Monday, March 3, 2014

WIVU HULETA MAFARAKANO KAZINI

Mafanikio huzaa mafanikio, lakini kwa bahati mbaya huleta wivu.

WAKATI unapokuwa na mafanikio katika kampuni ama eneo la kazi, unaweza kujikuta una marafiki wengi, pamoja na maadui wachache.

Hawa maadui mara nyingi wamekuwa wakijaribu kukuangusha ama kukufanya ushindwe katika kazi zako ama kukupa ushirikiano mdogo.

Wakati mwingine maadui hao huweza kutafuta namna ya kukukwamisha kwa kukufanyia visa mbalimbali ikiwemo wivu, fitina, ukorofi lengo likiwa ni kukukwamisha kimaendeleo na hata katika taaluma yako ama shughuli inayokukupatia kipato, pia wanaweza kukuwekea mitego ili ushindwe.

Hao wafanyakazi ambao wana wivu nawe au wasiopenda ufanikiwe katika kazi yako, ni rahisi kuwatambua kwa kukushusha thamani ama kukunenea maneno ya kushindwa kwa wengine na kukulinganisha na watu hata ambao hawana uwezo ulionao kuwa wapo juu yako kiutendaji ili mradi tu watimize lengo lao.

Kila utakachofanya kwa watu wa aina hii kwao kitakuwa ni gumzo, ama kukushusha thamani hata kama wakiwa wanaujua ukweli halisi juu yako kuhusu utendaji wako wa kazi.

Maadui wa aina hii hutumia fursa ya kuzungumza maneno mabaya au ya kukuvunja moyo pale utakapofanya kosa ama kushindwa jambo. Hawa ni hatari kwa kuwa wanajihesabia haki ama watenda mema wao wenyewe.

Jinsi ya kushughulika na watu wa aina hii katika eneo lako la kazi, kuna njia mbili. Njia ya kwanza ni kuwa kimya na kupuuzia kila wanalokufanyia na ya pili ni kuzungumzia jitihada zao kama zipo.

Katika mazingira kama hayo, inakubidi uwe jasiri na unayejiamini usimamie kile unachokiamini. Pia uwe mnyenyekevu katika kazi yako, toa kile ulichonacho kwa wengine kwa kuwafundisha mbinu mbalimbali za kuweza kufikia mafanikio.

Jitahidi kujiweka katika hali ya kawaida katika mazingira unayofanyia kazi, kuwa na amani na maadui zako, fanya mabadiliko ya kweli katika moyo wako.

Kutokana na umuhimu wa fani yako, epuka migogoro ama migongano isiyokuwa na lazima katika eneo lako la kazi.

Utakapofanya hivyo utapata heshima kutoka kwa wafanyakazi wengine.

Hata kama kwa upande wako umekosea katika eneo Fulani, ni wakati mzuri sasa wa kujirekebisha kutokana na makosa yaliyopita.

Kwa kufanya hivyo watu wataona mabadiliko yako, pia kuwa mtu wa kukubali kubadilika pale unapokosolewa.

Endapo utatambua kuwa wenzako ama msaidizi wako kazini hana furaha nawe, unaweza kuondoa ama kuzuia wivu wake kwako.

Inabidi kuwa mkimya, mtulivu lakini si kwa kiwango ambacho mchango wako utashindwa kuonekana.

Pia wapongeze wenzako katika mafanikio yao. Jitahidi kutokuwa na wivu, endapo nawe utakuwa na wivu kwa wengine, utakuwa huna tofauti na hao wenye wivu katika ofisi yako.

Kama utakuwa hauko imara kuondoa wivu miongoni mwa wafanyakazi, nawe utalazimika kuwa na tabia hiyo katika eneo lako la kazi.

Wakati wote uwapo katika eneo lako la kazi fanya kazi kwa bidii, simamia kile unachokiamini kamwe usijiingize katika makundi ya masengenyo ambayo yanatokea eneo ulilopo.

Kushughulika na watu wa aina hii mara nyingi inakuwa ni vigumu kwa kuwa, wako kwenye mazingira ambayo unataka kuyaepuka. Ni vizuri kufanya jitihada ili kuwa timu moja na kukatama mazingira ya wivu kwa kuwa hali hiyo ikiachwa italeta tatizo.

Mwisho.


0 Maoni:

Twitter Facebook