Friday, August 28, 2009

SAHAU MAUMIVU ULIYONAYO UPATE FURAHA

WIKI iliyopita tuliangalia jinsi ya kudhibiti hisia zetu ili tuendelee kuwa na furaha, imeonekana kuwa watu wengi wameshindwa kudhibiti hisia walizokuwa nazo na kujikuta wako katika hali ya kukata tamaa, pamoja na kuvunjika moyo.

Katika mfululizo wa makala hizi za maisha yetu, nimedhamiria kukuletea kitu kipya kila Alhamisi. Leo tutaangalia jinsi inavyokupasa uyaachie mambo yanayokusumbua, ili uishi kwa furaha. Tutaangalia jinsi ya kuachana na mambo mbalimbali tunayokutana nayo katika maisha ili kuweza kupata amani na utulivu katika mioyo yetu.

Kumbuka kuwa kama una tabia ya kuachana na ya maumivu na huzuni unayokabiliana nayo, utakuwa na maisha mazuri, lakini kinyume cha hapo, utaendelea kuwa mtu asiyekuwa na furaha siku zote.

Na pia ufahamu kuwa, kila mmoja wetu hukabiliana na changamoto mbalimbali katika sehemu fulani ya maisha yake, kama vile, hali ya huzuni au kukataliwa lakini njia nzuri ya kuishi vizuri ni kuwa jasiri katika kuikabili hali hiyo.

Japo wapo watu wengine hudhani, kwa kuwa wao ni washika dini sana, hali ya huzuni, kuhangaika, kukata tamaa haitawapata, la hasha! Kila mmoja anapatwa na hali hiyo, ila ni uamuzi wako kuchagua ni jinsi gani unapenda uwe, kuwa na furaha ama kutokuwa nayo.

Pia ukiangalia watu wengi ambao hawana furaha, hukabiliwa na magonjwa mbalimbali. Huweza kuwatambua kwa kuwaangalia muonekano wao kiafya, vile vile hupatwa na maradhi kama shinikizo la moyo, moyo kudunda kwa nguvu, kupooza na hata wakati mwingine kuugua kansa ambayo huzalishwa na hali ya msongo wa mawazo.

Kwa upande mwingine wa maisha haya tunayoyaishi, ujue kuwa nayo yana kanuni zake, kama unataka watu wakutendee mambo mema, nawe pia watendee yaliyo mema, kwa kila jambo unalotenda.

Kwa kila tendo jema, kuna mwitiko ulio mzuri, kinyume cha hapo hutabaki kuumia na kukosa furaha maishani. Wema wako unaowatendea wengine, ndivyo hivyo nawe utapokea katika maisha yako kutoka kwao.

Tiba ya kuishi maisha ya furaha ni hii ‘kuwa mzuri, kuwa mwema, usiwe mbinafsi. Watendee wengine vile unavyopenda wakutendee wewe’.

Kama kweli umedhamiria kupata furaha ya kutosha maishani, tumia kanuni hiyo ya maisha na kuifanyia kazi.

Kama unataka kuwa rafiki wa watu, nao wawe rafiki zako. Kuwa rafiki kwao na kama umezungukwa na watu wasio wazuri kwako, wabadili wawe watu wazuri kwa kuonyesha wema wako kwao, haijalishi jinsi watakavyokuchukulia.

Je, unadhani utawabadilishaje ili wawe watu wazuri? Ni kwa kushirikiana nao katika mambo yaliyo mema na kuwajali. Inawezekana wanaweza wasikukubali kirahisi, lakini jitahidi kuwa mwema kwao, bila kujali wanachokisema wala kukinong’ona.

Hebu tuangalie mfano wa mama mmoja, aliyekuwa ameolewa lakini hakuwa na furaha na mumewe, kwa kuwa kila alichokifanya mumewe huyo alikikosoa.

Mwanamke huyo aliamua kutafuta msaada kwa kiongozi wake wa dini na kumweleza kuhusu mumewe kwamba kila aliporudi nyumbani alikuwa na hasira na kukosoa kila jambo aliloliona limefanyika.

Lakini mama huyo, alipoomba ushauri, aliambiwa kuwa, inawezekana yeye ndiye chanzo cha yote kabla ya kumsema mumewe, ni vema akajiangalie yeye kwanza, jambo alilokubaliana nalo na kulifanyia kazi, baada ya muda, mumewe alibadilika. Furaha ikatawala nyumbani kwao.

Mwanamke huyo alisema, aliamua kubadilika kwa kumjali mumewe na kuwa karibu naye, bila kujali vile alivyokuwa akimtenda na kwamba kila mumewe huyo aliporudi nyumbani, na kuanza kukosoa kama alivyozoea, kwa kuwa mwanamke alikubali kubadilika, alijitahidi kumhudumia kwa upendo, kumpatia chakula, juisi na kumpa maneno matamu, bila kujali jinsi alivyokuwa akifoka kwa hasira.

Alisema aliendelea kuwa karibu na mumewe kila siku na mwishoni mumewe huyo alibadilika tabia yake ile aliyokuwa nayo. Kama unataka kuyabadili mazingira magumu unayokutana nayo, ni vema ukaanza kubadilika wewe kwanza.

Fikiri juu ya hili. Je, ni jambo gani linalotufanya kuwatendea watu mambo mema? Ni kwa kuwa, nasi tunapenda kutendewa mambo mema pia? Kamwe tusiruhusu hali ya chuki na hasira katika maisha tunayoyaishi. Mbaya zaidi hali ya hasira zilizofichika ndani vinginevyo utapata maumivu na majeraha yaliyofichika ambayo yanahitaji kuponywa.

Majeraha hayo yaliyofichika hukusababishia hasira, ugomvi ama hali yoyote ambayo hupendi utendewe na mtu mwingine. Baadhi ya dalili zinazomfanya mtu aonekana kama ana majeraha yaliyofichika ni maneno yake, mwonekano na vitendo vyake.

Sasa basi njia ya kukabiliana na maumivu ya ndani uliyonayo ni kuyasahau na kutokumbuka mambo uliyowahi kutendewa. Watu wengi wanakosa furaha ya kweli, kwa kuwa wamekuwa wakikumbuka jinsi walivyotendewa na baba au mama yake, alipokuwa mdogo, mke au mme wake alivyomtendea siku za nyuma, kwa kuwa wanashindwa kusamehe, miaka inapita huku maumivu hayo yakiwa yanaendelea.

Usilaani. Kamwe usiruhusu maumivu yakakufanye mtu mwenye uchungu, jaribu kusahau, kumbuka kuwa, huwezi kusahau maumivu yaliyokupata kama utakuwa unayakumbuka kumbuka.

Tukutane Alhamisi ijayo.

HALI YA KURIDHIKA INAONGEZA FURAHA

KATIKA mfululizo wa makala hizi za maisha yetu, nimedhamiria kukuletea kitu kipya, ambapo leo tutaangalia jinsi ya kudhibiti hisia zetu ili tuendelee kuwa na furaha.

Watu ambao hawawezi kudhibiti hisia zao wanajikuta wako katika hali ya kukata tamaa na kuvunjika moyo.

Lakini ukweli ni kwamba, inakupasa usikate tamaa mpaka kumwazia Mungu wako mambo mabaya, kutokana na wewe mwenyewe kushindwa kudhibiti hisia zako.

Hivyo ni vema kuwa imara katika hisia zako, bila kujali kama unapitia hali ya milima na mabonde, ili kutimiza malengo yako uliyojiwekea, kinyume cha hapo, utaendelea kuwa mtu usiyesonga mbele kutokana na hali ambayo umeiruhusu, ilhali ungeweza kuidhibiti.

Mfano mzuri ni kwa mtu aliyeelimika, kwa kuwa yuko tayari kufundishika, ambaye ni muelewa, hataabiki kwa kuonyesha kuwa anajua kila kitu, hata kama anajua.

Huwa na utayari wa kujifunza kila mara, ni msikivu. Na kama njia yake haiko sawa sawa, anakuwa tayari kubadilika, mtu wa namna hii, ni rahisi
kuwa na mafanikio ya haraka.

Pia mtu wa aina hii, endapo hajui jambo fulani, hukubali kuwa hajui na huwa tayari kukiri hivyo. Mtu wa aina hii, yuko tayari kusikiliza wengine, iwe ni mzee, kijana, mwenye busara ama mwenye uzoefu zaidi yake, humsikiliza.

Hakuna ubishi, kutoelimika ni jambo la hatari, hivyo ni busara kila mmoja akapenda kuelimika bila kujali umri alionao, kwa kuwa atapata busara zaidi na mafanikio ikiwa ni pamoja na kujisimamia katika maamuzi yake, kabla ya kufanya jambo linaloweza kumharibia kabisa.

Kamwe usikubali kujishusha thamani yako na kujiona wewe si kitu, kwamba huwezi kufanya jambo fulani, kwani huo si ubinadamu. Bali inakupasa kupiga moyo konde na kusonga mbele, hata kama kuna hali ngumu inayokukatiza, jaribu kukabiliana nayo.

Kujikubali ulivyo ni pamoja na kuwa tayari kukubali kuwa watu wengine pia wanaweza kukusaidia pamoja na kukupa uwezo wa kujiamini kuweza kukiri upungufu ulionao.

Kuwa wazi, kuwa mnyenyekevu, jisahihishe na penda kuelimika. Kwa kufanya hivyo, utaweza kuishi kwa furaha na amani.

Wengi wetu tumejikuta hatuna furaha katika maisha yetu, kwa kuwa tunajitaabisha na mambo mengi na kujikuta kila wakati wewe ni mtu wa shughuli na mipango mingi isiyokwisha.

Kwa maelezo mengine, tunashindwa kuwa na furaha kila siku, kutokana na hisia zetu kuzielekeza kwenye shughuli na matukio ya siku inayofuata.

Tumekuwa na shughuli nyingi katika mipango ya maisha, hali inayotufanya kushindwa kuwa na furaha kwa muda uliopo.

Ebu tuangalie mfano wa mtu mmoja ambaye mwanzoni alifikiri kuwa, endapo angekuwa na nyumba yake angekuwa na utajiri ambao ungempatia furaha, lakini hilo lilipotimia alihitaji kitu kingine zaidi.

Alijikuta akihitaji nyumba nyingine kubwa zaidi. Wakati ukafika, akapata nyumba nyingine, lakini alijikuta kila wakati akifurahia nyumba yake ya awali, hivyo ilimlazimu kwenda kwenye nyumba yake ya awali, mara kwa mara.

