Tuesday, January 27, 2009

UKIWEKA NIA UTAFANIKIWA

MIUJIZA inaweza kutokea kwenye maisha yako wakati unapotumia akili katika njia ya kukubali. Na pale unapotambua kwamba kitu pekee kitachokutenganisha kutoka kwenye mafanikio au kushindwa ni vile unavyofikiri, unavyohisi na kuamini.
Kama unavyofikiri na kuamini kila saa ya kila siku, unakuwa tayari umeshapanda mbegu ya mafanikio au kushindwa katika mawazo yako.
Amini kuwa kufikiri na kuhisi kunakuletea mafanikio. Unaweza kuwa na vipaji vingi vya asili vinavyosubiri kuendelezwa, jitahidi kuvivumbua.
Amini kuwa vipaji vyako ni vya thamani na unaweza kuvitimiza kwa kuvifanyia kazi. Amini kushinda mara kwa mara katika vita ya ushindi.
Ni bora kuwa na imani ndogo ya kufanya jambo kuliko kukosa kabisa. Huwezi kuwaza mara moja kuwa unataka kuhamia kwenye nyumba mpya bila kufanya maandalizi.
Lakini unaweza ukapata wazo hilo, ukalipangilia, ukachukua hatua na mwishoni ukapata matokeo mazuri. Unaweza kuwa na mawazo mazuri yaliyojaa utajiri katika maisha yako, afya njema na furaha kubwa kwa kumwamini Mungu.
Maendeleo hutokana na changamoto mbalimbali unazo kabiliana nazo. Unaweza kukua kwa kukutana na changamoto hizo na hapo ndipo utakapopata mafanikio, japo kwenye mafanikio vikwazo mbalimbali hutokea lakini inakubidi usikate tamaa.
Chukua changamoto mbalimbali kama mafanikio. Unapokutana na changamoto katika kupata mafanikio yako kabiliana nazo utashinda.
Mafanikio huja wakati unafanya jambo lenye ubunifu. Hujaumbwa kwa ajili ya hali fulani, bali umeumbwa kama wakala uliye huru wa maamuzi yako ambayo yako ndani ya uwezo wako.
Ukiwa na mawazo, malengo na changamoto za mafanikio ndipo utakapofanikiwa. Unafanya shughuli yoyote kwa ajili yako mwenyewe.
Izoeshe akili yako ikubali ukweli kuwa kila unalolipanga unalitimiza kwa kuchukua hatua zote muhimu kuanzia hapo ndio utakapoona mafanikio yako.
Kushindwa mara moja haimaanishi kwamba utashindwa siku zote, si kwamba mmoja anapofanikiwa atakuwa na mafanikio ya kudumu mpaka pale atakapotumia mafanikio hayo kwa kupiga hatua zaidi.
