Wednesday, December 12, 2012

Kwa nini wajasiriamali hukopo, hawafanikiwi? - 1


HAKUNA mtu asiyependa kufikia malengo yake aliyojiwekea kwa wakati.

Mara zote wajasiriamali wadogo au wafanyabiashara wa kati wamekuwa wakitamani kupata mafanikio, lakini wanakabiliana na changamoto mbalimbali.

Changamoto hizo ndizo zinazowafanya wasifikie ndoto zao za kuongeza biashara nyingine, ama kupanua biashara zao kwa muda maalumu.

Jambo hili limekuwa ni kilio kwa wajasiriamali wengi ambao wamekuwa wakiomba mikopo katika taasisi mbalimbali za fedha au benki, lakini matokeo yake fedha yote huishia kulipa madeni hayo. Hivyo wanajikuta hawasongi mbele.

Ninajua zipo sababu nyingi sana zinazowafanya wasisonge mbele, lakini leo tutaambiana kwa uchache. Zaidi nitapenda kujifunza kwa wajasiriamali wenyewe ambao nitapenda wanitumie maoni yao kupitia simu yangu ya mkononi ama e-mail yangu ambayo ipo katika safu hii ili tuweze kuyaandika na wengine waweze kupata mwanga.

Mojawapo ya changamoto inayosemwa ni ile ya wakopeshaji wengi kuwa kibiashara zaidi badala ya kulenga kumsaidia mjasiriamali wa kweli.

Wengi wa wakopeshaji hao huweka riba kubwa, lakini pia huwa hawana mafunzo kwa wajasiriamali wanaowakopesha.

Vile vile hawawaachii muda wa kuweza kujikusanya ili warudishe fedha hizo kwa utulivu na amani. Hapa namaanisha kuwa, mtu anapokopa mwezi huu, mwezi ujao anatakiwa kurejesha deni lile.

Pia unaweza ukakuta mjasiriamali huyo biashara yake haiendi vizuri, iwe ni nafaka, mifugo ama duka.

Anaamua kwenda kutafuta mtaji wa kuweza kumuinua, anapokwenda huko anakutana na vikwazo vingi vigumu kama vile hati za nyumba, pamoja na kuwa na wadhamini wa kueleweka wanaofanya kazi.

Mbali na hiyo, unakuta mtu anaomba mkopo mwezi huu anakaa miezi minne baadaye ndipo anaupata mkopo huo, hapo anakuwa ameshachoka na malengo yake yote yamevurugika.

Kwa mfano mtu anapokuja kuomba mkopo mwezi huu, lakini baada ya kukamilisha taratibu zote mkopo huo unatoka baada ya miezi mitatu au miwili.

Hali kama hiyo hurudisha nyuma maendeleo ya mtu anayetaka kusonga mbele. Hebu tujiulize ni watu wangapi hivi sasa wanazo hati za kuwawezesha kupata mkopo?

Je, upatikanaji wa hati hizo unachukua muda gani? ni kiasi gani mtu anapaswa kuwa nacho ili aweze kupatiwa hati hiyo.

Mbali na hilo, je, mkopeshaji anawezaje kuisemea vibaya biashara ya mkopaji? mfano, baada ya kukamilisha taratibu zote za kukopa, inabidi maofisa mikopo kutembelea kwenye eneo husika la biashara, je, ni vema kuanza kuzungumza kwa dharau kuhusu eneo ulilopo la biashara ama biashara unayoifanya?

Ni nani asiyependa kufanya biashara yake katika mazingira bora na mazuri ya kupendeza?

Binafsi nilitegemea maofisa hao badala ya ‘kuponda’ kama Waswahili wanavyosema, biashara ya mtu, ni vema wangemshauri mjasiriamali huyo kujitahidi katika biashara aliyonayo ili aweze kupata eneo zuri zaidi ama kuwa na mazingira mazuri ya kufanyia biashara yake.

Katika safu yetu hii ya ‘Maisha Yetu” leo ninapenda kumkaribisha kila mmoja aweze kutoa maoni yake kuhusiana na changamoto zinazowakabili wajasiriamali katika taasisi za fedha au benki, na wafanye nini ili wajikwamue kutokana na hali hiyo.

0 Maoni:

Twitter Facebook