Friday, February 6, 2009

KUFANIKIWA AU KUTOFANIKIWA NI UCHAGUZI WAKO

KARIBUNI wasomaji katika safu hii, leo tutazungumzia kufanikiwa au kushindwa ni uchaguzi wako mwenyewe.
Kumbuka umebarikiwa kuwa na uhuru wa maamuzi, kama vile kuchagua aina ya maisha unayotaka kuishi.
Kama hivyo sivyo, huwezi kuwa na uwezo wa kutumia vipaji vyako ulivyonavyo.
Fahamu kuwa, akili uliyonayo ni nyenzo muhimu ya kukufanya ufanikiwe, kwa kufikiri na kutumia vipaji ulivyo navyo kisha kuvifanyia kazi.
Kwa kuwa mafanikio yako yanatokana na akili yako uliyonayo. Endapo utatumia akili, hisia na imani yako kwa busara na kufanyia kazi, ni lazima maisha yako yatakuwa na mabadiliko makubwa ya mafanikio.
Una uhuru wa kuchagua namna unavyofikiri, unavyohisi na unavyoamini ili uweze kusonga mbele, kamwe usikubali kuwa na fikra mgando ambazo hazitakusogeza hapo ulipo.
Mafanikio au kushindwa kwako inategemea jinsi unavyofikiri.
Kwani afya isiyo njema, hali ya kutokuwa na furaha na umaskini, hizo ni dalili za kushindwa katika maisha ambazo zimesababishwa na kuwaza mawazo hasi.
Vile vile akili yenye afya bora na mawazo ya matumaini yanakufanya uwe na afya bora na maendeleo mazuri.
Safisha akili yako kwa mawazo mazuri. Siri ya kushinda katika maisha ni kusafisha akili kwa kuondoa tabia zinazokufanya uharibikiwe, kama vile imani potofu, mawazo hasi na badala yake uwe na tabia zenye kukufanya usonge mbele, kuwa na imani na mawazo ya kujenga na si kukubomoa.
Mara zote kuwa na mawazo ya kukujenga kwa mfano iambie nafsi yako kwamba, utafanikiwa katika mambo yote uliyopanga kufanikiwa.
Mara zote jione upo imara katika kufanikisha mipango yako mbalimbali, uwe mtu unayependa kuwajali wengine, uwe mwaminifu katika shughuli zako pamoja na familia yako.
Ukweli, ushindi na ujasiri ni silaha kubwa ya mafanikio katika maisha yako.
Kamwe usiruhusu mawazo ambayo hayana tija ya maendeleo kwako.
Jifunze kuwa jasiri, usikate tamaa, kuwa mtu mwenye msimamo, penda kwenda na wakati, usilewe na usiwachukie washirika wako katika biashara.
Njia yoyote ya kubadili hali yako ya kushindwa katika maisha ni kubadili mawazo hasi unayofikiria, utakapofanya hivyo utabadili tabia ya kufikiri, kuhisi na kuamini. Utakapobadili tabia yako ya ndani, hata tabia yako ya nje itajibadili.
Mawazo yana nguvu. Mawazo ya hofu na wasiwasi ni njia ya kushindwa. Utakaposhinda hali ya kutokuwaza kushindwa, kuwa na hofu au wasiwasi utaweza kukabiliana na hali ya ushindi.
Kuna kanuni moja inayotawala mawazo. Huwezi kufikiri kitu hiki na kuzalisha kingine.
Mara kwa mara, hali ya kushindwa inaweza kukujia ili kukujaribu. Ni wakati wako wa kutumia akili kwa vitendo ili uishinde hali hiyo.
Madhara ya kushindwa katika maisha yanaweza kukuletea hali ya uharibifu, imani potofu na mawazo hasi pamoja na hisia za maisha yako.
Kwa maelezo mengine, hali hiyo inakufanya ukose furaha, uwe mpweke, kukosa adabu, kuwa na uamuzi mbaya, magonjwa ya mara kwa mara yasiyoeleweka, kuchanganyikiwa na hali ya kushindwa.
Hali ya kufanikiwa inakufanya uwe na furaha, maendeleo mazuri, kujiamini, matumaini, amani katika moyo, umoja katika familia, mafanikio kibiashara, busara, ukweli na upendo.
Tukutane wiki ijayo.

0 Maoni:

Twitter Facebook