Maisha ni hatua.
Umezaliwa ushinde na utashinda kama utaamini ukweli huo. Ni asili ya mwanadamu kuwa na hali ya wasiwasi. Wasiwasi juu ya familia yake, majirani zake, kazi yake na maisha yake. Kumbuka wasiwasi unasababisha hofu na ndiyo chanzo kikuu cha kushindwa.
Unapokuwa na hofu juu ya siku ya kesho, haileti maana kwani hujui siku ya kesho itakavyokuwa kwako. Usiishi kwa ajili ya kesho, bali kwa ajili ya siku iliyopo yaani leo.
Kama una wasiwasi juu ya yatakayotokea kesho, mwezi ujao au mwaka ujao, unajiweka katika hali ya kushindwa katika mafanikio yako kwa kuvuruga mawazo mazuri uliyojipangia.
Kamwe usifikiri kuhusu matatizo ya kesho, ishi siku ya leo kwa kufanya mipango mizuri uliyoipanga. Huwezi kufanikiwa kama unakaribisha wasiwasi au hofu katika maisha yako. Kama una wasiwasi wa ratiba yako uliyoipanga kwa siku zijazo, ni kupoteza nguvu zako.
Shughulika na mambo yale ambayo ni ya muhimu. Fanya kitu kimoja kwa wakati, kazi moja kwa wakati usichanganye mambo. Unaporuhusu wasiwasi unakaribisha umaskini katika maisha yako. Kamwe usihofu kuhusu hali ya maisha yako ya siku zijazo.
Ujasiri na jitihada katika maisha ndiyo unaotakiwa. Kubali na kabiliana na changamoto unazokumbana nazo bila kuziogopa. Fikiria matarajio uliyoyapanga na uyape kipaumbele katika akili yako na mboni ya jicho lako. Kuwa jasiri katika kila hatua unayopitia.
Jua kwamba lazima utafanikiwa na simama katika ukweli huo.
Jua kuwa kila siku ni mpya.
Kesho bado haijafika hivyo ukiwa na hofu kwa ajili ya kuhofia matatizo ya siku ya kesho ni sawa na kupoteza nguvu katika akili yako. Ni vema kuzungumzia mafanikio katika kila jambo unalolifanya sasa.
Kama unasubiri mafanikio yakufuate, unakosea. Ni vema kuchangamkia mafanikio. Kila jambo linalokuletea mafanikio liko sasa, amani katika moyo wako unaweza kuwa nayo sasa.
Unaweza kuwa na mafanikio na afya njema uliyokuwa nayo sasa. Kila mara usiwaze yaliyopita au kushawishika kuishi matamanio ya siku zijazo.