Ilifikia mahali akasema kila alivyozidi kujiridhisha kwa kupata kile alichokihitaji, ndivyo alivyokuwa hafurahii vitu alivyokuwa navyo na kutamani kupata vingine zaidi. Hapa tunaona ni vizuri kuwa na kiasi katika maisha tunayoyaishi.

Hapa tunajifunza nini? Mwanadamu yeyote kama hana tabia ya kuridhika, anakuwa anajiongezea hali ya kukata tamaa na hata kuishi kwa hofu, kwa kutokufikia malengo makubwa aliyojipangia.

Ni sawa na kuamka usiku wa manane na kwenda kwenye jokofu kulifungua lakini hujui ni nini hasa unachokihitaji.

Kwa kuwa hujui unachokihitaji, unajikuta ukigusa hiki, unajaribu na kingine lakini katika vitu vyote hivyo hakuna unachokisikia ni kitamu.

Mwisho unafunga jokofu lako na kurudi kulala, huku bado ukiwa na njaa, hujatosheka.

Tunaona wengi wetu tunafanana tabia zetu kwa kuwa na hisia zisizotimizika.

Ili tuwe na mafanikio, inabidi kufanya uchaguzi katika kila tunachokiwaza. Inatakiwa kuondokana na mawazo yatakayoturudisha nyuma, kuwa na mawazo mazuri, ndoto nzuri na kufanya kazi kwa bidii.

Tukutane Alhamisi ijayo.

IKUBALI HALI ULIYONAYO UPATE FURAHA

MSOMAJI, katika mfululizo wa makala hizi za maisha yetu, nimedhamiria kukuletea kitu kipya kila Alhamisi.

Leo tutaangalia jinsi unavyoweza kupata furaha kwa kuikubali hali ya upungufu uliyonayo.

Si rahisi kwa mtu yeyote kukubali hali ya uhitaji aliyonayo, lakini kufanya hivyo ni jambo la muhimu.

Ni ukweli usiopingika kuwa, katika maeneo yote ya maisha tunayoyaishi, kanuni zake zinafanana.

Na kwamba, unakuwa na furaha pale tu unapokubali hali ile ya upungufu uliyonayo, kwa kuwa hapo ndipo kwenye hitaji lako.

Kama ni kweli kuwa kila mmoja wetu hajakamilika katika eneo fulani katika maisha, kwa nini basi unakuwa hauko tayari kuikubali hali hiyo?

Wengi wetu tumekuwa hatuko tayari kukubali hali ya upungufu tuliyonayo, kwa kuhofia kuwa jamii inayotuzunguka itatucheka, kututenga ama kudhalilika.

Lakini kinachotakiwa hapa, ni kutoogopa jambo lolote lile, liwe kutengwa, kukataliwa ama kudharauliwa.

Sasa ni jinsi gani hali hii ya kuwa na furaha inaweza kukubadili wewe na mimi? Ni pale tu utakapoonyesha unahitaji msaada ama una upungufu.

Kwa mfano unaweza kuhitaji msaada kwa mtu yeyote kwa kumuuliza maswali yafuatayo: "Nimepata tatizo, je, waweza kunisaidia?, "Sielewi jambo fulani unaweza kunielewesha?, "Sijakubaliana na wewe, je, tunaweza kuonana mahali na kujadili zaidi?", "Nimepata hasara, je, waweza kuniongoza cha kufanya?"

Maswali ya namna hiyo ndiyo mwanzo wa kukuweka huru katika maisha yako. Hivyo furaha inakuwepo kwa mtu yeyote yule anayejua kuwa, eneo fulani ana upungufu hivyo anaukubali na kuhitaji msaada kwa wengine.

Kama wewe hauko tayari kulikubali jambo linalokusumbua, usishangae usipoona kuwa, wengine hawakujali.

Hivyo suluhu ni kujiweka mbele, jaribu kuwa mtu fulani ambaye hukuwahi kuwa hivyo, pamoja na kujiweka maridadi wakati wote.

Na ukweli ni kwamba, katika hali ya kuumia uliyonayo, kuna mtu ambaye yuko tayari kukusaidia juu ya upungufu wako, endapo tu ataelewa tatizo lako na kuliachilia. Lakini kama utajionyesha kuwa huna matatizo, hakuna njia ambayo mtu yeyote ataweza kukusaidia.

Wakati wote kuna mtu ambaye yupo tayari kukusaidia. Na kwamba mtu yeyote husaidiwa pale atakapokubali kuwa ana uhitaji katika sehemu fulani.

Kuna mfano wa mtu mmoja ambaye alikuwa ni mtumwa wa ulevi kwa muda mrefu, aliteseka katika hali hiyo kwa kuwa hakuwa tayari kuikubali. Na pale alipoelezwa kuhusiana na athari zinazoweza kumpata, hakuwa tayari kupokea msaada.

Siku moja baada ya kulewa kupindukia na kugonga gari lake alilokuwa akiliendesha, kwa maneno yake mwenyewe alijikuta akisema kuwa: ''Nimeteseka kwa ulevi kwa muda mrefu, kwa kuwa nilikuwa nasema kuwa, ninaweza kuudhibiti unywaji wangu, nilikataa ukweli kuwa nilikuwa mlevi niliyepitiliza, ningepokea uponyaji endapo ningeonyesha ninahitaji msaada. Na sasa baada ya hali hii kunikuta ninahitaji msaada na kubadili maisha yangu."

Tokea siku hiyo, maisha ya mtu huyo yalibadilika kwa kuwa alijitambua na kuhitaji msaada.

Kwa upande mwingine, furaha ya kweli inapatikana pale ambapo unaacha hali ya kulaumu. Ama kumlaumu Mungu au kujilaumu mwenyewe.

Watu wengi wanapopata matatizo hujikuta wakimlaumu Mungu ama kujilaumu wenyewe, badala ya kutafuta njia ya kumtoa hapo alipo ili aweze kuwa huru.

Sasa basi endapo umefikia hatua ya kukata tamaa ya maisha, umekutana na kipindi kigumu, kamwe usimlaumu Mungu kwa kuwa kufanya hivyo hutapata jibu la tatizo ulilonalo.

Makosa mbalimbali ambayo mwanadamu huyafanya pindi awapo katika hali ngumu ni yale ya kuhukumu, yatokanayo na utashi, sababu, ubinafsi, ukaidi, upumbavu na mengineyo yafananayo na hayo. Yote hayo ni chanzo cha binadamu kinachomfanya awe maskini na kuteseka.

Ama wakati mwingine unakuta mtu analaumu kwa ugonjwa alionao, ilhali wakati mwingine yawezekana yeye mwenyewe ameshindwa kujilinda mpaka akapata magonjwa.

Kwani kwa upande mwingine tunaweza kusema kuwa, magonjwa mengi sisi wenyewe ndiyo tunayasababisha kwa kutokula vizuri, kutokulala vizuri, kutokufanya mazoezi vizuri, kutopumua vizuri, haya yote ni kutokana na mazingira yanayomzunguka binadamu. Hivyo tunaona mambo mengine ni sisi wenyewe tunajisababishia na Mungu si wa kulaumiwa.

Mengi ya magonjwa hayo, huwapata wanadamu kutokana na uelewa mdogo ama elimu waliyonayo juu ya athari zinazoweza kutokea endapo ulishindwa kufanya jambo fulani.

Vile vile si vizuri kujilaumu wewe mwenyewe kutokana na hali inayokukabili, kwani kwa kufanya hivyo hutaweza kutatua tatizo linalokusumbua wala kuibadili hali hiyo.

Unaweza kupata hali ya kufiwa na mtoto, mzazi ama mume wako mpenzi, hali itakayokufanya ujitenge na wenzako, uache kujichanganya na kufanya mambo mengine ya kukusaidia, kutokana na hali iliyokukuta endapo hautakuwa makini na kuendelea na shughuli zako za kila siku, utajikuta hali yako kimaisha na kiuchumi inazidi kudidimia.

Katika hali kama hiyo, ndugu ama rafiki zako hawataweza kuyainua maisha yako siku zote, watakusaidia kwa sehemu tu, lakini itabidi nawe unyanyuke na kutoka katika hali ile ya kutokuwa na furaha na kujichanganya ili uweze kusukuma gurudumu hili la maendeleo.

Tukutane Alhamisi ijayo

TATUA TATIZO LINALOKUSUMBUA ILI UWE NA FURAHA

MSOMAJI wangu, katika mfululizo wa makala hizi za Maisha Yetu, nimedhamiria kukuletea kitu kipya kila Alhamisi. Leo tutaangalia jinsi ya kuwa na furaha katika maisha yetu ya kila siku.

Hebu tuangalie mfano huu. Mwanamke mmoja alikuwa anahojiwa na mwandishi wa habari kwenye runinga na ghafla aliulizwa swali kama ‘anadhani ni watu gani siku hizi wana furaha’.

Kwa taharuki bila utulivu, mwanamke yule alikurupuka na kujibu lile swali kuwa kila mtu ana matatizo mengi, akimaanisha kuwa hakuna mtu yeyote aliye na furaha.

Hii inaonyesha dhahiri kuwa mwanamke yule kwa muda ule hakutarajiwa kuulizwa swali kama lile. Na aliulizwa bila kupewa nafasi ya kuwa na maandalizi. Na kwa muda huo, alikuwa ni mtu aliyejawa na mawazo.

Lakini ukweli ni kwamba furaha huwa ipo tu, bila kujali kama mtu ana matatizo ama hana. Inawezekana kabisa kila mmoja akawa na matatizo, lakini si kwamba kila moja hana furaha, kwani wapo watu wenye furaha lakini wana maisha duni, lakini wapo wengine hawana furaha ingawa ni matajiri wakubwa.

Tunaona kuwa kuna watu ambao wamejaaliwa kuwa na vitu vyenye thamani ya mabilioni ya fedha, lakini wamekuwa na matatizo ya kifedha. Utajiri wao upo kwenye mali walizowekeza.

Hupokea mshahara, lakini kiasi kikubwa kinakwenda kwenye madeni aliyonayo. Pia katika maisha haya tunayoyaishi kila mtu anakuwa na eneo fulani ambalo limekuwa likimkosesha furaha katika maisha yake. La msingi ni kuikabili hali hiyo na kutafuta ni jinsi gani utapata furaha na amani katika maisha.

Hata wewe inawezekana una hali hiyo katika shughuli zako uzifanyazo. Kama hilo unalikubali, hata kama una fedha nyingi bado kuna eneo utakuwa umekwama hivyo utakuwa huna furaha. Kila mmoja anapoanza maisha anakuwa na ndoto ya mafanikio. Inakubidi ujue ndoto ya shughuli unayotarajia kuifanya na jinsi ya kushikamana nayo.

