Tuesday, January 27, 2009

ARI YA KAZI INAPOKOSEKANA JARIBU NJIA NYINGINE

KARIBUNI wapenzi wasomaji katika safu hii ya kila Alhamisi. Tunamshukuru Mungu kwa siku hii ambayo tunaukaribisha mwaka mpya wa 2009.
Katika safu hii ya Maisha Yetu, tumejifunza kwa mifano mbalimbali kutoka kwa watu walioitumia na kufanikiwa katika maisha yao.
Leo, tutamuangalia Chall Wounder, aliyekuwa na meneja katika kiwanda chake ambacho wafanyakazi waligoma kuzalisha, kwa muda kwa kukosa ari ya kufanya kazi.
“Mnaendeleaje?” Wounder alimuuliza meneja huyo, ambaye asingeweza kukifanya kiwanda kizalishe kama ilivyotarajiwa, kutokana na mgomo uliokuwepo.
“Vizuri,” meneja huyo alijibu. “ Nimejaribu kuwashawishi, kwa viapo vyote bila mafanikio, nimewatishia na kuwaambia kuwa nitawafukuza kazi, lakini vitisho vyote vilikuwa bure. Wameendelea na msimamo wao wa kutokuzalisha,” anasema meneja huyo.
Mazungumzo hayo yaliendelea mpaka siku ilipokwisha, kabla ya zamu ya jioni kuanza. Ndipo Wounder alipomuomba meneja wake kipande cha chaki, kutoka kwa mtu wa karibu na kumuuliza, mmezalisha mara ngapi leo?
“Mara sita” bila kusema lolote Wounder aliandika kwa herufi kubwa namba sita katika sakafu na kuondoka. Wakati wafanyakazi wa zamu ya usiku walipoingia, waliona imeandikwa sita na kuuliza maana yake.
“Bosi mkubwa alikuwepo hapa leo,” anasema mmoja wa watu wa mchana waliyekuwepo. “Na alituuliza tumezalisha mara ngapi leo tukamjibu mara sita, akaandika sakafuni.”
Siku iliyofuata bosi huyo alikwenda kiwandani tena, akakuta waliokuwa zamu ya usiku walikuwa wameifuta namba sita na kuandika saba. Alitambua kuwa waliokuwa zamu ya usiku wamefanya vizuri zaidi ya waliokuwa mchana.
Tokea siku hiyo wafanyakazi hao wakaanza kufanya kazi kwa bidii na shauku, walipomalizia zamu yao ya usiku, walitembea kwa maringo na kuandika 10 sakafuni. Tangu siku hiyo, mambo yakaanza kubadilika katika kiwanda kile.
Kwa muda mfupi, kiwanda hicho ambacho kilianza kufa, kiliibuka tena na kupita viwanda vingine katika eneo lile. Je, wajua kanuni iliyotumika? Wonder anasema ukitaka mambo yafanikiwe ni kuanzisha mashindano baina ya wafanyakazi wako.
Anasema, haina maana kuwa, kwa kuanzisha mashindano ni kuwadhalilisha, la hasha, ahitaji kupata fedha nyingi, bali ni uamuzi wa kuwafanya wafanyakazi hao wafanye vizuri katika kuwapa changamoto.
Uamuzi wa kufanya vizuri na kuwapa changamoto, kumewafanya waache mgomo waliokuwa nao, na kuwa na moyo wa kufanya vizuri zaidi.
Mara nyingine unaweza kuwa kiongozi katika eneo lolote, iwe ni nyumbani, ofisini, shuleni au mtaani kwako. Wakati mwingine unaweza kuona kwa vitendo kwamba, mambo hayaendi sawa.
Kama kiongozi unaweza kutumia vitisho vingi au kukaripia bila mafanikio yoyote. Cha msingi ni kuangalia tatizo lipo wapi na kutafuta njia nyingine ambayo inaweza kutoa ujumbe badala ya kuzungumza.
Mfano unaweza kuwa kiongozi wa mtaa, lakini wananchi wa eneo lile ghafla wakaacha kufanya kazi za maendeleo za kuboresha mtaa, hivyo la msingi, ni kuanzisha mashindano baina ya mtaa mmoja na mwingine, ili wananchi hao wahamasike.
Au unaweza kuwa mzazi mwenye watoto zaidi ya watatu. Na mara nyingine watoto hao wakaanza kuwa wavivu, labda wa kutoa vyombo mezani, kufagia, kufua na shughuli nyingine ndogo ndogo.
Kama mzazi, unaweza ukawachapa au kuwafokea bila mafanikio, cha msingi na kuangalia na kuanzisha changamoto ambayo itaweza kuwabadili. Kwa mfano kumnunulia zawadi mtoto aliyefanya vizuri zaidi ya wengine, baada ya muda utaona kuna mabadiliko fulani yametokea.

0 Maoni:

Twitter Facebook