Wednesday, December 12, 2012

Jinsi ya kuepuka kupata hasara


BIASHARA yako inapokwenda mrama, ni vema kuweka tamko la kusitisha hasara uliyoipata, kwamba hauko tayari kukubali iendelee.

Jitahidi kuweka mikakati zaidi ya kuiboresha na kuomba ushauri wa kimaendeleo kwa waliofanikiwa.

Tumwangalie mfanyabiashara John Robert, aliyekuwa amepewa fedha na rafiki zake kiasi cha dola 200,000 za Kimarekani, ili kuwekeza katika soko la hisa.

Baada ya kupewa fedha hizo na kuzifanyia biashara, Robert alifikiri kuwa angepata faida ambayo ingemfanya awe na maendeleo zaidi katika maisha yake, lakini kwa bahati mbaya ilikuwa kinyume na matarajio yake.

Awali, alipoanza biashara hiyo alipata faida iliyomfanya asiwe mbunifu katika biashara yake, lakini matokeo yake ni kwamba baada ya muda mfupi alifilisika.

Baada ya kufilisika, alipata hofu kutokana na fedha alizopewa kwa ajili ya kufanya biashara.

“Sikujali kupoteza pesa zangu mwenyewe,” anasema mfanyabiashara huyo na kwamba kipindi hicho kilikuwa kigumu kwake, kutokana na kupoteza pesa za rafiki zake.

Lakini, mara baada ya kufanikiwa kuishinda hofu iliyokuwa ikimkabili, alijikuta amepata ujasiri mpya na kwenda kuwakabili tena rafiki zake na kuwaeleza kilichomsibu.

Pamoja na maelezo hayo, marafiki wale hawakuonesha mshangao katika jambo hilo, bali walilichukulia kuwa la kawaida.

Lakini kwa upande wake ilionekana kuwa halitatibika.

“Nilijua nilikuwa nafanya biashara katika mtindo wa 'pata potea' nikitarajia zaidi bahati na mawazo ya watu. Nilikuwa nikishiriki katika soko la hisa kwa kusikia,” anasema.

Kwa maelezo ya Robert, alianza kufikiria makosa yake na kufanya uamuzi kabla ya kuamua kurudi kwenye soko kwa mara nyingine, alijaribu kutafuta chanzo cha jambo hilo, pia alifikiri na kuamua kuja na mwongozo mpya wa mafanikio.

Baada ya hali hiyo kumtokea, alitafuta ushauri kutoka kwa rafiki zake, kwa kuwauliza ni jinsi gani wameweza kufanikiwa na kuendesha biashara zao, ambazo zinakwenda vizuri.

Mmoja wa marafiki zake, aliyeendesha biashara yake vizuri, alimweleza akiweka tamko la kusitisha hasara katika hofu yake kwenye majukumu aliyojipangia.

Hivyo, mtu yeyote anaweza kuondoa tabia ya hofu aliyonayo. Hivyo popote unaposhawishika kuweka pesa zako baada ya kupoteza, ni vizuri kutulia na kujiuliza maswali yafuatayo: Ni kwa kiasi gani umekuwa na hofu kuhusu jambo fulani juu yako? Ni kwa jinsi gani utaepuka kupata hasara katika hofu inayokukabili na kusahau? Ni kwa jinsi gani utaepuka kupata hasara katika wasiwasi na kusahau?

Kumbuka unapoanza kuwa na hofu ya vitu vilivyopita na kufanyika ni kama unakuwa ukijaribu kupanda mazao yako kwenye vumbi.

Maana yake ni kwamba yale yaliyopita usiyasumbukie, bali ugange yajayo. Ukiendelea kuyasumbukia utajisababishia mikunjo katika paji la uso wako na vidonda vya tumbo.

Hivyo, endapo una tatizo la kukumbuka mambo yaliyopita, iambie nafsi yako kwamba huishi kwa ajili ya mambo hayo. Badala yake unaweza kuwa na mipango mizuri zaidi kwa ajili ya maisha yako.

Unaweza kujishughulisha kwa kuandaa mashindano mbalimbali kama vile muziki, ngumi au uchoraji.

Lengo ni kuwa unajishughulisha kila mara ili usiwe na nafasi ya kufikiria mambo yaliyopita, ambayo yamekusababishia hasara na hofu maishani mwako.

1 Maoni:

Ahsante kwa ushauri wako mzuri, endelea zaidi.

Twitter Facebook