Endapo ndoto za malengo yako zitatimia, ni lazima utakuwa na mafanikio makubwa. Na hapo ndipo furaha yako itakapotimilika. Pia wengine wana sononeko katika ufahamu wao. Hapa utaona kuwa kila mtu amebahatika kupewa eneo lake alitawale. Kwa maana kwamba, wapo wenye akili za darasani, wenye ushauri wa busara, wenye akili ya biashara na mambo mengine.

Utaona hapa kila mmoja, Mungu amemjalia kwa sehemu yake. Kwa hiyo kila mmoja ana eneo ambalo hakubahatika kuwa nalo. Hebu tuangalie mfano huu. Wanafunzi wawapo darasani, wapo wanaoelewa kwa haraka zaidi somo fulani kuliko wengine. Wengine ni wepesi katika hisabati, wengine histori na wengine Geography. Inategemeana na vile alivyojaliwa.

Hivyo kama mwanafunzi mzuri unapoona somo fulani linakupiga chenga huku wenzako wakiwa wanalielewa kwa urahisi, unaumia na kukosa furaha. Kinachotakiwa ni kutafuta njia ya kutatua hali hiyo ili uwe na furaha katika eneo hilo.

Kwa mfano, kuna kijana aliyekuwa haelewi somo la historia wakati mwalimu wake alipokuwa akifundisha darasani. Hivyo kila mara mwalimu huyo alipoingia darasani alikuwa akikosa furaha.

Wakati huo, wenzake walikuwa wakilifurahia somo hilo kwa kuwa walikuwa wakilielewa vizuri pale mwalimu wao alipowafundisha.

Mwalimu wake aligundua hali hiyo kwamba kijana yule hana furaha kama wanafunzi wengine anapokuwa darasani. Na siku moja alimuuliza, ana tatizo gani ili aweze kumsaidia lakini kijana yule alimweleza kuwa hana tatizo.

Kwanza tunaona kuwa kijana yule alifanya kosa kwa kuwa hakuwa tayari kujieleza ili apate msaada kwa mwalimu wake. Hivyo ni ukweli usiopingika kuwa pale unapokuwa na tatizo na ukawa tayari kujieleza, unakuwa na amani na furaha moyoni, kwa kuwa unapata msaada zaidi. Kinyume cha hapo, unakosa furaha kila mara kipindi hicho kinapokaribia.

Kwa hiyo, tunaona kuwa mafanikio ya mwanafunzi yanapatikana pale anapokubali kuwa hawezi somo fulani, ili apatiwe msaada zaidi. Kwa upande mwingine, mtoto nyumbani anaweza kuwa na hali ya mfadhaiko na kushindwa kuwa na mawasiliano mazuri na wazazi wake, kutokana na jinsi ile wanavyomlea, kwamba wamekuwa wakali sana na hawamfundishi kwa upendo pale anapokosea.

Laiti mtoto yule angeweza kuwa wazi na kuwaambia wazazi wake hali aliyonayo inachangiwa na wao, angeweza kuwa na hali nzuri. Na ukawa mwanzo wa mahusiano mazuri kati yake na wazazi wake.

Vile vile kwa upande mwingine, ni vema wazazi wakawa wazi kwa watoto wao, pale wanapoona kuwa wamewakosea. Wawe tayari kukiri makosa hayo kwa watoto wao. Si vema mzazi akaonyesha kuwa yuko sahihi wakati wote hata kama amekosea. Ni vema kukiri kuwa jambo fulani limefanyika kimakosa.

Eneo jingine linalowanyima watu furaha ni upande wa hisia. Hapa utaona kuwa, watu wengi wamekuwa wakiugua maradhi mbalimbali, kutokana na hisia wanazokuwa nazo.

Wengine hufikia hatua ya kupungua uzito, kutokana na hali hiyo. Wengine kutokana na kupata msukosuko wa kimahusiano hufikia hatua hata ya kutaka kujiua.

Ni kweli kuwa katika maeneo yote ya maisha kanuni zinafanana. Hivyo unapokutana na tatizo ni vema kuikubali hali hiyo iliyokupata japo si jambo rahisi, ili urejeshe furaha yako uliyokuwa nayo. Na kwamba, furaha inapatikana pale tu unapokubali kuwa umepungukiwa hivyo unahitaji msaada.

Kuna swali moja la kujiuliza kwamba, kama kila mmoja kati yetu eneo fulani katika maisha ana uhitaji, kwanini basi tunakuwa wagumu kuikubali hali hiyo? Yawezekana ugumu unakuwepo kwa kuogopa kuwa, unaposema ukweli katika eneo fulani utakataliwa na jamii, rafiki ama familia.

Ama pia kukubali hali ile uliyonayo itakufanya upate aibu. La hasha, hiyo ndiyo njia sahihi ya maisha ya kujikubali na kuachana na mambo yale yanayokuumiza. Kinachotakiwa ni kujivika hali ya ujasiri bila kuogopa jambo lolote lile.

Furaha inakuja kwa mtu yule anayegundua eneo ambalo anahitaji msaada na kuwa wazi. Mafanikio yanakuja kwa mtu anayeomba kusaidia katika eneo lile aliloshindwa.

Tukutane alhamisi ijayo

FEDHA HAZIWEZI KUKUPA FURAHA

KARIBU mpenzi msomaji katika safu hii ya Maisha Yetu, inayokujia kila Alhamisi, lengo likiwa ni kujifunza mambo mbalimbali tunayoyapitia. Leo tutaangalia mambo yanayoweza kukupa furaha katika maisha.

Mara kwa mara waweza kufikiri kuwa kama ungekuwa na gari la aina fulani, nafsi yako ingeweza kufarijika. Kama ungeweza kumpata mtu mtakayeweza kuishi maisha ya ndoa katika raha na shida, ungekuwa na furaha, kama usingekuwa na hali ya msongo kutokana na ukosefu wa fedha, ungekuwa umejitosheleza.

Ni kweli unaweza kuwaza mengi zaidi ya hayo kwamba kama ungeweza kufanya jambo fulani ama kuwa na magari, nyumba, dhahabu na vitu vingine vya thamani, ungeweza kuwa na furaha, lakini hicho pia siyo kipimo halisi cha kuhitimisha furaha yako.

Sasa ni wapi ambako unaweza kuipata furaha, kama si kwenye utajiri, mazoezi, kukubalika ama kwenye mahusiano. Tunaona kuwa, ipo siri kwamba tabia yako ni muhimu kuliko hali halisi. Kinachotakiwa kufanya ni kuondoa mawazo hasi na kuwa na mawazo chanya.

Kuna mfano wa mtu mmoja aliyeona kuwa kama angekuwa na gari zuri la kifahari, furaha yake ingetimia. Kutokana na kupenda kuwa na gari, mara kwa mara alikuwa akiota kuwa na gari hilo.

Mtu huyo kila alipokuwa akijiwazia kama yupo kwenye usukani wa gari, alihisi ananusa harufu nzuri ndani ya gari. Na kwamba alihisi kama yupo barabarani analiendesha gari hilo.

Muda mfupi baadaye, alipandishwa cheo ofisini kwake na kujiona kuwa yale aliyoyatamani ameyapata. Na kwamba ataweza kujitosheleza kwa kile alichokihitaji. Baada ya kupata gari lile alilokuwa akilihitaji, alijikuta tena akitamani kila mwanamke aliyemuona, hali iliyofanya matumizi yake kuongezeka kuliko kipato kile alichokuwa akikipata.

Na kwamba wanawake aliowapenda hawakuwa na upendo wa dhati kwake, ila ni kwa kuwa walimuona anaendesha gari zuri la kifahari, kutarajia kupelekwa katika hoteli nzuri za kifahari, pamoja na kupewa zawadi nzuri za gharama.

Baada ya muda mchache alibaini kuwa, gari hilo badala ya kumpatia furaha, alipata maumivu, kwa sababu pesa yake ilitumika katika mambo ya kifahari zaidi. Taratibu alianza kufikiria gari lake na marafiki wapya aliowapata baada ya kuwa na gari, pamoja na kujiuliza kama kweli wanawake wale walikuwa wakimpenda kwa dhati ama walilipenda gari lake.

Furaha yake kuhusiana na gari lile ikaanza kutoweka, alianza kupata sononeko katika nafsi yake, pamoja na kuona gari lile kwamba ni mzigo. Hali hiyo ikamkatisha tamaa kwa yale aliyoyategemea, kwamba gari ndiyo utimilifu wa furaha katika maisha yake.

Ni vema kukumbuka kuwa vitu vinavyoonekana kwa macho haviwezi kuleta furaha ya kweli. Kwa sababu watu wanaotafuta furaha kwa kutumia fedha, ukuu walionao, utajiri ama mali walizowekeza, ni sawa na kuitafuta furaha hiyo kwa muda tu, na si ya kudumu. Kwa kuwa, siku zote fedha haziwezi kununua furaha.

Kuna mifano ya watu wengi ambao ni matajiri, lakini wamekuwa wakikabiliwa na matatizo mengi. Hawana furaha kama uliyo nayo wewe au mimi. Ni ukweli kwamba, fedha waliyonayo inawapa matatizo mengi na furaha kidogo.

Watu wengi mashuhuri wamekuwa wakiishi maisha ya kukata tamaa, matokeo yake, wengi wao huamua kujiua. Hivyo basi, furaha haipatikani kwenye utajiri, marafiki, kutumia dawa za kulevya ila ni katika kuituliza akili yako.

Tukiangalia katika maandiko matakatifu ndani ya Biblia, ambayo ndugu zetu Wakristo wanaiamini, yanasema kwamba heri wale walio maskini wa roho kwa maana ufalme wa Mungu ni wao, heri wale wenye huzuni kwa kuwa watarehemiwa. Heri wale wenye upole kwa kuwa watairithi nchi. Heri wale wenye njaa na kiu ya haki kwa kuwa watashibishwa. Heri wale wenye mioyo safi kwa kuwa watamuona Mungu. Heri wale wapatanishi kwa kuwa wataitwa wana wa Mungu.

Hivyo basi, neno heri lina maana ya furaha, hivyo bila kujali kama umeshinda ama umeshindwa, umefanikiwa ama hujafanikiwa, una furaha ama unatabika. Kwa hiyo mtu yeyote anayesoma maneno hayo na kuyarudiarudia moyoni mwake, anajikuta ni mwenye furaha wakati wote.


Tukutane Alhamisi ijayo.

