Thursday, February 12, 2009

MARAFIKI WANAWEZA KUWA KIKWAZO CHA MAFANIKIO YAKO

KARIBU mpenzi msomaji katika safu hii ya Maisha Yetu inayokujia kila Alhamisi. Madhumuini makubwa ya safu hii ni kukuelimisha, kukukosoa na kukujenga kiuchumi. Leo utaona ni jinsi marafiki wanavyoweza kuwa kikwazo cha mafanikio yako.
Endapo utapata nafasi ya kutulia na kutafakari marafiki ulio nao, utagundua kuwa una nafasi kubwa ya wewe kusimamia mambo yako mwenyewe.
Nimeanza kwa kusema hivyo kwa sababu mara nyingine rafiki yako ndiye anayekuwa kikwazo cha mafanikio yako kwa kukurudisha nyuma fikra zako kimaendeleo.
Rafiki huyo badala ya kukusaidia kimawazo, atakushawishi muende maeneo ya starehe mara nyingine unapotaka kufanya jambo hukukatisha tamaa kwamba hutafanikiwa na kukutolea mifano ya watu walioshindwa katika maisha yao.
Ieleweke wazi kuwa kwenda katika maeneo ya starehe si vibaya, maadamu ujue unakwenda pale kwa malengo. Sasa basi kupitia marafiki zako, utaweza kugundua mambo wanayoyapenda na shughuli wanazopenda kuzifanya zinazofanana na za kwako.
Vile vile ukiwaangalia kwa makini marafiki zako, utagundua kama wanastahili, wana ujasiri, furaha na wenye kupenda mafanikio yako, hapo ndipo utakuwa na uhakika kwamba unachanganyika na watu wa aina gani.
Endapo utagundua rafiki zako mawazo yao hayaendani na mawazo yako, ni vema ukaamua kuachana nao ili wasiweze kukukwamisha katika mipango yako.
Mtaalamu mmoja wa saikolojia, Dk. Freud, anasema kuna aina mbili za watu katika dhana ya mafanikio. Wapo wale wanaojiona kana kwamba wameshindwa kimaisha na wale wanaopenda kuwa na mafanikio kwa kufanya bidii.
Wale wenye mawazo ya kushindwa hujiona wanavuka hatua moja na kwenda hatua nyingine ya kushindwa, wale wanaopenda kufanikiwa hupiga hatua moja kila siku. Hujiambia nafsini mwao kwamba hawawezi kushindwa. Kuna msemo usemao ‘ tajiri atazidi kuongezewa na masikini hata kile kidogo alichonacho atanyang’anywa’.
Hivyo basi, utaona kuwa matajiri hufikiria utajiri, masikini hufikiria umaskini na kila mmoja anapata kile anachokifikiri. Kwa mtu anayependa kuwa na maisha ya mafanikio, ni vema akasimamia maisha yake katika kuyaandaa maisha yake ya baadaye anayoyapenda.
Usifikirie mambo ya zamani kwa kuwa yameshapita. Usipoteze muda na nguvu zako kwa makosa yaliyopita yalioyokufanya ukapoteza bahati yako.
Ni vyema katika maisha ukajua kuwa unasimamia mambo yako ya sasa na ya baadaye kwa kusimamia nia yako, wazo, hisia na imani kuhusu wewe, vitu na watu wengine.
Maisha bora kwako yatatokana na jitihada zako unazozifanya.Yale unayoyafikiria siku ya leo ndiyo yatakayofanyika siku ya kesho. Unajitengenezea mafanikio ya baadaye kwa kukuza fikra zako leo.
Kumbuka kuwa leo si jana. Kuna mabadiliko makubwa. Ni vema kujiuliza mabadiliko hayo ni kwa vipi? Unaweza kupata jawabu kuwa, mabadiliko hayo ni jinsi akili zetu na fikra zetu zinavyofanya kazi. Kwani mara nyingine mabadiliko huweza kuwa maumivu, lakini baadaye huwa ni faraja.
Kumbuka mabadiliko yoyote ni msingi wa mafanikio yako. Ni kweli kwamba watu wengi hawapendi mabadiliko si tu katika maisha yao lakini hata kwa maisha ya wengine. Wamekuwa waking’ang’ania mambo yaliyopita, wanakata mawazo mapya na changamoto mpya.
Mawazo hayo yanaondoa ubunifu ambao umekuwa ukija akilini mwake. Kumbuka wewe si yule uliyekuwa, hivyo, mwezi uliopita au mwaka uliopita. Kila dakika ya kila saa ya kila siku asili ya fikra zako hukua. Unakua kiakili, kiroho na kimaumbile.
Kile unachopanda ndicho unachovuna. Kama unajijengea mawazo ya utajiri, upendo na furaha hisia zako ndizo zitakavyokuwa. Ili uwe imara na maisha yako ni vyema kujiuliza maswali yafuatayo.
Kwa nini nipo hapa nilipo? Wapi ninakwenda na ni mahitaji gani ninayoyataka kubadili maisha ninayotaka kuishi? Ni vyema kuliangalia jibu lako kwa umakini - kutoka hapo ndipo utakapoweza kuchora ramani halisi ya maisha yako unayoyataka.
Tukutane wiki ijayo

1 Maoni:

Blogu nyingine ya maarifa. Kazi nzuri dada. Nitakuwa mmoja wapo wa wasomaji wako.

Twitter Facebook