KARIBUNI wapenzi wasomaji katika siku nyingine ya leo, ambayo Mwenyezi Mungu ametujalia kuiona tena. Tunakwenda kuangalia hali ya msongo inayowakabili watoto pamoja na vijana wadogo.
Ni ukweli usiopingika kuwa hali ya msongo inakuwepo katika hatua zote za maisha ya binadamu. Tunaona watoto wengi wenye umri wa miaka mitano na kuendelea, wamekuwa wakiona vitu mbalimbali katika nyumba zao ambavyo hufanywa na wazazi wao.
Kwa mfano, kuna familia nyingine kila mara wazazi hugombana mbele ya watoto wao. Kama wazazi tuelewe, hali hiyo huleta hofu kwa mtoto na kuona kuwa baba au mama yake anaweza kumpiga wakati wowote. Wakati mwingine unakuta mzazi anaumwa na jino, maumivu anayoyapata anayaonyesha mbele ya mtoto wake, hali hiyo humjengea hofu.
Kwani kuanzia hapo, inawezekana kabisa, mtoto huyo akapatwa hali ya woga na hofu, juu ya meno yake. Hata pale atakapoumwa atalia na maumivu makali. Tukiachana na hofu hiyo, hofu nyingine kwa watoto ni pale wanapomuona daktari au hospitali.
Inawezekana kwa wakati huo, mtoto haumwi lakini, anapomuona daktari akiwa amebeba sindano au vifaa vya hospitali,akiwa anatembea maeneo ya shuleni ama sehemu yoyote, hata kama daktari hana mpango wa kuongea na mtoto huyo, mtoto hubadilika muda huo huo, wengine huanza kulia.
Hivyo, kwa haraka haraka utaona ni jinsi gani mtoto anakuwa hajaandaliwa kukabiliana na mazingira mbalimbali ili asikabiliwe na hali ya wasiwasi katika maisha yake. Kuna maeneo mawili ambayo watoto hupatwa na hali ya msongo katika maisha yao, ambayo dalili zake huonekana kwenye maumbile ama tabia zao.
Tukiangalia kwenye dalili za kimaumbile, ni kama vile kupatwa na gesi tumboni, kupatwa na hali ya ubaridi kwenye viganja vya mkono na unyayo.
Hali ya kukosa choo, kuharisha, kukaukiwa midomo, uso kubadilika, tumbo kuvurugika, mikono kutetemeka, kichwa kuuma, moyo kudunda pamoja na kutokwa na jasho.
Nyingine ni mtoto kuuma kucha zake, kuwa na hofu, uso kuwa na mafuta, hali ya kutetemeka, kupumua kwa shida, kutokwa na jasho mikononi na miguuni, meno kukakamaa, kukaza kwa misuli, kukaza kwa tumbo na macho kuwa mazito.
Kwa upande wa dalili za tabia ni kama vile, kupata ajali na kuanguka kwa kuelekea mbele, kupenda ugomvi, kujilinda, kuwa tegemezi, kushituka shituka, kuwa na hofu, kutopenda kuwasiliana na watu, kuumwa mara kwa mara na kuchoka, kujiamini kupita kiasi, kuwa na hisia zilizopitiliza, kutopenda kujishughulisha na kitu, kukosa nidhamu, utukutu, mwenye mambo ya kuficha ficha, kukata tamaa haraka na kutokuwa na ushirikiano.
Pia anakosa utulivu wa kusikiliza jambo, anakuwa na tatizo la mara kwa mara la kulala na kuota ndoto za kuzungumza kwa sauti, hupenda kuzungumza uongo ama kupotosha ukweli, anachukulia vitu kama si vya kwao, maendeleo yake ya shule hushuka, anakuwa na mwonekana mbaya pamoja na umaridadi wake kupungua, anakosa hamu ya kupenda kujua vitu bila sababu ya msingi, ana kuwa na mabadiliko katika ulaji wake wa chakula, anaweza kula chakula kidogo ama kingi sana.
Mzazi ama mlezi huweza kubaini mabadiliko hayo kwa mtoto, kama anakuwa na uhusiano wa karibu na mtoto huyo.
Pia ni vizuri pale unapobaini mabadiliko hayo, uendelee kuwa karibu zaidi na mtoto huyo. Ni vizuri kumuandalia mlo uliokamilika, wenye virutubisho vyote, mpe nafasi ya kufanya mazoezi na kupumzika, mtie moyo aweze kusaidia shughuli ndogo ndogo na kumpa vichekesho.
Pia ni vizuri kuwaruhusu watoto wazungumzie mambo yale yanayo wakosesha raha, kwani wakati mwingine watoto waliokuwa kidogo hali hiyo husababishwa na kujiingiza katika mahusiano baina ya watoto wa kike na kiume.
Kwa upande wa wale watoto wenye umri kati ya miaka 9 na 20; mara nyingine hupatwa na hali ya msongo kutokana na umri huo, kwani hudhani kuwa wanaweza kujitawala wenyewe kwa kila jambo, hujihusisha kwenye mahusiano yasiyofaa, na wanapoonywa hufikiria kuhama nyumbani na kuwaacha wazazi wao.
Kipindi hicho, wazazi nao hupatwa na msongo kutokana na kitendo cha watoto hao ambao kuwa na maamuzi yao wenyewe, hali inayowafanya waondoke nyumbani. Wazazi huwaza kwa kuona watoto bado wanahitaji msaada kutoka kwao.
Hivyo, ni jukumu la wazazi kutumia nafasi hiyo kuwaelimisha watoto wao, kuwa vile wanavyofikiri sivyo maisha yalivyo. Pia wazazi wanapogundua mabadiliko mbalimbali juu ya watoto wao, ni vema kuchukua hatua za haraka na kuwasaidia kuliko kuwaacha wakaharibikiwa.
Mara nyingi wazazi wanaowafuatilia watoto wao, hugundua mapema kuwa, watoto wameshuka kimasomo ama hawapendi kwenda shule, ama mtoto kwa kipindi hicho badala ya kuwaza kusoma anafikiria kuacha shule na kufanya kazi.
Watoto wengine hukatiza kozi wanazozisoma, si kwa sababu wamekuwa hawafanyi vizuri bali ni kutokana na kutaka kuwa na ushindani wa kupata maisha bora, wakati anakuwa hajamaliza hata masomo yake. Kwa upande wa watoto wa kike, hali hiyo huwafanya kupata mimba wasizozitarajia, ama kuwaza kujiua.
Wengine hujiingiza kwenye ulevi ama mihadarati. Lakini kwa kufanya hivyo hawawezi kupata suluhisho, hivyo ni vema watoto wanapokumbana na hali hiyo kuidharau na kuendelea na masomo yao, wakielewa kuwa kipindi hicho ni cha muda tu, la maana ni kuongeza bidii katika masomo.
Hivyo, ni vema kukaa na mtoto wako na kumfundisha mambo mbalimbali ili aweze kuendelea katika dunia hii iliyojaa misukosuko ya maisha. Penda kumsikiliza mtoto wako na kumshauri jambo zuri na baya. Pia mtie moyo kwa matarajio yaliyoko mbele yake kwamba akimaliza masomo yake ya msingi, atakwenda sekondari, halafu chuoni, baada ya chuo atapata kazi nzuri ili awe na ari ya kusoma.
Tukutane wiki ijayo.
0 Maoni:
Post a Comment