Saturday, February 22, 2014

KWA NINI WATU WANAWAKATISHA TAMAA WENGINE?

FRANK John anasema, amekuwa akipata ujumbe mbalimbali kupitia simu ama barua pepe yake zikieleza kuwa kuna baadhi ya watu wamekuwa wakiwakatisha tamaa wengine wasifikie malengo ama mafanikio waliojiwekea.
 
Anasema sababu aliyoipata wakati anasoma ujumbe hizo ni kwamba baadhi ya wale wanaokatishwa tamaa wanawaamini hao wanaowakatisha tamaa.
 
Si vibaya kuwazungumzia hao wanaokukatisha tamaa, lakini pale unapoanza kujiuliza maswali baada ya kuzungumza nao jua kwamba uko kwenye hatari kubwa.
 
Njia inayoweza kukusaidia ambayo haitakudhuru kutokana na watu wa aina hiyo ni kutaka ujue kwa nini watu wanawavunja moyo ama kuwakatisha tamaa wengine.
 
Zipo sababu zinazowafanya baadhi ya watu kuwakatisha tamaa wengine.
 
Kwanza watu hao hawawezi kufanya mambo unayotaka kuyafanya., mfano “ Kama ninaamini kuwa siwezi kufanikiwa lakini ninafikiri kuwa wengine wana bahati hiyo, ndiyo maana ninapokutana na mtu ninayeamini anamafanikio ninaanza kumvunja moyo ama kumkatisha tamaa kutokana na imani yangu potofu,”.
 
Pili mtu wa aina hiyo anatishiwa na wewe kwa kila unachokifanya hata kama ni cha kawaida ambacho kama angejaribu kukifanya naye angefanikiwa.
 
Baadhi ya watu wanahisi kushindwa kufanya jambo pale wanapomwona mtu anajaribu kufanya kitu fulani. Kama wakati wote mtu fulani anataka kuwa tajiri lakini hajishughulishi kufanya shughuli binafsi, huhisi kutishika pale anapoona wewe unachukua hatua ya kuanza jambo la mafanikio.
 
Kutokana na hali hiyo, mtu wa aina hiyo hujaribu kukukatisha tamaa ili usiweze kuwa bora kumzidi yeye.
 
Sababu nyingine mtu wa aina hiyo anakuwa na wivu. Amini ama usiamini. Rafiki yako wa karibu anaweza kujaribu kukuvunja moyo kutokana na wivu alionao kwako. Kama anajihisi ni mnyonge kwako kwa jambo fulani ama kuna mambo unayoyafanya ambayo yeye hawezi kuyafikia hujaribu kukurudisha nyuma kutokana na wivu alionao.
 
Jambo jingine ni woga. Kuna mtu mmoja alitaka kuchapisha kitabu chake cha kwanza , hivyo alimwendea mshapishaji kwa makubaliano maalum kuwa atammalizia fedha zake atakapokiuza kitabu kile, lakini mshapishaji yule alimvunja moyo kuwa huchapisha vitabu vya siasa tu kwa kuwa ndivyo vina biashara. Lakini baadaye mtu huyo aliweza kuchapisha vitabu hivyo na kwa haraka alifanikiwa kuuza zaidi ya nakala milioni moja.
 
Anasema aligundua kuwa, mchapishaji yule aliogopa kupata hasara kwa sababu alimwona kuwa ni kijana, pia alidhamiria kumuangusha asisonge mbele.
 
Sababu nyingine ni kuchukiwa. Kama mtu anakuchukia hataki kukuona ukiendelea katika jambo lolote na ndio maana atajaribu kukuvunja moyo pale anapopata nafasi. Kuwa makini na maadui wa aina hiyo.
 
Vile vile watu wa aina hiyo hawakupi taarifa sahihi. Watu wengi wanapenda kusema ‘sijui’ wanapoulizwa jambo fulani. Wanakuwa hawana elimu muhimu kuhusu kile unachokipanga kukifanya hivyo kurudisha nyuma kwa kusema hawajui.
 
Jambo lingine ni kwamba watu wa aina hii hawawezi kuiona picha halisi uliyonayo juu ya mipango yako. Baadhi yao watakukatisha tamaa kwa kuwa tu hawaelewi picha unayoipanga katika maisha yako.
 
Sasa basi ni jinsi gani unaweza kuwazuia watu wasikukatishe tamaa.
Kuna mambo mawili unahitaji kuyafanya ili kuzuia hali hiyo. jambo la kwanza ni kutokuzungumza kuhusu mipango yako isipokuwa kwa mtu yule ambaye unadhani kuwa anakupenda kwa dhati. Kama utafanya kinyume na hapo utakuwa ukivunjwa moyo na watu wa aina hiyo kila mara.
 
Jambo la pili ni kuonyesha kuwa jambo ulilokusudia kulifanya unalishikilia hilo hilo mpaka linafikia mwisho na mafaniko yake unayaona. Kutokana na sababu hiyo wale wanaokurudisha nyuma wataanza kukuamini na kile unachokisimamia ni sahihi.
 
Makala hii imeandaliwa kwa msaada wa mtandao.
 
mwisho

0 Maoni:

Twitter Facebook