazi wanaweza kuwa imara na kuwashawishi watoto wao katika masuala ya elimu, lakini hawawezi kudhibiti mapungufu waliyonayo watoto wao. Unaweza kuwa imara kumdhibiti mume/mke au rafiki yako kuwa katika wakati mzuri, lakini huwezi kujihusisha katika jambo hilo moja kwa moja.
Lawama zilizopitiliza zinasababisha kukupokonya majukumu yako uliyonayo labda nyumbani, kazini au shuleni. Kuwa imara katika kudhibiti hali hiyo ili uweze kuondokana nayo. Kwani ikiendelea itakusababishia kukata tamaa, kuvunjika moyo na mwishowe kupatwa na msongo wa mawazo.
Kumbuka hali hiyo ukiiendeleza ni sawa na kujiongezea mzigo wa matatizo juu ya mabega yako. Jifunze kujisamehe hata kwa makosa yaliyokwisha kupita ambayo yanaumiza ufahamu wako.
Wengi wetu huwa mahakimu au washitaki juu ya makosa yao wenyewe, wakiendelea kujilaumu wenyewe. Unapokumbuka mambo ya aibu au ya kushindwa yaliyokupata zamani unazidi kuvunjika moyo na kujiona kuwa hustahili machoni pa watu. Hali hii itakuongezea machungu, wasiwasi, msongo wa mawazo pia inakuondolea ujasiri ulionao. Suluhisho ni kusahau yaliyopita na kuanza upya.
Ingawa inaweza kuwa ngumu kuzuia kumbukumbu za kushindwa kwako kukurudia, usizipe nafasi katika ufahamu wako. Kama Mungu au watu waweza kukusamehe si zaidi wewe mwenyewe kujisamehe? Achana na maamuzi mabaya uliyokwisha kuyafanya ya kibinafsi yaliyosababisha kuwaangusha marafiki zako, jamii au wewe mwenyewe.
Kabiliana na siku mpya kwani wewe si yule wa jana bali ni wa leo.
Pia usipende kuwalaumu watu wengine kwani ni sawa na kujiweka kwenye nafasi ya Mungu au hakimu, nafasi ambayo hata mmoja wetu haistahili. Tunapowalaumu wengine wakati mwingine tunataka kufunika mapungufu yetu wenyewe ambayo hatuko tayari kuyakabili.
Mfano utamkuta mwanamke akisema kwa ujasiri kuwa mumewe anatoka nje ya ndoa kwa sababu tu huchelewa kurudi nyumbani au kutumia pesa zake za mapato visivyo. Bila kujali kuwa mumewe anafanya kazi saa za ziada au anahifadhi fedha zake ili aweze kumnunulia mkewe zawadi nk. Yawezekana kuwa mwanamama huyu amekuwa akibeba hisia hizo za shutuma juu ya mumewe kwa muda mrefu kiasi cha kuweza kusababisha hata uhusiano wao kuyumba au ndoa yao kuvunjika. Lakini ukichunguza undani wa shutuma hizo huweza kukuta ni hitimisho iliyojaa hisia potofu.
Lawama yaweza kusababisha watu kufikia hitimisho lisilo sahihi hata kubeba uchungu kwa muda mrefu kiasi cha kuvunja ndoa/unyumba. Lawama huweza kusababisha hali ya maelewano na masikilizano kuwa kutoelewana au kutosikilizana.
Njia mojawapo ya kusaidia ndoa zenye msukosuko ni kumsaidia kila mhuhusika kuacha kumlaumu mwenzie au kuacha kumtazama mwenzie kwa jicho la lawama ila ajitazame mwenyewe na kuona ni wapi alipofanya makosa na nini anaweza kufanya ili kurekebisha ndoa yao.
Njia nyingine ni kumfanya kila mmoja aweze kukiri makosa mbele ya mwingine na kusema samahani, nimekosa. Katika hatua hiyo uhusiano uliovunjika unaanza kuimarika tena.
Hata mwanadamu wa kwanza alianza kwa kumlaumu mwanamke kwa kuelezea makosa yake kwa muumba wake. “Huyu mwanamke ndiye aliyenisababisha.” Mwanamke naye alitupa lawama zote kwa nyoka. “Nyoka ndiye aliyenisababishia kufanya hivi.”
Tunapowalaumu wengine tunaongeza ukubwa wa tatizo badala ya kulitatua. Hii inaonyesha kuwa aliye mwepesi kulaumu wengine ndiye mwenye makosa mengi zaidi. Waungwana ndiyo wanaoweza kukiri makosa yao au kushindwa kwao mbele ya jamii. Mtu muungwa ni yule aliye mwepesi kusema nimekosa.
Shinda lawama kwa kukiri makosa yako. Acha kufunika makosa kwani yataongeza ugumu wakati wa kutatua. Kuna njia moja ya kuweza kusafisha dhamira inayokushitaki nayo ni kukiri makosa. Acha kutafuta watu wa kulaumu, kabiliana na makosa yako mwenyewe. “Kubali makosa yako utapona. Kiri maovu utasamehewa.”
Tukumbuke tabia hiyo huanza tokea mtoto anapokuwa na umri mdogo. Kwani anapokimbia na kujigonga mahali hulaumu kile kilichomgonga, mfano kama amejigonga kwenye ukuta husema kuwa ukuta ule mbaya umemwumiza.
Tukumbuke kuwa lawama si kitu cha kufurahisha kwani huweza kusababisha hasara zaidi. Kwa mfano waweza kumwona mtu akigonga gari lake kwa hasira ukafikiria kuwa amechanganyikiwa kumbe analaumu kwa nini limeharibika au kwa nini limemwishia mafuta.
Kila wakati mambo yanapoharibika ni kasumba kwa mwanadamu kutafuta sababu ya lawama au mtu wa kumlaumu.
Mara nyingine tunapomwona kilema, kipofu au kichaa swali kubwa watu wanalojiuliza ni nani anayestahili kulaumiwa. Wengine humlaumu Mungu, wengine hulaumu uumbaji na wengine huwalaumu wazazi. Tunachotakiwa kujiuliza ni jinsi gani ya kumsaidia mtu huyo? Ni namna gani ya kumtoa katika hali ile aliyonayo sasa? Ni namna gani tunaweza kuboresha mazingira yanayomkabili. Ni jinsi gani twaweza kumfanya aanze upya na kwa ubora zaidi?
Ingawa lawama ni mchezo uliozoeleka na watu wengi siku hizi, bado ni mchezo ambao huleta athari kubwa sana. Siku zote lawama haiponyi bali huumiza moyo. Haijengi uhusiano bali huuvunja, haiunganishi bali hutenganisha, haijengi bali hugawanyisha na haitatui matatizo bali huongeza ukubwa wa matatizo.
lcyngowi@yahoo.comhttp://www.ngowil.blogspot.com/0713 331455, 0733 331455

EPUKA KUJINYONGA FIKIRIA SULUHU NYINGINE

KUKATA tamaa na kukosa tumaini kunaweza kukuongoza katika kufikiria hali ya kutaka kujinyonga. Lakini kumbuka kuwa una njia mbadala/suluhu nyingine zinazoweza kukusaidia kuepuka mara moja mgogoro huo na zikakusaidia kuibua mpango wa usalama wa muda mrefu.
Kuna wakati inapofikia hatua na kuona kuwa hakuna umuhimu wa kuishi, au matatizo yako yanaonekana kuwa mengi, kutokana na hali hiyo, hivyo unafikia hatua na kuona njia pekee ni kujinyonga.
Unaweza usiamini, lakini unaweza kuwa na njia nyingine itakayokufanya uendelee kuishi na kujisikia vizuri juu ya maisha yako, endapo utakuwa umefikia hatua ya kutaka kujinyonga.
Mara nyingine unaweza kufikiri kuwa umeshajaribu njia zote za kuondokana na hali hiyo ya kutaka kujinyonga, bila mafanikio, na kuona kuwa familia na rafiki zako wanakutenga.
Ni sawa kujisikia vibaya, lakini jaribu kutenganisha hisia zako na vitendo vyako kwa wakati huo. Tambua kuwa hali hiyo ya huzuni uliyonayo au mawazo uliyonayo au hali ya kukata tamaa ya muda mrefu uliyo nayo inaweza ikakugeuza vibaya mwelekeo wako kuondoa uwezo wako wa kufanya maamuzi.
Hisia za kujinyonga ni matokeo ya ugonjwa usiotibika. Kwa hiyo jaribu kuonyesha kuwa kuna uwezekano mwingine, hata kama hujauona kwa sasa.
Inaweza ikawa si rahisi kuondoka katika hali hiyo iliyokupata hata ikakusababisha usijisikie vizuri usiku kucha. Kutokana na hisia hizo ulizonazo za kukata tamaa, unaweza ukapata njia ya kutafuta ufumbuzi mpya kama matibabu na sababu za wewe kuishi.
Jitahidi kila siku uwe na mbinu za kuzuia hali hiyo kwa kuzungumza na daktari, familia au rafiki zako waweze kukusaidia kuondokana na hali hiyo.
Mbinu hizo zitakuwezesha kufanya vitu ambavyo hujisikii kuvifanya, kama kuzungumza na marafiki wakati umekuwa chumbani kwako siku nzima huku umeteremsha mapazia. Au unaweza kwenda hospitali kwa daktari wa akili kwa ajili ya kukufanyia tathmini. Lakini zingatia mbinu hizo, pale unapokuwa umevunjika moyo na kukosa matumaini.
Moja ya mbinu hizo ni kutunza orodha ya majina na namba zinazoweza kupatikana kwa urahisi, zikiwamo za madaktari, familia na ndugu zako ili endapo utakuwa na hali hiyo uweze kuwasiliana nao.
Kama malengo yako ya kujinyonga yanaendana na kunywa vidonge, hii inamaanisha kuwa badala ya kunywa vidonge viwili ulivyoelekezwa wewe unakunywa zaidi ya maelekezo ya daktari. Ni vizuri kutoa maelekezo yako ya dawa ulizonazo kwa yeyote anayeweza kutunza dawa zako na anayeweza kukupa dawa hizo kwa wakati, kuondokana na hali hiyo ya kujizidishia ambayo itakusababisha madhara.
Pia waweza kuondoa nyumbani kwako vitu vyote vya hatari kama visu, risasi, wembe au silaha nyingine zozote mtu anazoweza kuzitumia katika uharibifu wa maisha yako.
Hivyo ni vizuri ukawa na ratiba yako ya kila siku itakayokufanya uwe na shughuli na kukusahaulisha yaliyopita kama kutembea mwendo mfupi, kusikiliza muziki, kuangalia sinema inayovutia, na kutembelea maeneo ya makumbusho.
Baada ya kufanya yote hayo kama hutapata walau furaha kidogo, jaribu kitu kingine tofauti kitakachoondoa maumivu yanayokukabili. Jaribu kuwa pamoja na watu wengine, hata kama hujisikii kuwa nao, ili kuondoa hali ya kujitenga.
Epuka mihadarati na pombe. Zaidi ya kupata hisia za ganzi mwilini, pombe na mihadarati inakuongezea maumivu, unajiingiza zaidi kwenye kujidhuru mwenyewe au kuwa na wakati mwingine kuchanganyikiwa.
Andika kuhusu mawazo na hisia zako. Kumbuka pia kuandika vitu katika maisha yako ambavyo unavithamini na kuvikubali. Haijalishi ni kwa udogo gani unavyoviona.
Unapokuwa katika hali hiyo ya mawazo ya kujinyonga, kabla hujaamua kufanya hivyo, zungumza na mtu yeyote kama vile, kupiga simu kwa rafiki yako au huduma ya simu za dharura.
Kama hutaki kufanya hivyo kutokana na sababu yoyote ile, njia nyingine ni kuwasiliana na daktari wako, kiongozi wa dini au yeyote uliyenaye katika imani yako.
Zungumza na yeyote kuhusu hisia zako, kwani anaweza kukusaidia kukupa nafuu katika mzigo ulionao wa kuvunjika moyo na upweke, hata kama ni msaada wa muda. Itakusaidia kuhamisha mtazamo na kuona kuwa upo uwezekano mwingine zaidi ya kujinyonga.
Pia, zingatia kuweka ratiba maalumu ya shughuli ambayo utajaribu kuifuata wakati unajisikia vibaya. Ufunguo wa tatizo hilo ni kujiingiza kwenye shughuli mbalimbali kama kikwazo cha kuruhusu mawazo mabaya. Pia, uhakikishe kuwa shughuli hizo zinakupatia furaha na kukupa faraja, siyo kukuongezea msongo.
Jaribu kufanya haya ili uweze kujihisi kuwa unapenda kuendelea kuishi. Fanya zaoezi la kupumua pumzi kutoka ndani, piga muziki wa ala, oga kwa maji ya moto, kula chakula kizuri ukipendacho, andika jarida, fanya matembezi, wasiliana na familia, marafiki au wasiri wako unaowaamini.