HOFU HUSAIDIA KUEPUKA HATARI

KARIBU mpenzi msomaji katika safu ya Maisha Yetu inayokujia kila Alhamisi. Leo tutaangalia mbinu za kuwa jasiri katika uamuzi wako unaoufanya.

Katika maisha yetu ya kila siku, tunaona kwamba mbinu za kuwa jasiri ni nzuri katika kukabiliana na hatari iliyo mbele yako. Lakini kwa wakati mwingine, mtu anapokuwa na hali ya hofu inamsaidia kutokana na sababu iliyopo.

Ama tunaweza kusema unapokuwa na hofu, hali hiyo inakusaidia kwa kusudi maalumu. Ila kuna baadhi ya watu ambao hufikiri kuwa, si vizuri mtu kuwa na woga ama hofu. Lakini hii si kweli.

Kwani hali ya hofu husaidia, ni ishara katika ubongo wako kwamba pale huenda pakawa na hatari. Zipo sababu nzuri zinazopasa kuwa na hofu, kwa kuwa hofu inayozungumza ndani yetu ni vema kuilinda mwenyewe.

Kutokana na hofu unapokumbana na jambo, unajikuta hufikiri cha kufanya kwa wakati huo, ila unajikuta unaondoka katika eneo hilo kwa haraka.

Pia kuna baadhi ya watu wamejijengea tabia kama ya watoto wadogo ya kutokuwa na woga katika maisha yao. Lakini wakumbuke hali hiyo mara nyingine huwaletea matatizo.

Kwa mfano watoto wanapokuwa sio waoga, huwa na sehemu ya kuegemea ambayo ni wazazi wao. Wanakuwa hawana woga wa kuruka katika maeneo hatarishi, wakijiona kuwa wako salama.

Hivyo, kama watu wazima watafanya michezo ya kitoto watajikuta wakipoteza maisha kutokana na hatari mbalimbali kama vile ajali za barabarani au ugomvi.

Woga maana yake unatuepusha na hatari zilizoko mbele yetu. Hofu ipo ili kuwakinga watu wasipoteze vitu vyao vya thamani, kama vile pesa. Watu ambao hawana hofu ya kupoteza fedha zao, huzifanyia kazi zisizo na faida na baadaye kusababisha hasara kwao.

Pia hofu, humfanya mtu aliyepewa jukumu la kusimamia jambo fulani, kujiandaa mapema ili asiharibikiwe. Hebu fikiria mtu hana hofu anapohojiwa kwenye mhadhara kuhusu jambo fulani huku akiwa hana upeo nalo, pia hajajiandaa. Matokeo yake katika mjadala huo huonekana mjinga. Hivyo hofu humfanya mtu kuwa makini, pamoja na kuwa na maandalizi mazuri.

Unapaswa kuwa na hofu ili kuweza kujiandaa na hatari zilizo mbele yako, kama za kimaumbile, kifedha ama kijamii. Kama mvua zisiponyesha ina maana kutakuwa na njaa. Hivyo taifa lolote lililo makini hutafuta njia mbadala ya kukabiliana na hali hiyo.

Hii ni kutokana na hofu huenda siku za mbeleni, wananchi wakakosa chakula na kupata utapiamlo ama kufariki dunia. Lakini pia, ukumbuke kuwa, hali hiyo ikizidi inaingilia uhuru wa maisha yako. Watu wengi wamejikuta wakiwa na hali ya hofu ama woga kupita kiasi. Hali ambayo si nzuri kwao.

Kwa sababu hofu ni hisia zinazofanya damu yako ichemke, na mara nyingi unajikuta unahamaki kwa kusema kuwa ‘aah! Ngoja nitoke eneo hili ni la hatari’.

Na kama hali hiyo itakuwa inakutokea mara kwa mara, linakuwa sasa ni tatizo ambalo unatakiwa kulitatua. Kwa kawaida kila mmoja anakuwa na kiwango kidogo cha hofu isiyo ya kawaida.

Kwa mfano unakuta daraja kubwa linajengwa na kuanza kupatwa na hofu kwamba daraja hilo litabomoka. Huhisi hivyo hata kama inaonekana kuwa kwa hali ya kawaida si rahisi kwa daraja hilo kubomoka. Hilo ni tatizo linalohitaji ufumbuzi.

Wengine wanakuwa na woga wa kufanya mazoezi mbalimbali ya darasani, matokeo yake wanakwepa kabisa ama kufanya vibaya. Bahati nzuri ni kwamba kuna njia muafaka ya kuondoa hali hiyo, kwa kutathmini tatizo lililopo.

Kama vile, kuwa na mbinu ya ujasiri, ili kuweza kukabiliana na hali hiyo, kwa kuangalia ukubwa wa tatizo. Kwa mfano; mwanafunzi anatarajia kufanya mtihani wake, ambao una maswali 100; amejiandaa vizuri. Japo mwanafunzi anakuwa na hofu ya kushindwa kwa baadhi ya maswali, lakini kwa kuwa alishajiandaaa vizuri atakuwa katika nafasi nzuri.

Nini cha kufanya kuhusu hofu na hatari iliyopo. Cha msingi ni kuangalia ukubwa wa hali hiyo na kuitatua kabla. Kwa mfano, mtu anayehofu kuwa malipo yake yatapunguzwa. Hataogopa kwa hilo, bali atakuwa na hofu kwa kuwa hakutegemea hali hiyo.

Ili kukabiliana na hali hiyo ni vema kutafuta kazi nyingine itayomlipa zaidi, kwa kufanya hivyo atakuwa amelikabili tatizo hilo. Kuna mambo tunayoweza kuyafanya ya kuondoa hali hiyo ya hatari, iwe kubwa ama ndogo. Kuna mambo matatu ya kufanya tunayoweza kuyachagua.

Mojawapo ni homoni zinazoshtua mfumo wa damu, wakati upatwa na jambo linalokutia hofu. Homoni hizo zinasaidia kama mtu anataka kukimbia ama kujikinga na jambo.

Zinafanya mwili kuwa na utayari wa jambo lolote. Pia ni vizuri kujiepusha ama kuondoka katika sehemu inayoweza kuwa na hatari. Maana yake ni kwamba kama upo kwenye eneo hilo la hatari, yakupasa kuondoka mara moja.

Kwa kufanya hivyo, utakuwa umefanya uamuzi wa busara. Vema kujijengea uwezo na kuwa tayari katika kupambana na jambo la hatari. Hilo litakuwezesha kukabiliana na jambo lolote kwa urahisi.

Mfano kama wewe ni mwimbaji mzuri yakupasa ujiandae vema. Pia kufanya majaribio kunafanya kazi yako iwe nzuri yenye kiwango cha kuridhisha. Inamaanisha kuwa, unaiandaa akili yako kuimba mbele ya watu katika tamasha.

Hebu fikiria kuwa una hofu ya kuendesha gari, ni vema kukaa mbali na usukani. Kujijengea uwezo na maandalizi kunakufanya uwe mwangalifu na kumwangalia mwingine wakati anapoendesha. Hukufanya ujifunze mengi kupitia kwa mwingine, mwishoni hofu hiyo itaondoka.

Tukutane wiki ijayo.

ZUNGUMZA NA MTOTO WAKO ASIPATWE NA MSONGO

KARIBUNI wapenzi wasomaji katika siku nyingine ya leo, ambayo Mwenyezi Mungu ametujalia kuiona tena. Tunakwenda kuangalia hali ya msongo inayowakabili watoto pamoja na vijana wadogo.

Ni ukweli usiopingika kuwa hali ya msongo inakuwepo katika hatua zote za maisha ya binadamu. Tunaona watoto wengi wenye umri wa miaka mitano na kuendelea, wamekuwa wakiona vitu mbalimbali katika nyumba zao ambavyo hufanywa na wazazi wao.

Kwa mfano, kuna familia nyingine kila mara wazazi hugombana mbele ya watoto wao. Kama wazazi tuelewe, hali hiyo huleta hofu kwa mtoto na kuona kuwa baba au mama yake anaweza kumpiga wakati wowote. Wakati mwingine unakuta mzazi anaumwa na jino, maumivu anayoyapata anayaonyesha mbele ya mtoto wake, hali hiyo humjengea hofu.

Kwani kuanzia hapo, inawezekana kabisa, mtoto huyo akapatwa hali ya woga na hofu, juu ya meno yake. Hata pale atakapoumwa atalia na maumivu makali. Tukiachana na hofu hiyo, hofu nyingine kwa watoto ni pale wanapomuona daktari au hospitali.

Inawezekana kwa wakati huo, mtoto haumwi lakini, anapomuona daktari akiwa amebeba sindano au vifaa vya hospitali,akiwa anatembea maeneo ya shuleni ama sehemu yoyote, hata kama daktari hana mpango wa kuongea na mtoto huyo, mtoto hubadilika muda huo huo, wengine huanza kulia.

Hivyo, kwa haraka haraka utaona ni jinsi gani mtoto anakuwa hajaandaliwa kukabiliana na mazingira mbalimbali ili asikabiliwe na hali ya wasiwasi katika maisha yake. Kuna maeneo mawili ambayo watoto hupatwa na hali ya msongo katika maisha yao, ambayo dalili zake huonekana kwenye maumbile ama tabia zao.

Tukiangalia kwenye dalili za kimaumbile, ni kama vile kupatwa na gesi tumboni, kupatwa na hali ya ubaridi kwenye viganja vya mkono na unyayo.

Hali ya kukosa choo, kuharisha, kukaukiwa midomo, uso kubadilika, tumbo kuvurugika, mikono kutetemeka, kichwa kuuma, moyo kudunda pamoja na kutokwa na jasho.

Nyingine ni mtoto kuuma kucha zake, kuwa na hofu, uso kuwa na mafuta, hali ya kutetemeka, kupumua kwa shida, kutokwa na jasho mikononi na miguuni, meno kukakamaa, kukaza kwa misuli, kukaza kwa tumbo na macho kuwa mazito.

Kwa upande wa dalili za tabia ni kama vile, kupata ajali na kuanguka kwa kuelekea mbele, kupenda ugomvi, kujilinda, kuwa tegemezi, kushituka shituka, kuwa na hofu, kutopenda kuwasiliana na watu, kuumwa mara kwa mara na kuchoka, kujiamini kupita kiasi, kuwa na hisia zilizopitiliza, kutopenda kujishughulisha na kitu, kukosa nidhamu, utukutu, mwenye mambo ya kuficha ficha, kukata tamaa haraka na kutokuwa na ushirikiano.

