KARIBUNI wapenzi wasomaji katika siku nyingine ambayo Mwenyezi Mungu ametujalia kuiona. Leo katika safu yetu hii tunaangalia ni jinsi kuweza kufanikiwa.
Kumbuka ni juu yako kuchagua kama unataka kufanikiwa, kwani huwezi kupata mafanikio yoyote kwa kuangalia mambo yaliyopita ambayo hayakukuendea vizuri.
Ni vema ukimtegemea Mungu pamoja na kuongeza bidii kwa akili na ujuzi aliokupa. Usimtegemee mwanadamu yeyote katika kufanikisha mambo yako kwani atakukatisha tamaa.
Kama mwanadamu mwenye akili timamu, una uhuru wa kuchagua jambo unalohitaji. Ni vema ukachagua afya, furaha pamoja na kupata mafanikio. Ili ufanikishe malengo yako ni lazima uwe na mpango na siyo kufanya jambo kwa kubahatisha.
Kwani kila mmoja anao uwezo wa kufanikiwa, endapo atakuwa na mipango kamilifu. Kumbuka kila jambo unalolifanya ni kwa mpango maalumu, hivyo unatakiwa kulifanya katika mpango mzuri uliojiwekea ndipo litakapokuwa la ufanisi.
Ni jinsi gani unaweza kupanga utaratibu wa maisha yako vizuri. Ni pale unapokuwa na utaratibu mzuri uliojiwekea, kwani haiwezekani jua likawaka usiku, au mwezi kuwaka mchana, kila kitu kilicho na mafanikio maishani kinakuwa kimepangwa.
Hakuna kitu kilichokuwa na mafanikio bila kuwepo kwa mpangilio. Vile vile si rahisi kufanikisha malengo yoyote ya maisha kwa wakati unaohitaji pasipo kuwa na mpangilio. Kwa kuwa, wote waliofanikiwa walipangilia maisha yao.
“Mafanikio ya kuondoka kwa ndege yametokana na ubunifu wa mtu wa kuangalia mfano wa ndege wanaoruka angani. Mfano mwingine ni wa kompyuta, haiwezi kufanya kazi katika eneo lenye joto, kwani itashindwa kufanya kazi inavyotakiwa na ndiyo maana ikatengenezewa mpango (programu).
Vile vile hakuna watu wanaooana bila kuwapo kwa mipango, naamini hufanya mipangilio kabla ya kuchukua hatua hiyo. Chagua sasa njia zilizo sahihi za kupanga maisha yako. Acha kuwa kama meli isiyokuwa na usukani katika bahari iliyo na mawimbi.
Maisha ni mchezo unaohitaji ubunifu. Kwa kuwa na mipango ya ndoto zako, na kuwa na hamu ya kupata unachokikusudia , epuka hali ya mazoea, kukata tamaa na kushindwa.
Hatua muhimu za kufanya ufanikiwe
Kwanza ni vema kutunza kumbukumbu za maisha yako ya kila siku. Kwa kuwa ni vigumu kukumbuka kila kitu kinachotokea kwa kila siku. Vile vile, kutunza majina ya watu wote unaokutana nao kwa siku, maeneo uliyopita, vitu ulivyoambiwa au ulivyojifunza.
Hivyo, tabia ya kukusanya ujuzi na kuuhifadhi kwa ajili ya kumbukumbu za siku zijazo ni utajiri mzuri na inalipa. Hatua ya pili kuwa mtu unayependa kunukuu. Kuwa na kitabu cha kuhifadhia kumbukumbu na andika mawazo mbalimbali yanayokuvutia.
Utakuwa unajifunza njia mbalimbali za mafanikio kutoka kwenye mijadala mbalimbali unayohudhuria. Andika kwenye kitabu chako kwa ajili ya siku zijazo.
Nyingine ni kuhifadhi makala za jinsi ya kufanikiwa zinazokuvutia kutoka kwenye magazeti au majarida mbalimbali, hiyo itakusaidia katika kukabiliana na changamoto za mafanikio katika maisha yako.
Kumbuka, vitabu vizuri vinavyokusaidia kuwa na uwezo wa kufikiri. Vinakusaidia kuwa mbunifu wa mawazo na hisia kuhusu wewe, vitu na wengine. Vitabu vizuri vinakuwezesha uweze kufanikiwa. Ni nyenzo nzuri kwa yeyote anayetaka kusonga mbele kimaendeleo. Kupitia vitabu hivyo ni njia rahisi ya kukuelimisha.
Soma kitabu chochote kinachokuwa rahisi kwako kukinunua. Kama bajeti yako inakuzuia kununua vitabu vizuri mbalimbali, ni vema ukaazima. Kuwa na tabia ya kujisomea angalau kwa nusu saa kila siku. Anza kwa kusoma magazeti na majarida. Endelea kwa vitabu vinavyochochea mafanikio, au kukupa uwezo mkubwa wa kuelewa maisha.
Kuwa na maktaba yako binafsi, kwa kuwa ni hazina nzuri. Katika maktaba yako, weka vitabu vizuri vya maendeleo. Kwa kuwa, ni mtaji wako mkubwa wa mafanikio. Jivunie maktaba yako, ongeza vitabu kadiri uwezavyo. Usiviache vikaharibika na kupata vumbi, chukua mawazo yote mazuri na uyafanyie kazi.
Friday, February 6, 2009
KILA MTU ANAWEZA KUFANIKIWA
Posted in:
0 Maoni:
Post a Comment