Monday, June 16, 2008

MBINU ZA MAFANIKIO KWA WAFANYABIASHARA

KATIKA haya mabadiliko ya milenia mpya, wajasiriamali wameweza kujitofautisha na wafanyabiashara wakubwa ili kuwaridhisha wateja wao. Kuwa na ujuzi, ustadi na uwezo wa kupigania kupata bidhaa bora ni njia mahususi ya kufanikisha biashara.
Hivyo basi, mjasiriamali au mfanyabiashara mkubwa anatakiwa kuwa na mipango mizuri na ya kitafiti kufanikisha hili, kwani huo ni ufunguo wa mafanikio.
Mara nyingi mfanyabiasgara lazima awe mbunifu. Hivyo unatakiwa kuwa mfikiriaji mzuri wa kuuza bidhaa unazozivumbua. Ni muhimu kuongeza thamani katika bidhaa ulizo nazo na huduma zako.
Unapokuwa mjasiriamali unatakiwa kuwa na uvumbuzi wa mawazo yanayofanana na biashara yako kwa kuongeza thamani au huduma. Kwa matokeo hayo wateja watagundua ubora wakati watakapoona uhalisia wa bidhaa ulizo nazo.
Unapotaka kuwa mfanyabiashara wa kiwango cha kuthaminiwa inakubidi uwe mtawala mzuri na meneja aliyebobea.
Uwe hodari katika kujifunza na kupata faida ya teknolojia mpya ili iweze kukusaidia kukuza biashara yako katika uchumi mpya. Kukamilisha teknolojia mpya katika biashara yako ni lazima, hivyo utaendelea kukuza na kuifanya iende na wakati.
Uwe mwendelezaji anayelenga kuimarisha mtandao. Kujihusisha na wafanyabiashara wengine ni muhimu sana kwa kuwa itakusaidia katika ukuaji wa biashara yako.
Pia kuwa mwangalifu kuimarisha mawasiliano uliyo nayo kwa wateja wako na kujenga mawasiliano mengine mapya ili uweze kuwa na mazingira ya kiushindani.
Baadhi ya mbinu za kufanya mabadiliko mazuri katika biashara yako ni pamoja na uwazi, mpango wa kibiashara ulio wazi au unaoeleweka na utaalamu. Uwazi unahitajika katika biashara yako, hivyo ni muhimu kutozuia habari zozote muhimu na kuwa mkweli kwa wateja wako.
Kuwa na mpango wa biashara inayoeleweka kunakufanya uweze kuimarisha ubora wa bidhaa na huduma, ili kufikia mahitaji ya wateja wako na kuwaridhisha. Mpango wako wa biashara mara zote uwe unauangalia na kuuimarisha uweze kuelewa mabadiliko na mahitaji ya wateja wako.
Unatakiwa kuimarisha na kutathmini utaalamu ulio nao ili kuweza kufanya kilicho bora zaidi. Usisahau kwamba unahitaji kutoa muda ili kuzingatia eneo lako la utaalamu ulionao.
Kumbuka matangazo na masoko kwa biashara ndogo yanaongeza bidii na mipango ya kukuwezesha kufanikiwa zaidi. Wamiliki wengi wa biashara ndogo ndogo wanavunjwa moyo kwa haraka kwa sababu hawaelewi upepo wa biashara kwa wateja wao wanaowategemea baada ya kufanya kampeni ya matangazo yao ya awali.
Matangazo ni sanaa inayokuwezesha kutazama na kutengeneza mpango wa muda mrefu utakaokuongoza katika mafanikio.
Kuna mambo matatu wamiliki wa biashara ndogo ndogo wanayoweza kufanya katika kuongeza nafasi ya mafanikio katika kampeni ya kutangaza.
Kwanza, unatakiwa kujiaminisha katika mpango wako wa muda mrefu. Kama hukufanya hivyo bilashaka unahitaji mpango mwingine.
Jambo jingine ni kuwa unapokuwa na mipango ya kufungua biashara ni matangazo. Kujitangaza ni njia moja nzuri sana, lakini nayo inahitaji kuwe na hiyo mipango ya kujitangaza. Angalau unatakiwa kuwa na mpango wa kutangaza biashara zako kwa miezi sita, lakini ukweli ni kwamba inatakiwa ujitangaze kwa mwaka mzima. Hii itakusaidia kuimarisha mkataba wa muda mrefu na watangazaji, kwani kwa kufanya hivyo utakuwa unapunguza gharama za uangazaji.
Hii inakusaidia kufikia ukomo uliojiwekea wa uchapaji na kutoa ujumbe mbalimbali unaotaka uwafikie wateja wako katika vipindi mbalimbali vya mwaka.
Na jambo la tatu ni ongezeko la thamani - kama biashara ndogo unashindana na ushirika wa wateja wako. Unatakiwa kuwa tofauti. Zungumza kutokana na kile wateja wako wanachokihitaji na jinsi ya kuwapatia, lakini pia unaweza kuwa sehemu ya wateja.
Inaweza kukuvunja moyo wakati unashindana na biashara ndogo na kubwa endapo hutapata matokeo mazuri ya biashara kutokana na ulivyojitangaza. Ili kuleta utofauti unayo nafasi kubwa ya kupata wateja wote ambao hawakufanyi ukatulia.
Pata faida kwa kutoa huduma za bure – huduma za kawaida ambazo wafanyabiashara wadogo wanashindwa kufaidika nazo ni kutoa taarifa kwa vyombo vya habari. Kama una bidhaa mpya au huduma au kitu chochote kipya katika kiwanda chako ambacho unafikiri kuwa wateja wako wanatakiwa kujua, andika taarifa kwa vyombo vya habari. Pia unaweza kutoa taarifa hiyo kwenye magazeti binafsi.
Tukutane wiki ijayo.
lcyngowi@yahoo.comwww.ngowil.blohdpoy.com0713 3314550733 331455

VYANZO VYA MIGONGANO NA JINSI YA KUVIKABILI

JINSI jamii inavyokuwa na mfumo wa aina fulani kuna uwezekano wa kujenga mizizi inayosababisha mikwaruzano mbalimbali.
Ni vema kuelewa kuwa jamii yoyote ina mfumo wake, hivyo kuwa na baadhi ya watu wanaojikuta hawatendewi haki kama wengine, hali inayochangia kuwapo kwa migongano, mikwaruzo au kutokuelewana.
Hali hiyo hutokea hasa pale kiongozi wa mtaa, wilaya, nchi, eneo, kazi au katika shughuli yoyote inayowashirikisha watu wengi anaposhindwa kuwawakilisha wote kwa usawa.
Kumbuka kuwa kila mwanadamu ana mahitaji muhimu, kwani kila mmoja hupenda kuwa salama na kutambulika. Ikiwa mahitaji yake hayafikii malengo, husababisha maamuzi mabovu kutolewa, amani kutoweka na kutokuelewana.
Tunaweza kuona vyanzo mbalimbali vinavyosababisha migongano katika jamii tunamoishi. Zinaweza kuwa za kisiasa au kijamii. Tunaona kuwa mara nyingi kutokuelewana hutokea pale watu wanapokosa kuelewana katika jambo linalofanana. Endapo kunakosekana usawa katika mojawapo ya mambo, kwa mfano, utofauti wa kipato unaosababisha mifarakano kutokana na rasilimali za nchi kama vile ardhi na maji.
Pia tunaona hali ya kutokuelewana huibuka pale watu wanapokuwa hawana furaha kutokana na watawala wanaowaongoza.
Mara nyingi tumeshuhudia kuwa migongano ya mara kwa mara hutokea wakati kikundi fulani kinapotaka kuwa huru kutokana na utawala uliopo madarakani, madai yao inaposhindwa kuwasilishwa serikalini, serikali inapowadharau na kutowaheshimu au kukutana na mahitaji yao ya muhimu.
Migongano mingine inatokea kuhusu masuala ya dini na siasa. Wakati mwingine husababishwa na kikundi cha dini au siasa kilichohujumiwa. Hata hivyo, migongano yoyote inaibuka wakati watu wanapoumizwa.
Ingawa mara nyingi migongano hiyo huonekana ni kinyume, inaweza kufikiwa muafaka kama utatuzi utapatikana. Pia katika maeneo ya kazi mara nyingi kumekuwa na mifarakano ya mahitaji. Wafanyakazi wanapozidiana katika rasilimali na kutambuliwa kazini, migongano hutokea.
Kwa mfano, utakuta kuwa mkuu wa idara amekuwa akiwapendelea baadhi ya wafanyakazi kwa kuwapa motisha zaidi, hali inayowavunja moyo wafanyakazi wengine na kusababisha migongano.
Pia ufahari au jinsi ya kuishi na watu maeneo ya kazi huleta kutokuelewana kama tu hutajishusha na kuishi maisha ya kawaida katika jamii inayotuzunguka.
Kumbuka kila mtu ana tabia zake binafsi, kunakuwa na tofauti katika kuwafikia watu na matatizo yao. Kama kiongozi jihusishe nao kuelewa mitindo yao ya maisha na jifunze jinsi ya kuepuka migongano inayoweza kusababishwa na hali hiyo.
Kwa mfano, itakapotokea mfanyakazi mmoja anapofanya kazi katika mazingira bora na mazuri wakati mfanyakazi mwingine anafanya kazi katika mazingira yasiyoridhisha, wafanyakazi hao wawili ni rahisi kukorofishana na kutokuelewana, kwa vile mmoja wao ataona kuwa hatendewi haki kwa hilo.
Matatizo mengine huchangiwa pale mtu asipoweza kufikia lengo alilokusudia kutokana na kutowezeshwa na mwajiri wake - kwa upande wa vitendea kazi, hali inayochangia kuchelewa kutekeleza majukumu yake.
Wakati mwingine mwajiri anaweza kukulaumu mara kwa mara kutokana na uzembe wa kampuni hiyo kwa kutoona umuhimu wa kuwa na vitendea kazi vya kutosha, au wakati mwingine idara mojawapo hupewa vitendea kazi na nyingine kukosa. Hiyo huleta hali ya mvutano na kutokuelewana katika maeneo ya kazi.
Shinikizo kutoka kwa viongozi wa kazi huchangia migongano. Kwa kuwa inaweza kutokea watu wawili au zaidi katika kitengo kimoja wanapokuwa na majukumu tofauti yanayotakiwa na bosi wao kwa wakati mmoja.
Kwa mfano, kiongozi wa kazi anapotaka taarifa kamili ikamilike saa tisa alasiri - muda anaotakiwa mfanyakazi mwingine kukamilisha taarifa yake - ambapo wote kwa pamoja wanahitaji kutumia mashine moja kwa kuwa mashine nyingine ni mbovu, kipi ni suluhu? Matokeo yake mgongano unatokea.
Migongano mingine husababishwa na hali ya upendeleo kwa baadhi ya wafanyakazi. Utakuta bosi bila uficho wowote anaonyesha hali ya kuwathamini baadhi ya wafanyakazi na kuwadharau wengine.
Ubaguzi katika maeneo ya kazi unasababisha minong’ono, tuhuma, na hatimaye migongano. Hivyo ili kuondoa hali hiyo, kiongozi mkuu wa kampuni anatakiwa kuwa thabiti katika kuhakikisha kampuni yake haiwi na mgawanyiko wowote na kuwafanya wafanyakazi wake wafanye kazi zao kama timu moja imara.
Mingine husababishwa na sera mpya ambazo hazikutarajiwa.
Popote sera za kampuni zinapobadilika, kutokuelewana kunatokea, wafanyakazi wanahitaji kufahamishwa sheria na sera za kampuni, pale mabadiliko mapya yanapotokea hawatakiwi kubahatisha. Vinginevyo vitu visivyotarajiwa vitatokea kama kupeana taarifa potofu.
Njia mbalimbali zinazoweza kumsaidia mkurugenzi wa kampuni, mkuu wa idara au yeyote mwenye dhamana ya kuwaongoza wenzake, jinsi ya kutatua migogoro katika maeneo ya kazi.
Ni vizuri ukatambua kuwa baadhi ya migogoro hatima yake hujenga mahusiano bora zaidi tofauti na ilivyokuwa mwanzo endapo itatatuliwa kwa umakini.
Ukumbuke kuwa migongano katika sehemu za kazi ni sehemu ya maisha na haiepukiki, lakini ni jinsi gani tunaishughulikia inapotokea kama bosi bila kuathiri biashara na shughuli za uzalishaji katika kampuni yako. Kama viongozi kunakuwepo na majukumu imara ya kusuluhisha migogoro kwa haraka.
Viongozi wa kisasa hawaatakiwi kuwa ‘wanyapara’, bali wawe viongozi wanaodhihirisha fani zao, heshima na usawa katika mazingira yoyote na zaidi wanaposhughulikia migongano.
Kwanza yampasa kiongozi atathmini chanzo cha tatizo. Mafanikio ya kutatua tatizo la kutokuelewana kwa kikundi au jamii yanatokana na kuelewa chanzo halisi cha mgongano huo. Ni muhimu sana kuangalia mgogoro kutokana na mtazamo wa kila mmoja unaomhusu.
Kutokuelewa chanzo cha tatizo kutafanya utatuaji wa tatizo hilo kuchukua muda mrefu kutambua aliyehusika na sababu za kuhusika kwake, na sababu zinazofanya tatizo hilo kuwa gumu. Kutegemeana na hali ya tatizo lilivyo, unaweza kuzungumza ‘chemba’ na kila mmoja aliyehusika katika mgongano huo au unaweza kuzungumza nao wote kama kikundi. Kusikiliza ni silaha mojawapo muhimu itakayoweza kukusaidia na kulielewa tatizo.
Pia katika utatuaji wa tatizo unatakiwa kuwa makini na kujua kwa undani chanzo. Kuwa mkweli katika kulishughulikia tatizo. Sikiliza kwa umakini kukuwezesha kutoa mawazo yasiyopendelea upande wowote na kukuwezesha kutatua tatizo. Mruhusu kila mmoja kuwa mhusika katika hatua hizo na hakikisha uko wazi, mkweli na kutenda kwa usawa kama unavyozungumza na mtu binafsi. Usihukumu.
Ainisha njia bora zaidi ya kutatua matatizoMara unapokuwa na vielelezo vya uhakika mbele yako ni kazi yako kuongoza kikundi katika kufikia suluhu au kuainisha njia bora ya utatuzi. Mafanikio ya utatuzi wa matatizo mbalimbali mara zote inahusisha pande zote katika kutathmini tatizo na kipindi cha kutafuta utatuzi.
Muulize mtu binafsi kama anaweza kutoa mawazo ya jinsi ya kutatua tatizo. Unaweza kushangaa ni jinsi watu mara nyingi wanavyokuwa kamini kufikia mwafaka wa tatizo na kuwa na maamuzi yao binafsi.
Kama hawatakuwa na uwezo wa kufanya hivyo, unaweza kutumia njia bora ya kutatua tatizo. Malengo yako ni kuhakikisha unapatikana mwafaka wa usawa na utatuzi wa tatizo lililokuwepo ambalo litaleta utatuzi thabiti katika kampuni yako au kwa mtu binafsi.
Suluhisho
Wakati mwingine linapotokea tatizo, chukua muda na kujiuliza maswali yafuatayo:Nini kinachosababisha migongano katika kampuni yako? Kwa nini wewe au mwingine anahitaji vitendea kazi? Je, mtindo wa mfanyakazi fulani ni tofauti na mtindo wako uliouzowea?
lcyngowi@yahoo.comwww.ngowil.blogspot.com0713 3314550733331455Mwisho

