Na Mwandishi Wetu
WAZIRI wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia Profesa Makame
Mbarawa ameagiza wataalamu kutayarisha
mwongozo kwa ajili ya kampuni za simu, utakaoelekeza jinsi ya kutuma meseji
katika kipindi cha kuelekea uchaguzi mkuu mwakani.
Mbarawa alisema jana alipokuwa akifungua mkutano wa
kuadhimisha siku ya Teknolojia ya Habari
na Mawasiliano ya Jumuiya ya Mawasiliano Afrika, Jijini Dar es Salaam,
ulioandaliwa na Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA).
Waziri Mbarawa alisema, mwakani ni kipindi cha uchaguzi hivyo
kuna baadhi ya watu wamekuwa wakitumia simu kutuma meseji ambazo zinaweza
kuhatarisha usalama wa raia.
“Watu wanatuma meseji hizo, nimeshawaagiza wataalamu kutoka
wizarani na TCRA kwa ajili ya kuandaa mwongozo huo kwa ajili ya kutuma meseji
kwa sababu teknolojia imekuwa, watu wanaweza kuitumia vibaya,” alisema.
Vile vile alivitaka vyombo vya habari vitumike kuwaelimisha
wananchi vizuri kuhusu masuala ya uchaguzi kwa kutahadharisha kuwa mwongozo
walioupata usiwe kwenye makaratasi tu bali wautekeleze.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa TCRA Profesa John Nkoma
alisema kuwa, hivi sasa Tanzania imepiga hatua kubwa kwa kuwa wanaotumia kadi
za simu ni milioni 28, mtandao wa mawasiliano ni milioni tisa ikiwa na pamoja
na ukuaji wa huduma za simu ambazo zimewezesha kutuma na kupokea fedha.
Pia alisema serikali imewekeza dola milioni 200 katika mkongo
wa taifa kwa ajili ya maboresho kwenye upande wa utangazaji.
mwisho
0 Maoni:
Post a Comment