Monday, December 8, 2014

NHC kutatua matatizo ya wananchi



Na Mwandishi Wetu
MKURUGENZI Mkuu wa Shirika la Nyumba  nchini (NHC), Nehemia Mchechu, amesema kuwa wanaiangalia miradi waliyonayo ni jinsi gani inaweza kutatua matatizo waliyonayo wananchi.
Mchechu alisema hayo jjijini Dar es Salaam, alipokuwa akizungumza katika mjadala ulioandaliwa na Chuo Kikuu Ardhi (ARU), wakati akiwasilisha mada yake.
Alisema NHC inaangalia ni jinsi gani watengeneze vitovu vya miji ambavyo kutakuwa na makazi ya watu, biashara mbalimbali pamoja na ofisi ili kumpunguzia mwananchi usumbufu wa kutembea muda mrefu.
“Je NHC katika miradi yao wanafanya nini ili wananchi waishi vizuri? Tunachoangalia miradi yetu tuliyonayo ni jinsi gani inaweza kutatua matatizo na kurahisisha huduma kwa wananchi,” alisema Mchechu.
Mchechu alisema kuna miradi Kawe ‘apartment’ iliyopo Dar es Salaam ambayo itawezesha watu kupata mahitaji yote kwa pamoja.
“Ukimfanya mtu akaishi na kufanya kazi karibu na ofisi, ataongeza kipato na kupunguza matumizi kwa kuwa hatasafiri tena mwendo mrefu kwa ajili ya kuwahi kazini, pia itafanya awe na afya bora kwa kupunguza msongo unaotokana na foleni,” alisema Mkurugenzi huyo.
Naye Profesa Lusugga Kironde ambaye anashughulika na masuala ya Maendeleo ya Ardhi na Uthamini (ARU),alisema kuwa siku hizi watu wanakuja mjini kuishi siyo kuondoka tofauti na zamani, hivyo wanaangalia masuala ya kazi, makazi na jinsi wanavyojitambua ili kuwezesha waishi vizuri.
Pia alishangazwa na kitendo cha kuvunja majengo ya zamani na kuwekwa mapya kwa kuwa kinadhoofisha fursa za utalii.
mwisho

0 Maoni:

Twitter Facebook