Friday, March 14, 2014

JENGA MAZINGIRA MAZURI KAZINI


 KUNA vitu mbalimbali ambavyo kiongozi au meneja anaweza kuvifanya ili kuweka mazingira ya kazi yako yawe katika hali nzuri na kujenga hali ya umoja, mshikamano na furaha miongoni mwa wafanyakazi.
 
Miongoni mwa vitu hivyo ni kiongozi au meneja huyo kujenga kuaminiwa na wale anaowaongoza. Kujenga uaminifu ni jambo muhimu kwa wale wote wanaomhusu katika eneo la kazi.
 
Kiongozi unatakiwa kuaminiwa kwa kile unachokizungumza kwamba utakifanya. Ni njia ya kuwaonyesha wafanyakazi kuwa kila unachokifanya ni kwa ukamilifu sio ubabaishaji, ni jukumu lako.
 
Pia kuwaonyesha wale unaowaongoza kuwa unatarajia kupata mambo kama hayo unayostahili kuwafanyia kutoka kwao.
 
Endapo maneno yako unayoyazungumza na tabia yako vinakwenda sambamba hapo utaaminiwa sana . Inaweza kuchukua muda fulani kwa wafanyakazi wako kuelewa kuwa, kile unachokizungumza ndicho unachokitenda.
 
Lakini kinyume cha hapo utaonekana kuwa mbabaishaji, kama maneno yako hayataendana na matendo yako hutaaminiwa. Siri ni kwamba, inachukua muda mrefu kujenga kuaminika lakini muda mfupi kuondoa uaminifu huo endapo utaenda tofauti na unayoyazungumza.
 
Pale unapoondoa uaminifu wako kwa wale unaowaongoza, itachukua muda mrefu kujenga kuaminiwa tena, pia kamwe hautaaminiwa kama ilivyokuwa mwanzo.
 
Kwa hiyo, ni muhimu yale unayoyazungumza ukayatendea kazi ili kuendelea kujenga uaminifu wako kwa wafanyakazi.
 
Hata kama uko katika mazingira ambayo siyo mazuri, kama wewe ni mwaminifu itarahisisha mambo katika utendaji wako. Kile unachokizungumza na kile unachokifanya kinakueleza wewe ni nani.
 
 
Hata kama hawatapendezwa na kile unachokisema. Kama utakizungumza kwa uaminifu, ukarimu  na umakini utaheshimika na kuaminiwa.
 
Uaminifu wa wafanyakazi wako utazingatia jinsi unavyojenga hali ya kujiamini na uwazi katika mazungumzo yako.
 
Pia wanataka kujua kama wanazungumza nawe kuhusu mambo muhimu au taarifa zitachukuliwa katika hali ya usiri mkubwa.
 
Siri ni jambo la muhimu katika mazingira ya kazi, haitakiwi kutoa siri ya mtu kw amwingine isipokuwa umeizungumza katika hali chanya.
 
Pia  matatizo mengine yanayowakuta wafanyakazi wako yanatakiwa yahifadhiwe kati yako na mwajiri pamoja na kiongozi wako, kama itawezekana.
 
Kiongozi mzuri hawezi kuzungumza mtazamo mbaya juu ya timu yake anayofanya nayo kazi.
 
Pia kiongozi mzuri anapaswa kuwasiliana kwa upole na uwazi na wafanyakazi wake. Ili kujenga mazingira mazuri kazini kila mfanyakazi anahitaji kuheshimiwa. Hili linafanyika kupitia kuwasikiliza kila mmoja na kumheshimu kwa kile anachozungumza.
 
Kwa kufanya hivyo unaonyesha kuwa unajali na kumheshimu kila mmoja. Jambo moja muhimu ni kuweka uwazi kwa wafanyakazi wako ili wawe huru nawe katika kuzungumza maono na malengo ya kampuni waliyonayo.
 
Baada ya kuwasikiliza wafanyakazi wako yale waliyonayo pia nawe chukua muda wa kuwaeleza maono na mipango uliyonayo. Eleza jinsi unavyoona jinsi ya kufanya kazi kama timu kwa kuwa kila mtu  ni sawa anastahili heshima, kuliko kufanya kazi kwa matabaka.
 
Kila mtu ni sawa kwa kuwa kila kazi ina umuhimu sawa katika kufanikisha maono ya kampuni. Pia zungumza nao kuhusu maadili, miiko ya kazi pamoja na uthamani wake.
 
Kuzungumza kuhusu maadili ya kazi kutaonyesha mfano wa matarajio unayotaka kuyaona katika utendaji wa wafanyakazi wako na tabia zao. Hiyo ni pamoja na kujivunia kazi unayoifanya, kumjali kila mmoja kutokana na utendaji wake, pia kutumia kazi yako kama njia mojawapo ya kuendelea kujifunza.
 
mwisho

0 Maoni:

Twitter Facebook