Pia anakosa utulivu wa kusikiliza jambo, anakuwa na tatizo la mara kwa mara la kulala na kuota ndoto za kuzungumza kwa sauti, hupenda kuzungumza uongo ama kupotosha ukweli, anachukulia vitu kama si vya kwao, maendeleo yake ya shule hushuka, anakuwa na mwonekana mbaya pamoja na umaridadi wake kupungua, anakosa hamu ya kupenda kujua vitu bila sababu ya msingi, ana kuwa na mabadiliko katika ulaji wake wa chakula, anaweza kula chakula kidogo ama kingi sana.

Mzazi ama mlezi huweza kubaini mabadiliko hayo kwa mtoto, kama anakuwa na uhusiano wa karibu na mtoto huyo.

Pia ni vizuri pale unapobaini mabadiliko hayo, uendelee kuwa karibu zaidi na mtoto huyo. Ni vizuri kumuandalia mlo uliokamilika, wenye virutubisho vyote, mpe nafasi ya kufanya mazoezi na kupumzika, mtie moyo aweze kusaidia shughuli ndogo ndogo na kumpa vichekesho.

Pia ni vizuri kuwaruhusu watoto wazungumzie mambo yale yanayo wakosesha raha, kwani wakati mwingine watoto waliokuwa kidogo hali hiyo husababishwa na kujiingiza katika mahusiano baina ya watoto wa kike na kiume.

Kwa upande wa wale watoto wenye umri kati ya miaka 9 na 20; mara nyingine hupatwa na hali ya msongo kutokana na umri huo, kwani hudhani kuwa wanaweza kujitawala wenyewe kwa kila jambo, hujihusisha kwenye mahusiano yasiyofaa, na wanapoonywa hufikiria kuhama nyumbani na kuwaacha wazazi wao.

Kipindi hicho, wazazi nao hupatwa na msongo kutokana na kitendo cha watoto hao ambao kuwa na maamuzi yao wenyewe, hali inayowafanya waondoke nyumbani. Wazazi huwaza kwa kuona watoto bado wanahitaji msaada kutoka kwao.

Hivyo, ni jukumu la wazazi kutumia nafasi hiyo kuwaelimisha watoto wao, kuwa vile wanavyofikiri sivyo maisha yalivyo. Pia wazazi wanapogundua mabadiliko mbalimbali juu ya watoto wao, ni vema kuchukua hatua za haraka na kuwasaidia kuliko kuwaacha wakaharibikiwa.

Mara nyingi wazazi wanaowafuatilia watoto wao, hugundua mapema kuwa, watoto wameshuka kimasomo ama hawapendi kwenda shule, ama mtoto kwa kipindi hicho badala ya kuwaza kusoma anafikiria kuacha shule na kufanya kazi.

Watoto wengine hukatiza kozi wanazozisoma, si kwa sababu wamekuwa hawafanyi vizuri bali ni kutokana na kutaka kuwa na ushindani wa kupata maisha bora, wakati anakuwa hajamaliza hata masomo yake. Kwa upande wa watoto wa kike, hali hiyo huwafanya kupata mimba wasizozitarajia, ama kuwaza kujiua.

Wengine hujiingiza kwenye ulevi ama mihadarati. Lakini kwa kufanya hivyo hawawezi kupata suluhisho, hivyo ni vema watoto wanapokumbana na hali hiyo kuidharau na kuendelea na masomo yao, wakielewa kuwa kipindi hicho ni cha muda tu, la maana ni kuongeza bidii katika masomo.

Hivyo, ni vema kukaa na mtoto wako na kumfundisha mambo mbalimbali ili aweze kuendelea katika dunia hii iliyojaa misukosuko ya maisha. Penda kumsikiliza mtoto wako na kumshauri jambo zuri na baya. Pia mtie moyo kwa matarajio yaliyoko mbele yake kwamba akimaliza masomo yake ya msingi, atakwenda sekondari, halafu chuoni, baada ya chuo atapata kazi nzuri ili awe na ari ya kusoma.

Tukutane wiki ijayo.


WANAWAKE HUKABILIWA NA MSONGO KATIKA MAZINGIRA TOFAUTI

KARIBU mpenzi msomaji katika siku nyingine ambayo Mwenyezi Mungu ametujalia pumzi na uhai. Leo tutaangalia hali ya msongo inayowakabili wanawake.

Wanawake wengi duniani, wamekuwa wakikabiliwa na changamoto nyingi, hali inayowafanya kupatwa na hofu, wasiwasi pamoja na kutojiamini.

Changamoto nyingi huwakabili wanawake hao katika maeneo yao ya kazi, nyumbani na hata katika mazingira mbalimbali wanayokuwamo.

Kwa mfano, kuna msemo usemao kuwa, binadamu wote ni sawa, lakini ukifuatilia msemo huo utaona kuwa, mara nyingi baadhi ya wanaume hawataki kukubaliana na msemo huo, kwa maelezo kuwa, wanawake hawana uwezo wa kufanya kazi zile ambazo wao huzifanya kwa umakini na uhodari.

Kutokana na hali hiyo, ndiyo maana katika siku hizi za leo, wanawake nao wamekuwa wakihamasishana kugombea nafasi mbalimbali za uongozi katika serikali na kwenye ofisi mbalimbali, ili nao waonyeshe kuwa wanaweza kuongoza.

Pamoja na jitihada hizo, wanawake wamejikuta katika kipindi kigumu, pale wanaposhika nyadhifa mbalimbali, hujikuta wakidharauliwa ama kutokukubalika katika jamii, hata kama ana uwezo wa kuongoza, cha msingi ni kukabiliana na changamoto hizo, endapo unajiamini na kujiona kuwa una viwango vya kuwa kiongozi bora, na si bora kiongozi.

Wengine kwa fikra zao hudhani kuwa, wanawake hawawezi kuwa viongozi bora kwa sababu ya mwonekano wao, huamini kuwa, wanawake wengi hawajiamini.

Kutokana na changamoto hizo, wanawake wengi walio katika nafasi mbalimbali za uongozi hujikuta wakikabiliwa na hali ya msongo, inayomfanya kushusha kiwango chake cha utendaji na kuwapa nafasi nzuri wanaume kuamini kuwa wao pekee ndiyo wanaweza.

Lakini utafiti mwingine umebaini kuwa, wanawake wenye uwezo na elimu ya kuridhisha wamekuwa wakijiamini kuwa wanaweza, hali iliyowafanya kukubalika katika maeneo wanayoyaongoza.

Vile vile kwa suala la maumbile, wanawake wengi wamejikuta wakikabiliwa na hali ya woga, ama hofu ya kupoteza kazi. Wanawake hukabiliwa na changamoto ya kuona siku zao katika kila mwezi, hivyo wapo ambao huumwa sana hata kuwafanya walazwe hospitali ama kushindwa kwenda kazini kabisa.

Hali hiyo, huwafanya wakose amani, furaha ama hofu ya kwamba, huenda wakafukuzwa kazi.

Na wengine hujitahidi kwenda hivyo hivyo kazini lakini hujikuta wanapatwa na maumivu makali ya viungo, kichefuchefu, tumbo kuuma, macho kuwa mazito na hali ya kukata tamaa.

Katika hali kama hiyo, ni uhakika kuwa hataweza kuendelea na kazi zake hivyo itambidi arudi nyumbani na kwenda kupumzika.

Hivyo ni vema kwa kila mwanamke kujikubali katika hali hiyo aliyonayo, ili asiruhusu hali ya wasiwasi katika maisha yake, inayoweza kumwongezea maradhi mengine ya ziada.

Vile vile msongo huwapata baadhi ya wanawake, pale anapokaa muda mrefu bila kupata mtoto. Hivyo asipokuwa makini na kukabiliana na hali hiyo mwili wake utapatwa na maradhi mengine ambayo hakuyatarajia.

Vile vile hupatwa na msongo pale anapohisi maumivu makali kipindi cha kujifungua, ama kujifungua mtoto mwenye matatizo kiafya.

Pia kushindwa kuzaa kwa njia ya kawaida na kumfanya afanyiwe upasuaji, vitendo vya udhalilishwaji anapokuwa kwenye wodi ya wazazi wanaosubiri kujifungua, upungufu wa wakunga au kusikia kelele katika wodi hiyo.

Wengine hufikiria kuwa, waume zao hawatakuwa tayari kumfurahia mtoto aliyezaliwa, kutofurahia ndoa yake pamoja na kuruhusiwa kutoka hospitalini, huku akiwaza mtu wa kumsaidia anaporudi nyumbani kwake.

Hofu zote hizo zinazowakabili wanawake, huwafanya kutokujiamini na kuongeza msongo katika maisha yao.

Wengine hufikiri kuwa, endapo waume zao wangekuwepo wakati wanapojifungua, hofu hiyo ingewatoka.

Pia wanawake wengine hukabiliwa na hali ya hofu na wasiwasi, kipindi kile anachonyonyesha, hasa wakati wa usiku.

Vile vile wanawake hukabiliwa na hofu na wasiwasi pale wanapotengana ama kufiwa na waume zao, pia wanapopewa talaka.

Kutokana na matatizo hayo, hali yake ya kawaida huondoka na kama hatapata msaada wa haraka anaweza kupatwa na magonjwa mbalimbali yatakayodhoofisha afya yake.

Hata pale wanawake hao, wanapofiwa na watoto wao wachanga hukabiliwa na msongo. Utafiti uliowahi kufanywa ulibaini kuwa, baadhi ya wanawake wanapofiwa na watoto wao, hujiua ama hupata ajali kutokana na kuwa na mawazo mengi wakati wanapotembea.

Wengine hufariki dunia kwa maradhi ya moyo, kansa ama ugonjwa mwingine. Hivyo, ni vema kila mmoja akaigundua hali hiyo mapema na kuidhibiti, kwa kupata ushauri kutoka kwa daktari.

Wakati mwingine mwili wake hudhoofika kwa kuwa hapendi kula, ama huwa anachagua vyakula vya kula, ama jambo analolifikiri kwa kipindi hicho.

Hali hiyo huweza kudhoofisha mwili wake hata mifupa. Kwani mlo usio kamili ama kula bila kufuata mpangilio, kunaathiri uimara wa mifupa mwilini.

Pia wanawake wengi wanakabiliwa na suala la msongo kutokana na suala la kiuchumi, pale wanapoona wanashindwa kukabiliana na maisha hujikuta na hofu pamoja na wasiwasi, kwa kuwa, wengi wao hawapati msaada kutoka kwa waume zao.