TABIA 10 ZA KUEPUKA KUHUSU PESA

“YEYOTE anayepata kipato na kujihudumia mwenyewe anapaswa kuwa na bima ya ulemavu,” aliwahi kusema mwanasaiokolojia mmoja wa nchini Marekani aitwaye Simon.
Baraza la Usalama la Taifa nchini Marekani liliarifu kuwa zaidi ya watu milioni 20 walikumbwa na majeraha yaliyowasababishia ulemevu kwa mwaka 2002 pekee.
Hili laweza lisiwe jambo la kawaida hapa kwetu lakini kitu tunachoweza kujifunza ni kwamba tunapaswa kuwa na utaratibu wa kujikatia bima.
Hebu fikiri jambo ambalo linakufanya uwe nje ya kazi kwa siku kadhaa au miezi kadhaa litakugharimu kiasi gani na ni iwapo utapata pesa hizo na itakuwaje utakaporejea katika shughuli zako za kawaida?
Ni wazi kuwa utajikuta umebakia nyuma kwa kiasi fulani lakini kama utakuwa na bima ya ulemavu basi shirika la bima linge gharamia matibabu na ungelipwa malipo ya ulemavu.
Msomaji wa safu hii huu ni ulimwengu wa sayansi na maendeleo na unaweza kujiunga na bima bila ya usumbufu wowote na pasipo kuchukua muda mrefu.
Ni rahisi kufanya hivyo iwapo mwajiri wako hayuko tayari kufanya hivyo waweza kuangalia mfukoni kuwa ni kiasi gani ulichonacho na ukawasiliana na kampuni au mashirika ya bima na kujiunga. Kumbuka kuwa unapojiunga na bima ni vyema ukapata sera za aina ya bima unayotaka kujiunga nayo na zisome vyema na ikiwezekana pata maelekezo kwa mtaalamu kabla ya kuamua kujiunga rasmi na aina hiyo ya bima.
Kutotambua ongezeko dogo la matumizi
Matumizi madogo ya pesa, kama ilivyo kwa uvujaji mdogo katika chombo, yanaweza kumaliza pesa ulizonazo katika pochi yako.
Njia ya kuepuka hilo ni kutambua wastani wa matumizi yako kwa siku, wiki au mwezi na iwapo kuna ongezeko basi tambua ni kiasi gani, na iwapo litaweza kuathiri matumizi yako au la.
Baada ya hapo sasa unaweza kuamua kufanya matumizi hayo au kuaachana nayo au kubadilisha na matumizi mengine. Yapo matumizi kama vocha za muda wa maongezi ya simu, safari zisizo za lazima au idadi ya vinywaji ni baadhi ya vitu ambavyo huongeza matumizi japo kwa sehemu ndogo lakini huwa na mabadiliko makubwa katika hali ya fedha ya mhusika.
“Jaribu kuangalia kumbukumbu zako na angalia pesa ulizonazo na madeni unayodaiwa yanatokana na nini? Utaratibu wa aina hii utakupa hali halisi katika matumizi yako ya pesa na utang’amua athari za ongezeko dogo tu la matumizi,” alisema Berkeley Calif, wa Marekani.
Njia muhimu ya kukwepa hilo ni kujiuliza kuwa je, matumizi yaliyoongezeka yana umuhimu wowote?
Kungojea malipo ya pensheni ili kuwekeza
Hili ni moja ya makosa makubwa yanayofanywa na watu wengi. Wafanyakazi wengi wanashindwa kuwekeza wakati wakiwa kazini na hivyo kusubiri hadi walipwe malipo ya kustaafu. Hali hii inawafanya wengi kujikuta wakistaafu huku hawana kitu na hivyo kutumia malipo ya kustaafu katika kutekeleza mahitaji yao na hivyo kukuta pesa hiyo ikimalizika bila ya kufanya jambo la msingi lililokusudiwa ambalo ni kumtunza mstaafu hadi anakufa.
Wengi tunaweza kufikiri kuwa ni jambo lisilowezekana lakini kumbuka kuwa ili uwekeze ni lazima ujinyime na unaweza kufanya hivyo kwa kutenga asilimia ndogo tu kutoka katika mapato yako au kwa wale ambao si wafanyakazi wa ofisini wanaweza kuweka utaratibu wa kuchangiana na wenzake kwa mzunguko na inapofika zamu yake anaweza kuwa na utaratibu wa kuweka pesa benki hadi atakapoona imefikia kiwango cha kufungua mradi fulani anaweza kufanya hivyo.
Ni rahisi kuanza, angalia mfumo wa mapato yako na jiulize kuwa unaweza kuanza na kiasi gani na uamue kuanza kwa ujasiri.
Kusubiri hadi dakika ya mwisho ndipo ukusanye pamoja mtajiWatu wengi huwa na kawaida ya kutaka wapate mtaji wote wa kuwekeza kwa wakati mmoja. Si ajabu kusikia mtu akisema ifikapo Mei nitafanya jambo fulani, au mshahara wa mwezi ujao nitafanyia jmbo fulani.
Kwa utaratibu huo ndugu msomaji utajikuta ukibakia kupanga kuwa nitafanya jambo fulani ifikapo mwezi au siku fulani na siku hiyo haitafika kamwe.
Nilipanga kuwa mwezi huu nitanunua viatu vya watoto wa shule lakini imetokea dharura…” alisikika mama mmoja akisema.
Mama huyu ambaye ni mfanyakazi wa kipato cha mwisho wa mwezi alishindwa kuwa na utaratibu wa kujiwekea akiba kila anapopokea mshahara wake na akafikiri kuwa anaweza kutenga mshahara wake wote kununulia viatu vya watoto lakini dharura ikamkwamisha. Iwapo mama huyo angekuwa na utaratibu wa kujiwekea akiba, dharura isingeingilia mambo yake.
Kulipa kila mtu na kuweka akiba kilichobakiaKamwe usije ukasema kuwa nitaweka akiba kwa kile kitakachobaki. Iwapo utakuwa na mazoea hayo, basi ni wazi kuwa malengo yako ya kujiwekea akiba yanaweza yakashindwa.
Kuweka akiba ni moja ya matumizi muhimu hivyo hakikisha kuwa unalipa kipaumbele miongoni mwa matumizi yako muhimu.
Amua kuwa asilimia 5 au 10 ya kipato changu ni kwa ajili ya kuweka akiba na hakikisha kuwa una nidhamu wakati wa kutekeleza hilo. Usithubutu kulipa madeni yote na kusema kuwa kitakachosalia ndicho nitakachoweka akiba la badala yake waweza ukaamua kulipa sehemu ya madeni na sehemu iliyosalia unaweza kuonana na wadai wako na ukawaomba ulipe wakati mwingine lakini kuweka akiba ni jambo lisiloweza kuahirishwa kamwe iwapo unataka kufanikiwa katika malengo yako.
Iwapo utakuwa na mazoea ya kulipa madeni na kufanya matumizi mengine huku ukisubiri kinachosalia ili kuweka akiba unaweza kujikuta unastaafu kazi bila ya kubakiwa na kiasi cha kuweka akiba. Kumbuka kesho nzuri huanza leo, hivyo kuweka akiba yenye manufaa kunatakiwa kuanza leo, hivyo msomaji wa safu hii panga na uanze leo kujiwekea akiba.
Kushindwa kusimamia vitega uchumi vyako
Hili ni jambo linalowakabili watu wengi na kufanya waishi katika maisha ya kushindwa kila siku.
Ni vyema kutambua kuwa kuweka akiba ya pesa ni jambo moja na kuwekeza pesa hiyo ni jambo jingine. Kuwekeza ni namna ya kufanya pesa uliyojiwekea akiba iweze kuzalisha faida.
Njia nzuri ya kufanya hivyo ni kuwekeza katika miradi mbalimbali, sababu ya kufanya hivyo ni kuogopa kuwekeza katika mradi mmoja ambao unaweza kufa na kukufilisi kabisa. Kumbuka ule msemo wa kwamba ‘usiweke mayai yote katika kikapu kimoja kwani kikianguka yote yanaweza kupasuka’.
Wekeza katika maeneo tofauti au kiasi fulani cha fedha ulizojiwekea akiba. Hii itakusaidia kutambua iwapo mradi uliowekeza unaendelea vyema au la, kama unaendelea vyema unaweza kuongeza mtaji zaidi na iwapo mradi haufanyi vyema unaweza kuachana nao na ukafikiria kufungua mradi mwingine. Dhana ya kuwekeza katika maeneo tofauti inalenga kuhakikisha kuwa mtaji wako wote haupotei.
Kuhakikisha uwiano na kumudu vyema vitega uchumi vyako kunaweza kukusaidia kutambua ni wakati gani biashara ni nzuri na ni wakati gani si nzuri. Hili laweza kuonekana jambo dogo lakini ni muhimu sana na halikwepeki, iwe kwa wafanyabiashara wadogo au wakubwa. Wachumi wanasema kuwa uwekezaji katika maeneo tofauti tofauti huleta faida kubwa ikilinganishwa na uwekezaji wa eneo moja kwa wakati mmoja. Kwa mfano, utafiti uliofanywa na taasisi ya biashara ya taifa nchini Marekani mwaka 2005 ulionyesha kuwa watu waliowekeza katika eneo moja waliweza kupata faida ya asilimia 2.5 kwa mwaka ikilinganishwa na 6 kwa wale waliowekeza katika maeneo zaidi ya mawali kwa wakati mmoja.
Angalia mfano huu waweza kuwa wa kufurahisha laikini una mafunzo ndani yake.
Kwanini unakuwa na samani nyingi ndani ya nyumba? Kwanini uwe na kiti na kochi wakati vyote vinatoa huduma moja tu ya kukalia?
Ni rahisi kuwa vinashirikiana kutoa huduma hiyo na hivyo kumpa faida zaidi mtumiaji. Tambua malengo yako na ona jinsi ya kutekeleza malengo hayo kisha jitoe kikamilifu katika kutekeleza malengo yako.
Kutawaliwa na hisia katika vitega uchumi
Yapo makosa makubwa mawili hapa: watu kuwa na mapenzi mazito dhidi ya vitegea uchumi vyao na kujikuta wakati wowote wakielekeza au kujitoa kwa ajili ya vitega uchumi kuliko kawaida au, wakati vitega uchumi vinapoanza kwenda mrama au kombo hutaka kuachana na mambo mengine na kuhangaika navyo hadi vitakaporejea katika hali ya kawaida. “ Hili ni kosa kubwa japo wengi wanaweza kudhani kuwa ni jambo jema na la muhimu,” anasema mwanasaikolojia wa nchini Uingereza Simon.
Hii ni hatari kwani inaweza kukuletea athari ambazo zinaweza kukufanya ushindwe kufanya mambo mengine ya maisha. Simon anasema kuwa katika utafiti alioufanya kati ya mwaka 2000 na 2002 aligundua kuwa watu waliokuwa na mapenzi makubwa na vitega uchumi vyao walipata hasara ya asilimia 30 na 50 baada ya mambo kwenda kinyume na walivyotarajia. Sababu kubwa ilikuwa ni kwamba walikuwa na mapenzi makubwa mno na miradi yao na wakajikuta wakiacha kufanya mambo mengine na kusikitikia miradi yao kuwa haiendi vyema na hatimaye wakajikuta wakipata hasara katika maeneo mengine.
Nini cha kufanya ili kuepukena na hili? Fanya jambo rahisi kiasi hiki, tambua ni wakati gani biashara fulani inakuwa na soko zuri na ni wakati gani hali ya soko si nzuri.
Jambo jingine ni kuhakikisha kuwa unawekeza katika maeneo tofauti na hapa ni kazi au biashara na usije ukawekeza katika mapenzi.
Tukutane wiki ijayo.
lcyngowi@yahoo.comwww.ngowil.blogspot.com0713 3314550733 331455

