Friday, August 28, 2009

TATUA TATIZO LINALOKUSUMBUA ILI UWE NA FURAHA

MSOMAJI wangu, katika mfululizo wa makala hizi za Maisha Yetu, nimedhamiria kukuletea kitu kipya kila Alhamisi. Leo tutaangalia jinsi ya kuwa na furaha katika maisha yetu ya kila siku.

Hebu tuangalie mfano huu. Mwanamke mmoja alikuwa anahojiwa na mwandishi wa habari kwenye runinga na ghafla aliulizwa swali kama ‘anadhani ni watu gani siku hizi wana furaha’.

Kwa taharuki bila utulivu, mwanamke yule alikurupuka na kujibu lile swali kuwa kila mtu ana matatizo mengi, akimaanisha kuwa hakuna mtu yeyote aliye na furaha.

Hii inaonyesha dhahiri kuwa mwanamke yule kwa muda ule hakutarajiwa kuulizwa swali kama lile. Na aliulizwa bila kupewa nafasi ya kuwa na maandalizi. Na kwa muda huo, alikuwa ni mtu aliyejawa na mawazo.

Lakini ukweli ni kwamba furaha huwa ipo tu, bila kujali kama mtu ana matatizo ama hana. Inawezekana kabisa kila mmoja akawa na matatizo, lakini si kwamba kila moja hana furaha, kwani wapo watu wenye furaha lakini wana maisha duni, lakini wapo wengine hawana furaha ingawa ni matajiri wakubwa.

Tunaona kuwa kuna watu ambao wamejaaliwa kuwa na vitu vyenye thamani ya mabilioni ya fedha, lakini wamekuwa na matatizo ya kifedha. Utajiri wao upo kwenye mali walizowekeza.

Hupokea mshahara, lakini kiasi kikubwa kinakwenda kwenye madeni aliyonayo. Pia katika maisha haya tunayoyaishi kila mtu anakuwa na eneo fulani ambalo limekuwa likimkosesha furaha katika maisha yake. La msingi ni kuikabili hali hiyo na kutafuta ni jinsi gani utapata furaha na amani katika maisha.

Hata wewe inawezekana una hali hiyo katika shughuli zako uzifanyazo. Kama hilo unalikubali, hata kama una fedha nyingi bado kuna eneo utakuwa umekwama hivyo utakuwa huna furaha. Kila mmoja anapoanza maisha anakuwa na ndoto ya mafanikio. Inakubidi ujue ndoto ya shughuli unayotarajia kuifanya na jinsi ya kushikamana nayo.

Endapo ndoto za malengo yako zitatimia, ni lazima utakuwa na mafanikio makubwa. Na hapo ndipo furaha yako itakapotimilika. Pia wengine wana sononeko katika ufahamu wao. Hapa utaona kuwa kila mtu amebahatika kupewa eneo lake alitawale. Kwa maana kwamba, wapo wenye akili za darasani, wenye ushauri wa busara, wenye akili ya biashara na mambo mengine.

Utaona hapa kila mmoja, Mungu amemjalia kwa sehemu yake. Kwa hiyo kila mmoja ana eneo ambalo hakubahatika kuwa nalo. Hebu tuangalie mfano huu. Wanafunzi wawapo darasani, wapo wanaoelewa kwa haraka zaidi somo fulani kuliko wengine. Wengine ni wepesi katika hisabati, wengine histori na wengine Geography. Inategemeana na vile alivyojaliwa.

Hivyo kama mwanafunzi mzuri unapoona somo fulani linakupiga chenga huku wenzako wakiwa wanalielewa kwa urahisi, unaumia na kukosa furaha. Kinachotakiwa ni kutafuta njia ya kutatua hali hiyo ili uwe na furaha katika eneo hilo.

Kwa mfano, kuna kijana aliyekuwa haelewi somo la historia wakati mwalimu wake alipokuwa akifundisha darasani. Hivyo kila mara mwalimu huyo alipoingia darasani alikuwa akikosa furaha.

