Wednesday, July 23, 2008

KUBALIANA NA HALI USIYOWEZA KUIBADILI

KARIBUNI wapenzi wasomaji katika Safu ya Maisha Yetu, ambayo huelimisha, huadilisha na kubadilisha mambo mbalimbali tunayokabiliana nayo katika maisha yetu ya kila siku.
Wiki iliyopita tulimwona Steven baada ya kufiwa na watoto wake wawili mfululizo aliishi kwa hofu na kukata tamaa kwa muda mrefu, lakini siku moja mtoto wake wa kiume (5) alimwomba baba yake amtengenezee boti, ambayo ilimchukua muda mrefu kuimaliza.
Kwa maelezo ya Steven, kutengeneza boti hiyo kulichukua muda wa saa tatu, lakini ilipokwisha aligundua muda huo alioutumia katika kazi aliyokuwa akiifanya, uliweza kumpumzisha akili yake na kumpa amani ambayo aliipoteza kwa muda mrefu baada ya kufiwa na watoto wake.
Tokea hapo, aligundua kuwa ni vizuri mtu ajishughulishe katika kipindi kigumu anachopitia kama vile kufiwa na mke, mume, wazazi au watoto. Kwa kuwa mtu anapojishughulisha hukosa muda wa kufikiri hali ile iliyompata huko nyuma na badala yake anafiki kile anachokifanya kwa wakati huo.
Leo tutakwenda kumwangalia George ambaye anasema alipokuwa mtoto alikuwa na wasiwasi. Kwa maelezo yake, kila ilipofikia kipindi cha radi na ngurumo alikuwa akipatwa na hofu kuwa huenda mwanga wa radi utamuua.
Vilevile katika kipindi kigumu cha kutokuwa na mazao shambani mwao, alikuwa akihofu huenda watakosa chakula cha kutosha, na kuwasababisha wakae na njaa.
Hofu yake haikuishia hapo, bali aliendelea kuwaza kuwa endapo atakufa atakwenda motoni. Alikuwa akimwogopa kijana ambaye alimtishia kuwa angemkata masikio yake na kuwaogopa wasichana kuwa wangemcheka endapo angeongea nao. Wasiwasi wake ni kwamba hakuna msichana yeyote atakayekubali kuolewa naye.
Yote hiyo ni hali ya wasiwasi aliyokuwa nayo kijana huyo na kumfanya aishi kwa hofu muda mrefu, mpaka pale alipokuwa mkubwa na kugundua asilimia 90 ya vitu alivyokuwa akiviogopa havikumtokea.
Hivyo unaweza kuona, hofu inapoumbika katika maisha yako inasababisha shida kubwa na kurudisha nyuma maendeleo yako kwa kuwa kila ukitaka kupiga hatua unakuwa na hofu kuwa huenda ukafariki au kuugua.
Hivyo wasiwasi ni mbaya sana. George anasema hali hiyo ilikuwa ikimtesa katika kipindi cha ujana, lakini kadiri alivyokuwa anakuwa aliipuuza kwa kuwa ilimtesa.
Endapo unasumbuliwa na hali hiyo, jitahidi kuiondoa kwa gharama yoyote ili isikuletee uharibifu siku za usoni. Mara nyingi mwishoni mwa wiki, watu wengi hupenda kwenda matembezi mbalimbali kama madukani, sokoni au kutembelea ndugu, jamaa na marafiki.
Safari hiyo itakuwa nzuri kama mtu huyo atatuliza akili yake katika matembezi anayoyafanya. Lakini kinyume chake kama utakuwa haujaishinda huko uliko, utaanza kuwa na wasiwasi labda umeacha pasi inawaka au nyumba yako inaungua.
Unaweza kuwa na wasiwasi, kwamba msichana unayeishi naye ametoroka na kuwaacha watoto wako peke yao au hofu yako wamegongwa na gari na kufariki wakati wakiendesha baiskeli zao.
Hali hiyo itakuondolea raha ya matembezi hivyo usipoidhibiti itakuletea matatizo katika familia na hata ndoa yako. Unapokuwa na hali ya hofu ni vema ukaupumzisha mwili na kufikiri njia ya kuondokana na hali hiyo.