MAKOSA 10 YA KUACHANA NAYO KATIKA MATUMIZI YA PESA

SI jambo la ajabu kumsikia mtu akisema fulani ana matumizi mabaya ya pesa au yule akipata pesa zinamtawala.
Hata hivyo, tunashindwa kutambua kuwa hiyo si njia ya kumsaidia mtu wa aina hiyo kwani hawezi kubadilika.
Mtu huyo tunamuona mfujaji wa pesa kutokana na ukweli kuwa hajui jinsi ya kushughulikia tatizo alilonalo.
Ni vema ukatambua kuwa, kamwe huwezi kubadilisha mwenendo wako kuhusu hali ya kifedha, isipokuwa unaweza kushughulikia baadhi ya matatizo.
Hii inahusu tabia ya kufanya au kutofanya mambo fulani. Tabia zetu nyingi kuhusu pesa huundwa bila ya sisi kujitambua au kutojali katika kipindi kirefu.
Hakuna hata mmoja wetu ambaye hukaa chini na baada ya kufikiri kwa muda mrefu, akatoka na jibu kwamba, kuwa na uwiano katika kitabu cha hundi ni jambo la kijinga. Badala yake tabia huibuka yenyewe baada ya muda mrefu.
Tabia yetu kuhusu pesa husababishwa na namna tunavyotunza pesa, tunavyotumia, tunavyothamini na tunavyofikiri kuhusu mustakabali wetu. Hivyo kile tutakachojifunza kuhusu pesa, kinaweza kufanya tuwe na mwenendo mzuri au mbaya wa pesa zetu.
Ni vema ukakumbuka kuwa, unapogundua juu ya jambo fulani ambalo limekosa mwenendo mzuri, basi utafute namna ya kuachana nalo.
Acha kurudia makosa yale yale kila mwaka na ujiulize ni kwa nini huweki akiba kutokana na kipato chako? Njia pekee ya kuepekuna na tabia hiyo ni kufuta mfululizo wa makosa hayo yenye tabia ya kujirudia na udhamirie kubadili maisha yako.
Baadhi ya watu huishi huku wakiendelea kurudia makosa katika sekta ya kiuchumi. Bila shaka hutakiwi kuwa mmoja wa watu wa aina hiyo.
Ili uepukane na mkosaji anayerudia kosa, unapaswa kuhakikisha kuwa hufanyi kosa lolote miongoni mwa makosa haya kumi ambayo wengi wetu huyafanya kuhusu pesa.
Hata hivyo unapaswa kuhakikisha kuwa unaitambua vyema hali halisi ya gharama duniani, huku ukichagua njia muafaka ya kukabiliana na kila hali.
1. Kutumia pesa bila ya bajeti
Mara nyingi watu hufikiri juu ya mipango mbalimbali ya kuwaingizia fedha, mfano wapo wanaofikiri ni jinsi gani watawekeza ili kuifanya pesa hiyo iongezeke, lakini ni wachache sana ambao hufikiri juu ya kuandaa bajeti, hasa kwa kuzingatia uwezo wao kifedha.
Mshauri mmoja wa masuala ya kifedha kutoka nchini Marekani, John Ritter, aliwahi kusema iwapo una kipato na Ankara, unahitaji pia kuwa na bajeti.
“Mara nyingi kuna kikubwa kinachotoka kuliko kipato,” anasema.
Je, kutumia pesa bila bajeti kunaweza kukugharimu nini? Wengi wetu wanaweza wasikubaliane na hili kwa kuamua kutokubaliana nalo, au wamekuwa wakisumbuka bila ya kuelewa kinachowasumbua.
Jambo hili si jingine, isipokuwa kukosa utulivu wa akili na mawazo kuhusu pesa pamoja na uwezo wa kuandaa bajeti ya muda mrefu.
Mwisho wa hali kama hii ni kushindwa kuwa sahihi juu ya kile ulichotumia kuwa ni asilimia 15 au 20 au zaidi katika chakula au afya.
Namna ya kuepukana na athari hiyo, hakikisha unaweka utaratibu wa kutambua kila aina ya matumizi unayoyafanya ili kung’amua ni wapi pesa zako zinakwenda.
Njia nzuri ya kumudu jambo hilo ni kuhakikisha unaorodhesha mahitaji yote ambayo hayalipwi kwa utaratibu wa ankara, mfano vinywaji, burudani mbalimbali, kuchangia sherehe miongoni na mengine mengi.
Baada ya kufanya hivyo hakikisha unatenga kiasi fulani cha pesa kwa ajili ya dharura, mfano matengenezo ya gari iwapo umebarikiwa kuwa nalo, au hata pesa ambayo itakuwezesha kusafiri kwenda kuona mgonjwa au kuhudhuria msiba.
Watu wengi hudharau mahitaji ya aina hii na kuyaweka kando ya bajeti kwa sababu hayana umuhimu kwao.
Hata hivyo, mara yanapotokea, umuhimu wake huonekana na hapo ndio hutambua kuwa kumbe katika wakati wote kuna matumizi.
2. Kutembea na kadi inayoruhusu ukope
Hili ni tatizo kubwa kwa nchi za wenzetu walioendelea, na wengi hifikiri kuwa hiyo ni sehemu ya ustaarabu na maendeleo.
Kutembea na kadi inayoruhusu ukope, ni hatari kwani inakufanya kuwa na tamaa ya kupata mahitaji. Sharti la ukopaji wa aina hii ni kukatwa riba kubwa ikilinganishwa na mtu anayenunua moja kwa moja.
Hapa kwetu kuna taasisi na mashirika yanayotoa huduma na vitu kwa njia ya mkopo, lakini iwapo utachunguza vema, utagundua kuwa muda ambao unakaa na deni unakugharimu zaidi, kwani utalazimika kulipa kwa asilimia kadhaa zaidi ya yule aliyenunua kwa kulipia moja kwa moja.
“Mara nyingi watu wanaotaka kulipia huduma au kitu kidogo kidogo hawawezi kufanya chochote na badala yake wanapata hasara kubwa,” anasema John Ritter.
Kwa ujumla kadi za aina hii ni njia mojawapo ya kukufanya uwe mtumwa wa mahitaji yako au madeni.
Ushauri ambao ningependa kukupatia hapa ni kwamba, hakikisha unafanya malipo yanayotakiwa kwa wakati na usikubali kubaki na deni lisilo la lazima.
Baada ya hapo, hatua inayofuata ni kuhakikisha kuwa unadhamiria kwa hali na mali, hata ikiwezekana kwa kujinyima, ili uweze kulipa na kuachana na madeni hayo kabisa, ukianza na moja na baada ya jingine.
Tambua kuwa siku zote deni kubwa ni gumu kulimaliza, lakini hiyo isikukatishe tamaa na badala yake ione kuwa changamoto kwako. Iwapo ulifurahia matunda ya deni hilo, basi uwe tayari kubeba mzigo wake.
Kwa ujumla njia rahisi ya kuepukana na madeni, ni kuhakikisha kuwa unalipia mahitaji yako yote kwa ukamilifu, kila ifikapo mwisho wa mwezi.
Iwapo utahitajika kutumia kadi inayokuruhusu kukopa wakati una dharura, basi hakikisha kuwa unakopa kiasi cha kutosha kukidhi dhahruara hiyo tu (mfano, ugonjwa, ajali au safari).
Baada ya kufanya matumizi hayo, hakikisha kuwa hutumii kadi hiyo hadi utakapokamilisha malipo ya deni hilo.
3. Kudharau riba zitolewazo na benki
Bila ya kujali kiwango cha riba kinachotolewa katika masoko ya hisa, mabenki au kuwekeza katika taasisi zinazotoa mikopo kwa ajili ya ujenzi wa nyumba, ni jambo la muhimu kuweka pesa katika taasisi zinatoa riba.
Unaweza kujenga utaratibu wa kununua hisa katika makampuni, mashirika au hata taasisi za fedha. Jambo la kuzingatia, ni kwamba, hii ni njia ya kuzalisha pesa ambazo huzitumii kwa sababu siku utakapoamua kuuza hisa hizo au kuhitaji pesa zako, hazitarejea kama zilivyokuwa, zitaongezeka.
Ipo faida ya kuwa mwanachama unayechangia katika taasisi zinazotoa mikopo, kwani hupata unafuu wakati wa kurejesha mkopo huo.
Mfano, mwanachama anayekopa kutoka taasisi ambayo hutoa mikopo kwa ajili ya ujenzi wa nyumba, ni wazi kuwa atapata unafuu wakati wa kurejesha mkopo huo kuliko mtu anayekopa wakati si mwanachama, kwani riba ya urejeshaji wa mkopo wake itakuwa ya juu zaidi.
Kwa leo tuishie hapa, juma lijalo tutaendelea na makosa yaliyosalia.

UMUHIMU WA NENO SAMAHANI

SAMAHANI hutumika kama njia ya kuomba kusamehewa, lakini siku hizi neno hilo hutumika katika maana ya vitu vingi.
“Mara zote inaonekana kwangu neno samahani kama neno gumu kulitamka,” anasema Elton John.
Lakini katika miaka ya sasa, neno hilo huwa ni jepesi kulitamka kwa kuwa limepoteza thamani yake ya awali.
Mara nyingi baadhi ya watu huamua kutenda jambo la kumsikitisha mtu kwa kudhamiria na kisha kukimbilia kusema samahani kwa hilo alilolitenda.
Samahani ni neno la kiasili ambalo hutumika kuelezea masikitiko kwa kufanya jambo lisilopendeza.
Siku hizi, tunatumia neno samahani si tu kuelezea masikitiko yetu kutokana na mazoea, lakini pia hutumika neno hilo kama kumwomba mtu arudie maneno aliyokuwa akikueleza.
Mfano ‘samahani, sijakupata vizuri ulichosema.’ Inaonyesha kuwa katika Bara la Ulaya neno hili hutumika mara nyingi zaidi kuliko katika Bara la Afrika.
Asilimia 86 ya watu wanaotumia neno hili hulitumia kwa mzaha, kama neno rahisi kulitamka na kama njia inayofaa ya kuomba samahani kwa tabia mbaya wanayoifanya.
Tuangalie sababu tano kuu zinazomaanisha neno samahani: Sababu ya kwanza ni pale tunapokuwa hatuna muda wa kuzungumza na mtu au kufanya kitu. Mfano (samahani, sitakuwa na muda wa kuzungumza kwa sasa).
Ya pili ni kuomba radhi kwa niaba ya mtu mwingine, kama kwa watoto wetu, kwa rafiki zetu au kwa wafanyakazi wenzetu. (samahani, Jimmy mara zote ni mtu wa vurugu).
Ya tatu ni pale ambapo hujaweza kumsikia mtu akiwa anazungumza kwa ufasaha, hivyo unamwomba arudie. (samahani, unaweza kurudia?).
Nne, ni pale unapotaka jambo fulani lirudiwe kuelezwa kwako (samahani, sina uhakika na kile ulichomaanisha).
Mwisho ni wakati pale tunapojihisi kuwa tunahitaji kuomba radhi kwa kumsaliti mtu, na kumfanya mwingine asifanikiwe, hatuna budi kuomba radhi. (nimekosa).
Pia tunatakiwa kusema samahani kwa wabia wetu, kama vile unavyosema kwa mkuu wako wa kazi.
Utafiti uliofanywa umebaini kuwa, asilimia 27 ya matumizi yetu kwa neno samahani tunatumia kusema hivyo kwa wabia wetu, asilimia 19 linasemwa kwa wageni, asilimia 14 kwa watoto wetu, asilimia 14 kwa wafanyakazi wenzetu, asilimia nane kwa rafiki zetu, asilimia tano kwa wazazi wetu, asilimia tatu kwa ndugu zetu na kama asilimia moja kwa wakuu wetu wa kazi (bosi).
Inaonyesha kuwa Waingereza wamekuwa ni watumiaji wazuri wa neno hilo. Hujulikana kama taifa la sorry-sayers.
Inaelezwa kuwa Waingereza wamekuwa wakitumia neno hilo katika mazingira mbalimbali, kwa mfano ‘samahani, ninaweza kusema chochote?’ Au samahani umenipa pungufu ya fedha uliyostahili kunirudishia.
Tunaona ni kwa jinsi gani neno samahani linakuwa ni rahisi kulitamka, kwa kuwa linatumika kama mhimili, pia njia ya kukiri makosa uliyoyatenda.
“Kusema samahani mara kwa mara ni tabia iliyojengeka kwa Wazungu, neno samahani linatamkwa kwa adabu, liko pale kwa ajili ya mshikamano wa kijamii.”
“Pia tunasema samahani mara nyingi kama tunahisi kuwa tunalaumiwa kwa kitu fulani - ambayo hali hiyo inakusababishia ‘maumivu ya ndani.’
Wakati mwingine tunafikiri kuwa neno hilo linaonyesha kuwa tuna tabia nzuri, lakini inaweza kuwa tofauti na fikra zetu ila ni hali tu ya kuonyesha kuwa unajali.
Peter Carvin, anasema kuwa, baba yake alimweleza kuwa neno samahani linamaanisha kutorudia kosa lile lile, tofauti na miaka ya sasa limeonekana kuzoeleka vinywani mwa watu wengi na pengine unakuta mtu hamaanishi kutoka ndani ya moyo wake.
Laura anasema kuwa anachukia tabia ya baadhi ya watu ambao wanatenda ukatili wa kukusudia kwa wenzao kwa nia ya kuomba samahani baada ya tendo hilo. Ni vizuri wakafikiria kwa upya tabia hiyo isiyopendeza.
Hivyo ushauri mzuri ni kwamba pamoja na neno hilo kuelezwa katika maana nyingi, lakini ile iliyozoeleka hasa ni pale unapotenda jambo halafu ukajisikia kuwa na hatia katika moyo wako, hivyo basi hali hiyo inapokutokea ni bora ukaomba msamaha kwa yule uliyemtendea isivyostahili.
Unapokuwa mtu wa kukubali kuwa umekosea na kuomba samahani kwa yule uliyemuumiza, aidha kwa maneno yako au matendo yako, itakuwa faraja kwake na kuona kuwa unajali kutokana na hali ile ya kukubali kushuka na kusema neno samahani, hivyo naye ataonyesha hali ya kupokea msamaha wako.
Inakuwa haipendezi endapo utamuudhi mtu halafu ukatamka kwake neno la msamaha kisha akagoma kukusamehe, ninaamini vitabu vyote vya dini vinasisitiza neno msamaha. Hivyo basi kama mhusika uliyemuudhi hajakubali ombi lako, inategemea umelitoa vipi.
Yawezekana kabisa umelitoa kwa kejeli, mzaha au dharau ndiyo maana mhusika hakulikubali ombi lako hilo, hivyo ni vizuri ukalitoa neno hilo kwa kuonyesha hali ya kujali na kujutia kile ulichokitenda.
Tukumbuke tuwapo majumbani mwetu, shuleni, vyuoni na kazini mara zote vikombe viwili vikikaa pamoja ni lazima vigongane, hivyo ni vyema pale unapogundua umemfanya mtu akaumia katika nafsi yake kutokana na matendo au maneno yako, usiache kusema neno hilo ili liwe faraja kwake.
lcyngowi@yahoo.comwww.ngowil.blogspot.com0713 3314550733 331455