Kutokana na hali hiyo wanayokabiliana nayo, wanawake wengine hujikuta wakijiingiza kwenye ulevi wa kupindukia kwa nia ya kuondoa mawazo, hali inayowafanya kushindwa kufanya kazi kwa bidii.

Tukutane Alhamisi ijayo

MSONGO KATIKA SEHEMU ZA KAZI (4)

NAWAKARIBISHA tena katika safu hii ya Maisha Yetu yenye lengo la kukufahamisha jinsi maisha yalivyo na yanavyopaswa kuwa.

Leo tunaendelea na mada yetu ya msongo katika maeneo ya kazi ili uweze kujua jinsi ya kukabiliana na hali hiyo mara unapokutana nayo.

Watafiti mbalimbali wamegundua kuwa, endapo bosi katika kampuni, atakuwa na hali ya msongo wa mawazo, ofisi, kampuni au shirika hilo litakuwa na mawasiliano mabaya.

Naye mwanasaikolojia mmoja anayeshughulika na masuala ya viwandani amewahi kuelezea jinsi meneja mzuri anavyopaswa kuwa.

Kwa maelezo ya mwanasaikolojia huyo, meneja mzuri anapaswa kuwa mshauri mzuri kwa wafanyakazi wake, ari ya kupenda kujituma, kupenda kufanya kazi na kushirikishana mambo mbalimbali na wafanyakazi wake.

Kwa maelezo ya mwanasaikolojia huyo, endapo bosi atakuwa karibu na wafanyakazi wake, ushauri mwingi utakaotoka kwa wafanyakazi hao, utampa mwanga wa kujua nini cha kufanya kwa kipindi hicho katika kuboresha ofisi.

Ndiyo maana katika ofisi nyingi ni rahisi kutambua sababu za meneja fulani kuwa mzuri, au wa kawaida ama mbaya katika utendaji wake, kutokana na jinsi anavyojishughulisha na watu wake.

Meneja mzuri ni yule anayependa kuwa karibu na wafanyakazi wake, kuwasikiliza na kufuatilia uzalishaji unavyokwenda katika kampuni.

Pia anakuwa mwadilifu katika utendaji wake, hatetereki katika malengo yake ya uzalishaji, pia huwasikiliza wafanyakazi wake wanapokuwa na mahitaji.

Bosi wa wastani katika utendaji wake, ni yule anayeangalia ufanisi wake pekee, bila kuona umuhimu wa wengine. Kama vile wanavyowajibika katika kazi zao.

Kwa upande wa bosi mbaya ni yule anayefanya kazi kwa kutumia vitabu, pamoja na kujenga hali ya kujilinda kila wakati.

Utafiti mwingine uliofanywa, ulionyesha kuwa, msongo katika kazi unawafanya watu wengi kutumia vileo na kujikuta wanashindwa kufikia malengo katika kazi zao, hali inayowafanya kufukuzwa kazi.

Wengine wanaokabiliwa na msongo, hutumia dawa za kulevya, hali inayowafanya kupatwa na magonjwa ya akili, kuathiri utendaji wao katika uzalishaji na kuhatarisha ajira walizonazo.

Utafiti mwingine unaonyesha kuwa, msongo mwingine kwa wafanyakazi huchangiwa na uamuzi unaofanywa na kampuni kwa kuwapunguza kazini wafanyakazi kutokana na sababu mbalimbali.

Hivyo basi, ni vyema kwa mameneja katika ofisi zao kuzungumza na kuwasikiliza wafanyakazi wao.

Pia wawe wanawauliza wafanyakazi hao kuchanganua mambo matatu yanayoweza kuboresha kampuni au ofisi hiyo na mambo matatu yatakayoweza kuzorotesha uzalishaji katika kampuni hiyo.

Bosi huyo apende kujua kama mazingira wanayofanyia kazi wafanyakazi wake, yanaridhisha.

Ni vema bosi kuwaheshimu watu aliowaajiri ama anaowasimamia katika kampuni hiyo na kuwajulisha kuwa yuko tayari kushughulikia taarifa yoyote itakayomfikia.

Ni vema wafanyakazi wakawa wanashirikishwa katika maamuzi yanayofanyika ili wajione nao ni sehemu ya ofisi hiyo.

Si mbaya wakaorodhesha matatizo mbalimbali yaliyowapata wafanyakazi na kuangalia jinsi ya kuyashughulikia.

Ni vizuri kiongozi huyo akawa anaongoza kwa vitendo. Asiwe mwepesi wa kuzungumza.

Hayo yote yatakapoweza kutekelezwa na mameneja ama waajiri wa kampuni, msongo katika eneo hilo la kazi hautawapata wafanyakazi wake.

Ugonjwa mbaya katika kampuni ni ile hali ya wafanyakazi kukosa ari ya kufanya kazi kutokana na msongo wanaokabiliana nao.

Hiyo ni pamoja na kupunguza ari ya kupenda kazi kwa wafanyakazi, utendaji mbovu na unaopunguza uzalishaji, kuongezeka kwa magonjwa miongoni mwa wafanyakazi, wafanyakazi kuchelewa kazini hali inayosababisha kampuni hiyo kutokufikia malengo iliyokusudia.

Vile vile baada ya kampuni kupunguza wafanyakazi, wale wanaobakia nao wanaendelea kupatwa na hali hiyo ya msongo kwa kuwa, kunakuwa na ongezeko kubwa la kazi hali itakayowafanya washindwe kupata muda wa kupumzika.

Tukutane alhamisi ijayo

MSONGO KATIKA SEHEMU ZA KAZI (3)

KARIBUNI wapenzi wasomaji katika siku nyingine ambayo Mwenyezi Mungu ametujalia kuiona.

Leo tutaendelea kuangalia mada kuhusu msongo katika sehemu za kazi.

Wengi wetu tumekuwa tukikabiliana na hali ya msongo katika vipindi mbalimbali vya maisha, kuanzia kipindi cha utoto hadi uzee.

Hali hiyo humpata mtu anayefanya kazi, mzazi katika kipindi cha kulea watoto wake na katika vipindi mbalimbali vya maisha.

Ila humjia kila mmoja kwa jinsi yake.

Mafanikio yetu katika maisha na thamani ya maisha, inategemea ni jinsi gani tunavyokabiliana na hali hiyo.

Tunahitaji kuelewa msongo ni kitu gani na kujifunza jinsi ya kukabiliana na hali hiyo.

Mtaalamu mmoja aliwahi kuelezea fani saba ambazo haziepukiki katika suala la msongo, ambazo ni fani ya ualimu, uuguzi, umeneja, ustawi wa jamii, udereva, upolisi na ofisa magereza.

Je, umejiona katika kundi lolote hapo juu? Usijali kuhusu hilo, cha msingi ni kujua unafanya nini na jinsi gani ya kujiepusha na msongo katika kazi yako.

Pia inawezekana wewe ni miongoni mwa watu zaidi ya 200,000 ambao hupatwa na maradhi yanayotokana na hali ya msongo katika kazi zao, kila mwezi na kulazimika kupumzika nyumbani ili kuondoa hali hiyo.

Pia yawezekana kwamba, wewe ni miongoni mwa asilimia 27 ya watu wanaolalamikia mazingira ya kazi zao, ama kati ya asilimia 19 ambao hawana mazingira bora ya kufanyia kazi, au asilimia 17 ya wale ambao ofisi zao haziko katika muundo wa kisasa hivyo kufanya kazi zao kuwa ngumu, kwa kuwa hakuna mwanga au hewa ya kutosha.

Pia yawezekana umo miongoni mwa asilimia 14 ya wale wafanyakazi ambao hawana nafasi ya kutosha ya kukutana na wenzao, kutokana na kazi kuwa nyingi, asilimia 13 ya wale ambao hawajaridhika na eneo ambalo ofisi yao ipo, asilimia 12 ya wale wasio na vifaa vya kisasa ofisini kwao, asilimia 5 ya wale wanaolalamika kuhusu kukosa uhuru wa kuvuta sigara ama mazingira wanayofanyia kazi hayana uhuru wa kumfanya avute sigara na asilimia nne wanakosa ushirikiano na wafanyakazi wengine.

Je, hofu kuhusu kazi yako inaongezeka bila kupata suluhu? Uamuzi wako wa mwisho ni kubadili kazi na kuchukua tahadhari kwa hatari unazoweza kukabiliana nazo katika kazi hiyo mpya.

Lakini lazima uchukue tahadhari, kwa sababu ni gharama.

Pia utaona kuwa, mpangilio mbaya wa kazi zako unaweza kukusababishia maradhi.

Utawala mzuri huwafanya wafanyakazi kuwa na afya bora, hivyo uzalishaji unakuwa mzuri pia.

Utafiti mwingine uliofanywa kwa wafanyakazi 600, asilimia 60 kati ya hao wamewalalamikia watengenezaji wa barabara kuwa wanachangia msongo katika maisha yao, kutokana na kusababisha foleni wawapo barabarani, asilimia 40 wamesema kuwa, malengo waliyojiwekea hawajaweza kuyafikia hivyo yanawasababishia hali hiyo.

Wengine walisema kuwa, hali ya hofu na wasiwasi wanayoipata wanasababishiwa na rafiki zao, ama kutoelewana kwa wafanyakazi ndani ya ofisi.

Pia katika ofisi nyingi, suala la mapumziko limekuwa ni kitendawili, wafanyakazi hawapati mapumziko wawapo kazini, hali inayosababisha hofu, wasiwasi na hasira za mara kwa mara.

Ni wafanyakazi wachache wanaoweza kupata muda wa mapumziko na kwenda kupata chakula cha mchana, wengine kutokana na muda kuwa mdogo kwa ajili ya kazi nyingi hujikuta wakipitisha mchana bila kula chakula.

Vile vile haijalishi wewe ni nani, unaweza kukabiliwa na msongo katika mazingira ya ofisi.

Tuangalie mfano wa sekretari, ambao wamekuwa wakisumbuliwa na hali ya hofu na wasiwasi katika kazi zao.

Hivyo msongo mkubwa huwakabili kutokana na kazi zao za kila siku wanazozifanya.

Sekretari hupatwa na msongo pale anapokuwa ana kazi nyingi mara simu inaita au wageni wanafika na kuuliza habari mbalimbali zinazomhusu bosi wake, ilhali kipindi hicho anahangaika akamilishe kazi ya bosi wake anayoisubiri ili aanze kikao.

Vile vile hupatwa na msongo pale mashine yake ya kutolea ‘photocopy’ inapokwamisha karatasi au kukwama ama inaposhindwa kufanya kazi kwa kipindi hicho anachohitaji kuitumia huku akiwa anakabiliwa na kazi nyingine.

