NAWAKARIBISHA tena katika safu hii ya Maisha Yetu yenye lengo la kukufahamisha jinsi maisha yalivyo na yanavyopaswa kuwa.
Leo tunaendelea na mada yetu ya msongo katika maeneo ya kazi ili uweze kujua jinsi ya kukabiliana na hali hiyo mara unapokutana nayo.
Watafiti mbalimbali wamegundua kuwa, endapo bosi katika kampuni, atakuwa na hali ya msongo wa mawazo, ofisi, kampuni au shirika hilo litakuwa na mawasiliano mabaya.
Naye mwanasaikolojia mmoja anayeshughulika na masuala ya viwandani amewahi kuelezea jinsi meneja mzuri anavyopaswa kuwa.
Kwa maelezo ya mwanasaikolojia huyo, meneja mzuri anapaswa kuwa mshauri mzuri kwa wafanyakazi wake, ari ya kupenda kujituma, kupenda kufanya kazi na kushirikishana mambo mbalimbali na wafanyakazi wake.
Kwa maelezo ya mwanasaikolojia huyo, endapo bosi atakuwa karibu na wafanyakazi wake, ushauri mwingi utakaotoka kwa wafanyakazi hao, utampa mwanga wa kujua nini cha kufanya kwa kipindi hicho katika kuboresha ofisi.
Ndiyo maana katika ofisi nyingi ni rahisi kutambua sababu za meneja fulani kuwa mzuri, au wa kawaida ama mbaya katika utendaji wake, kutokana na jinsi anavyojishughulisha na watu wake.
Meneja mzuri ni yule anayependa kuwa karibu na wafanyakazi wake, kuwasikiliza na kufuatilia uzalishaji unavyokwenda katika kampuni.
Pia anakuwa mwadilifu katika utendaji wake, hatetereki katika malengo yake ya uzalishaji, pia huwasikiliza wafanyakazi wake wanapokuwa na mahitaji.
Bosi wa wastani katika utendaji wake, ni yule anayeangalia ufanisi wake pekee, bila kuona umuhimu wa wengine. Kama vile wanavyowajibika katika kazi zao.
Kwa upande wa bosi mbaya ni yule anayefanya kazi kwa kutumia vitabu, pamoja na kujenga hali ya kujilinda kila wakati.
Utafiti mwingine uliofanywa, ulionyesha kuwa, msongo katika kazi unawafanya watu wengi kutumia vileo na kujikuta wanashindwa kufikia malengo katika kazi zao, hali inayowafanya kufukuzwa kazi.
Wengine wanaokabiliwa na msongo, hutumia dawa za kulevya, hali inayowafanya kupatwa na magonjwa ya akili, kuathiri utendaji wao katika uzalishaji na kuhatarisha ajira walizonazo.
Utafiti mwingine unaonyesha kuwa, msongo mwingine kwa wafanyakazi huchangiwa na uamuzi unaofanywa na kampuni kwa kuwapunguza kazini wafanyakazi kutokana na sababu mbalimbali.
Hivyo basi, ni vyema kwa mameneja katika ofisi zao kuzungumza na kuwasikiliza wafanyakazi wao.
Pia wawe wanawauliza wafanyakazi hao kuchanganua mambo matatu yanayoweza kuboresha kampuni au ofisi hiyo na mambo matatu yatakayoweza kuzorotesha uzalishaji katika kampuni hiyo.
Bosi huyo apende kujua kama mazingira wanayofanyia kazi wafanyakazi wake, yanaridhisha.
Ni vema bosi kuwaheshimu watu aliowaajiri ama anaowasimamia katika kampuni hiyo na kuwajulisha kuwa yuko tayari kushughulikia taarifa yoyote itakayomfikia.
Ni vema wafanyakazi wakawa wanashirikishwa katika maamuzi yanayofanyika ili wajione nao ni sehemu ya ofisi hiyo.
Si mbaya wakaorodhesha matatizo mbalimbali yaliyowapata wafanyakazi na kuangalia jinsi ya kuyashughulikia.
Ni vizuri kiongozi huyo akawa anaongoza kwa vitendo. Asiwe mwepesi wa kuzungumza.
Hayo yote yatakapoweza kutekelezwa na mameneja ama waajiri wa kampuni, msongo katika eneo hilo la kazi hautawapata wafanyakazi wake.
Ugonjwa mbaya katika kampuni ni ile hali ya wafanyakazi kukosa ari ya kufanya kazi kutokana na msongo wanaokabiliana nao.
Hiyo ni pamoja na kupunguza ari ya kupenda kazi kwa wafanyakazi, utendaji mbovu na unaopunguza uzalishaji, kuongezeka kwa magonjwa miongoni mwa wafanyakazi, wafanyakazi kuchelewa kazini hali inayosababisha kampuni hiyo kutokufikia malengo iliyokusudia.
Vile vile baada ya kampuni kupunguza wafanyakazi, wale wanaobakia nao wanaendelea kupatwa na hali hiyo ya msongo kwa kuwa, kunakuwa na ongezeko kubwa la kazi hali itakayowafanya washindwe kupata muda wa kupumzika.
Tukutane alhamisi ijayo
0 Maoni:
Post a Comment