JINSI YA KUONYESHA UPENDO

NI jinsi gani unaonyesha upendo wako kwa rafiki. Ni muhimu kuwa rafiki mzuri, kwa sababu wakati mwingine wakati familia yako haipo karibu nawe, unahitaji mtu wa kuongea naye. Pia ni muhimu kuwa rafiki mzuri kwa sababu unajifunza ni jinsi gani ya kukutana na watu wapya na unajifunza kutokana na makosa yako.
Tafuta watu ambao unapenda wawe rafiki zako, kwa kujitambulisha, na kumwacha mtu mwingine kukueleza juu ya mambo anayoyapendelea. Mwonyeshe mtu huyo kuwa unamwamini, mwache ajue kuwa ni sawa kupendana, mwache ajue kuwa uko pale kwa ajili yake na atakuwa rafiki yako wa kudumu. Mara zote mfanye atabasamu hata kama ana huzuni. Pia mwache ajue kuwa upo tayari kusikiliza chochote atakachosema.
Zawadi za kila sikuUnawezaje kuonyesha upendo bila kutumia fedha? Wakati mwingine tunajitahidi kwa bidii kutafuta zawadi ambayo ni sahihi tunayofikiria kuwa ina maana kwa yule unayempelekea.
Au, tunaishikilia zawadi hiyo, tukifikiria kama kuna sababu maalum ya kutoa zawadi hiyo. Ninakutia moyo kutoa zawadi yako kwa uhuru na iwe ni mara kwa mara, kumbuka kuwa utoaji ni shughuli ambayo inamnufaisha mtu kila mara anapofanya hivyo.
Tuangalie zawadi kumi ambazo zinafaa kwa siku yoyote ya kawaida na katika siku maalum. Pia, ni zawadi ambazo mtu yeyote anaweza kutoa kwa sababu halazimishwi ila ni kwa nia ya kuleta ushirikiano.
Muda Kuutoa muda wako na kushirikiana na wenzako ni moja ya zawadi kubwa unayoweza kuitoa. Kama unatoa dakika kumi kwa kupiga hadithi na mtoto wako, kupata chakula cha mchana na rafiki yako, au kutumia muda wa mchana kwa shughuli za nyumbani, shambani au shughuli ndogo ndogo ukiwa na mume au mke wako, unakuwa unajitolea nafsi yako na kujenga uhusiano mzuri kwa muda huo huo.
Kukiri kwa uaminifu Tumekuwa tukisikia watu wachache wakisema kuwa wamepokea shukrani nyingi au pongezi nyingi. Wote tunajisikia vizuri wakati tunapata taarifa nzuri na shukrani kwa vile tulivyo au tunayoyafanya.
Anza kuzingatia kuimarika katika hilo na kutoa sifa nzuri kwa wengine na kujenga tabia ya kukiri jambo zuri linalofanywa na wengine kwa kile unachokiona.
MsamahaMsamaha ni zawadi nzuri mno yenye nguvu. Wakati tunasamehe wengine, tunaacha kuwaadhibu. Tunawaruhusu ili wajisikie hatia au kuona aibu ili waweze kugundua makosa yao. Msamaha pia ni zawadi ya kutuweka huru kutoka kwenye uzoefu ulioupata wakati ulipoumizwa moyo wako au maumivu katika matukio yaliyopita.
UpendoWakati unapotaka kuuonyesha upendo wako kwa wengine, usiwahukumu wengine, na uwaone kama ni watu wa muhimu kwako, watakatifu na wa thamani, hiyo ni zawadi kubwa.
Tunaposhiriki kwa uwazi upendo wetu na wengine inasaidia kuponya majeraha, kujenga uhusiano mzuri, na pia kumsaidia mtu katika kupitia changamoto za maisha na kuwa na maisha mapya ya uhakika.
Usiugawe usikivu wakoIngawa tunatoa muda wetu kwa ajili ya wengine, akili zetu zinaweza kuwa popote kutokana na uzoefu. Jiruhusu nafsi yako kuwa kwa mtu mwingine, kupanga naye shughuli nyingine, mawazo, au ajenda mpaka utakapofikia malengo yako uliyokusudia.
Kama utafanya hivyo watu watakuona unastahili kupata asilimia zote, kwa usikivu wako na kwa upande mwingine inawezekana ukawa hujafikia kiwango hicho ila kutokana na hali hiyo uliyojiwekea kwa watu.
HeshimaMara kwa mara tunakuwa na shughuli nyingi au tunajishughulisha sana katika maisha yetu ambayo yamekuwa na matukio mfululizo ya kuvutia ambapo tunasahau kama kuna watu wengine wanaotuzunguka. Iache nafsi yako ipumue na kutoa heshima kwa watu ambao unakutana nao kila siku.
Yapo mambo madogo madogo ambayo yanaweza kufungua milango kwa watu wengine kuthamini mambo ambayo unawafanyia kama kumpa lifti kwenye gari yako, kumbebea gazeti lake mpaka mlangoni pake, au kusimamisha gari yako mbele ya mtu unayemfahamu na kumpa lifti kipindi cha msongamano wa abiria kituoni.
Mambo yote hayo yataonyesha hali ya kujali kwa mtu ingawa wakati mwingine mtu hawezi kuelewa wema wako na kukushukuru.
ShtukizaZawadi za aina hii zinamfanya mtu kuwa mbunifu wa hali ya juu. Je, unataka kumpa dada yako kadi ambayo inasema unampenda? Unajisikiaje unapomtumia mumeo bunda la maua? Je, ni kweli utamshtusha? Au labda umechagua kujitolea kumpa mfanyakazi mwenzako kigari cha kusukuma cha watoto ili aweze kufurahia jioni anapokuwa matembezi na rafiki zake.
Zawadi kama hizo zinakuwa tukio kubwa kwa yule unayempelekea katika siku yake ya kawaida kwa sababu hakutarajia kufanyiwa jambo kama hilo kwa siku hiyo.
ShukraniKutoa zawadi ya shukrani kwa mtu inasababisha mtu huyo kujua kuwa umekuwa makini kwa lile alilokufanyia. Kama ukiri wa dhati, na neno lingine ni kusema asante linaonekana ni jambo ambalo si la kawaida.
Endapo utachagua kusema au kuandika shukrani zako, hii ni zawadi ambayo inakwenda ndani ya moyo wa mpewa shukrani.
Tabasamu Katika dunia ya kisasa, mara nyingi tunaona tabasamu chache na nyuso zenye furaha ya kweli. Kinyume cha mwelekeo kwa kujivisha tabasamu kama sehemu yako ya kila siku.
Tabasamu linajulisha moyo mkunjufu, mapokezi na urafiki. Pia inafanya kuonekana kwa urahisi kwa wote wenye nyuso za tabasamu. Itoe zawadi hii ya tabasamu itoe ujumbe. Mfano "nina furaha uko hapa".
Maombi ya kimya kimyaWote tunakuwa na maombi ya ziada na ya baraka katika maisha yetu. Hata kama hufahamu, mtu mwingine anaweza kukubariki wakati unampa zawadi ya maombi yenye nguvu.
Kama unajua au la, mazingira ya mtu au dini yake, unaweza kuuliza kwa msaada au usikivu. Maombi rahisi unaweza kumwombea kwa kutumia "Mungu/Allah, ninakuomba umbariki mtu huyu na ukutane na mahitaji yake yoyote ambayo anayo katika maisha yake, asante."
lcyngowi@yahoo.comwww.ngowil.blogspot.com0713 3314550733 331455

VITU VINAVYOSABABISHA KUKOSEKANA KWA UPENDO

KARIBUNI wapenzi wasomaji katika safu hii ya Maisha Yetu inayokujia kila wiki. Ninawatakia heri ya mwaka mpya 2008 uwe wa mafanikio.
Wiki iliyopita tuliangalia maana ya upendo, leo tutaangalia vitu vinavyosababisha kukosekana kwa upendo kwa watu wapendanao.
Kijana Jerry Bright anasema kuwa, utafiti wake alioufanya amegundua kuwa kwa watu wapendanao wanapokosa muda wa kuwa pamoja, hali hiyo huchangia sana upendo wao kuvunjika au kuhitilafiana. Kwa kuwa inaonyesha kuwa lazima kutakuwa na chanzo cha hali hiyo kuwepo, aidha mmoja wa marafiki kuamua kujipa shughuli nyingi ilimradi amvunje moyo rafiki yake kwa makusudi yake maalum.
Pamoja na suala hilo la kukosa muda wa kuwa pamoja, Bright anaeleza kuwa wakati mwingine heshima hukosekana kwa watu wapendanao, si lazima kwa wapenzi ambao hutarajia kuoana hata kwa wale ambao ni marafiki wa kawaida kama mwanamke kwa mwanamke mwenzake au mwanaume kwa mwanaume mwenzake au marafiki wa jinsia tofauti.
Anasema heshima ni kitu cha bure na si cha kulazimishwa. Hivyo basi, ni vizuri kwa mtu awaye yote kumheshimu mkubwa wake, au mdogo au hata kama mtu huyo unalingana naye, kwani huchochea upendo wa kweli kati yao.
Endapo heshima itakosekana lazima kutakuwa na mpasuko mkubwa wa upendo. Hata kama kama kuna jambo la kutatiza likiwa limejitokeza kwa watu wapendanao, ni vizuri likatafutiwa utatuzi wa haraka kwani hali hiyo uchangia kuongezeka kwa upendo kwa kuwa mmoja wao ameonyesha hali ya kujali.
Pia kama mmoja wa wapendanao hataonyesha hali ya kujali kwa mwenzake endapo anaugua, amefiwa, au amepatwa na jambo lililomvunja moyo na kumkatisha tamaa, hali hiyo itachangia pendo lililokuwepo kati yao kutoweka mara moja kwa kuwa si hali ya kiubinadamu.
Hivyo kama hayo yote yatakosekana kwa watu wapendanao, itajitokeza hali ambayo itasababisha mawasiliano kupungua, ugomvi kuwepo, na hali ya kutokujali kama kuna mtu ambaye unaweza kumshirikisha jambo lako upatapo na msuko suko.
Hali nyingine itakayojitokeza ni kukosa uangalifu kwa wapendanao, kutokuelewana, kutokuheshimiana. Pia ukosefu wa kusimamia mambo mbalimbali kwa wapendanao.
Kumbuka suala la talaka linapojitokeza na matatizo katika mahusiano ni chanzo cha kukosa upendo.
Kijana Benson anasema kuwa yeye na mke wake wameishi katika ndoa miaka 9, wamebahatika kupata watoto wawili. Mke wake amewahi kumwambia kuwa hana furaha na anafikiri kuwa wangeachana. Anasema kuwa hakushangaa sana kusikia maneno hayo kutoka kwa mkewe kwa sababu alimwona hana furaha kabla na kuna wakati hali hiyo ilikuwa ikimtokea.
Alikuwa akilalamika kuwa kila kitu ninachomfanyia si kitu, na hajisikii kumpenda. Anasema kuwa anajutia kuolewa naye. Anasema kuwa alifikiri kuwa mambo yangekwenda vizuri kila wakati kuwa na matukio makubwa katika maisha kama kuoana, watoto n.k. Benson anasema wamekuwa wakienda kwa washauri ili apatiwe msaada na amekuwa akichanganyikiwa afanye nini. Anasema yeye anampenda mkewe kutoka ndani ya moyo wake na hapendi kuachana naye. Pia anaogopa madhara yatakayowatokea watoto wao ambao bado ni wadogo. Anasema na ushirika mzuri katika mambo yote isipokuwa eneo la upendo. Amekuwa mbali na hana uamuzi katika kujamiiana, amekuwa wa kulaumu na kusema kuwa hamvutii.
Watu wengi wanakosana kutokana na amri. Mara nyingi wanaume ndio wamekuwa watoa amri katika familia zao, japo pia wapo baadhi ya wanawake ambao hupenda kuwa watu wa amri kila wawapo nyumbani kwao.
Mary anasema, alifikiri mume wake hana kasoro, atakuwa na njia nyingi za kumpa furaha, atamtimizia mahitaji yake, mwenye uwezo wa kiuchumi na mtafutaji, mtoaji, lakini yale yote aliyokuwa akiyatarajia kwa mumewe yamekuwa tofauti, amekuwa mtu wa kutoa amri, si wa kuaminika, mfano: "Ninakupa dakika kumi na tano ya kubadili nguo zako na kutengeneza nywele zako, hakikisha chakula cha jioni kinakuwa tayari kabla sijarudi nyumbani."
Kwa maelezo ya Mary, ana mambo mengi ya kuzungumza na mumewe, lakini mara zote amekuwa akielezea matukio ya siku nzima anayoyafanya awapo kazini kwake, na hana nafasi ya kumsikiliza. Mary amechoka pia kutokana na amri za mumewe na anataka kuwa huru.
Lakini Mary kwa upande mwingine anakosea. Anatakiwa awe wazi kwa mume wake na kumweleza yale asiyoyapenda ambayo mumewe huyo huyafanya aidha kwa kujua au kutokujua. Endapo angemshirikisha mumewe hali anayojisikia, ninafikiri kuwa asingekuwa na uamuzi wa kutaka kuwa huru, ili hali hiyo imsimtokee tena.
Kiongozi mmoja wa dini anasema kuwa hali kama hiyo kwa wapendanao ni kosa. Anahoji kuwa mtu anawezaje kumfanya mke wake kama mtumwa? Anasema hata kwa watu ambao hawajasoma hawawezi kuwa na tabia hiyo kwa wake zao. Anasema kuwa mume anatakiwa kumsikiliza mke wake kama mkewe anavyomsikiliza ndipo maisha yao yatakapokuwa na furaha.
Kuna wanaume wengi wenye tabia kama hizo, wanapenda kutoa amri na wanapenda mambo yafanyike kama wanavyotaka wao. Mara zote ndio wanaotoa maamuzi ya mwisho.
Kama mwenzako hatakuwa na mawasiliano mazuri nawe ni hakika utajisikia vibaya. Hali hiyo inamfanya mwanamke kukata tamaa na kuvunjika moyo. Ni vizuri ukamweleza ajirekebishe kwani wewe ni mke wake na anatakiwa akujali.
Inaonekana kuwa kama mwanamke ni mtumwa wa sheria za mumewe. Jaribu kuzungumza naye kuhusu hali hiyo ili irekebishike. Kama kusipokuwa na masikilizano ni hakika uhusiano huo utavunjika.
Kama ilivyoelezwa hapo juu, usiache kuongea naye kuhusu tatizo hilo juu ya tabia hiyo, inawezekana ana msongo wa mawazo katika kazi yake na hajielewi kama yuko hivyo.
Tukutane wiki ijayo.
lcyngowi@yahoo.comwww.ngowil.blogspot.com0713 3314550733 331455

