Tuesday, January 27, 2009

JINSI GANI UNAWEZA KUFANIKIWA - 2

KARIBUNI wapenzi wasomaji kwa siku nyingine tena ya leo, ambayo tutaangalia ni jinsi gani tutaweza kufanikiwa katika maisha yetu. Makala hii ni mwendelezo wa Alhamisi iliyopita katika safu hii ya Maisha Yetu.
Kumbuka hukuzaliwa katika dunia hii kuishi au kukabiliana na maisha kwa bahati mbaya. Kila mmoja anajua kuwa maisha ni safari ndefu, mwanzo wa mwanadamu ni kuzaliwa. Na siku yoyote anaweza kufa.
Katika maisha tuliyonayo, mwanadamu ana uhuru wa kufanya kile atakacho na kusimamia maisha yake katika jambo alitakalo, kwa nia ya kula matunda mazuri katika maisha. Hivyo mwanadamu anatakiwa kuwa na utayari katika kuyatengeneza maisha yake, ni lazima ajue yeye ni nani na anaelekea wapi.
Malengo makubwa ya kiroho ya mwanadamu ni kuwa karibu na Mungu, malengo katika akili ya mwanadamu ni kutambua na kutumia vipaji alivyonavyo kwa ajili ya faida yake na familia yake. Kumbuka Mungu amekuumba kuwa mbunifu na anakutaka ufanikiwe na siyo ushindwe.
Wewe ni wa thamani kwa nini usiwaache wengine wakalitambua hilo? Hakuna mwingine katika dunia hii kama wewe, ingawa wengine wana mtazamo kama wako na kukuiga. Lakini hakuna atakayeweza kufanya vitu kama vile uvifanyavyo wewe kwa namna hiyo hiyo. Una mawazo yako tofauti yanayokuongoza kufanya jambo tofauti na wengine.
Watu wote ni muhimu, wana vipaji vya kipekee vinavyosubiri kuonyeshwa kipekee na kwa uthamani wake. Leo, zaidi ya ilivyokuwa, wafanyabiashara, wenye taaluma zao na viongozi wa viwanda, huangalia kwa kipekee yule anayeweza kuonyesha kipaji chake katika njia ya ubunifu. Cha msingi ukumbuke kuwa, hauko kama mwingine katika mawazo yako, vitendo na vipaji.
Jaribu kuwa na wazo, wengine wanaoweza kukusaidia waweze kuona kuwa wewe ni wa tofauti na unaweza kuwa wathamani katika vitu muhimu. Kuwa mbunifu na siyo mwigaji. Ni jambo la busara kuelewa, katika ulimwengu huu hakuna mtu anayefanana na wewe. Uwezo ulionao na jinsi unavyowaeleza hawawezi kujieleza kama ulivyo kwa wengine.
Hivyo huwezi kuwa na mshindani bali waigaji. Watu wanaoiga wenzao mara chache hufikia upeo wa juu. Lakini wale wanaobuni na kuzalisha mawazo yao ndiyo wanaofanikiwa, huwa viongozi. Wewe una akili ya ubunifu ya kuzalisha fikra na mawazo yako binafsi na kuelezea vipaji hivyo katika njia ya kipekee.
Acha kushindana na wengine. Wewe ni wewe. Hauko sawa na wengine kiakili, kiroho na kimuonekano. Jitahidi kubuni kitu chako na siyo kuiga. Kuna alama tano zinazoonyesha vipaji vilivyojificha. Kwani kila mmoja ana tabia zilizojificha. Kazi yako ni kugundua na kuviendeleza. Katika maisha unaweza kushangaa kwamba unakosa nafasi muhimu kwa sababu ya kushindwa kuendeleza vipaji vyako. Ni jinsi gani unavyoweza kugundua tabia zilizojificha? Kwanza, tenga dakika thelathini ukiandika tabia zako nzuri na za kawaida ulizo nazo.
Pili, orodhesha vitu ulivyovifanikisha na uvyotarajia kuvifanikisha. Tatu, andika ukurasa mmoja wa wasifu wa maisha yako mpaka hapo ulipo. Nne, tengeneza orodha ya maneno ya sifa ulizowahi kupokea kutoka kwa familia yako na marafiki zako kama tabasamu zuri, mkono wa pongezi, utanashati, utumiaji wa sauti yako, uwezo wako wa kuelezea jambo na mengine mengi.
Tano, tengeneza orodha ya vitu ambavyo unafanya vizuri kuliko vingine, jambo unalolipenda kuliko lingine, michezo na vipaji. Changanya vyote kwa ujumla na uchague vile vilivyobora zaidi kuliko vingine uvifanyie kazi.
Baada ya hapo utajijua kuwa wewe ni mtu wa aina gani, na unataka uweje. Kwa uangalifu changanua vile ulivyoandika na utaona kuwa unazo sifa ambazo hukuwahi kuwaza kwamba unamiliki sifa fulani.
Endeleza tabia zinazopendeza kwa wengine, hakikisha unawajua hao ni akina nani, uwafanye wakufanyie kazi kwa kiwango kinachoridhisha

0 Maoni:

Twitter Facebook