WIKI mbili zilizopita nilizungumzia kwanini wajasiriamali wengi na wafanyabiashara wa kati licha ya kukopa kwenye taasisi za fedha wanashindwa kufikia malengo waliyojiwekea.
Baadhi ya wajasiriamali hao walitoa sababu katika safu hii ya Maisha Yetu inayowafanya wasisonge mbele katika shughuli wanazozifanya.
Pamoja na sababu hizo zilizotolewa, bado elimu kwa wajasiriamali hao inahitajika kwa kiasi kikubwa. Inatakiwa wapate elimu kuhusu biashara wanazozifanya na kwamba endapo watapeta fedha wanatakiwa kuzitumia vipi.
Ukweli ni kwamba kumpa mjasiriamali fedha tu, hapo unakuwa hujamsaidia. Cha msingi ni kumpa fedha hiyo pamoja na elimu ya jinsi ya kuboresha biashara anayoifanya.
Wapo wajasiriamali waliofanikiwa kutokana na nidhamu ya fedha wanayoipata ikiwemo pia elimu kuhusu shughuli anayoifanya.
Ni vema basi, taasisi za fedha zinazokopesha wajasiriamali wakaliangalia suala hilo ili mjasiriamali huyu aweze kupiga hatua.
Mfano unapompa mjasiriamali elimu ya jinsi ya kutengeneza batiki, anapomaliza anajua kuwa anahitajika kununua vitambaa, rangi na dawa kwa ajili ya kutengenezea batiki hizo, anapotengeneza akichanganya na ubunifu wake anakuwa na mafanikio makubwa.
Pia ukiangalia soko la batiki lipo ndani na nje ya nchi. Mbali na elimu pia mjasiriamali huyu anapaswa kuunganishwa kwenye mtandao wa wajasiriamali wa ndani na nje ya nchi. ili apate soko ndani na nje pia asiwe muuzaji wa hapa hapa.
Kumuunganisha mjasiriamali na mitandao mingine ya ujasiriamali kunatoa fursa ya mjasiriamali huyo kujifunza kutoka kwa wengine na kujua katika biashara yake hiyo aongeze ama apunguze nini.
Hivyo basi mbali na kutoa mikopo yenye riba kubwa, yenye usumbufu, inayomfanya mjasiriamali huyu kuzunguka anapoupata soli ya viatu inakuwa imekwisha, ni vema akapewa elimu hiyo.
Naamini penye nia pana njia, shime wajasiriamali msikate tamaa katika kufikia mafanikio mnayoyatarajia, ama maono yale mliyonayo juu ya mafanikio katika maisha yetu.
Miongoni wa wajasiriamali walitoa maoni yao ni Alexander kutoka Dar es Salaam ambaye anasema tatizo kubwa kabisa ni wajasiriamali wengi wanakuwa hawana ndoto ya kufanya wanachotaka, hivyo wanapokopeshwa fedha hizo hushindwa kuendelea.
Mjasiriamali huyo aliyejitambulisha kwa jina moja anasema matokeo yake wajasiriamali hujikuta wakitanga tanga katika biashara nyingi kwa kuwa hawakujua wanataka kufanya nini.
Msomaji mwingine kutoka Mwanza ambaye hakujitambulisha jina lake alisema kuwa, taasisi nyingi za fedha ama benki zimekuwa ni kikwazo kwa wajasiriamali wadogo na wakati.
Anasema amekutana na adha ya kusotea mkopo japokuwa amekwisha kamilisha taratibu zote zinazohitajika katika benki aliyoiombea mkopo ikiwemo hati ya nyumba, huu ni mwezi wa pili anazungushwazungushwa na kila akiulizia anaambiwa ripoti imetumwa Dar es Salaam, hivyo kumfanya kushindwa kutimiza malengo aliyojiwekea.
Andondile Anjawe kutoka Ludewa, anasema katika mambo yanayoumiza wajasiriamali kwenye mikopo na kutolea mfano wa benki aliyoomba mkopo, ni zile gharama mbalimbali zinazotozwa kabla ya kupata mkopo husika.
Anasema unalipia gharama ya mkopo, pili unalipia mhuri, tatu unalipia mahakamani, hivyo unajikuta mkopo wote unamalizika kabla hujaushika mkononi.
Hapo hapo bado unatakiwa kurudisha mkopo huo mwezi unaofuata baada ya kuupata.
Maoni mengine yaliyotolewa na mjasiriamali ambaye hakutaja jina lake anasema wengi wana sifa za kukopa kiasi kidogo ambacho hakiwezi kutoa faida ya kubadilisha maisha.
Naye Msofe kutoka Morogoro anasema, tatizo la wakopaji Watanzania si waaminifu hivyo inawafanya wakopeshaji kuweka mazingira magumu.
Pia ikumbukwe kuwa wakopeshaji nao wapo kibiashara zaidi, si kwa nia ya kuinua wajasiriamali.
Mwandishi wa safu hii anashukuru kwa maoni yote yaliyotolewa, anakaribisha maoni mengine kutoka kwa wataalamu wa benki mbalimbali kwa lengo la kujenga nchi yetu na si kubomoa.
Wednesday, December 12, 2012
Kwa nini wajasiriamali hukopa, hawafanikiwi? - 3
Posted in:
0 Maoni:
Post a Comment