MAANA YA UPENDO NA KUWA NA UPENDO

UPENDO unatofautiana kutoka moyo mmoja na mwingine, unaweza kuwa mzuri au mbaya. Kupenda na kupendwa ni viungo kamili vya furaha katika maisha, lakini inapotokea unampenda mtu asiyekupenda, hali hiyo itakuletea shida katika nafsi yako. Kwani kuwa ndani ya upendo ni sawa na tone la maji baada ya ukame wa miaka mingi.
Kijana Bright anasema kuwa, upendo hauchoshi, upendo ni mwema, hauna husuda, hauwazii mambo yako mwenyewe, hauna hasira ya haraka, hauhesabu makosa, upendo una nguvu kwa mambo yote yaliyofichika, una kuaminiana katika kila jambo, huamini yote na hauna mwisho.
Upendo hauelezeki tangu mwanadamu alipoumbwa, kwa hiyo tunatumia mioyo yetu na akili zetu katika maamuzi. Husababisha kupata hisia na msisimko katika mwili wako umwonapo mtu unayempenda. Katika upendo ni hali ya kawaida kuvutiwa kimaumbile na mwenzako awe mwanamke au mwanamume. Ni hali ya kawaida kwa kuwa suala la mahusiano linaanzia hapo. Upendo una heshima, hukufanya kumsaidia mtu katika hali zote za maisha yake, kumhifadhi kutoka kwa maadui, na kujua kuwa akili ya kila moja kati ya wapendanao ipo hapo kwa asilimia mia moja, kujisikia salama kwake, kujivuna unapokuwa naye, kushirikishana katika matarajio na ndoto za kila mmoja na mambo yote mazuri pamoja na kujihisi kama ni mshindi katika dunia.
Unapompenda rafiki yako hutasita kumwambia ukweli pale anapokosea. Pia kupatana naye pale mnapotofautiana. Ikitokea mmetofautiana kauli, mawazo au jambo lolote, ni vizuri kukaa pamoja na kuangalia chanzo cha tatizo ili muweze kutatua.
Mtu anayesema kuwa anawapenda wengine na kuwajali kuliko kujijali yeye mwenyewe, huo ni upendo. Unampenda mtu na kujaribu kumfanya awe na furaha, pia katika nafsi yako utakuwa na furaha. Upendo unaweza kuelezwa hivyo.
Kijana Julius anasema kuwa, anaamini upendo unaelezeka kwa njia nyingi na pia ana uhakika kuwa kuna aina mbalimbali za upendo unaouhisi kwa mtu. Inapotokea ukashindwa kula au kulala kutokana na mawazo unayomuazia mtu aliye maalumu kwako, ni hakika unakuwa na upendo halisi. Unapokaa kwenye kochi kwa ajili ya kupumzika wakati ukisoma kitabu au kitu kingine chochote na kuangalia chini, unaweza ukawa ukurasa wa kumi wa kitabu chako lakini kwa sababu akili yako inafikiri kuhusu mtu ambaye hujamwona ili kuondoa mawazo hayo unajikuta unarudia rudia kufungua kurasa mbalimbali za kitabu chako, au kama una miadi na huyo mtu unayemuwaza na kama mmeonana kwa mara ya kwanza, usiku huo tumbo lako litakuwa linakusumbua na ghafla utajikuta unaumwa kwa sababu ya hisia za upendo.
Julius anauelezea upendo kuwa ni ile hali ambayo huwezi kusubiri kumwona yule unayempenda kwa mara nyingine na kutafuta njia ya kuwasiliana naye, kama kuondoka nyumbani na kwenda kutafuta kibanda cha kupigia simu au kununua kadi ya simu ilimradi tu usikie sauti ya yule unayempenda kwa mara nyingine tena, na wakati mwingine mnapokuwa wote, unadiriki kumpa kitu chochote cha kula ili uendelee kuwa naye kwa dakika nyingine tano.
Unamwamini kwa moyo wako wote, una kuwa na uhuru naye ukiamini kuwa unaweza kuongea neno lolote mbele yake. Mnakuwepo pale kwa jambo lolote, bila kujali kama ni la kufurahisha au la huzuni. Jambo lingine ni kumshirikisha mambo muhimu ambayo siku moja unaamini itakuwa kumbukumbu ya kushangaza katika maisha yenu.
Kwa maelezo mengine upendo wa kweli ni pale mmoja anapomjali mwingine. Kumfanya mwenzako awe na furaha ni jambo la muhimu, upendo wa kweli unasimama katika usawa na ulinganifu katika jambo lolote linalohitaji uaminifu.
Upendo ni hisia, ambayo haiwezi kuelezeka. uhitaji uvumilivu. Ni mzuri. hauna husuda, haujivuni, haukosi adabu, hauchoki katika kufanya shughuli za kujitegemea. Hauna hasira, hauweki kumbukumbu mbaya. Upendo mara zote unahifadhi, unaamini, unatumaini. Mara zote upendo unahifadhi, unasema ukweli, unaamini na haushindwi.
Nini maana ya upendo na kuwa katika upendo? James anasema hafikirii kama yeyote anaweza kulijibu swali hilo. Bila shaka unaweza kuelezeka lakini kuuelezea vizuri ni vigumu kwa sababu upendo wa kila mmoja ni tofauti na wa mwingine. Upendo ni hisia ambao ni kwa watu wawili wanaohusika wanaelewa, na kama huelewi, yakupasa uendelee kusubiri. Usijaribu kutafuta maana ya kitu ambacho hukielewi. Upendo upo kila mahali, ni kitu kinachotafutwa na kueleweka, hakielezeki.
Kuna baadhi ya vitabu vinaeleza kuwa wasichana hawataki kuwa wajasiri tu, bali kuwa sehemu ya ujasiri huo ambao kwa wapendanao unakuwa na hisia za kuthaminiana. Wasichana wengi wanakuwa na mawazo mazuri ya kile wanachokitaka na inakuwa mara kwa mara.
Lakini inaonekana kwa nadharia kuwa upendo unawafanya wasichana wengi kukubali mabadiliko na mara nyingi wanakuwa imara kujifunza kwa mtu anayetaka kumwongoza, hali hii inakuwa tofauti kwa wanaume. Hali hii inawafanya kubadili kwa haraka tabia mbaya walizokuwa nazo awali na kuwa na uwezo mzuri wa kuishi na waume zao. Inafikiriwa kuwa wasichana wengi au wanawake wanakuwa na maisha ya kuvunjwa moyo kama hawajui njia yoyote, wanajikuta wanalazimika kutafuta njia ya kuwafanya waishi, kusimamia kila kitu katika maisha ya wapendanao, kwa mfano kwa mwanamume ambaye husababisha hali hiyo. Kwa hiyo wanakuwa wakarimu, wanajitoa ili kuwaridhisha wenzi wao, na kuonyesha uthamani wa upendo.
Lilly anasema anafanya kazi ya uuguzi, ambapo miaka yote ameona upendo umekuwa ukihitajika. Kwa mfano, amekuwa akifanya kazi nyumbani kwa mwanamke mwenye miaka 87, ambaye alikuwa haongei ila mara zote anatabasamu kwa kila mtu siku nzima anapokuwa pale. Mume wake, amekuwa mtu wa kelele, huenda mara chache kukaa naye na kwenda naye matembezi. Kutokana na kelele hizo si rahisi kwa mtu kukaa na mwanamke huyo, ila kutokana na upendo ndiyo maana yeye ameweza kukaa naye.
Wakati mwingine kwa wapendanao, busu moja linaondoa migongano iliyokuwepo baina yao. Inavunja kila kitu na kinyongo chochote ulichokuwa nacho, unajikuta katika dakika chache unasahau mahali ulipo, na wewe ni nani. Kwa dakika chache unajihisi vizuri kuliko ulivyowahi kusikia, migongano uliyokuwa nayo huisikii tena, wasiwasi unaoandoka. Kutokana na mguso mmoja wa hisia ulioupata kwenye kichwa chako, utajikuta imara, mwenye furaha kubwa na ya kudumu siku nzima.
Tukutane Alhamisi ijayo.
lcyngowi@yahoo.com www.ngowil.blogspot.com 0713 3314550733 331455

ELEWA JINSI YA KUUKABILI MSONGO

KARIBUNI wapenzi wasomaji katika safu hii tena leo.
Kwa wiki saba mfululizo tulikuwa tukiangalia maana ya msongo wa mawazo, vyanzo vyake, dalili zake na jinsi ya kutatua tatizo hilo linapokukabili.
Leo tumefikia tamati katika mada hii, tutamalizia kwa kujibu swali moja kati ya mengi tuliyotumiwa kwenye safu hii.
Swali hilo ni kwamba, baba mmoja alipatwa na msongo wa mawazo ambao ulimsababishia kupooza, lakini kwa bahati nzuri ametibiwa, anaendelea vizuri. Kwa maelezo ya baba huyo, hali hiyo imempata kutokana na mkewe kumsababishia msongo kwa makusudi, kutokana na kumnyima unyumba, kutotimiza wajibu wake ama kumfanyia jeuri tu.
Anauliza, afanye nini ili kuepuka hali hiyo ambayo inahatarisha uhai wake? Anasema anafikiria kuvunja ndoa lakini anakumbuka athari zake zitaathiri watoto na yeye bado anahitaji msaada kutoka kwa mkewe.
Pole sana ndugu yangu kwa yanayokusibu. Kumbuka hali unayokabiliana nayo wewe si wa kwanza kukutana nayo, ila kinachotakiwa, uwe jasiri katika hali hiyo bila kusahau kumshirikisha Mungu.
Kwani wengi waliochukua uamuzi wa haraka bila kuwashirikisha ndugu, jamaa au rafiki zao wamejikuta wakijutia uamuzi huo.
Vile vile njia nyingine nzuri ni kuzungumza na ndugu, rafiki, kiongozi wa dini au daktari wako juu ya matatizo yanayokusibu. Hali hiyo itakusaidia kupunguza msongo unaokukabili.
Kwa kufanya hivyo itakusaidia, kwani marafiki na familia yako wanaweza wasijue kuwa unakabiliana na kipindi kigumu, watakapoelewa watafanya jitihada za kukusaidia.
Pia si vibaya ukisoma vitabu mbalimbali vinavyoweza kukusaidia, tazama filamu, video na kuhudhuria kozi mbalimbali juu ya hali uliyonayo.
Soma vitabu vizuri vya siasa, literature, jamii, historia pamoja na vitabu vinavyoelezea matatizo mbalimbali ya kijamii.
Lakini waweza kuishi maisha ya kawaida bila kuwaza mambo makubwa, hasira, au hali ya hofu. Usimdharau mke wako pamoja na yote anayokutenda. Atajisikia aibu na kubadilika.
Jitahidi kuwa na uhusiano mzuri wa kirafiki na mke wako, itakuongezea furaha na maisha mazuri katika familia, mke wako na wewe mwenyewe.
Katika kipindi unachokipitia, unaweza tu kujaribu kwa kudhibiti mihemko pamoja na hisia zako. Kitu muhimu ni kukuza ‘hobby’ yako na kutumia muda wako mwingi katika hiyo. Kuwa mbunifu wa kazi kama usanii, muziki, dansi, ushonaji, ufundishaji na kuelekeza nguvu zako zote na vipaji katika mambo hayo.
Hata kama hutaweza kufanya kitu kingine chochote, utaisikia nafsi yako ikikuelekeza katika kazi za jamii. Kuwa na kusudi sahihi na malengo katika maisha yako. Fanya baadhi ya mabadiliko katika aina yako ya maisha uliyozoea kuishi.
Kula vyakula vyenye chumvi kidogo visivyokuwa na joto kali, pamoja na viungo vingi. Kataa kitu chochote kitakachokufanya usisimke au kukupa mhemko. Usitazame picha za x, pamoja na kusoma vitabu vitakavyo kusababishia msisimko katika mwili wako.
Idadi kubwa ya barua zinazoandikwa kwa washauri mbalimbali wa saikolojia katika magazeti ni kutoka kwa wanawake ambao hawapendelei matendo ya kimapenzi wanapokuwa na waume zao, kutokana na mahusiano mapya na watu wengine ambapo kwa sasa wanalipa gharama kwa ajili yao. Wanatafuta muafaka katika mambo magumu wanayopitia, kuwa njia panda katika maamuzi, kuwa na hatia ambayo matokeo yake ni kutokana na mahusiano mapya ya kimapenzi na mtu mwingine.
Wanasaikolojia wanachambua mabadiliko yanayowapata waume zao kuwa katika kadhia na kuhisi uadui, kudhamiria jambo baya, huzuni, wasiwasi au hasira kwa wake zao katika hali iliyofichika katika akili zao. Hisia hizo zinakuwa na mizizi ya siku nyingi, wakati waume zao wamekuwa na uchungu juu ya wake zao, na hali hiyo inakuwa haijawekwa wazi.
Wanawake wengine walio na uhusiano nje ya ndoa zao, wanakuwa hawana ari ya kutenda jambo na waume zao.
Kama mke atakuwa hana hamu na tendo la ndoa, waume zao huanzisha uhusiano mwingine. Katika jamii zetu sheria haziwi kali kwa wanaume kama zinavyokuwa kwa wanawake wanapotoka nje ya ndoa zao.
Kamwe usimdharau mumeo endapo itatokea ongezeko la kazi katika kampuni aliyoko hata kukosa muda wa kuwa na familia yake kama ilivyokuwa awali, anapopatwa na mawazo, udhaifu, ugonjwa au hali yake kubadilika kutokana na ratiba yake ya ofisini kubana, hivyo kushindwa, kuwa na mkewe katika matukio mbalimbali, kumridhisha mkewe kimapenzi, kamwe usithubutu kumdharau kutokana na hali hiyo au umri mkubwa.
Kwa maelezo mengine, mtie moyo mume wako ili aweze kukushirikisha hisia na mawazo yake ili aweze kukufikiria kama rafiki wake wa karibu anayemtegemea katika maisha yake.
Hivyo basi, si vema wala busara kuivunja ndoa yako kutokana na hali ya kukuvunja moyo katika familia yako unayokutana nayo.
Jitahidi kumuenzi mkeo, familia yako na kuiokoa ndoa yako kwa gharama zozote. Kamwe usilipize kisasi kwa mkeo hata kama anakufanyia mambo mabaya ili umuache.
Ijenge familia yako kwa kuwa na muda wa kutosha na watoto wako katika kipindi kigumu unachopitia. Kama ni watoto wenye upeo wataweza kukupa furaha zaidi kwa kujifunza kushirikishana matatizo yanayowakabili na wewe baba kuwaeleza yale matatizo yanayokukabili juu ya kazi na masomo hivyo wote mtatafuta njia nzuri ya kurekebisha mambo.
Ushirika wa baba, mama na watoto katika familia ni muhimu. Unazilinda nyumba nyingi zilizoanza kuweka nyufa.
Tukutane wiki ijayo katika mada mpya.
lcyngowi@yahoo.comwww.ngowil.blogspot.com0713 331455