JINSI GANI UNAWEZA KUFANIKIWA - 2

KARIBUNI wapenzi wasomaji kwa siku nyingine tena ya leo, ambayo tutaangalia ni jinsi gani tutaweza kufanikiwa katika maisha yetu. Makala hii ni mwendelezo wa Alhamisi iliyopita katika safu hii ya Maisha Yetu.
Kumbuka hukuzaliwa katika dunia hii kuishi au kukabiliana na maisha kwa bahati mbaya. Kila mmoja anajua kuwa maisha ni safari ndefu, mwanzo wa mwanadamu ni kuzaliwa. Na siku yoyote anaweza kufa.
Katika maisha tuliyonayo, mwanadamu ana uhuru wa kufanya kile atakacho na kusimamia maisha yake katika jambo alitakalo, kwa nia ya kula matunda mazuri katika maisha. Hivyo mwanadamu anatakiwa kuwa na utayari katika kuyatengeneza maisha yake, ni lazima ajue yeye ni nani na anaelekea wapi.
Malengo makubwa ya kiroho ya mwanadamu ni kuwa karibu na Mungu, malengo katika akili ya mwanadamu ni kutambua na kutumia vipaji alivyonavyo kwa ajili ya faida yake na familia yake. Kumbuka Mungu amekuumba kuwa mbunifu na anakutaka ufanikiwe na siyo ushindwe.
Wewe ni wa thamani kwa nini usiwaache wengine wakalitambua hilo? Hakuna mwingine katika dunia hii kama wewe, ingawa wengine wana mtazamo kama wako na kukuiga. Lakini hakuna atakayeweza kufanya vitu kama vile uvifanyavyo wewe kwa namna hiyo hiyo. Una mawazo yako tofauti yanayokuongoza kufanya jambo tofauti na wengine.
Watu wote ni muhimu, wana vipaji vya kipekee vinavyosubiri kuonyeshwa kipekee na kwa uthamani wake. Leo, zaidi ya ilivyokuwa, wafanyabiashara, wenye taaluma zao na viongozi wa viwanda, huangalia kwa kipekee yule anayeweza kuonyesha kipaji chake katika njia ya ubunifu. Cha msingi ukumbuke kuwa, hauko kama mwingine katika mawazo yako, vitendo na vipaji.
Jaribu kuwa na wazo, wengine wanaoweza kukusaidia waweze kuona kuwa wewe ni wa tofauti na unaweza kuwa wathamani katika vitu muhimu. Kuwa mbunifu na siyo mwigaji. Ni jambo la busara kuelewa, katika ulimwengu huu hakuna mtu anayefanana na wewe. Uwezo ulionao na jinsi unavyowaeleza hawawezi kujieleza kama ulivyo kwa wengine.
Hivyo huwezi kuwa na mshindani bali waigaji. Watu wanaoiga wenzao mara chache hufikia upeo wa juu. Lakini wale wanaobuni na kuzalisha mawazo yao ndiyo wanaofanikiwa, huwa viongozi. Wewe una akili ya ubunifu ya kuzalisha fikra na mawazo yako binafsi na kuelezea vipaji hivyo katika njia ya kipekee.
Acha kushindana na wengine. Wewe ni wewe. Hauko sawa na wengine kiakili, kiroho na kimuonekano. Jitahidi kubuni kitu chako na siyo kuiga. Kuna alama tano zinazoonyesha vipaji vilivyojificha. Kwani kila mmoja ana tabia zilizojificha. Kazi yako ni kugundua na kuviendeleza. Katika maisha unaweza kushangaa kwamba unakosa nafasi muhimu kwa sababu ya kushindwa kuendeleza vipaji vyako. Ni jinsi gani unavyoweza kugundua tabia zilizojificha? Kwanza, tenga dakika thelathini ukiandika tabia zako nzuri na za kawaida ulizo nazo.
Pili, orodhesha vitu ulivyovifanikisha na uvyotarajia kuvifanikisha. Tatu, andika ukurasa mmoja wa wasifu wa maisha yako mpaka hapo ulipo. Nne, tengeneza orodha ya maneno ya sifa ulizowahi kupokea kutoka kwa familia yako na marafiki zako kama tabasamu zuri, mkono wa pongezi, utanashati, utumiaji wa sauti yako, uwezo wako wa kuelezea jambo na mengine mengi.
Tano, tengeneza orodha ya vitu ambavyo unafanya vizuri kuliko vingine, jambo unalolipenda kuliko lingine, michezo na vipaji. Changanya vyote kwa ujumla na uchague vile vilivyobora zaidi kuliko vingine uvifanyie kazi.
Baada ya hapo utajijua kuwa wewe ni mtu wa aina gani, na unataka uweje. Kwa uangalifu changanua vile ulivyoandika na utaona kuwa unazo sifa ambazo hukuwahi kuwaza kwamba unamiliki sifa fulani.
Endeleza tabia zinazopendeza kwa wengine, hakikisha unawajua hao ni akina nani, uwafanye wakufanyie kazi kwa kiwango kinachoridhisha

