Friday, August 28, 2009

HALI YA KURIDHIKA INAONGEZA FURAHA

KATIKA mfululizo wa makala hizi za maisha yetu, nimedhamiria kukuletea kitu kipya, ambapo leo tutaangalia jinsi ya kudhibiti hisia zetu ili tuendelee kuwa na furaha.

Watu ambao hawawezi kudhibiti hisia zao wanajikuta wako katika hali ya kukata tamaa na kuvunjika moyo.

Lakini ukweli ni kwamba, inakupasa usikate tamaa mpaka kumwazia Mungu wako mambo mabaya, kutokana na wewe mwenyewe kushindwa kudhibiti hisia zako.

Hivyo ni vema kuwa imara katika hisia zako, bila kujali kama unapitia hali ya milima na mabonde, ili kutimiza malengo yako uliyojiwekea, kinyume cha hapo, utaendelea kuwa mtu usiyesonga mbele kutokana na hali ambayo umeiruhusu, ilhali ungeweza kuidhibiti.

Mfano mzuri ni kwa mtu aliyeelimika, kwa kuwa yuko tayari kufundishika, ambaye ni muelewa, hataabiki kwa kuonyesha kuwa anajua kila kitu, hata kama anajua.

Huwa na utayari wa kujifunza kila mara, ni msikivu. Na kama njia yake haiko sawa sawa, anakuwa tayari kubadilika, mtu wa namna hii, ni rahisi
kuwa na mafanikio ya haraka.

Pia mtu wa aina hii, endapo hajui jambo fulani, hukubali kuwa hajui na huwa tayari kukiri hivyo. Mtu wa aina hii, yuko tayari kusikiliza wengine, iwe ni mzee, kijana, mwenye busara ama mwenye uzoefu zaidi yake, humsikiliza.

Hakuna ubishi, kutoelimika ni jambo la hatari, hivyo ni busara kila mmoja akapenda kuelimika bila kujali umri alionao, kwa kuwa atapata busara zaidi na mafanikio ikiwa ni pamoja na kujisimamia katika maamuzi yake, kabla ya kufanya jambo linaloweza kumharibia kabisa.

Kamwe usikubali kujishusha thamani yako na kujiona wewe si kitu, kwamba huwezi kufanya jambo fulani, kwani huo si ubinadamu. Bali inakupasa kupiga moyo konde na kusonga mbele, hata kama kuna hali ngumu inayokukatiza, jaribu kukabiliana nayo.

Kujikubali ulivyo ni pamoja na kuwa tayari kukubali kuwa watu wengine pia wanaweza kukusaidia pamoja na kukupa uwezo wa kujiamini kuweza kukiri upungufu ulionao.

Kuwa wazi, kuwa mnyenyekevu, jisahihishe na penda kuelimika. Kwa kufanya hivyo, utaweza kuishi kwa furaha na amani.

Wengi wetu tumejikuta hatuna furaha katika maisha yetu, kwa kuwa tunajitaabisha na mambo mengi na kujikuta kila wakati wewe ni mtu wa shughuli na mipango mingi isiyokwisha.

Kwa maelezo mengine, tunashindwa kuwa na furaha kila siku, kutokana na hisia zetu kuzielekeza kwenye shughuli na matukio ya siku inayofuata.

Tumekuwa na shughuli nyingi katika mipango ya maisha, hali inayotufanya kushindwa kuwa na furaha kwa muda uliopo.

Ebu tuangalie mfano wa mtu mmoja ambaye mwanzoni alifikiri kuwa, endapo angekuwa na nyumba yake angekuwa na utajiri ambao ungempatia furaha, lakini hilo lilipotimia alihitaji kitu kingine zaidi.

Alijikuta akihitaji nyumba nyingine kubwa zaidi. Wakati ukafika, akapata nyumba nyingine, lakini alijikuta kila wakati akifurahia nyumba yake ya awali, hivyo ilimlazimu kwenda kwenye nyumba yake ya awali, mara kwa mara.

Ilifikia mahali akasema kila alivyozidi kujiridhisha kwa kupata kile alichokihitaji, ndivyo alivyokuwa hafurahii vitu alivyokuwa navyo na kutamani kupata vingine zaidi. Hapa tunaona ni vizuri kuwa na kiasi katika maisha tunayoyaishi.

Hapa tunajifunza nini? Mwanadamu yeyote kama hana tabia ya kuridhika, anakuwa anajiongezea hali ya kukata tamaa na hata kuishi kwa hofu, kwa kutokufikia malengo makubwa aliyojipangia.

Ni sawa na kuamka usiku wa manane na kwenda kwenye jokofu kulifungua lakini hujui ni nini hasa unachokihitaji.

Kwa kuwa hujui unachokihitaji, unajikuta ukigusa hiki, unajaribu na kingine lakini katika vitu vyote hivyo hakuna unachokisikia ni kitamu.

Mwisho unafunga jokofu lako na kurudi kulala, huku bado ukiwa na njaa, hujatosheka.

Tunaona wengi wetu tunafanana tabia zetu kwa kuwa na hisia zisizotimizika.

Ili tuwe na mafanikio, inabidi kufanya uchaguzi katika kila tunachokiwaza. Inatakiwa kuondokana na mawazo yatakayoturudisha nyuma, kuwa na mawazo mazuri, ndoto nzuri na kufanya kazi kwa bidii.

Tukutane Alhamisi ijayo.

0 Maoni:

Twitter Facebook