Wednesday, December 12, 2012

Ugumu wa maisha wawatatiza vijana 2


NAKUKARIBISHA katika safu hii ili kupata elimu juu ya maisha yetu ya kila siku.

Wiki iliyopita nilizungumzia vijana wenye umri wa kujitegemea kuendelea kuishi na wazazi wao kutokana na ugumu wa maisha uliopo.

Leo nitaendelea na mada hiyo huku nikizungumzia jinsi gani kijana anayekaa na wazazi wake anapaswa kufanya nini ili kuonesha kama amekomaa.

Ili kuonesha kama umekomaa unapoishi na wazazi wako, onesha kuwa upo nao kwa muda tu, kwa kuwa una mpango wa kwenda kuishi katika eneo lako.

Kabla ya kuondoka nyumbani kwa wazazi ni vizuri ukawaeleza ni lini unatarajia kuanza maisha ya kujitegemea.

Kijana anapokuwa nyumbani kwa wazazi wake anazungukwa na maadili yaliyopo katika nyumba yao.

Kwa mfano atapenda kuangaliwa kwa ukaribu na wazazi wake katika mahitaji yake. Lakini kama kijana huyo anataka aonekane amekuwa akiwa nyumbani kwa wazazi wake ni vema akafanya mambo yote yanayomhusu mwenyewe bila kumtegemea yeyote.

Mfano kufua nguo zake mwenyewe, kusafisha chumba chake, kununua chakula pamoja na kutatua matatizo yake mwenyewe.

Na pale unapogundua kuwa, mama yako anakukumbusha ratiba ya kumuona daktari wako labda wa meno, lakini unaona ya kwamba mambo hayo unayamudu mwenyewe ni vema ukawaeleza kuwa unafurahi vile wazazi wanavyokufanyia lakini hapo ulipofikia una uwezo wa kujiongoza mwenyewe.

Pia ni vema kuchanganua uhusiano uliopo baina yako na wazazi wako. Elewa unapokaa na wazazi wako sebuleni muda wa jioni watakukumbusha kuhusu kufuata maadili mema, mila na desturi pamoja na jinsi ya kuishi na watu.

Lakini ukumbuke kuwa hivi sasa umekua, uhusiano na wazazi wako inabidi ubadilike, badala ya kuzungumza nao kama mtoto mdogo inakubidi uzungumze nao kama mkubwa mwenzao kwa kuzingatia heshima na maadili bora.

Zungumza nao kuhusu matarajio yao kwako na wanatarajia nini kuhusu mipango yako ya kujitegemea.

Kama kijana katika familia yako, je, unachangia kitu chochote? Kama unataka kujihisi kuwa sasa ni mtu mzima hata kama unaishi na wazazi wako, inabidi uchangie katika nyumba ya wazazi wako chakula na mambo mengine.

Ni vema kuheshimu mawazo ya wazazi wako kwa marafiki wanao kutembelea. Kama una uhusiano na kimapenzi si vizuri kulala na rafiki yako huyo chumba kimoja kwenye nyumba ya wazazi wako. Heshimu nyumba ya wazazi wako kwa kutokuruhusu jambo hilo kufanyika kwenye nyumba ya wazazi wako.

Hii ni kutokana na mila na desturi zilizopo katika familia nyingi.

Ni vema wazazi wako wakajua ratiba zako vizuri ili endapo ikatokea umechelewa kurudi nyumbani wasipate wasiwasi au utakapowagongea usiku wakiwa wamelala wajue vema ulipokuwa, hii itakufanya uheshimike katika familia yako.

Jione wewe kuwa ni mgeni katika nyumba ya wazazi wako. Pale unapotaka kula kitu chochote ni vema ukaomba ruhusa badala ya kujichukulia tu kama ni mali yako.



0 Maoni:

Twitter Facebook