Wakati huo huo, kunakuwapo na watu wanaosubiri kuweka ahadi ya kuongea na bosi wake, ambao hawako kwenye ratiba ya siku hiyo.

Vile vile hukabiliwa na msongo pale anapopata kazi nyingine ya dharura ilhali alishajiandaa kwenda nyumbani.

Mbali na hali ya msongo wa kawaida, wanayokabiliana nayo katika shughuli zao za kiofisi, kwa upande mwingine hulalamika kupewa kazi za dharura na mabosi wao, wakati hakuna posho.

Wanapewa kazi zinazopoteza nguvu zao na kuwafanya washindwe kuwasiliana na watu wengine, pia wapo wanaolalamikia masuala ya ngono.

Hayo yote yanajumuisha mazingira mabovu ya ofisi, muundo mbaya wa viti vya ofisi ambavyo havimpi starehe mtumiaji na badala yake vinamfanya achoke na kuchukia mazingira ya ofisi anayofanyia kazi.

Hivyo unapoona una dalili ya kuchoka, ama kuumwa mara kwa mara, ni vema kuangalia afya yako ilhali isiwe mbaya zaidi.

Utafiti uliofanywa katika nchi za wenzetu mwaka 2003, ulibaini kuwa, asilimia 35 ya mabosi wamekuwa wakikubali majukumu mbalimbali ya ofisi zao ili kuwafanya wafanyakazi wao, wasipate msongo ama kupunguza hali hiyo kabisa.

Tukutane wiki ijayo

MSONGO KATIKA SEHEMU ZA KAZI

KWA mara nyingine nawakaribisha tena katika safu hii ya Maisha Yetu, inayokujia kila Alhamisi, lengo likiwa ni kuelimisha.

Wiki iliyopita tulizungumzia kuhusu msongo katika maeneo ya kazi, tuliona sababu zinazosababisha mtu kupatwa na msongo katika eneo la kazi ni hofu, ongezeko la muda wa kazi, ilhali masilahi ni madogo na msisitizo wa kuongeza uzalishaji kazini wakati hakuna ongezeko la marupurupu yoyote.

Leo ni mwendelezo wa makala ile na tutaangalia jinsi ya kuondoa hali hiyo, ambayo kwanza inakubidi ujijali wewe mwenyewe.

Wakati msongo katika kazi yako unaingilia uwezo wako wa kufanya kazi, ni vema kujijali wewe mwenyewe, au kusimamia maisha yako mwenyewe, ni wakati wa kuchukua hatua.

Wakati unapodhamiria kujali mahitaji yako, unakuwa na nguvu ya kushinda hali hiyo ya msongo.

Vile vile unavyojihisi, unavyoweza kujizatiti, ndipo utakapoweza kusimamia kazi yako bila kuendelea kujisababishia msongo mwingine.

Kujijali mwenyewe hakujalishi maisha uliyonayo kama ni ya kifahari au la. Hata katika kufanya vitu vidogo vidogo vinaweza kuinua tena hali yako ya kuvunjika moyo na kukata tamaa, vitu hivyo vinaweza kukuongezea nguvu.

Fanya kitu kimoja kwa wakati na kufanya vile ulivyoamua maisha yako yawe, hapo utagundua kuwa kuna tofauti katika hali ile ya msongo uliyokuwa nayo, nyumbani hata kazini kwako.

Vile vile unaweza kuondoa hali hiyo kwa kuangalia picha mbalimbali. Kwa kufanya hivyo kunaweza kuinua tena hisia zako, kukuongezea nguvu, kukufanya uwe na matarajio ya baadaye na kutuliza akili na mwili wako.

Kwa kiasi kikubwa utaondoa hali iliyokuwa inakutesa. Pia kutengeneza chakula unachokipenda kutakufanya ujisikie vizuri.

Unapopangilia mlo wako, hata kama ni kidogo kutakufanya upate nguvu katika mwili wako na kujisikia vizuri.

Ili kuondokana na hali hiyo ni vema, kulala usingizi wa kutosha. Kwani hali hiyo inakufanya ukose usingizi.

Lakini hali ya kukosa usingizi, inaweza kukusababishia ukapatwa na maradhi mengine.

Unapolala na kukosa usingizi, hali hiyo inakuweka katika hatari ya kuwa na msongo zaidi. Lakini wakati unapokuwa umepata mapumziko mazuri, inakuwa ni rahisi kukabiliana na hali hiyo ya msongo.

Pia unaweza kuondoa hali hiyo kwa kutoa vipaumbele na kuwa na mpangilio katika kazi zako.

Wakati unazungukwa na hali ya msongo katika kazi na eneo lako la kazi, unaweza kukabiliana na hali hiyo kwa kuamua kuikubali hali hiyo ngumu inayokutesa na kujitahidi kukamilisha kazi zako kwa wakati.

Jitahidi kujitawala katika kazi zako wewe mwenyewe bila kusaidiwa na mtu, pamoja na kujenga mahusiano bora katika kazi.

Haya ni baadhi ya mapendekezo katika kupunguza hali hiyo kwa kutoa vipaumbele na kuwa na mpangilio katika majukumu yako.

Baadhi ya mambo yanayoweza kukuondolea hali hiyo

Ni vema kutengeneza ratiba. Changanua utaratibu wako wa kufanya kazi, majukumu, na shughuli za kila siku.

Kamwe usivuruge utaratibu uliojiwekea kwa kazi isiyokuwepo. Jaribu kutafuta uangalifu kati ya kazi, maisha ya familia, shughuli za kijamii na mambo binafsi na majukumu ya kila siku.

Kamwe usijiwekee ratiba zilizo nje ya uwezo wako. Epuka kuwa na ratiba ya mrundikano wa kazi katika siku moja.

Unapokuwa na ratiba ya kazi nyingi kwa siku moja, mara nyingi kazi hizo hufanywa chini ya viwango.

Ondoa kazi zile ambazo hazina umuhimu kwa siku hiyo katika ratiba yako.

Jaribu kuondoka mapema muda wa asubuhi. Dakika moja mpaka 15; zinaweza kufanya tofauti kwa kuweza kukamilisha kazi zako vizuri kwa siku hiyo na kukurahisishia utendaji wako wa siku hiyo.

Kamwe usijiongezee kiwango cha msongo unaokukabili kwa kuendelea kuchelewa ofisini.

Ni vema kuwa na ratiba ya kupumzika. Hakikisha unakuwa na muda mfupi wa kupumzika kwa ajili ya kuisafisha akili yako.

Pia ni vema kwenda mbali na meza yako unayofanyia kazi kwa ajili ya kupata chakula.

Na kwa kufanya hivyo kunaongeza ari yako ya kufanya kazi, kinyume cha hapo kutakufanya uwe na uzalishaji mdogo.

Mambo yanayoweza kukuondolea msongo katika kazi yako endapo wewe ndiyo mmiliki mkuu, ama mkurugenzi ni pale, unapotoa kipaumbele kwa kazi zilizopo.

Andika ratiba ya kazi unazoweza kuzifanya na uzifanye kulingana na umuhimu wake. Anza na kazi ile yenye umuhimu. Na kama una jambo la muhimu, ni vema kuamka mapema.

Kwa kuamka mapema, shughuli nyingine za siku hiyo zitakuwa na matokeo mazuri.

Ni vema kukabidhi majukumu yako kwa wengine. Huwezi kufanya kazi zote wewe mwenyewe, iwe nyumbani, shuleni au kazini.

Kama wapo watu wengine wanaoweza kufanya kazi hiyo, ni vema ukawashirikisha.

Hali hiyo itakupunguzia kuwa na msongo usio na lazima.

ONYESHA UPENDO KWA RAFIKI, FAMILIA

KARIBUNI wapenzi wasomaji katika safu hii ya Maisha Yetu. Leo tunaangalia jinsi unavyoweza kuonyesha zawadi ya upendo kwa watu, hata kama huna fedha.

Kila mtu anapenda kupendwa, hivyo yakupasa kuwa na rafiki wa karibu atakayekushirikisha katika mambo mbalimbali anayokabiliana nayo. Kutokana na ukweli huo ni vema kuwa na rafiki mzuri na kuonyesha upendo wako kwake, kwa sababu wakati mwingine unajikuta hata familia yako inakuwa mbali nawe, ilhali katika kipindi hicho unahitaji mtu wa kuongea naye.

Ni muhimu kuwa rafiki mzuri kwa sababu unajifunza ni jinsi gani ya kukutana na watu wapya na unajifunza kutokana na makosa yako. Tafuta watu unaopenda wawe rafiki zako, kwa kujitambulisha na kumwacha mwingine kukueleza juu ya mambo anayoyapendelea.

Mwonyeshe mtu huyo kuwa unamwamini, mwache ajue kuwa ni sawa kupendana, mwache ajue kuwa uko pale kwa ajili yake na atakuwa rafiki yako wa kudumu. Mara zote mfanye atabasamu hata kama ana huzuni. Pia mwache ajue kuwa upo tayari kusikiliza chochote atakachosema.

Je? unawezaje kuonyesha upendo bila kutumia fedha? Wakati mwingine tunajitahidi kwa bidii kutafuta zawadi ambayo ni sahihi tunayofikiria kuwa ina maana kwa yule unayempelekea.

Au tunaishikilia zawadi hiyo tukifikiria kama kuna sababu maalumu ya kutoa zawadi hiyo. Ninakutia moyo kutoa zawadi yako kwa uhuru na iwe ni mara kwa mara, kumbuka kuwa utoaji ni shughuli inayomnufaisha mtu kila mara anapofanya hivyo.

Tuangalie zawadi 10 zinazofaa kwa siku ya kawaida na maalumu. Pia, ni zawadi ambazo mtu yeyote anaweza kutoa kwa sababu halazimishwi ila ni kwa nia ya kuleta ushirikiano.

Zawadi ya kwanza ni muda. Kumbuka kuutoa muda wako na kushirikiana na wenzako ni moja ya zawadi kubwa unayoweza kuitoa. Kama unatoa dakika 10 kwa kupiga hadithi na mtoto wako, kupata chakula cha mchana na rafiki yako au kutumia muda wa mchana kwa shughuli za nyumbani, shambani au nyinginezo, ukiwa na mume au mke wako, unajitolea nafsi yako na kujenga uhusiano mzuri kwa muda huo.

Zawadi nyingine ni kukiri kwa uaminifu. Tumekuwa tukisikia watu wachache wakisema kuwa wamepokea shukrani nyingi au pongezi nyingi.