NI JINSI GANI UNAWEZA KUFANIKIWA

UMEZALIWA ili ufanikiwe, mtu yeyote anayekueleza tofauti na hilo, ni mjinga asiyeielewa dunia inavyokwenda.
Mafanikio huwafikia wote wanaokubaliana na kanuni, pamoja na sheria zinazokuelekeza kuwa tajiri na kufanikiwa kwenye maisha.
Ujuzi huu au ukosefu wa ujuzi ni sababu ya kwanini wengine wanafanikiwa wakati wengine wanashindwa katika maisha.
Kanuni hii ya jinsi gani ya mtu anaweza kufanikiwa inamfanya mtu abuni mbinu mbalimbali za kuibua vipaji vipya na kufuata sheria mbalimbali za maendeleo katika akili yake.
Ujuzi utakapokua ndiyo silaha yako katika maisha, utakuwa tayari kuyabadili maisha yako. Kama vile mafanikio kutoka kwenye kushindwa, afya kutoka kwenye ugonjwa na furaha kutoka kwenye majonzi.
Utawala wa akili yako ni ufunguo wa mafanikio. Kile unachofikiri, kihisi na kukiamini, ndicho kitakachokuwa.
Hali ya kukatatamaa, hofu, wasiwasi na woga vinaharibu nguvu ya kujiamini na kukufanya kuwa na mawazo hasi.
Hali hiyo inatakiwa uibadili kabla ya hali ya hewa haijabadilika katika maisha yako. Mawazo ya kukubali na kukataa hayatamiliki akili yako kwa wakati mmoja, lazima moja litatawala.
Wazo litakalotawala katika akili yako litatokana na uamuzi wa maisha yako, kufanikiwa au kushindwa.
Kumbuka njia ya mafanikio haifanywi kwa haraka, bali ni hatua kwa hatua au kidogo kidogo. Hiyo ndiyo njia ya kufanikiwa au kuwa na busara na kupata furaha katika maisha.
Ni jinsi gani kufanikiwa kuna maana kwako. Mafanikio yana uhusiano. Ina maana kuwa vitu tofauti, kwa watu tofauti. Kwa mtu binafsi inaweza kuwa rahisi kupata mafanikio kwa haraka.
Kwa mwingine, anaweza kufanikiwa kuwa na nyumba nzuri na maisha mazuri ya kifamilia, mwingine kupata utajiri na nguvu.
Jinsi ya umuhimu wa kufanikiwa kwa mtu mmoja hakuna maana kuwa ni sawa sawa na mwingine.
Kwa hali yoyote, kila mmoja anaamini kuwa mafanikio yanatokana na kutokuwa na hofu, wasiwasi, dukuduku, kukata tamaa, kushindwa na umaskini, kipato kinachompa mtu furaha, afya, amani katika akili yako, upendo, kujiheshimu, makubaliano ya kifamilia na utumiaji mzuri wa fedha.
Mafanikio huja kutokana na kutamani malengo mazuri yenye mafanikio, na kuwa mbunifu. Ina maana ili ufanikiwe katika maisha ni muhimu ukawa na malengo.
Kwa nini mwingine anashindwa na mwingine anafanikiwa? Katika utafiti uliowahi kufanywa kwa nini watu wanashindwa katika maisha wakati wengine wanafanikiwa, watu mbalimbali kama wafanyabiashara, wanasaikolojia, wanafalsafa pamoja na viongozi wa dini walikuwa na maelezo tofauti.
Kutokana na utafiti huo, ilibainika kuwa, sababu ya wengine kufanikiwa na wengine kushindwa, ni kwa kuwa mtu aliyefanikiwa anajua sababu zilizomfikisha alipo pamoja na kuwa mbunifu katika kufikiri.
Kwa wale walioshindwa katika maisha wamekuwa wakikabiliana na maisha pasipo na utayari wa kujua ni kwanini yupo hivyo alivyo.
Unapokuwa upande wa mafanikio, ni pale unapojua ukweli kuhusu wewe mwenyewe na kuelewa kwa nini na jinsi gani akili yako inafanya kazi na jinsi gani utafikia malengo ya maisha yako uliyojiwekea.
Mwanadamu ana mahitaji ya kiroho na kimwili pia. Kwa muonekano katika ulimwengu wa Kimagharibi, wamekuwa wakijitahidi katika jitihada za kimwili zaidi, wamekuwa wakipuuza za kiroho.
Wanafalsafa wamekuwa wakifundisha kuwa, muonekano wa kimwili siyo muhimu lakini wa kiroho ni wa milele.
Hivyo ni vyema mtu akajielewa yeye mwenyewe, vitu vinavyomzunguka na watu wengine