VITU VINAVYOWEZA KUBADILISHA MSONGO WA MAWAZO

KARIBUNI wapenzi wasomaji katika siku nyingine tena. Leo tunaendelea na mfululizo wetu wa kuangalia jinsi ya kukabiliana na hali ya msongo wa mawazo uliyonayo.
Kwa kuwa kila mmoja wetu ni tofauti na mwenzake, hakuna njia moja ya kuweza kukabili msongo wa mawazo. Hata hivyo, kuna idadi ya vitu mbalimbali ambavyo vinaweza kuondoa mawazo hayo yanayompata mtu. Ambavyo vinaweza kuchukua muda mrefu au muda mfupi, kupunguza msongo unaokukabili.
Kwanza ni vizuri ukajua matatizo yako yanayokukabili. Kama ni kazi yako, uhusiano wako na mtu fulani, au masuala ya kiuchumi yanayokufanya kuwa na mawazo. Pale unapojua uhakika wa tatizo lako, unaweza kufanya kitu cha kukusaidia ili kuondokana nalo.
Tatua matatizo yako kwa kuanza kufikiria jinsi ya kuyapatia muafaka. Utafanya nini kama utakuwa na msongo juu ya hitaji la kazi, au ushauri katika ndoa yako, au unahitaji ushauri wa mtaalamu wa uchumi aweze kukueleza jinsi ya kutumia fedha zako? Nini kitatokea kama hautafanya chochote? Kama utafuta njia za kuondoa tatizo hili, utakuwa na uwezo wa kufanya baadhi ya mabadiliko ya kuondoa mawazo na hali ile ya wasiwasi inayokukabili. Njia hii ndefu ya kupunguza mawazo katika maisha yako kwa kila mmoja, mapema au kwa haraka, itafanikiwa.
Zungumza kuhusu matatizo yako. Utakuta inakusaidia kuzungumza kuhusu msongo wako. Marafiki na familia yako wanaweza wasijue kuwa unakabiliana na kipindi kigumu. Mara watakapoelewa, wanaweza kukusaidia katika njia mbili. Kwanza, kwa kukusikiliza na pili kwa kuangalia uwezekano wa kutatua matatizo yako. Kama utahitaji kuzungumza na mtu mwingine aliye nje ya marafiki na ndugu zako, daktari wa familia yenu anaweza kukusaidia kwa kukuelekeza kwa mshauri wa afya katika masuala ya akili.
Jifunze jinsi ya kutawala msongo. Kuna vitabu vingi vinavyosaidia, filamu, video na kozi mbalimbali ambazo zitakuwezesha kukabiliana na hali uliyonayo. Pia wapo washauri ambao wamebobea katika masuala ya msongo wa mawazo, muulize daktari wako wa familia kwa maelekezo zaidi. Pia kuna kozi katika vyuo vingi vya jumuiya na jinsi ya kutawala msongo unaokukabili, katika jamii inayokuzunguka.
Punguza hali ya wasiwasi inayokukabili. Shughuli mbalimbali unazozifanya zinaweza kuwa msaada mkubwa kwako wa kupunguza msongo. Fanya matembezi, cheza michezo mbalimbali, lima bustani, fanya usafi ndani ya nyumba. Utakuta inakusaidia sana katika kuuweka mwili wako katika hali ya kuchangamka. Pia hali ya kupumua taratibu (kuvuta pumzi kutoka ndani ya tumbo), bila kuruhusu pua zako kuvuta hewa halafu kuitoa pumzi kwa nguvu kupitia mdomoni. Mazoezi mengine ni kujinyosha na kupumzika katika kila kiungo katika mwili wako, kwa kuanzia shingo yako na kuishusha chini.
Kama utakuwa na tabia la kupuuza hali mbalimbali zinazokusababishia msongo, kwa kujiongoza mwenyewe vile unavyotaka, utajikuta huna tatizo la msongo na mwepesi wa kutatua hali hiyo ambayo mwanzoni bila kufahamu ilikusababishia kupata msongo.
Usiruhusu akili yako kushikilia matatizo uliyonayo. Unaweza kuondoa hali hiyo kwa kujishughulisha. Kama unajihusisha na michezo mbalimbali au kazi, unaweza kuipa akili yako mapumziko kutoka kwenye msongo uliokuwa nao. Kutokufikiria matatizo yako kwa muda kunaweza kukupa wepesi katika kutatua hali hiyo kwa mapema.
Jinsi ya kuzuia msongo.
Mara utakapofanikiwa kupunguza hali ya msongo uliyokuwa nayo, ni busara kuangalia njia za kuzuia msongo usijirudie tena. Njia rahisi ya kukabiliana nayo ni kuzuia. Baadhi ya njia nzuri za kufanya hivyo ni:
Kufanya maamuzi. Maamuzi hayo yasikuletee hofu na baadaye msongo.
Epuka kudharau baadhi ya vitu vyako. Unatakiwa kuwa na ratiba yako ya wiki, ambayo itajumuisha shughuli za starehe pia kusikiliza nyimbo mbalimbali.
Ushirikiano. Waachie wengine wafanye shughuli zile uzifanyazo ili kuepuka hali ya kufanya kila shughuli wewe mwenyewe.
Kumbuka, haiwezekani kuwa na maisha yasiyo na msongo. Malengo yako lazima yaepuke kuwa katika daraja la msongo ambapo nguvu yako uliyonayo inanyonywa.
Je, unahitaji msaada zaidi? Kama kuna mtu unayemfahamu na ambaye ameathirika sana kwa msongo wa mawazo, wasiliana na jamii inayokuzunguka kama kikundi cha afya ambacho kitaweza kukusaidia kukutafutia msaada zaidi.
Mara zote jitahidi kuondoa hali hiyo inapokupata. Utafanyaje endapo utakabiliana na hali hiyo? Njia muhimu itakayoweza kukusaidia kuondokana na hali hiyo, ni kujifunza jinsi ya kuidhibiti hali hiyo ambayo inakuja katika changamoto mpya, kwa uzuri au kwa ubaya.
Usijione kama wewe umekamilika katika kila kitu kwani hakuna aliye kamili. Na unapowatarajia wengine kuwa ni bora kuliko wewe, inakuongezea hali ya msongo, kama unahitaji msaada wa kitu chochote omba msaada kwa wengine.
Jitahidi kupata usingizi mzuri. Kuwa na muda mzuri wa kulala, kunaufanya mwili na akili yako kutulia, kuwa na maamuzi thabiti pamoja na kudharau misongo inayokuletea madhara. Kama utakaa muda mrefu usiku bila kulala na unahitajika kuamka asubuhi kuwahi kazini au shuleni, huwezi kupata muda mzuri wa kulala unaotakiwa, hivyo itakuletea athari.
Jifunze kupata muda wa kupumzika. Muda huo uwe unasoma kitabu, unasikiliza muziki, unaangalia luninga au unaoga na kuupumzisha mwili wako baada ya shughuli za siku.
Utunze mwili wako vizuri. Wataalam wanaamini kuwa kupata mazoezi ya kawaida kunasaidia watu kupunguza mawazo. Pamoja na kula vizuri kuwezesha mwili wako kufanya kazi yake vizuri. Kumbuka mwili unahitaji virutubisho mbalimbali. Ingawa vileo au dawa za kulevya zinaelezwa kuwa zinapunguza msongo kwa muda, ukweli ni kwamba zinazidisha tatizo kwa sababu zinaufanya mwili uchoke na kushindwa kufanya kazi yake vizuri.
Mara zote jitahidi kutatua matatizo ya kila siku ambayo unaweza kuyakabili, lakini kuyaepuka kutakusababishia hali ya kujiona unashindwa na hatimaye kuibuka tatizo kubwa zaidi.
Tukutane tena Alhamisi ijayo .
lcyngowi@yahoo.comwww.ngowil.blogspot.com 0713 3314550733 331455

