Tuesday, January 27, 2009

UKIWEKA NIA UTAFANIKIWA

MIUJIZA inaweza kutokea kwenye maisha yako wakati unapotumia akili katika njia ya kukubali. Na pale unapotambua kwamba kitu pekee kitachokutenganisha kutoka kwenye mafanikio au kushindwa ni vile unavyofikiri, unavyohisi na kuamini.
Kama unavyofikiri na kuamini kila saa ya kila siku, unakuwa tayari umeshapanda mbegu ya mafanikio au kushindwa katika mawazo yako.
Amini kuwa kufikiri na kuhisi kunakuletea mafanikio. Unaweza kuwa na vipaji vingi vya asili vinavyosubiri kuendelezwa, jitahidi kuvivumbua.
Amini kuwa vipaji vyako ni vya thamani na unaweza kuvitimiza kwa kuvifanyia kazi. Amini kushinda mara kwa mara katika vita ya ushindi.
Ni bora kuwa na imani ndogo ya kufanya jambo kuliko kukosa kabisa. Huwezi kuwaza mara moja kuwa unataka kuhamia kwenye nyumba mpya bila kufanya maandalizi.
Lakini unaweza ukapata wazo hilo, ukalipangilia, ukachukua hatua na mwishoni ukapata matokeo mazuri. Unaweza kuwa na mawazo mazuri yaliyojaa utajiri katika maisha yako, afya njema na furaha kubwa kwa kumwamini Mungu.
Maendeleo hutokana na changamoto mbalimbali unazo kabiliana nazo. Unaweza kukua kwa kukutana na changamoto hizo na hapo ndipo utakapopata mafanikio, japo kwenye mafanikio vikwazo mbalimbali hutokea lakini inakubidi usikate tamaa.
Chukua changamoto mbalimbali kama mafanikio. Unapokutana na changamoto katika kupata mafanikio yako kabiliana nazo utashinda.
Mafanikio huja wakati unafanya jambo lenye ubunifu. Hujaumbwa kwa ajili ya hali fulani, bali umeumbwa kama wakala uliye huru wa maamuzi yako ambayo yako ndani ya uwezo wako.
Ukiwa na mawazo, malengo na changamoto za mafanikio ndipo utakapofanikiwa. Unafanya shughuli yoyote kwa ajili yako mwenyewe.
Izoeshe akili yako ikubali ukweli kuwa kila unalolipanga unalitimiza kwa kuchukua hatua zote muhimu kuanzia hapo ndio utakapoona mafanikio yako.
Kushindwa mara moja haimaanishi kwamba utashindwa siku zote, si kwamba mmoja anapofanikiwa atakuwa na mafanikio ya kudumu mpaka pale atakapotumia mafanikio hayo kwa kupiga hatua zaidi.
Maisha ni hatua.
Umezaliwa ushinde na utashinda kama utaamini ukweli huo. Ni asili ya mwanadamu kuwa na hali ya wasiwasi. Wasiwasi juu ya familia yake, majirani zake, kazi yake na maisha yake. Kumbuka wasiwasi unasababisha hofu na ndiyo chanzo kikuu cha kushindwa.
Unapokuwa na hofu juu ya siku ya kesho, haileti maana kwani hujui siku ya kesho itakavyokuwa kwako. Usiishi kwa ajili ya kesho, bali kwa ajili ya siku iliyopo yaani leo.
Kama una wasiwasi juu ya yatakayotokea kesho, mwezi ujao au mwaka ujao, unajiweka katika hali ya kushindwa katika mafanikio yako kwa kuvuruga mawazo mazuri uliyojipangia.
Kamwe usifikiri kuhusu matatizo ya kesho, ishi siku ya leo kwa kufanya mipango mizuri uliyoipanga. Huwezi kufanikiwa kama unakaribisha wasiwasi au hofu katika maisha yako. Kama una wasiwasi wa ratiba yako uliyoipanga kwa siku zijazo, ni kupoteza nguvu zako.
Shughulika na mambo yale ambayo ni ya muhimu. Fanya kitu kimoja kwa wakati, kazi moja kwa wakati usichanganye mambo. Unaporuhusu wasiwasi unakaribisha umaskini katika maisha yako. Kamwe usihofu kuhusu hali ya maisha yako ya siku zijazo.
Ujasiri na jitihada katika maisha ndiyo unaotakiwa. Kubali na kabiliana na changamoto unazokumbana nazo bila kuziogopa. Fikiria matarajio uliyoyapanga na uyape kipaumbele katika akili yako na mboni ya jicho lako. Kuwa jasiri katika kila hatua unayopitia.
Jua kwamba lazima utafanikiwa na simama katika ukweli huo.
Jua kuwa kila siku ni mpya.
Kesho bado haijafika hivyo ukiwa na hofu kwa ajili ya kuhofia matatizo ya siku ya kesho ni sawa na kupoteza nguvu katika akili yako. Ni vema kuzungumzia mafanikio katika kila jambo unalolifanya sasa.
Kama unasubiri mafanikio yakufuate, unakosea. Ni vema kuchangamkia mafanikio. Kila jambo linalokuletea mafanikio liko sasa, amani katika moyo wako unaweza kuwa nayo sasa.
Unaweza kuwa na mafanikio na afya njema uliyokuwa nayo sasa. Kila mara usiwaze yaliyopita au kushawishika kuishi matamanio ya siku zijazo.

3 Maoni:

Amani, Heshima na Upendo kwako Dada Lucy. Nimejifunza kuwa UKIWA NA MAANDALIZI UKAKUTANA NA "WAKATI MUAFAKA" BASI KINACHOFUATIA NI MAAJABU. Ukimuangalia yeyote ambaye amefanikiwa utagundua kuwa kulikuwa na maandalizi aliyoyafanya akakutana na "nafasi" (opportunity) ya kutekeleza maandalizi yake na kinachofuata hapo ni mafanikio. Ndio maana asilimia kubwa ya walioshinda mamilioni ya pesa kwenye bahati nasibu za Marekani wanaishia kuwa ombaomba kwa kuwa hawajajiandaa kabla ya kukutana na "nafasi hiyo ya kufanya vema.
Nia inatakiwa kama ulivyosema na ndio iongozayo kuelekea maandalizi ambayo yakikutana na mwanya wa mafanikio basi twaona MAAJABU.
Nimefurahi kulijua jamvi hili.

Sikujua kwamba wenzangu wanachota maarifa huku!
katika pita pita zangu nimejikuta nikiingia humu bila kukaribishwa, kweli kazi ipo!

Nimepita leo kuchota hekima zako, ahsante sana kwa kutuhabarisha.

Kusema ukweli sina cha kuchangia kwa leo, nikipata wasaa mwingine nitakuja kuweka mawili matatu.

Kazi ni nzuri na inavutia sana.

nakutakia kazi njema.

He hivi niko wapi hapa!!!
na mimi kwa kuzurura, hata sijui nimefikaje hapa.

Kumbe kuna kibaraza kizuri huku wenzangu mnajichotea maarifa ya bure.

je u hali gani dada Lucy, nimepita kibarazani kwako kupata elimu kidogo, ahsante kwa makala nzuri zenye maarifa na utambuzi kama ule tunaousoma kwa kaka kaluse katika kijiwe chake cha utambuzi na kujitambua na kaka Kamala.

Nitakuwa nikipita mara kwa mara , na wewe ukipata nafasi usisite kunitembelea ili kusoma ujinga wangu pale VUKANI.

Twitter Facebook