ARI YA KAZI INAPOKOSEKANA JARIBU NJIA NYINGINE

KARIBUNI wapenzi wasomaji katika safu hii ya kila Alhamisi. Tunamshukuru Mungu kwa siku hii ambayo tunaukaribisha mwaka mpya wa 2009.
Katika safu hii ya Maisha Yetu, tumejifunza kwa mifano mbalimbali kutoka kwa watu walioitumia na kufanikiwa katika maisha yao.
Leo, tutamuangalia Chall Wounder, aliyekuwa na meneja katika kiwanda chake ambacho wafanyakazi waligoma kuzalisha, kwa muda kwa kukosa ari ya kufanya kazi.
“Mnaendeleaje?” Wounder alimuuliza meneja huyo, ambaye asingeweza kukifanya kiwanda kizalishe kama ilivyotarajiwa, kutokana na mgomo uliokuwepo.
“Vizuri,” meneja huyo alijibu. “ Nimejaribu kuwashawishi, kwa viapo vyote bila mafanikio, nimewatishia na kuwaambia kuwa nitawafukuza kazi, lakini vitisho vyote vilikuwa bure. Wameendelea na msimamo wao wa kutokuzalisha,” anasema meneja huyo.
Mazungumzo hayo yaliendelea mpaka siku ilipokwisha, kabla ya zamu ya jioni kuanza. Ndipo Wounder alipomuomba meneja wake kipande cha chaki, kutoka kwa mtu wa karibu na kumuuliza, mmezalisha mara ngapi leo?
“Mara sita” bila kusema lolote Wounder aliandika kwa herufi kubwa namba sita katika sakafu na kuondoka. Wakati wafanyakazi wa zamu ya usiku walipoingia, waliona imeandikwa sita na kuuliza maana yake.
“Bosi mkubwa alikuwepo hapa leo,” anasema mmoja wa watu wa mchana waliyekuwepo. “Na alituuliza tumezalisha mara ngapi leo tukamjibu mara sita, akaandika sakafuni.”
Siku iliyofuata bosi huyo alikwenda kiwandani tena, akakuta waliokuwa zamu ya usiku walikuwa wameifuta namba sita na kuandika saba. Alitambua kuwa waliokuwa zamu ya usiku wamefanya vizuri zaidi ya waliokuwa mchana.
Tokea siku hiyo wafanyakazi hao wakaanza kufanya kazi kwa bidii na shauku, walipomalizia zamu yao ya usiku, walitembea kwa maringo na kuandika 10 sakafuni. Tangu siku hiyo, mambo yakaanza kubadilika katika kiwanda kile.
Kwa muda mfupi, kiwanda hicho ambacho kilianza kufa, kiliibuka tena na kupita viwanda vingine katika eneo lile. Je, wajua kanuni iliyotumika? Wonder anasema ukitaka mambo yafanikiwe ni kuanzisha mashindano baina ya wafanyakazi wako.
Anasema, haina maana kuwa, kwa kuanzisha mashindano ni kuwadhalilisha, la hasha, ahitaji kupata fedha nyingi, bali ni uamuzi wa kuwafanya wafanyakazi hao wafanye vizuri katika kuwapa changamoto.
Uamuzi wa kufanya vizuri na kuwapa changamoto, kumewafanya waache mgomo waliokuwa nao, na kuwa na moyo wa kufanya vizuri zaidi.
Mara nyingine unaweza kuwa kiongozi katika eneo lolote, iwe ni nyumbani, ofisini, shuleni au mtaani kwako. Wakati mwingine unaweza kuona kwa vitendo kwamba, mambo hayaendi sawa.
Kama kiongozi unaweza kutumia vitisho vingi au kukaripia bila mafanikio yoyote. Cha msingi ni kuangalia tatizo lipo wapi na kutafuta njia nyingine ambayo inaweza kutoa ujumbe badala ya kuzungumza.
Mfano unaweza kuwa kiongozi wa mtaa, lakini wananchi wa eneo lile ghafla wakaacha kufanya kazi za maendeleo za kuboresha mtaa, hivyo la msingi, ni kuanzisha mashindano baina ya mtaa mmoja na mwingine, ili wananchi hao wahamasike.
Au unaweza kuwa mzazi mwenye watoto zaidi ya watatu. Na mara nyingine watoto hao wakaanza kuwa wavivu, labda wa kutoa vyombo mezani, kufagia, kufua na shughuli nyingine ndogo ndogo.
Kama mzazi, unaweza ukawachapa au kuwafokea bila mafanikio, cha msingi na kuangalia na kuanzisha changamoto ambayo itaweza kuwabadili. Kwa mfano kumnunulia zawadi mtoto aliyefanya vizuri zaidi ya wengine, baada ya muda utaona kuna mabadiliko fulani yametokea.

Twitter Facebook