Ni vema ukakubaliana na hali ile ambayo huwezi kuibadili au kuizuia. Unapokutana na jambo linalokuumiza, ni vema ukakubaliana nalo. Mfano unaweza kupata ajali na kukatika vidole vya mguu wa kushoto, kabla ya hapo ulikuwa ukiuona mguu wako ukiwa na vidole vyote vitano, usipokubali hali hiyo, siku zote utakuwa mtu wa hofu na kukata tamaa. Hivyo ni vizuri kukubaliana na hali ile ambayo huwezi kuizuia au kuiepuka.
Katika vipindi mbalimbali tunavyopitia, tumekuwa tukikutana na hali isiyo nzuri katika maisha yetu, na hivyo ndivyo ilivyo. Tuna uamuzi, tunaweza kukubali hali hiyo kuwa haiwezi kubadilika na kuwa tayari kukabiliana nayo, au kutokubaliana na hali hiyo, ambapo mwisho wake ni kuwa na wasiwasi kila wakati.
“Kukubaliana na kile kilichokutokea ni hatua ya kwanza ya kukabiliana na jambo lolote lililo gumu,” anasema Godfrey Johnson. Usiiruhusu nafsi yako kukata tamaa hadi kushindwa kufanya jambo la maendeleo katika maisha yako. Isifikie hatua ukaona kuwa hakuna faida ya kuishi kutokana na misukosuko inayokukabili.
Watu wengine wanapokumbana na hali ngumu katika maisha yao hufikia hatua ya kuidharau kazi anayoifanya na hata kujitenga na marafiki zake. Isifikie hatua ukaachilia kila jambo ulilokuwa ukilifanya kutokana na hali hiyo.
“Nilipopata habari za kunitia hofu niliacha kazi yangu, na kwenda mbali ambako nilijificha nikalia kwa uchungu,” alisema Mary. Kwa maelezo yake alikumbuka wakati alipofiwa na mama yake mzazi alitumiwa ujumbe ambao ulisema kuwa; “Jipe moyo kwa yale yaliyokupata. Zuia huzuni zako kwa tabasamu na kuinuka.”
Alisema maneno hayo alipoyatafakari kwa mara nyingine yalimwinua na kumtia nguvu mpya. Alisahau tabu na huzuni zote zilizomkabili. Baada ya kupata faraja hiyo, aliondoka na kurudi kazini kwake kuendelea na kazi, kwa kuwa, aliikataa hali ile iliyokuwa ikimsononesha, kwa kuiambia nafsi yake kuwa, “imetokea. Siwezi kuibadili hali hiyo.”
Hivyo ni vema kila unapokabiliana na hali hiyo, kukubali kuuchosha mwili wako kwa kuanza masomo ya jioni, kujifunza mambo mapya na kuwa na marafiki wapya. Baada ya kufanikiwa kufanya hivyo utaishi maisha mapya ya furaha yasiyo na huzuni, kwa kuwa hautairuhusu nafsi yako kukumbuka yaliyopita.
Hivyo ni kawaida, mazingira pekee hayawezi kutufanya tuwe na furaha au kutokuwa nayo. Ni kwa jinsi gani tunakabiliana nayo inategemea hisia zetu. Tuangalie mfano wa kijana mmoja ambaye alizoea kusema kuwa, hawezi kuwa na wasiwasi hata kama atapoteza fedha zote alizonazo kwa sababu haoni atakachopata endapo atairuhusu hali hiyo zaidi ya kujipa maumivu.
Ila alisema kitakachofuata baada ya hapo, ni kufanya kzi kwa bidii vile atakavyoweza, na matokeo yake atayaacha mikononi mwa Mungu. Unapokuwa katika wakati mgumu, kama unaweza kuiondoa hali hiyo ni vizuri, kama huwezi usiipe nafasi katika moyo wako hali hiyo.
Makala hii ni kwa msaada wa mtandao wa intanenti na kitabu kijulikanacho kama ‘Ondoa wasiwasi anza maisha mapya’.
Tukutane alhamisi ijayo
www.lngowi.blogspot.comlcyngowi@yahoo.com0713 331455 or 0733 331455

0 Maoni:

Twitter Facebook