Wote tunajisikia vizuri wakati tunapata taarifa nzuri na shukrani kwa vile tulivyo au tunayoyafanya.

Anza kuzingatia kuimarika katika hilo na kutoa sifa nzuri kwa wengine na kujenga tabia ya kukiri jambo zuri linalofanywa na wengine kwa kile unachokiona.

Nyingine ni msamaha. Hii ni zawadi nzuri mno yenye nguvu. Wakati tunasamehe wengine, tunaacha kuwaadhibu, tunawaruhusu wajisikie hatia au kuona aibu ili waweze kugundua makosa yao. Msamaha pia ni zawadi ya kutuweka huru kutoka kwenye uzoefu ulioupata wakati ulipoumizwa moyo wako au maumivu katika matukio yaliyopita.

Vile vile upendo. Wakati unapotaka kuuonyesha upendo wako kwa wengine, usiwahukumu wengine, na uwaone kama ni watu wa muhimu kwako. Tunaposhiriki kwa uwazi upendo wetu na wengine inasaidia kuponya majeraha, kujenga uhusiano mzuri na kumsaidia mtu katika kupitia changamoto za maisha pia kuwa na maisha mapya ya uhakika.

Usiugawe usikivu wako. Ingawa tunatoa muda wetu kwa ajili ya wengine, akili zetu zinaweza kuwa popote kutokana na uzoefu. Jiruhusu nafsi yako kuwa kwa mtu mwingine, kupanga naye shughuli nyingine, mawazo au ajenda mpaka utakapofikia malengo yako uliyokusudia.

Kama utafanya hivyo, watu watakuona unastahili kupata asilimia zote, kwa usikivu wako na kwa upande mwingine inawezekana ukawa hujafikia kiwango hicho ila kutokana na hali hiyo uliyojiwekea kwa watu.

Heshima. Mara kwa mara tunakuwa na shughuli nyingi au tunajishughulisha sana katika maisha yetu ambayo yamekuwa na matukio mfululizo ya kuvutia, tunasahau kama kuna watu wengine wanaotuzunguka. Iache nafsi yako ipumue na kutoa heshima kwa watu unaokutana nao kila siku.

Yapo mambo madogo madogo yanayoweza kufungua milango kwa watu wengine kuthamini mambo unayowafanyia kama kumpa lifti kwenye gari yako, kumbebea gazeti lake mpaka mlangoni pake au kusimamisha gari lako mbele ya mtu unayemfahamu na kumpa lifti kipindi cha msongamano wa abiria kituoni.

Mambo yote hayo yataonyesha hali ya kujali kwa mtu ingawa wakati mwingine mtu hawezi kuelewa wema wako na kukushukuru. Shitukiza. Zawadi za aina hii zinamfanya mtu kuwa mbunifu wa hali ya juu. Je, unataka kumpa dada yako kadi inayosema unampenda? Unajisikiaje unapomtumia mumeo maua?

Je, ni kweli utamshitusha? Au labda umechagua kujitolea kumpa mfanyakazi mwenzako kigari cha kusukuma cha watoto ili aweze kufurahia jioni anapokuwa matembezi na rafiki zake?

Zawadi kama hizo zinakuwa tukio kubwa kwa yule unayempelekea katika siku yake ya kawaida kwa sababu hakutarajia kufanyiwa jambo kama hilo kwa siku hiyo.

Shukrani ni zawadi pekee kwa yule unayempa, kwani inasababisha mtu huyo kujua kuwa umekuwa makini kwa lile alilokufanyia. Kama ukiri wa dhati, na neno jingine ni kusema asante, linaonekana ni jambo ambalo si la kawaida.

Endapo utachagua kusema au kuandika shukrani zako, hii ni zawadi inayokwenda ndani ya moyo wa mpewa shukrani. Tabasamu katika dunia ya kisasa, mara nyingi tunaona tabasamu chache na nyuso zenye furaha ya kweli.

Tabasamu linajulisha moyo mkunjufu, mapokezi na urafiki. Pia inafanya kuonekana kwa urahisi kwa wote wenye nyuso za tabasamu. Iache zawadi hii ya tabasamu itoe ujumbe. Mfano “Nina furaha uko hapa.”

Maombi ya kimya kimya. Wote tunakuwa na maombi ya ziada na ya baraka katika maisha yetu. Hata kama hufahamu, mtu mwingine anaweza kukubariki wakati unampa zawadi ya maombi yenye nguvu.

Kama unajua au la, mazingira ya mtu au dini yake, unaweza kuuliza kwa msaada au usikivu. Maombi rahisi unaweza kumwombea kwa kutumia “Mungu, ninakuomba umbariki mtu huyu na ukutane na mahitaji yake yoyote ambayo anayo katika maisha yake, asante.”

Tukutane wiki alhamisi ijayo.

JIFUNZE KUSHUKURU

KARIBUNI wapenzi wasomaji wetu katika safu hii ya Maisha Yetu inayokujia kila alhamisi. Leo tutaangalia jinsi ya kutoa shukrani. Kila siku ni njema ya kukuwezesha wewe kutoa shukrani kwa vitu vyote ulivyonavyo katika maisha yako.

Kuna baadhi ya watu, wamekuwa wakifikiri ni jambo gani la kuweza kulitolea shukrani. Wengi wenu wanaweza wakawa wamepoteza kazi au nyumba zao. Pengine umekabiliana na changamoto katika afya yako au uhusiano wako.

Bila kujali hali uliyo nayo, ni vema ukawa mtu wa kushukuru kwa kuwa Mungu kwani ndiye anayejua mambo mema anayokuwazia kila siku.

Kamwe sijawahi kukutana na yeyote ambaye hana kitu chochote cha kumfanya ashukuru.

Inapokuwa unahisi kuwa huna jambo lolote la kulitolea shukrani, unakuwa unakosea kwa sababu ulimwengu hauwezi kukupa zaidi ya kile ulichonacho.

Kinachotakiwa ni kushukuru na kuonyesha unajali kwa kile ulicho nacho.

Kama wewe ni mmoja wa watu wanaohisi kuwa hawana jambo lolote la kushukuru, ngoja nikupe maelekezo machache.

Je, umeamka asubuhi hii ya leo? Yakupasa utoe shukrani kwa zawadi ya siku inayofuata, nafasi nyingine ya kuanza upya na kutembea.

Unasoma maneno haya muda huu? Hivyo utoe shukrani kwa zawadi ya kuona, uwezo wa kusoma na kuelewa.

Kwa zawadi hii utapata ujuzi wote unaohitaji wa kubadilisha hali uliyonayo kwa mambo mazuri. Unajua idadi ya mchanga unaokuzunguka? Hivyo, toa shukrani kwa zawadi hiyo. Kama unaweza kusikia vicheko vya watoto, kusikia sauti za ndege juu ya miti na kusikia wimbo uupendao katika redio, hiyo ni zawadi tosha.

Bila kujali kwamba jambo hilo ni dogo kiasi gani au kuliona kuwa halina umuhimu, toa shukrani kwa hilo. Wakati unafanya hivyo, utaanza kuwa na mabadiliko mazuri katika mwili na hisia zako. Pale unapotoa shukrani na kuonyesha unajali kwa kile ulichonacho katika maisha yako, ndivyo watu wengi zaidi watakavyokushukuru.

Utakaposhukuriwa na watu wengi zaidi, ndivyo utakavyojisikia vizuri na ndivyo utakavyoongeza jitihada kwa kila kinachokuzunguka. Hivyo ni jambo gani unalopaswa kushukuru? Vile vile katika suala hili la kushukuru ni vema likifanywa na waajiri pamoja na waajiriwa, kwa kuwa huleta hamasa kwa kila mmoja.

Unaweza kuwaambia washirika wako, wafanyakazi na waajiri ni jinsi gani unawathamini na mchango wao wa kila siku. Ni ukweli usiopingika kuwa neno la shukrani lina maana kubwa sana kwa mtu yeyote kuliko zawadi.

Pia shukrani huwafanya watu katika kazi zao kipindi chote cha mwaka kujiona kuwa ni wathamani kubwa, kuliko kubaki kuwasema na kuwanenaa mabaya.

Zifuatazo ni njia ambazo zinaonyesha shukrani kwa wafanyakazi na waajiri.

Ni vema kupongeza kitu chochote ambacho wafanyakazi wako wamekifanya vizuri. Elezea kwa ufasaha kile hasa kilichokufurahisha.

Sema asante. Onyesha shukrani kwa kazi wanayoifanya na michango yao. Mahusiano mazuri katika kazi yanajenga heshima, nidhamu na utukufu kwa kila mmoja.

Penda kuulizia habari zinazohusu familia za wafanyakazi wako, vitu wanavyopendelea na matukio maalumu wanayopenda kuhudhuria.

Pia waeleze kile unachokipenda, mambo hayo huwafanya watu wajisikie wanathamani na wanajaliwa.

Toa mapumziko kwa wafanyakazi wako katika siku za sikukuu, kama upo uwezekano. Kama kwa siku hiyo haitawezekana tafuta siku nyingine utayowapa wafanyakazi wako mapumziko.

Jitahidi kufahamu mambo ambayo wafanyakazi wako wanayapenda, ili uweze kutoa zawadi siku za sikukuu. Kutoa zawadi kama kuonyesha shukrani na kutambua uthamani yao, kunainua ari ya wafanyakazi wako siku hadi siku tofauti na kuonyesha kutowajali.

Pia kama unaweza kutoa pesa kwa wafanyakazi wako, kama vile mwisho wa mwaka kutoa bonasi pamoja na cheti cha kuonyesha kuwa unajali kuwapo kwao.

Kila mmoja anafurahia chakula. Hivyo wakaribishe chakula cha mchana wafanyakazi wako katika sikukuu za kuzaliwa au matukio muhimu katika mwaka au bila kuwepo kwa sababu yoyote ile.

Pia unaweza kuwa mbunifu wa vitu mbalimbali katika ofisi yako ili mradi kuwe na mawasiliano mazuri kati ya bosi na wafanyakazi wake. Pia unaweza kuwapa wafanyakazi wako zawadi za bagia, donate au vitu vingine kama hivyo. Kutoa zawadi kama hizo ambazo umezipika nyumbani kwako ni zawadi kubwa.

Pia unaweza kutoa nafasi, watu wanataka nafasi kwa ajili ya mafunzo zaidi. Wanapenda kushiriki vitu mbalimbali wanavyovipendelea vinavyoweza kuwasaidia katika kazi zao.

Vitu kama hivi huongeza umoja, ushirikiano pamoja na uzalishaji katika kampuni au shirika lako.

Twitter Facebook