Wakati huo, wenzake walikuwa wakilifurahia somo hilo kwa kuwa walikuwa wakilielewa vizuri pale mwalimu wao alipowafundisha.

Mwalimu wake aligundua hali hiyo kwamba kijana yule hana furaha kama wanafunzi wengine anapokuwa darasani. Na siku moja alimuuliza, ana tatizo gani ili aweze kumsaidia lakini kijana yule alimweleza kuwa hana tatizo.

Kwanza tunaona kuwa kijana yule alifanya kosa kwa kuwa hakuwa tayari kujieleza ili apate msaada kwa mwalimu wake. Hivyo ni ukweli usiopingika kuwa pale unapokuwa na tatizo na ukawa tayari kujieleza, unakuwa na amani na furaha moyoni, kwa kuwa unapata msaada zaidi. Kinyume cha hapo, unakosa furaha kila mara kipindi hicho kinapokaribia.

Kwa hiyo, tunaona kuwa mafanikio ya mwanafunzi yanapatikana pale anapokubali kuwa hawezi somo fulani, ili apatiwe msaada zaidi. Kwa upande mwingine, mtoto nyumbani anaweza kuwa na hali ya mfadhaiko na kushindwa kuwa na mawasiliano mazuri na wazazi wake, kutokana na jinsi ile wanavyomlea, kwamba wamekuwa wakali sana na hawamfundishi kwa upendo pale anapokosea.

Laiti mtoto yule angeweza kuwa wazi na kuwaambia wazazi wake hali aliyonayo inachangiwa na wao, angeweza kuwa na hali nzuri. Na ukawa mwanzo wa mahusiano mazuri kati yake na wazazi wake.

Vile vile kwa upande mwingine, ni vema wazazi wakawa wazi kwa watoto wao, pale wanapoona kuwa wamewakosea. Wawe tayari kukiri makosa hayo kwa watoto wao. Si vema mzazi akaonyesha kuwa yuko sahihi wakati wote hata kama amekosea. Ni vema kukiri kuwa jambo fulani limefanyika kimakosa.

Eneo jingine linalowanyima watu furaha ni upande wa hisia. Hapa utaona kuwa, watu wengi wamekuwa wakiugua maradhi mbalimbali, kutokana na hisia wanazokuwa nazo.

Wengine hufikia hatua ya kupungua uzito, kutokana na hali hiyo. Wengine kutokana na kupata msukosuko wa kimahusiano hufikia hatua hata ya kutaka kujiua.

Ni kweli kuwa katika maeneo yote ya maisha kanuni zinafanana. Hivyo unapokutana na tatizo ni vema kuikubali hali hiyo iliyokupata japo si jambo rahisi, ili urejeshe furaha yako uliyokuwa nayo. Na kwamba, furaha inapatikana pale tu unapokubali kuwa umepungukiwa hivyo unahitaji msaada.

Kuna swali moja la kujiuliza kwamba, kama kila mmoja kati yetu eneo fulani katika maisha ana uhitaji, kwanini basi tunakuwa wagumu kuikubali hali hiyo? Yawezekana ugumu unakuwepo kwa kuogopa kuwa, unaposema ukweli katika eneo fulani utakataliwa na jamii, rafiki ama familia.

Ama pia kukubali hali ile uliyonayo itakufanya upate aibu. La hasha, hiyo ndiyo njia sahihi ya maisha ya kujikubali na kuachana na mambo yale yanayokuumiza. Kinachotakiwa ni kujivika hali ya ujasiri bila kuogopa jambo lolote lile.

Furaha inakuja kwa mtu yule anayegundua eneo ambalo anahitaji msaada na kuwa wazi. Mafanikio yanakuja kwa mtu anayeomba kusaidia katika eneo lile aliloshindwa.

Tukutane alhamisi ijayo

0 Maoni:

Twitter Facebook