JINSI YA KUPUNGUZA MSONGAMANO WA MAWAZO

KARIBUNI wapenzi wasomaji wetu katika safu hii ya kila Alhamisi. Leo ni mwendelezo wa pale tulipoishia. Tutaangalia njia mbalimbali za kupunguza msongo wa mawazo.
Ili kupunguza msongo wa mawazo unatakiwa kupangilia muda wako kabla ya kuangalia e-mail yako au kusoma meseji kwenye simu yako, kabla hujaruhusu ulimwengu kuingilia himaya ya akili yako au ubongo wako.
Utakapofanikiwa katika hilo simama na jinyooshe au tenga dakika tano za mawasiliano. Bada ya hapo iwapo utakaa chini huenda ukawa umepata eneo la kuanzia.
Usiache kuyapa mambo yako kipaumbele cha kwanza, kwani ni muhimu, kama hutafanya hivyo utajikuta unakabiliwa na ufinyu wa muda. Ukipangilia mambo yako vizuri utajikuta unapata muda wa kuonana na rafiki zako wazuri kila ifikapo mwanzo wa mwezi.
Jipe ruhusa ya kurekebisha uhusiano unaolegalega pamoja na mambo mengine ambayo yanakuumiza.
Fanya yaliyo mazuri na jitahidi kuondokana na mambo ambayo yanakuweka katika hali isiyo nzuri. Hii ni muhimu, kwa sababu tunapofanya kile kilicho kizuri, ufanisi wa kazi utakuwa katika kiwango kizuri pia.
Siku zote iruhusu akili yako kutambua kuwa baadhi ya mawazo mazuri tuwazayo huja pale ambapo hatuna kitu cha kufanya na tunapokuwa tumeruhusu akili kupumzika. Sanaa za wakati huo zimesahaulika.
Mambo yote hayo hugusa mtu fulani na unaweza kuhisi hilo na kujikuta ukitambua kuwa umefanikiwa kwa hilo hivyo utatakiwa kufuata mambo hayo mazuri ili uweze kuwa mtu mwenye furaha na kuwafanya wengine pia wawe watu wa furaha. Ni jambo linaloweza kuwa na madhara fulani iwapo utakuwa mtu mwenye malengo makubwa lakini hutaki kuruhusu akili yako iyafanyie kazi.
“Mara zote baba yangu alinishauiri nifanye yafuatayo aliponiona nina shughuli nyingi.
Aliniambia mwanangu, unatakiwa angalau ule mlo wako kwa wakati na baada ya kula chakula chako cha mchana au usiku, unatakiwa kupata muda wa kuwa peke yako na nafsi yako kwa dakika chache. Sasa kama utakuwa na muda mzuri wa kujiuongoza na kutumia kila sekunde katika maisha yako, unaweza pia kujaribu kusoma baadhi ya vitabu wakati unapata mlo wako.
Bill Gates na watu wengine pia wamekuwa wakifanya biashara kubwa kuliko wewe. Sifikirii kama wanakuwa na shughuli nyingi kama wewe. Na iwapo watakuwa hivyo yawezekana wakawa watu wabunifu ambao wanaibua mawazo ya kibiashara. Iwapo hawaonekani kubanwa zaidi na kupata kipato kikubwa zaidi, basi ujue kuwa wewe si mzuri na makini katika kusimamia na kudhibiti muda wako kwa ufanisi.
Tumia baadhi ya muda kwa jamii, familia, ndugu na marafiki. Unaweza ukapata baadhi ya mawazo ya kibiashara kama ya kuchochea akili yako. Pangilia muda wako. Utajikuta unapata vitu vingi vipya.
Nini cha kufanya unapokuwa na msongo wa mawazo? Hizi ni mbinu za kukuwezesha kuudhibiti msongo wa mawazo kabla ya msongo huo haujakudhibiti. Nitajaribu kukuonyesha njia za ufumbuzi za zamani na zile za kisasa
Mfumo wa ulaji:Ufumbuzi wa zamani:
Chakula kimekuwa ni moja ya wapambanaji wakubwa wa msongo wa mawazo. Baada ya siku iliyojaa kazi nyingi unarudi nyumbani na unajikuta ukiishia kula mikate. “Watu wengi hupendelea kula vyakula vya wanga kwa sababu husaidia mwili kuwa na nafuu na hivyo kupumzika kwa urahisi,” anasema Lisa Dorfman ambaye ni mtaalamu wa chama cha walaji na matokeo ya vyakula nchini Marekani.
Ufumbuzi mpya:
Lakini ipo nji anyingine ya kupambana na msongo wa mawazo mbali na mfumo wa ulaji na unywaji. Waweza kufanya hivi, badala ya kujirundikia mikate, oga maji ya moto au yanayotiririka katika bomba la juu bafuni ‘shower’ na kisha pumzisha misuli na akili yako. Au lala chini na upumue kwa utulivu. Kama utaamua kula, fanya uamuzi huo kwa kudhamiria. Jiulize nafsi yako: Nini matokeo ya jambo hilo? Faida zake? Baada ya kujibu maswali hayo, utajikuta uko katika hali nzuri.
Iwapo umegombana na mwenza wako:
Ufumbuzi wa zamani baada ya mapambano na mwenza wako, unaweza kutoka nje ukaingia katika gari lako na kuondoka maeneo ya nyumbani. Hii inaweza kukusaidia kwa kuruhusu hasira zipoe ana uondokane na mawazo ambayo yangesababishwa na wewe kuona mazingira ambayo mligombana na mwenza wako.
Iwapo huna namna ya kuondoka nyumbani unaweza kuwasha TV yako na kuangalia mambo ambayo yatavuta akili yako kiasi cha kukusahaulisha yaliyotokea na hii huenda ikawa njia nzuri zaidi kuliko hata ile ya kulala.
Ufumbuzi mpya:
Ili kupunguza hisia za msongo wa mawazo unaokulemea, zungumza na rafiki yako wa karibu, andika majarida, fanya matembezi yatakayokuchangamsha, au pata aina nyingine ya mazoezi. Kama akili yako itaanza kufikiri baada ya kuipumzisha, chukua kitabu usome ili kuikimbia hali hiyo.
Iwapo unakabiliwa na madeni:
Kama una uwezo wa kwenda katika masoko ambayo huruhusu kununua kwa mkopo litakuwa jambo zuri zaidi, kwani utapata mahitaji yako na kisha utafikiri jinsi ya kupata pesa za kulipia mahitaji hayo baadaye.
Njia hii ya ununuzi ni nzuri zaidi na hukufanya uwe mtu wa haiba nzuri siku zote na inashauriwa kuwa uitumie hata uwapo na pesa. Mbali na kufanya ununuzi wa kununua kwa mkopo, waweza ukaamua kupangilia ununuzi wa mahitaji yako kwa wingi lakini kwa wakati mmoja.
“Matumizi katika manunuzi ni jambo ambalo litakusaidia kuondokana na msongo iwapo utalipangilia ipasavyo,” anasema Dk. James Roberts, mtafiti wa matumizi ya majumbani kutoka chuo kikuu cha Baylor.
Ufumbuzi mpya:
Iwapo umegundua kuwa kufanya manunuzi ya mahitaji yako hukufanya ujisikie vyema, jaribu kuepuka hali au mazingira ambayo yatakufanya uhitaji kuwa na maamuzi.
Jaribu kufanya jambo jingine kwanza: Inaweza kuendesha baiskeli au pikipiki au hata fanya mazoezi ya kukimbia kwa muda mfupi. Afya ya ubongo inaweza kukusaidi namna ya kushughulika na tabia zako. Na unaweza kuonana na washauri wa masuala ya kifedha ili uweze kudhibiti mfumo wako wa kifedha.
Tukutane wiki ijayo
lcyngowi@yahoo.comwww.ngowil.blogspot.com0713 3314550733 331455

MABADILIKO YA KIMAUMBILE NA MSONGO WA MAWAZO

Karibu mpenzi msomaji wa safu hii. Leo tutakaangalia jinsi ya kumsaidia mtoto, mambo yanayokupata, hali za kimaumbile na kihisia unazokabiliana nazo uwapo na msongo wa mawazo. Endelea nami pale ulipoishia wiki iliyopita.
UNAWEZA kumsaidia mtoto wako aweze kukabiliana na msongo wa mawazo kwa kuongea naye juu ya mambo yanayoweza kusababisha hali hiyo, ili aweze kuelewa. Ninaamini kuwa kwa pamoja, mnaweza mkapata baadhi ya njia zitakazoleta ufumbuzi kwake.
Baadhi ya majukumu anayokabiliana nayo mtoto, yanaweza kupunguzwa baada ya kutoka shuleni, pia ni vizuri kama atatumia muda wake mwingi kuzungumza na wazazi au walimu wake. Pia awe anafanya mazoezi ya viungo kama kwa kucheza michezo mbalimbali, au unaweza kupanga safari na kwenda.
Pia unaweza kumsaidia mtoto wako kwa kumwandalia kwenda kwenye warsha au mafunzo ambayo yatamwezesha kukabiliana na hali hiyo. Pia umpe uhuru aweze kujua muda atakaoweza kumwona daktari kwa ajili ya kuzungumza naye juu ya hali hiyo.
Kumbuka baadhi ya misongo ni hali ya kawaida, hivyo mwache mtoto wako aelewe kuwa si jambo la ajabu kuwa na hasira, kushtuka, upweke, au hali ya wasiwasi. Mwache ajue kuwa watu wengine nao wanapatwa hali kama hiyo siyo yeye peke yake.
Jinsi ya kushughulika na mtoto aliyepatwa na msongo wa mawazo Wakati watoto wanapatwa na shida katika kuzungumzia hali hiyo, itasaidia utakapozungumza na mtoto wako kuhusu mambo yako mwenyewe yanayokushughulisha. Hii itamsaidia kuona kuwa uko tayari kuzungumza naye kuhusu mambo yako unayokabiliana nayo, hali hiyo itamwezesha naye kujihisi utayari wa kuzungumza nawe jambo lolote linalomtatiza.
Kama mtoto wako ataendelea kuwa na hofu na kushindwa kuzungumza nawe kama mzazi wake, njia nyingine ya kumsaidia ni kumtafutia mshauri mwingine au daktari aliyebobea katika masuala hayo na kuzungumza naye.
Wazazi wengi wana uwezo wa kujua mawazo yanayowapata watoto wao, ikiwamo wakati wanaposoma na kukosa muda wa kupumzika. Mzazi kama utashindwa kukabiliana na hali inayomsumbua mtoto wako baada ya kufanya jitihada mbalimbali, mwone daktari wa mtoto wako, zungumza na washauri pamoja na walimu pale mtoto wako anaposoma. Baada ya kuzungumza nao, watakuwezesha kujua ukutane na mtaalamu gani ili aweze kumsaidia mtoto wako.
Tukiachana na jinsi ya kumsaidia mtoto wako ili aweze kukabiliana na msongo anaokuwa nao, pia kuna mabadiliko mbalimbali ya kimaumbile kwa mtu mwingine yeyote anapokuwa na msongo wa mawazo.
Mwitikio wa kimaumbile katika hisia kali uliumbwa ili kuweza kutuokoa katika siku zile ambazo watu waliishi katika mapango. Kwa mtu wa Zama za mawe, mwitikio wa kimaumbile uliojulikana kama ‘ruka au pigana’ ulimwandaa kwa ajili ya jambo lolote.
Mwitikio huo ulikuwa ni muhimu sana kwa matukio yaliyokuwa yakitokea mara chache pale alipokuwa akikimbizwa na wanyama wakali kama vile chui au alipokuwa akifanya mawindo kwa ajili ya chakula. Kwa sasa baada ya mamilioni ya miaka kuwa yamepita, bado mwitikio huo una visababisho sawa na vile vya wakati ule, lakini ni matokeo ya mibinyo tunayokumbana nayo katika maisha ya kila siku.
Ni kitu gani kinachotokea katika miili yetu tunapokuwa na msongo wa mawazo? Tunajikuta tunapatwa na shinikizo la damu, tunapumua kwa nguvu, masikio, macho na pua zetu zinakuwa na tahadhari mara zote. Mabadiliko haya ni matokeo ya kemikali zinazokwenda kwenye damu na kusababisha msongo kutokea.
Wakati unapoendelea kuwa na mawazo kwa muda mrefu, au yanapotokea mara kwa mara na kwa wakati mbaya inachangia kuwepo kwa hisia mbaya. Mwanadamu anapata onyo la kutoka kwenye ubongo ambalo linamwambia acha na upumzike.
Wakati tunapokataa kuchukua ushauri kutoka kwenye ubongo, inatuletea matatizo katika miili yetu. Hali hii inatofautiana kati ya mtu na mtu.
Ni jinsi gani mwonekano wako unavyoathirika?Baadhi ya watu wanaonekana kuishi katika maisha yenye mambo mengi ya kimitindo. Wengine wanaonekana kuwa na misongo kwa kiwango kidogo. Wote tuko kipekee kutokana na jinsi tunavyoshughulikia msongo. Kwa hakika msongo hautokani tu na yale yanayotusibu, lakini pia hutegemeana na jinsi tunavyofikiri.
Wanasaikolojia wanasema kuwa haiba tofauti hutenda tofauti na kukabiliana na msongo kwa njia tofauti. Kundi A la haiba ni wale ambao huwa na haraka katika mambo fulani, washindani na walio makini na hao ni wepesi wa kukumbwa na msongo. Kundi B la haiba ni wale ambao hawaonekani kujali sana, huchukulia kila jambo kama la kawaida tu hata kama ni kubwa kiasi gani. Hawa ni rahisi kukabiliana na msongo.
Kwa upande mwingine tuangalie tabia za kimaumbile katika msongo wa mawazo. Tabia hizo husababisha mtu kuogopa sana hadi kusababisha maumivu ya tumbo, kukosa hamu ya kula, kupatwa na maumivu ya kifua, kuharisha, kukondesha watoto, kukauka midomo, kutoka mkojo mara kwa mara, kuumwa kichwa, chakula kutokusagika vizuri tumboni, kukaza kwa misuli, kuwa na tahadhari ya mara kwa mara, mapigo ya moyo kupiga kwa nguvu bila kutegemea, kutopata usingizi, kutoka jasho jingi na kupatwa na maumivu yasiyoelezeka.
Tabia za kihisia unapokuwa na msongo wa mawazo. Mtu hujikuta kuwa na mabadiliko makubwa ambayo huchangia kuongezeka kwa wasiwasi, kero na kuwa na hali ya kutoeleweka. Hujikuta mambo madogo madogo yamkasirisha mara kwa mara na kumfanya ashindwe kuwa mstahamilivu.
Kwa mfano, ukweli ni kwamba watoto wanataka kucheza mchezo kwenye luninga, na wakati huo ndiyo kwanza umerudi nyumbani kutoka kazini, na unachotaka kukifanya ni kukaa na kunywa kinywaji chako huku ukiangalia luninga, kutokana na hali uliyonayo inakukusukuma kuwaondoa watoto wako na kukaa mwenyewe.
Pia kunakuwa na mabadiliko ya kutokuwa na hamu ya kula na wakati mwingine uzito kupungua. Baadhi ya watu wanakosa hamu ya kula, wengine wanakula kawaida. Uwezo wako wa kuendana na mazingira ya kazini na nyumbani unaweza kuwa tofauti, na unaweza kujikuta kuwa huwezi kulipa Ankara zinazokukabili lakini mambo huwa mabaya zaidi pale ambapo unakuta simu yako imekatwa kutokana na deni, ubongo wako unakuwa unawaza mambo tofauti na kukuongezea msongo. Unaanza kuvuta sigara au kunywa pombe au vyote kwa pamoja, hali ambayo unafikiri inakupunguzia mawazo, unapokuwa unakosa usingizi usiku.
Hali ya kihisia inayokupata unapokuwa na msongo wa mawazo. Unakuwa na hali ya kuhangaika au sononeko, unajikuta huwezi kufanya maamuzi, siku zote anakuwa na hofu au hali ya kutishika, hofu ya kutokea kuzimia au kuanguka, kusikia hali ya kupatwa na shinikizo la damu, kuhisi ubongo umekauka, kuhisi wasiwasi na kushindwa kupumzika, kuhisi kutoelewana na watu, kupatwa na msukumo wa kutaka kukimbia au kujificha, kuongeza majonzi pamoja na kuwa katika hali ya kutokutulia, na kutokuwa na uwezo wa kuwa makini na jambo.
Tukutane wiki ijayo.
lcyngowi@yahoo.com0713 331455/0733 331455

Twitter Facebook