Wednesday, December 12, 2012

Kwa nini wajasiriamali hukopa, hawafanikiwi? - 2


WIKI iliyopita katika safu hii tuliangalia kwa kifupi ni kwanini wajasiriamali wengi na wafanyabiashara wa kati, pamoja na kukopa kwenye taasisi za fedha au benki wanashindwa kufikia malengo yao.

Leo tutachapisha maoni mbalimbali ya wasomaji wa safu hii ambao wameyatoa katika kuelezea changamoto hiyo inayowakabili wajasiriamali.

Mmojawapo wa wasomaji hao aliyejitambulisha kuwa ni Alexander kutoka Dar es Salaam, anasema tatizo kubwa kabisa ni wajasiriamali wengi wanakuwa hawana ndoto ya kufanya wanachotaka, hivyo wanapokopeshwa fedha hizo hushindwa kuendelea.

Matokeo yake hujikuta wakitangatanga katika biashara nyingi kwa kuwa hawakujua wanataka kufanya nini.

Msomaji mwingine kutoka Mwanza ambaye hakujitambulisha jina lake alisema kuwa, taasisi nyingi za fedha ama benki zimekuwa ni kikwazo kwa wajasiriamali wadogo na wakati.

Anasema amekutana na adha ya kusotea mkopo japokuwa amekwisha kamilisha taratibu zote zinazohitajika katika benki aliyoiombea mkopo ikiwepo hati ya nyumba, huu ni mwezi wa pili anazungushwazungushwa na kila akiulizia anaambiwa ripoti imetumwa Dar es Salaam, hivyo kumfanya kushindwa kutimiza malengo aliyojiwekea.

Andondile Anjawe kutoka Ludewa, anasema katika mambo yanayoumiza wajasiriamali kwenye mikopo na kutolea mfano wa benki aliyoomba mkopo, ni zile gharama mbalimbali zinazotozwa kabla ya kupata mkopo husika.

Anasema unalipia gharama ya mkopo, pili unalipia mhuri, tatu unalipia mahakamani hivyo unajikuta mkopo wote unamalizika kabla hujaushika mkononi.

Hapo hapo bado unatakiwa kurudisha mkopo huo mwezi unaofuata baada ya kuupata.

Maoni mengine yaliyotolewa na mjasiriamali ambaye hakutaja jina lake anasema wengi wana sifa za kukopa kiasi kidogo ambacho hakiwezi toa faida ya kubadilisha maisha.

Pia familia inachangia kukwama akizungumzia familia za Kitanzania mtu akiwa na maisha mazuri kidogo ndugu wanajikusanya kwake.

Jambo lingine anasema ni kwamba, mikopo mingi hukopwa kwa ajili ya ubarikio, harusi ama shughuli nyingine na si kufanyia kazi ya kuzalisha.

Vile vile kodi kubwa na ushuru, pia benki nyingi zinadai fidia kubwa, pamoja na ugumu wa maisha kiasi kwamba mkopo unaotoka mwingine anaweza kulipia ada ya mtoto au kununulia chakula.

Msomaji mwingine anasema katika sekta ya biashara ukitaka kukopa inabidi uwe na mtaji wako kwanza.

Tatizo la ukopaji wa vikundi ni kulaza deni likiwa kubwa wote mnakatwa akiba zenu.

Mkopo binafsi ni mgumu kwa kuwa unawashinda wengi lazima uwe na hati ya nyumba, mdhamini naye anataka kupewa kitu kidogo, au itafika siku atakuomba umkopeshe hivyo hela uliyoipata unaanza kuigawa kwa mambo mengine.

Msomaji mwingine wa safu hii, Elimringi Mero anatolea mfano benki moja iliyoko Dar es Salaam, ambayo wafanyakazi walifika dukani kwake eneo la Bunju B wakihamasisha wafanyabiashara wadogo wafungue akaunti na kupewa mikopo, kigezo ni biashara na leseni yenye umri wa mwaka mmoja, na dhamana ni duka lake.

Hivyo alihamasika kujiunga, lakini chakushangaza alipotaka mkopo aliambiwa apelike wadhamini watatu wenye vitanda na magodoro, pamoja na kusema ana nyumba ambayo haijapauliwa aligonga mwamba.

Anasema akaunti yake ilikuwa na sh 30,000 baada ya miezi sita akataka alipotaka kuchukua aliambiwa haina pesa na kuambiwa kila mwezi wanakata sh 5,000. Hivyo mtaji wake ulizidi kushuka.

Naye Msofe kutoka Morogoro anasema, tatizo la wakopaji Watanzania si waaminifu hivyo inawafanya wakopeshaji kuweka mazingira magumu.

Pia ikumbukwe kuwa, wakopeshaji nao wapo kibiashara zaidi si kwa nia ya kuinua wajasiriamali.

Mwandishi wa safu hii anashukuru kwa maoni yote yaliyotolewa, anakaribisha maoni mengine kutoka kwa wataalamu wa benki mbalimbali kwa lengo la kujenga nchi yetu na si kubomoa.

0 Maoni:

Twitter Facebook